Tafakari Dominika ya Kumi na Moja Mwaka A wa Kanisa: Waamini Wanaitwa na Kutumwa
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Familia ya Mungu, Leo ni Dominika ya 11 mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu, Dominina ya 11 ya Mwaka A wa Kanisa inatualika kutafakari juu ya wito wetu sisi Wakristo kwamba “Tumeitwa, Tumestahilishwa na Kutumwa” Wokovu wa Mwanadamu ni zawadi ya huruma na ya upendeleo ya Mungu mwenyewe, Mungu anayeona na kuguswa na mahangaiko na shida za watu wake. Aliona mahangaiko ya taifa lake teule, akawatoa utumwani, akafanya nao Agano, ili kupitia wao mataifa mengine yote wabarikiwe. Katika Agano jipya, sisi sote tumefanyika taifa jipya la Mungu, Manabii, Makuhani na Wafalme kwa njia ya Kristo katika ubatizo wetu. Tunatumwa hivyo nasi kuendeleza kazi ya ukombozi, kazi ile ile Kristo aliyowapatia mitume wake, ya kuwa vyombo vya huruma yake kwa watu wote. Tuombe neema ya kuitika wito wa Mungu, kuishi maisha matakatifu, na kuwa tayari kujitoa bila masharti katika kuitenda kazi ya Mungu, kazi ya kuitangaza Injili. Tusali pia kuiombea miito mitakatifu katika kanisa, kwa kuwa mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache.
Somo la Kwanza ni Kutoka Katika Kitabu cha Kutoka 19:2-6. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Kutoka sura hii ya 19, ni sehemu muhimu sana katika historia ya taifa la Israeli. Kabla ya sura hii, wana wa Israeli hawakuwa wametambulika rasmi kama taifa, bali mkusanyiko wa kabila kumi na mbili za Israeli, waliotoka utumwani Misri. Katika sura hii ya 19, chini ya Mlima Sinai, Mungu anawakusanya na kuwapa utambulisho rasmi wa kisheria na kijamii taifa lake hili teule kwa kuweka nao Agano. Hapa ndipo Israeli inapoacha kuwa mkusanyiko wa watumwa na kuwa Taifa rasmi lenye Katiba yake ambayo ni Amri Kumi zinazofuata mara katika sura ile ya 20. Katika somo hili ningependa tujadili mambo yafuatayo yatakayotusaidia kuweka msingi katika kuelewa ujumbe wa dominika hii ya kumi na moja ya mwaka A. Fundisho la kwanza: Wito wa Taifa la Mungu kama taifa pekee, taifa teule la Mungu ni kilelezo cha upendo na ukarimu wa Kimungu. Katika sehemu hii tuliyoisikia, sura hii ya 19:2-6, Mwenyezi Mungu ananena na Musa kwa wana wa Israeli, ambao walikuwa wamefika chini ya Mlima Sinai, wakiwa katika safari yao kutoka utumwani Misri. Na hapa anawakumbusha tena mambo kadhaa, akielekea sasa kuweka nao Agano. Kwanza, anawakumbusha historia, jinsi alivyowakomboa kutoka Misri kwa nguvu na uweza wake, akisema, “Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta kwangu mimi” (Kut 19:4). Mungu aliwakomboa kwa ajili ya mpango maalum, ili wawe taifa pekee, Taifa takatifu la Mungu kati ya mataifa mengine yote. Aliwakomboa kwa mkono wake wenye nguvu ili watambue kuwa sio kwa mastahili yao, bali ni upendeleo wa Kimungu. Hawakua bora, wala watakatifu, wala wema zaidi ya mataifa mengine, bali ni upendeleo wa Kimungu uliozidi mastahili yao wenyewe.
Mwenyezi Mungu anatumia lugha ya picha, akifananisha upendo na ulinzi aliowapatia watu wake na mfano wa tai. Tai ni moja ya ndege wanaolinda makinda yao kwa namna ya pekee sana. Ili kuwaweka salama, huwachukua wanawe wakiwa bado wadogo mgongoni mwake na kuruka nao hadi anga za juu mbali sana, ili kuwalinda na maadui, wanyama wakali, na mishale ya wawindaji. Kisha baada ya muda huwafundisha taratibu kuruka kwa kuwaachia angani waruke peke yao, kisha yeye akiruka chini yao ili kuwalinda wasianguke wakati watakapochoka. Hivi ndivyo Mungu alivyofanya kwa taifa lake. Aliwalinda katika hatari zote, akawapitisha jangwani ili waimarike, ili wakue na wakomae katika imani na matumaini yao kwa Mungu, wakitazama daima nyuma na kukumbuka mambo makuu Mungu aliyowatendea. Kila mara walipoona kama wanazama, Mwenyezi Mungu aliwawahi na kuwainua tena. Ni upendo wa ajabu wa Mungu wetu. Ndugu mpendwa Ndugu, Mwenyezi Mungu anapotumia picha hii ya tai, anatukumbusha mimi na wewe kuwa yeye hatubebi sisi kama mzigo, bali anatubeba kama hazina ya thamani kubwa. Anaturuhusu wakati mwingine tupitie jangwa la maisha au changamoto ili tujifunze kupiga mabawa yetu ya imani, lakini hataruhusu kamwe tuanguke na kuvunjika. Kila ukiona ndugu mpendwa maisha yanakuelemea, kumbuka uko juu ya mbawa za Mungu, uko mikono salama na chini ya ulinzi imara wa Mungu.
Fundisho la Pili: Wito wa taifa teule la Mungu uliendana na utambulisho wao mpya, kama taifa teule la Mungu, kama hazina ya Mungu. Nasi tumepewa utambulisho mpya, sisi tu wa thamani machoni pa Mungu. Katika somo hili la kwanza, Mwenyezi Mungu anaweka wazi nia yake kwamba, “Ikiwa mtaitii sauti yangu na kulishika Agano langu, hapo ndipo mtakuwa tunu kwangu...” Huu unakuwa ndio msingi wa teolojia yote ya Agano la Kale. Unabii wote wa baadaye (Isaya, Yeremia, Ezekieli) unajengwa juu ya uaminifu au ukosefu wa uaminifu wa Israeli kwa Agano hili la Sinai na kwa wito huu wa kipekee wa Mungu. Mwenyezi Mungu anawaahidi kuwa wakitii sauti yake, watakuwa “tunu kwake” (Segullah katika lugha ya asili ya kiebrania), yaani mali ya thamani kubwa ya Mfalme, inayolindwa kwa namna ya pekee kabisa. Kumbe walipaswa kuiishi tunu hii ya thamani ya wito wao. Matokeo ya kuishi kwao kadiri ya Agano lao na Mungu ni kuwa wangekuwa daraja la baraka za Mungu kwa mataifa mengine yote, yaani ufalme wa makuhani na taifa takatifu. Ndugu mpendwa, sisi sote tulioitwa na kustahilishwa na Mungu mwenyewe tumepewa utambulisho mpya kabisa na tunapaswa kuuishi kama watu wenye thamani kubwa kabisa isiyoelezeka machoni pa Mungu na machoni pa watu wengine. Thamani hii kubwa tumeipata kwa njia ya ubatizo wetu, tumekuwa pia taifa teule la Mungu, ukuhani wa kifalme na watu wa milki ya Mungu. Hatupaswi kuishi utambulisho wa kale, bali kuishi ndani ya mpango wa Mungu. Huenda tumewahi kusikia hadithi ya yai la tai lililookotwa na kuwekwa kwenye kiota cha kuku. Yai hili liliatamiwa pamoja na mayai ya kuku, na yule mtoto wa tai akazaliwa akizungukwa na vifaranga vya kuku.
Ndugu zangu, yule mtoto wa tai alikua akiamini yeye ni kuku. Alijifunza kudokoa takataka chini, kupiga kelele kama kuku, na hakuwahi kujaribu kuruka juu kwa sababu kuku hawaruki juu. Siku moja, alitazama angani akamwona ndege mkubwa mwenye nguvu akipaa kwa fahari katikati ya mawingu. Akawauliza kuku wenzake, “Yule ni nani?” Kuku wakamjibu, “Yule ni Tai, mfalme wa angani. Sisi ni kuku wa ardhini, hatuwezi kufika kule. Yule tai mdogo alikua akijua yeye ni kuku na alikufa akiamini yeye ni kuku. Mwenyezi Mungu anawaambia Waisraeli na anatuambia sisi leo kupitia Ubatizo kuwa ulimwengu, marafiki wabaya, uregevu, hofu, na hata shetani, vinaweza kutufanya tukasahau kabisa utambulisho wetu. Vinaweza kutufundisha au vimetufundisha kuishi kama kuku, tukiishi kwa hofu, na kuhangaika ardhini ilihali sisi tunapaswa kuyatafuta ya mbinguni. Lakini Mungu anasema, “Mimi niliwatoa huko, niliwabeba juu ya mabawa ya tai kwa sababu ninyi ni tai! Hamkuumbwa kuishi kwenye takataka za dhambi na udhaifu, mmeumbwa kupaa juu katika utakatifu.” Tuombe nasi neema ya kuishi kweli kadiri ya wito wetu, tukiuchuchumilia kwa uvumilivu utakatifu kama wana wapendwa na wateule wa Mungu kati ya ulimwengu uliojaa kila aina ya undanganyifu. Mtume Petro anasema, tumekombolewa si kwa fedha wala dhahabu, vyenye kuharibika, bali kwa Damu ya thamani kubwa sana ya Mwana wa Mungu. Ni kwa njia ya Ubatizo, sisi tumefanyika kuwa ufalme wa makuhani. Tunafanyika kuwa daraja kati yetu sisi na Mungu ili kwa njia yetu watu wengine waweze kufika mbinguni. Maisha yetu yanatudai ibada ya kweli kwa Mungu, sadaka na upendo usio na mipaka kwa Mungu na kwa wengine ili tuweze kuwa kweli daraja la baraka za Mungu.
Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 5:6-11. Fundisho la kwanza: Tumestahilishwa kwa huruma ya Mungu sio kwa haki yetu. Tusione woga, mashaka na aibu kuanza maisha mapya. Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anatupa sote changamoto kujiuliza kila mara kila mmoja kwanza kabisa kama mbatizwa, na kisha kwa wito binafsi kadiri Mungu alivyotuita. Je, tulistahili kuitwa hazina ya Mungu? Ninastahili kushirikishwa tunu hii kubwa ya wokovu iliyo ndani mwangu kwa mastahili yangu? Jibu ni hapana. Mtume Paulo anasema katika somo hili la pili kwamba, Kristo alikufa kwa ajili yetu “tulipokuwa bado wadhaifu” na “tukiwa bado wenye dhambi.” (Warumi 5:6,8). Kibinadamu, ni vigumu sana mtu kukubali kufa kwa ajili ya mtu mwema au mwenye haki. Lakini Kristo alionyesha upendo wa kiwango cha juu mno kwa kufa kwa ajili ya waasi na wenye dhambi ili watakaswe. Na kimsingi ndiyo mimi na wewe. Kawaida Kibinadamu, tunapofanya usaili wa kazi au interview, tunatafuta watu wenye sifa zilizokamilika, wasifu mzuri (CV), na wasio na madoa, watu sio na historia mbaya. Lakini Mungu hafanyi kazi hivyo. Mungu hachagui watu ambao tayari ni watakatifu; badala yake, anawachagua walio dhaifu na kuwatakasa kupitia wito wake kama alivyofanya kwa taifa lake Israeli. Ndio maana katika Somo la Pili, Mtume Paulo anasisitiza kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu “tulipokuwa bado wadhaifu” (Warumi 5:6). Maana yake, Mungu alitupenda tukiwa katika hali yetu mbaya zaidi ya dhambi. Hakusubiri tubadilike kwanza ndipo atupende. Upendo wake ndio uliotubadilisha. Je hatuna budi nasi kupenda hivyo kama yeye alivyotupenda sisi?
Neno “Kustahilishwa” maana yake ni kupewa hadhi au haki ambayo hukuwa nayo. Sisi hatuna uwezo wa kujisafisha dhambi zetu wenyewe kwa nguvu zetu au kwa matendo yetu mema pekee. Ni Damu ya Yesu Kristo msalabani iliyofuta hati ya mashtaka dhidi yetu. Unaposimama mbele ya Mungu leo, yeye hakuoni kupitia madhambi yako ya zamani; anakuona kupitia Damu Takatifu ya Mwanae iliyotuhesabia tena haki. Hii ndiyo hadhi mpya! Mara nyingi, watu wengi wanajihukumu na kusita kumtumikia Mungu (kama vile kuwa makatekista, viongozi wa jumuia, wanakwaya, au wazazi wema) kwa sababu ya hofu, aibu, hatia, historia au makosa ya maisha yao ya nyuma. Kila mara tunapojaribu kusimama na kutamani kuanza upya, huenda huja sauti masikioni mwetu zikitukumbusha maisha yale ya kale na historia zetu ambazo pengine zilikua mbaya hapo. Lakini tumtazame Mtume Paulo mwenyewe, aliyekuwa mtesaji wa kanisa na muuwaji, alikuwa mhubiri mkubwa kwa watu wa mataifa, tumtazame Petro Mtume, aliyemkana Yesu akawa kiongozi wa Mitume na Kanisa, tumtazame Mathayo (katika Injili ya leo) alikuwa mtoza ushuru, kazi iliyoonekana kama ya usaliti na dhambi kubwa lakini Yesu alimwita kutoka kwenye meza ya ushuru na kumfanya mwandishi wa Injili. Wale waliowahi kuanguka na kuinuliwa na huruma ya Mungu, ndio wanaojua kuhubiri huruma hiyo kwa upendo mkubwa zaidi kwa sababu wanaelewa maumivu ya dhambi. Sote tumewahi kuanguka na kuinuliwa, Yesu, tunakushukuru kwa kutupenda na bado ukatuita tena tukutumikie.
Somo la Injili ni kadiri ya Ni Injili ya Mathayo 9:36:10:8. Katika somo la Injili Takatifu, tunaona matokeo ya huruma hiyo ya Mungu, aliyetuita, na aliyetustahilisha yakigeuka kuwa utume. Viongozi wa Kidini wa Israeli walipaswa kuwa wachungaji wema na daraja la huruma ya Mungu kwa watu lakini hawakutenda hivyo, hawakuwajali maskini, waliwahukumu watu, waliweka sheria ngumu na nyingi ambazo baadaye zilikuwa ni mzigo mzito sana kuubeba. Matokeo yake watu walikata tamaa kabisa. Yesu anautazama umati wa watu hawa na kuwaonea huruma. Walikuwa wamechoka, wametawanyika kama kondoo wasiokuwa na mchungaji (Mt 9:36). Yeye kama mchungaji mwema, hafumbii macho maumivu na shida za kondoo wake, bali anaunda taifa jipya na wachungaji wapya, anawaita mitume na kuwapa uwezo bure wa kuendeleza kazi ya ukombozi. Katika somo hili ningependa tutafakari mafundisho yafuatayo: Fundisho la kwanza: Yesu mwema anatutazama sote kwa jicho la upendo, anatuonea huruma. Anatuita kila mmoja tena kwenda kuwachunga kondoo wake. Neno la Kigiriki linalotafsiriwa kama “aliwaonea huruma” ni "Splagchnizomai", neno lenye maana kubwa na ya kina sana. Neno hili linamaanisha siyo tu huruma ya juu juu ya kusema pole; bali ni huruma inayomfanya mtu asikie maumivu ya mwingine ndani ya mwili wake mwenyewe. Na hii ndio huruma ya Mungu kwetu, Mungu aliyekuja na kukaa kati yetu ili asikie na ashiriki kabisa maumivu yetu.
Ndugu zangu, Injili ya leo inatupatia picha ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Yesu anapotutazama leo katika karne hii ya 21, bado anaona umati wa watu waliochoka, waliotawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Anaona ndoa zilizochoka na karibu kuvunjika, familia zenye changamoto kubwa za kuhuzunisha; anaona vijana waliotupwa kwenye uraibu wa pombe na dawa za kulevya na upotevu wa maadili, kupotea kwa nguvu kazi ya taifa; anaona watoto wa mitaani wanaoongezeka kila kukicha katika ulimwengu wenye kila rasilimali ya kuwasaidia watu wote kuishi kama ndugu, anaona wagonjwa walio hoi vitandani bila msaada wowote, bila huduma bora za afya, bila huruma na msaada wa watu, anaona dunia iliyotawaliwa kwa ubinafsi, uchoyo na chuki na vita vya wenyewe kwa wenyewe, unyanyasaji, rushwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, anaona walimu na manabii wa uongo wanavyowadanganya na kuwapotosha watu wa Mungu kutoka katika imani yao ya kweli kwa sababu ya faida zao binafsi, kwa kutumia Injili na jina la Yesu. Nini jibu la la Yesu? Yesu halaumu viongozi waliofeli kutimiza wajibu wao, bali anawachagua mitume kumi na wawili. Ndugu Mpendwa, Kristo Hatuulizi, wala hawaulizi makutano kwa nini walichoka, au kwa nini walitawanyika na kukata tamaa. Badala yake, anageuka kwako wewe na mimi na kusema, Mavuno ni mengi, watenda kazi ni wachache. Mimi nimekupa wewe uwezo, maarifa, karama, nimekupa amani yangu, nimekupa neno langu. Nenda ukawashike mkono. Nenda ukawainue wengine. Anatualika pia kusali kumwomba Bwana wa mavuno, ili apeleke watenda kazi katika shamba lake, katika ulimwengu unaohitaji uinjilishaji wa kina, si tu wa maneno bali wa ushuhuda thabiti wa maisha hasa katika wakati wetu wa sasa.
Fundisho la pili: Kuhubiri Injili na kuwa wamisionari, tunapaswa daima kuanzia nyumbani kwetu. Hatuwezi kuhubiri mbali ilihali ndani kwetu Injili haipo. Katika kuwatuma Mitume, tumesikia agizo ambalo tunaweza kuliona kama la kibaguzi kidogo. Kristo anawaita mitume wake kwa majina na anawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Lakini anawakataza kwenda kwa watu wa mataifa akiwaambia, afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo wa nyuma ya Israeli iliyopotea. Kwa nini wasiende kwa watu wa mataifa? Moja ya sababu ni kwamba, kama tulivyochambua katika somo la kwanza katika kitabu cha Kutoka 19, Mwenyezi Mungu hakuwateua Waisraeli ili waokolewe peke yao, bali ili wawe Ufalme wa Makuhani, yaani daraja la kuwaleta mataifa mengine kwa Mungu. Hivyo Yesu alitaka kwanza kulirejesha na kulisafisha taifa hili lililopotoka ili likishasimama imara, liweze kuwa mwanga wa mataifa. Ndugu zangu, Yesu anawaambia mitume waende kwanza kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Hii inatufundisha kanuni kubwa ya utume wetu leo kwamba, Utume wa kweli unaanza nyumbani, unaanza pale ninapoishi. Huwezi kuwa mtume mzuri wa kwenda kubadilisha dunia au jamii huko nje, wakati watoto wako nyumbani hawajui kusali, au mke/mume wako analia kwa kukosa amani kwa sababu yako, mwenzangu katika jumuiya anajuta kwa nini tupo naye jumuiya moja. Kabla ya kwenda kuokoa ulimwengu, anza kwanza na wale kondoo waliopotea waliopo ndani ya familia yako, ukoo wako, na parokia yako. Amsha moto wa upendo kwanza ndani yako wewe mwenyewe, nyumbani kwako kwanza, nao utaleta mwanga kwa dunia nzima.
Fundisho la tatu: Tumepewa karama za Mungu bure, tuzitumie kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya watu wake bila masharti. Mwishoni mwa Injili hii Yesu anatoa ujumbe mzito sana juu ya utume huu anaowapatia mitume wake na huu ndio msingi wa utume wote wa Kikristo. Yesu anawapa Mitume mamlaka makubwa, kuponya wagonjwa, kufufua wafu, kutakasa wenye ukoma, na kufukuza pepo. Hizi ni neema kubwa sana, lakini anawapa angalizo, “Mlipokea bure, toeni bure.” Ndugu mpendwa, Kristo anatoa onyo hasa katika siku zetu hizi dhidi ya Biashara ya Kiroho. Zawadi za Mungu (karama, vipaji, baraka, huduma) hazipaswi kugeuzwa kuwa biashara ya kujipatia pesa au umaarufu na faida binafsi. Huu si ujumbe kwa mapadri pekee bali ni ujumbe kwa kila mbatizwa. Kama Mungu amekubariki wewe ukiwa na elimu, fedha, hekima, au afya njema hukuvipata kwa sababu una akili sana au una haki kuliko wengine. Ulipokea bure kama zawadi. Kwa hiyo, unapaswa kutumia baraka hizo kuwasaidia na kuwanyanyua wengine bila kuwatoza gharama za kiburi au masharti magumu. Hitimisho: Ndugu mpendwa, tumeitwa kwa sababu sisi ni hazina ya pekee ya Mungu. Tumestahilishwa kwa damu ya Kristo tulipokuwa bado wenye dhambi. Na sasa tumetumwa kwenda kuwa mabawa ya tai kwa wengine, kuwabeba wale waliochoka, waliovunjika moyo, na kondoo waliopotea katika jamii yetu. Tuseme kila mmoja moyoni kwa ujasiri, “Nimepokea bure upendo wa Mungu, ninakwenda kutoa bure kwa ndugu zangu.” Tuombee miito katika Kanisa ili watenda kazi wasipungue katika shamba hili la mavuno. Mungu atubariki sote, Amina.