Siku ya Mashahidi,Uganda:Sifa ya kiafrika lazima ipanuliwe hadi ya jumuiya ya kiraia,kitaifa hata kimataifa!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kundi la watumishi 22 Wakatoliki(karibu wote ni Waganda) wa mahakama ya Mfalme (Kabaka) Mwanga II wa Buganda, ambao Mama Kanisa aliwatangaza kuwa Watakatifu, waliteswa sana na baadaye kuuawa kishahidi kati ya 1885 na 1887 kwa kutetea imani yao ya kidini. Watu wengine 150 walikufa katika mapigano kati ya vikundi tofauti vilivyohusishwa na ushawishi wa wamisionari Wakatoliki au Waprotestanti na wafanyabiashara wa Kiswahili au Wamisri. Kifo cha kwanza cha shahidi mnamo Januari 1885 kilifuatiwa mnamo Oktoba na kile cha Askofu wa Kiingereza J. Hannington na Joseph Mukasa Balikuddembe. Kundi la Waislamu lilimshawishi Mwanga kuhusu kuhusika kwa Wakristo katika kuchomwa moto kwa eneo la kifalme (1886) na kwa hiyo ukatili wa mfululizo mpya wa mauaji uliwashtua sana viongozi wasio Wakristo kiasi kwamba walizuia mauaji zaidi na hata kusababisha ongezeko la ubatizo. Mashahidi 22 Wakatoliki walitangazwa kuwa watakatifu mnamo 1964 na Papa Paulo XIV ambaye pia alifanya Ziara ya Kitume nchini Uganda.
Mtakatifu Paulo VI alitimiza ziara hiyo kuanzia tarehe 13 Julai hadi tarehe 2 Agosti 1969. Ziara hiyo ya Uganda mara nyingi imekumbukwa kwa kutia moyo Kanisa changa la Afrika kukua katika ukomavu, kwa ajili ya kukuza ubinadamu na kwa ajili ya kutafuta amani. Papa Mtakatifu akikutana na baadhi ya waamini wa kiislamu katika Ubalozi wa Vatican mjini Kampala alieleza kuwa: “Tuna uhakika wa kuwa katika ushirika nanyi, tunapomwomba Mwenyezi Mungu aamshe mioyoni mwa waamini wote barani Afrika hamu ya upatanisho na msamaha, ambayo mara nyingi hupendekezwa katika Injili na Kurani. Na tunawezaje kushindwa kuhusisha na ushuhuda wa uchamungu na uaminifu wa mashahidi Wakatoliki na Waprotestanti kumbukumbu ya wale wanaoungama imani ya Kiislamu, ambao historia yao inatukumbusha kwamba walikuwa wa kwanza, mnamo 1848, kulipa kwa maisha yao kwa kukataa kukiuka maagizo ya dini yao?”
Hotuba ya Papa Paulo XIV kwa mamlaka ya Uganda mnamo Agosti 1,1969
Ndugu msikilizaji na msomaji vile vile Mtakatifu Paulo VI akikutana na Rais, Mamlaka za kiraia na kikosi cha Kidiplomasia, wa Uganda katika Ukumbi wa Bunge huko Kampala tarehe 1 Agosti 1969 wakati wa hija yake ya kitume alitoa hotuba yake. Katika mutadha huu wa maadhimisho ya Mashahidi, tunapenda kukumbusha hotuba hii ya kinabii katika ziara yake ya kwanza Barani Afrika. Maono yake na utabiri wake ulikuwa kama wa watangulizi wake na wale ambao walifuata hadi leo hii.Mapapa wote kilio ni kimoja. Katika ulimwengu uligawanyika vipande vipende na vita unahitaji amani, haki na usawa.
Mabwana! Itakuwa vizuri sisi kujitambulisha kwa kila mmoja na mwingine. Sisi ni nani? (Msidanganyike, kwa bahati yoyote, kwa maoni ambayo mawazo fulani ya sasa yanatuhusu); sisi ni wadogo na dhaifu, kama kila mtu mwingine(na labda zaidi kuliko wengine). Tafadhali tuvumilieni katika udogo wetu binafsi. Hata hivyo, tunathubutu kujiwasilisha kwenu kwa wadhifa wenye sura mbili: Mojawapo, ni upendo mkuu tulionao kwa Afrika, kwenu, kwa watu mnaowatawala na kuwawakilisha; Wadhifa mwingine, si wetu, tulitunukiwa sisi, na ndiyo unaotufanya tuwe wanyenyekevu na wenye ujasiri kuja kati yenu. Ni wadhifa mnaojua, ule wa Papa, ambao unamaanisha Baba; na tumeurithi kutoka kwa Mtakatifu Petro, ambao hatustahili, lakini sisi ni warithi wake halisi, kwamba Mtakatifu Petro, ambaye Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, ndiye aliyeunda msingi wa Kanisa lake, ambalo kwa karibu karne ishirini limeenea duniani kote, hata Uganda. Kama Mchungaji wa Kanisa Katoliki, tuko hapa, na tunakuja mbele yenu kuwaambia pia neno lake rahisi na la dhati: amani iwe nanyi!
"Ninyi ni Waafrika mliopewa mamlaka na uwajibikaji"
Na tunaposema "ninyi," tunatambua nyinyi ni nani: Waafrika, mliopewa mamlaka na uwajibikaji, ambao mnaiga katika nafsi zenu na kazi zenu taswira, hasa uhalisia, wa Afrika mpya. Ndani yenu, tunaipongeza Afrika yenu, Afrika yote, hata ile ambayo haiwakilishwi hapa kimwili. Hatufichi hisia ambayo mkutano huu unaleta mioyoni mwetu. Tunatambua kwa hiari umuhimu wa pekee na maana kubwa ya wakati huu. Afrika, katika utambuzi wake wa hali ya juu, wa kweli na wa kiraia, inapokea salamu za Kanisa Katoliki lote kutoka katika sauti ya kiongozi wake mnyenyekevu. Inaonekana kwetu kwamba Afrika mpya, iliyo huru kutoka zamani na iliyoiva kwa ajili ya upyaisho, inapokea utambuzi wa pekee hapa; na tunamwomba Mungu kwamba iwe na thamani ya kihistoria na ya kinabii kwa hatima yake bora ya baadaye. Acheni utambuzi kamili na wa kweli wa matashi haya utoke mioyoni mwetu hadi midomoni mwetu: muishi Afrika kwa muda mrefu!
Pia tunachukua fursa hii kuwaambia kile ambacho Kanisa Katoliki hufanya na kile ambacho halifanyi katika bara hili, kwani kila mahali linatekeleza utume wake. Kanisa linawashukuru kwa uhuru mnaoutambua: kuwepo na kutimiza utume wake. Linathamini uhuru huu, ambao unamaanisha uhuru katika nyanja yake, ya kidini; unamaanisha tofauti na heshima kuhusiana na mamlaka ya kisiasa. Halina maslahi yake ya kidunia; hajihusishi na siasa kwa maana sahihi ya neno; humpatia Kaisari yaliyo ya Kaisari, na humpatia Mungu yaliyo yake Mungu(rej. Mt 22:21); wala halina nia ya, katika kutekeleza utume wake, kulazimisha sifa maalum za kile kinachoitwa utamaduni wa Magharibi kwa uharibifu wa sifa nzuri na za kibinadamu za utamaduni wa Kiafrika.
"Msiogope Kanisa linawaheshimu!
Msiogope Kanisa; linawaheshimu, linawaelimisha kama raia waaminifu, halichochei uhasama na migawanyiko, linatafuta kukuza uhuru wenye afya, haki ya kijamii, na amani; Kanisa halina upendeleo wowote, ni kwa ajili ya maskini, kwa ajili ya elimu ya watoto wadogo na kwa ajili ya watu, kwa ajili ya kuwatunza wanaoteseka na walioachwa(rej. Mater et Magistra, utangulizi na Katiba ya Gaudium et Spes, na. 42, 76, 88, nk). Kanisa haliwatenganishi waamini wake na maisha ya kiraia na maslahi ya kitaifa; badala yake, linawaelimisha na kuwashirikisha katika huduma ya manufaa ya umma (taz. Gaudium et Spes, na. 75, n.k.). Kanisa leo linafuata mpango wa asili ya kidunia, mpango ambao si wake, bali wenu, ambao unakusudia kutoa msaada wake wa kimaadili na, kwa kadiri iwezekanavyo, pia msaada wa vitendo: mpango wa maendeleo ya watu. Mnajua kwamba tumeandika Waraka, yaani, ujumbe kwa Kanisa na kwa ulimwengu mzima kuhusu mada hii wa Populorum progressio, na tulirudia malengo yake katika ujumbe tuliouandikia Afrika tarehe 29 Oktoba 1967, wa Africae terrarum (A.A.S., 1967, n. 1073 nk.).
"Pamoja na usaidizi wake wa kimaadili na kivitendo Kanisa linawaletea tumaini"
Msiogope Kanisa! Halichukui chochote kutoka kwenu; na linawaleteeni, pamoja na usaidizi wake wa kimaadili na kivitendo, tafsiri pekee, tunaamini kuwa ndiyo tafsiri ya kweli, kuu ya maisha ya mwanadamu kwa wakati na baada ya wakati: ile ya Kikristo. Na ni kwa kuzingatia tafsiri hii ndipo Kanisa linapoona matatizo yenu makubwa, ambayo, kwa maoni yetu, yanaweza kuzingatiwa kutoka katika mitazamo miwili: wa uhuru wa maeneo ya kitaifa na ule wa usawa wa rangi. Kwa neno hili lenye pande nyingi "uhuru," sasa tunamaanisha uhuru wa kiraia, kujitawala kisiasa, na ukombozi kutoka katika utawala wa mamlaka mengine ya kigeni kwa watu wa Afrika. Hili ni tukio linalotawala historia ya dunia, ambalo Mtangulizi wangu Yohane XXIII alilielezea kama ishara ya nyakati (rej. Waraka: Pacem in terris, n. 40-41; A.A.S. 1963, n. 268). Hiyo ni ukweli unaotokana na ufahamu mkubwa ambao wanadamu wamepata kuhusu hadhi yao, kama watu binafsi na kama jamii ya watu; ni ukweli unaofichua mwelekeo usiobadilika wa historia na hakika unalingana na mpango wa maongozi, ambao unaonesha mwelekeo ambao wale walio na majukumu lazima waende mbele, hasa katika nyanja ya kisiasa. Hakuna mtu anayependa kuhisi, Mtangulizi wangu aliona kuwa, chini ya mamlaka ya kisiasa nje ya jamii yao ya kitaifa au kikabila.
"Watu wa Afrika wamechukua jukumu la hatima yao wenyewe,Nchi ya Uganda, ya mashahidi waliomwaga damu"
"Hali zilizoibuka na kuleta wasiwasi Afrika, za chuki ya kuishi pamoja kwa amani"
Hapa, hukumu ya hali halisi iko moja kwa moja kwa mamlaka zinazohusika na, katika baadhi ya kesi nzito hasa, pia kwa dhamiri za raia. Tunapaswa kutaja kurasa ndefu na nzuri kutoka katika Katiba ya Kichungaji ya Mtagusi wa Kiekumeni ya hivi karibuni (Gaudium et Spes, n. 73, 74, 75). Kwa bahati mbaya, hali zimeibuka ulimwenguni kote na hata barani Afrika, za wasiwasi na chuki kubwa ya kuishi pamoja kwa amani kiasi kwamba maneno ya kutisha ya vita, yaliyotolewa kana kwamba ni kwa hitaji lisiloepukika, yanaingia tena. Kanisa, hasa kwa sababu ya asili yake, kwa sababu ya kanuni yake ya kiinjili ya "kutotumia vurugu," haliwezi kutumia lugha hii isiyo ya kibinadamu, huku likiteseka sana kutokana na sababu zake zinazodhaniwa na matokeo yake. Hatuwezi kushindwa kutaja wakimbizi na mateso yao miongoni mwa waathiriwa wa matukio haya mabaya. Tutaendelea kuwa thabiti, hadi matokeo yake ya mwisho, tukiwa na mpango mmoja tu: ule wa "haki na amani," ambao ni wa Kristo. Vurugu hazipaswi tena kuwa kanuni ya maamuzi kwa migogoro ya wanadamu, bali sababu na upendo. Si mwanadamu tena dhidi ya mwanadamu, bali mwanadamu kwa mwanadamu na na mwanadamu, kama ndugu.
"Tunaamini migogoro kati ya watu inaweza kutatuliwa"
Nitasema zaidi, hata nikizungumza tu kama mwanadamu. Tunaamini kwamba leo migogoro kati ya watu inaweza kutatuliwa kwa njia bora na yenye ufanisi zaidi kuliko ile ya vurugu. Mahusiano ya kibinadamu hayapaswi kutawaliwa na mapambano ya nguvu zinazoachiliwa kwa ajili ya mauaji na uharibifu, bali kwa mazungumzo ya busara, yanayoungwa mkono na taasisi za kimataifa, ambazo lazima tuzipe mamlaka, ufanisi, na uaminifu. Katika tukio hili pia, tunaelezea matumaini yetu kwa ufanisi unaoongezeka wa taasisi hizi. Hata katika suala linaloendelea kushuhudiwa la ukoloni na ukoloni mamboleo barani Afrika, ambalo linaweza kukosolewa kwa kuruhusu mara nyingi maslahi ya kiuchumi kutawala juu ya mambo ya kibinadamu ni wazi kwamba watu husika wana haki ya kutamani uhuru wao halali; lakini katika hali fulani maalum, njia bora ya kufikia hili itakuwa, labda polepole kidogo, lakini kwa uhakika zaidi, kuwaandaa mapema watu na taasisi zenye uwezo wa kujitawala kiukweli na imara.
"Ushirikiano kati ya watu wa kiasili na wale wa sili ya kigeni"
Maandalizi haya, ambayo tunaamini hayatazuiliwa tu, bali yatahimizwa, kwa utaratibu na ushirikiano, na mamlaka husika, wakati wa kipindi cha ushirikiano kati ya watu wa kiasili na wale wa asili ya kigeni. Hii itawezesha maendeleo ya miundo ya kiutamaduni, kiraia, na kiuchumi inayoweza kuandaa ngazi zote za jamii kwa ajili ya uwajibikaji na hisia ya manufaa ya wote, kwa ajili ya kupata uhuru wa kweli na kuepuka kuanguka katika mitego ya aina nyingine za utumwa zenye hila. Kwa upande wetu, Kanisa, licha ya kuwa katika hali tofauti sana, tayari linafuata njia hii, likiwaandaa Maaskofu, mapadre, watawa, na walei wa eneo ambalo linatekeleza utume wake wa imani na upendo. Na tunaamini kwamba kuanzishwa kwa uongozi wa kiasili kunaweza kuanzishwa hivi karibuni katika nchi za Afrika pia, ambapo hili halijawezekana bado.
"Utofauti wa rangi na kishinda ukosefu wa usawa wa haki na chuki"
Tatizo jingine kubwa: ni lile la utofauti wa rangi. Hata katika hatari ya kuonekana kama mjinga, tutaendelea kuthibitisha kwamba lazima litatuliwe kwa urahisi sana, yaani, kwa kulivua tabia yake ya uadui, ya ushindani, ya ukosefu wa usawa wa haki, ya chuki ya kikabila, na ya chuki ya kimwili. Kwa maneno mengine, ni tatizo ambalo linaweza kutatuliwa kwa kulipunguza iwezekanavyo. Hatufichi matatizo makubwa ya vitendo vinayojitokeza. Kunaweza kuwa na vipimo huru na vya busara, vya heshima kwa desturi, tabia, na utamaduni wa makundi tofauti ya kikabila; lakini sisi kama Wakristo hatuwezi kusahau kamwe kwamba: "Kanisa linalaani . . . ubaguzi wowote au mateso yanayofanywa miongoni mwa watu kwa misingi ya rangi, utaifa, hali ya kijamii, au dini." (Tamko la Mtaguso:Nostra aetate, n. 5). Mtaguso unaendelea: "Watu wote," "wamepewa roho yenye mantiki na wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Wana asili moja na asili moja; na wote, waliokombolewa na Kristo, wanafurahia wito mmoja na hatima moja ya kimungu. Kwa hivyo, usawa wao wa kimsingi lazima utambuliwe zaidi" (Gaudium et Spes, n. 29); na sisi pia, kama wanadamu, lazima tukumbuke kila wakati kwamba njia ya ustaarabu inaongoza kuelekea utambuzi wa usawa wa watu wote, wamepewa, kama hivyo, heshima sawa ya msingi na haki zinazotokana nazo. Kwa sababu hii, tunalaani kuendelea kwa hali za kijamii katika baadhi ya sehemu za ulimwengu kulingana na ubaguzi wa rangi, ambao mara nyingi hutamaniwa na kuungwa mkono na mifumo ya mawazo: hali hizi ni ukiukaji dhahiri na usiokubalika kwa haki za msingi za binadamu na sheria za maisha ya kiraia. Uwingi unaoeleweka wazi hutatua tatizo hasi la ubaguzi wa rangi uliofungwa.
“Ninyi waafrika mna maana ya kina ya jumuiya”
Ninyi Waafrika mnajua maana kubwa ya jumuiya; ni mojawapo ya sifa zenu nzuri na za kibinadamu; lakini hisia ya maana ya jumuiya ya mtu binafsi haitoshi tena; lazima ipanuliwe hadi ile ya jumuiya ya kiraia, kitaifa, na hata kimataifa. Uzoefu wenu utatuambia kwamba uhuru haumaanishi upinzani au kutengwa kati ya watu wa Kiafrika na wasio Waafrika; kiukweli, mataifa mapya ya Kiafrika yanaweza kuwa huru kweli kwa kiwango ambacho yanashirikiana kwa uhuru na mataifa mengine na familia nzima ya kimataifa iliyopangwa kimataifa. Kwa hivyo, amri kuu ya Kikristo ya kupenda jirani ina matumizi mapana zaidi; inaelekea kwenye upendo wa ulimwengu wote: Kanisa Katoliki linaweza kuwa mwalimu mzuri katika suala hili kwa wote. Ni amri nzuri sana, lakini ni ngumu, kwa sababu inahitaji kushinda ubinafsi fulani; na ni amri inayobeba ndani yake zawadi kubwa ya amani.
Tunataka kuhitimisha hotuba yetu kuhusu neno hili: amani! Ni neno chungu: kwa sababu leo hii, katika eneo la Afrika tunalolipenda zaidi, kama tulivyolitembelea na kulipenda miaka iliyopita, mgogoro unaovunja moyo bado unaendelea, kama mjuavyo. Tumejaribu sio tu kuwapatia msaada katika mfumo wa chakula na dawa, bila upendeleo na kwa kila hatua inayowezekana, lakini pia kuwaletea suluhisho la maridhiano ya awali. Bado hatujafanikiwa! Na tunateseka kwa ajili yake kwa moyo wote, tukiazimia kuendelea na kazi yetu ya unyenyekevu, lakini ya upendo na uaminifu ya kushawishi ili kusaidia kutatua mgogoro huu mbaya.
"Amani ni neno la kibinadamu na la Kikristo"
Amani: ni neno la kibinadamu na la Kikristo, linalostahili kueleweka na kulishi na vijana wa Afrika, ambapo kwa amani, linaweza kupata utulivu wake wa kisiasa na kijamii wa kisasa na ustawi wake wa kiuchumi na kiutamaduni, na linaweza kutoa kwa ulimwengu, ambao unaonekana tena kujaribiwa na pepo wa ugomvi, silaha, na ushindani, mfano wa dhana mpya na ya kweli ya ustaarabu, uliojengwa juu ya udugu wa kweli kati ya watu, kati ya matabaka, kati ya vyama, kati ya rangi, kati ya dini, kati ya familia. Amani: ni neno zuri na la ukarimu zaidi tulilonalo mioyoni mwetu na ambalo tunawaelekeza kwenu, Mheshimiwa Rais, kama ishara ya shukrani kwa mapokezi tuliyopokea, tunawapatia wageni wote mashuhuri waliopo, na tunawapa baraka, kama baraka, barani Afrika nzima: Amani kwa Afrika yote!
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.