Tafuta

Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Kumi na Moja Mwaka A wa Kanisa: Ujumbe mkuu umejikita katika wito wa kila mtu kuwa mkamilifu na kuishi kitakatifu. Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Kumi na Moja Mwaka A wa Kanisa: Ujumbe mkuu umejikita katika wito wa kila mtu kuwa mkamilifu na kuishi kitakatifu.   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika Kumi na Moja Mwaka A wa Kanisa: Wito na Wajibu

Ujumbe mkuu umejikita katika wito wa kila mtu kuwa mkamilifu na kuishi kitakatifu. Licha ya kuwa wito huu ni wa kila mtu mmoja mmoja, lakini unapaswa kijidhihirisha katika maisha ya kijumuiya, ili kumpa kila mmoja nafasi ya kuiishi amri ya mapendo katika ukamilifu wake kwa msaaada wa neema za Mungu, ambaye daima anasikiliza sala zetu tunapomwomba na kumlilia kwa moyo mnyoofu kama mzaburi anavyoimba: “Ee Bwana, usikie, sauti yangu ninalia."

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 11 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu umejikita katika wito wa kila mtu kuwa mkamilifu na kuishi kitakatifu. Licha ya kuwa wito huu ni wa kila mtu mmoja mmoja, lakini unapaswa kijidhihirisha katika maisha ya kijumuiya, ili kumpa kila mmoja nafasi ya kuiishi amri ya mapendo katika ukamilifu wake kwa msaaada wa neema za Mungu, ambaye daima anasikiliza sala zetu tunapomwomba na kumlilia kwa moyo mnyoofu kama mzaburi anavyoimba katika wimbo wa mwanzo akisema; “Ee Bwana, usikie, sauti yangu ninalia. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, wala usiniache, ee Mungu wa wokovu wangu” (Zab. 27:7, 9). Na katika sala ya mwanzo mama Kanisa kwa tumaini hili anasali; “Ee Mungu, uliye nguvu yao wanaokutumaini, uwe radhi kusikiliza dua zetu. Na kwa kuwa pasipo wewe hatuwezi kitu sisi wanadamu dhaifu, utujalie daima msaada wa neema yako, tupate kukupendeza kwa moyo na matendo katika kutimiza amri zako.”

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Kutoka (Kut 19: 2-6). Ni maagizo ya Mungu kwa waisraeli kupitia Musa, namna walivyopaswa kuishi. Kwanza kabisa anawakumbusha makuu aliyowatendea katika kuwatoa utumwani Misri akiwaambia; “Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai...” Mungu akitumia lugha hii ya picha, anajifananisha na tai kuonesha nguvu na uweza wake kuwa ziko juu ya nguvu za mungu wa wamisri – horus – aliyewakilishwa kwa ishara ya mwewe. Ndiyo maana aliweza kuwanyakuwa na kuwatoa utumwani mwa wamisri. Katika kukumbuka hayo makuu aliyowatendea Mungu, Waisraeli wanapasa kuchagua kuisikiliza au kutoisikiliza sauti ya Mungu, kulishika au kutokulishika Agano alilofanya nao. Kama wataisikiliza sauti ya Mungu na kulishika Agano lake kwa uhuru, watakuwa watu wake Mungu, ambaye kwa upande wake anachukua jukumu la kuwalinda na kuwakinga na kila baya litakalojitokeza, maana wao watakuwa taifa lake teule, makuhani wake, watu aliowawekwa wakfu ili kwa njia yao watu wote na mataifa yote wamtambue na kumwabudu Mungu wa kweli aliyeumba mbingu na dunia. Huu ni ufunuo kuwa Israeli ilichaguliwa kumpokea Masiha, Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu kwa ajili ya watu wote. Lakini wakawa wakaidi, wakamkataa.

Ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu
Ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu   (@Vatican Media)

Sisi nasi kwa njia Ubatizo tumechaguliwa, tumetengwa na kuwekwa wakfu, na kupewa kazi ya kuwafanya watu wengine ambao bado hawamjui Mungu wa kweli aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo, waweza kumjua, kumpenda na kumtumikia, na mwisho tuweza kufika kwake mbinguni kwa pamoja tukamsifu milele yote. Ndiyo maana Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafundisha kuwa kwa njia ya ubatizo, Waamini wakristo wanakuwa wameunganika na Kristo na kufanywa kuwa Taifa la Mungu, na kwa sababu hiyo, kwa namna yao wanashiriki kazi ya Kristo ya kikuhani, kinabii na kifalme. Nao wanaitwa kutekeleza, kila mmoja kadiri ya hali yake, utume ambao Mungu amelikabidhi Kanisa (rej. KKK 871.) Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; Mtumikieni Bwana kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba. Jueni ya kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele, na uaminifu wake vizazi na vizazi” (Zab. 99:2-3, 5).

Waamini walei wanatumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili
Waamini walei wanatumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la waraka Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 5:6-11). Ni ujumbe wa matumaini kuwa utukufu na heri ya milele ni hakika kwa kila anayemwamini Kristo Yesu, kwa kuwa alitupatanisha na Mungu Baba tulipokuwa bado wenye dhambi. Hivyo itakuwa ni rahisi zaidi siku ya hukumu ya mwisho kwa wale wanaoweka tumaini lao kwa tendo la upendo la kiukombozi wa Yesu Kristo uliojidhihirisha kwa kifo chake msalabani. Ni katika tumaini hili tunapaswa kuwa mitume, manabii na mawakilishi waaminifu wa upendo wa Mungu kwa binadamu wote uliojifunua na kujidhihirisha kwetu kwa njia Yesu Kristo, na kukubali kuendelea kupatanishwa naye kila tunapotenda dhambi, kwa sakramenti ya kitubio kwa njia ya Yesu Kristo katika nafsi za Mapadre.

Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha
Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 9: 36-10:8). Nayo inatuonesha jinsi huruma ya Mungu ilivyo kuu kwa Yesu Kristo, kuwaonea huruma watu walikuwa wamechoka na kutawanyikwa kama kondoo wasio na mchungaji. Baada ya kuona hivyo aliwaasa mitume wake wasali na kumwomba Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Kisha aliwapa amri juu ya pepo wachafu na mamlaka ya kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina, na kuwaagiza wakaihubiri habari njema ya wokovu na kukaribia kwa ufalme wa mbinguni, kwa wao kuwaponya wagonjwa, kuwafufua wafu, kuwatakasa wenye ukoma na kuwatoa watu pepo wachafu, bure bila malipo yoyote. Sisi nasi kwa njia ya Ubatizo tumeyashirikishwa majukumu hayo. Mtume Petro anasema hivi; “Ninyi ni makuhani, mlioitwa kuwa watakatifu, mmeitwa kutolea sadaka za kiroho ambazo Yesu Kristo alizifanya zipokelewe na Mungu” (1Pet 2:5). Hivyo, Mungu ametuita kuwa taifa lake teule, kuwatangazia habari njema watu ambao wametawanyika, wamechoka, na kukata tamaa na maisha – wajane, yatima, wagonjwa na walemavu, waathirika wa dawa za kulenya na pombe, watu wasiojiweza kwa mahitaji ya kawaida ya kila siku. Kama mitume wa sasa tunao wajibu wa kutangaza habari njema ya wokovu na kuwahudumia ndugu zetu hawa na kupata mahitaji ya muhimu katika maisha yao. Tukumbuke kuwa vyote tulivyo navyo tumepewa bure, tutoe bure. Huu ndio wito wetu tulioitiwa, tulipobatizwa.

Dhamana na wajibu wa maisha ya Kikristo kutangaza Injili ya Kristo Yesu
Dhamana na wajibu wa maisha ya Kikristo kutangaza Injili ya Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua fundisho hili ikisema kuwa, kwa Ubatizo na kipaimara, waamini wote, wanapokea wajibu toka kwa Mungu. “Wakiwa wana wa Mungu kwa kuzaliwa upya, wabatizwa wana wajibu wa kukiri mbele za watu imani ambayo wameipokea kwa Mungu kwa njia ya Kanisa na kushiriki utendaji wa kitume na wa kimisionari wa taifa la Mungu” (KKK 1270). Kwa upande wao, “waamini walei wanashikwa na wajibu na wana haki, mmoja mmoja au wakiungana katika vyama, kufanya kazi ili ujumbe wa Mungu wa wokovu ujulikane na kupokelewa na watu wote duniani. Wajibu huu unadai zaidi katika mazingira ambayo ni kwa njia yao tu, watu wanaweza kusikiliza Injili na kumjua Kristo. Katika jumuiya za kikanisa utendaji wao ni wa lazima hivi kwamba, bila huo, utume wa wachungaji hauwezi kupata matunda yake katika ukamilifu” (KKK 900). Basi tukumbuke kuwa, tunao pia wajibu wa kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, ili tupate watendakazi wengi, wema na watakatifu. Lakini kuomba tu, haitoshi. Tunapaswa pia kuwasaidia kwa hali na mali wale walioitika ili waweza kukua na kukomaa hatua kwa hatua, waje kuwa watenda kazi wema katika shamba la Bwana. Na zaidi sana maisha yetu yawe ya kumpendeza Mungu ili yawe mfano na kuwavutia wengine watamani kuishi kitakatifu kama sisi ili mwisho wa maisha ya hapa duniani tukafurahi sote milele yote mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu, umetujalia mazao haya ya nchi yawe chakula cha kulisha miili yetu na sakramenti ya kutufanya wapya rohoni. Tunakuomba utujalie tusitindikiwe fadhili hiyo kwa ajili ya miili na roho zetu”. Na katika sala baada ya Komunyo anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali hivi; “Ee Bwana, Komunyo hii takatifu tuliyopokea, inaonyesha umoja wa waamini ndani yako; tunaomba ilete vile vile umoja katika Kanisa lako.” Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika ya 11 Mwaka A
13 Juni 2026, 09:35