Tafakari Dominika ya 12 Mwaka A wa Kanisa: Utu na Heshima ya Mwanadamu! Msiogope!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 12 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 20 Juni 2026 amefanya hija ya kichungaji kwa kutembelea Mkoa wa Lombardia, Kaskazini mwa Italia katika miji miwili ya Pavia na Sant’Angelo Lodigiano; miji ambayo imeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Leo XIV. Mtakatifu Augustino ni Muasisi wa Shirika la Waagostiniani: “The Order of St. Augustine, OSA.” Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Leo XIV alitia nia ya kutembelea maeneo ya maisha na utume wa Mtakatifu Augustino. Mji wa Pavia unahifadhi masalia ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa ambaye katika mafundisho yake aliutazama unyenyekevu kama msingi wa imani ya Kikristo. Kwa tajiriba ya maisha na utume wake, Mtakatifu Augustino hatimaye alitambua kwamba ni mtu tu aliye na unyekekevu ndiye anaweza kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni unyenyekevu wenyewe maana “hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu.” (Flp. 2:6-7). Ujumbe mkuu katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 12 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni kuwa utu, hadhi, na thamani ya mwanadamu haiwezi kulinganishwa na cho chote kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Leo XIV katika Waraka wake wa Kitume wa “Magnificat humanitas,” ukuu wa mwanadamu, kuwa katika kuulinda utu wake, na hadhi yake, kwa kufuata misingi ya kiinjili, hatupaswi kuogopa, kuwa na mashaka wala hofu ya mtu yeyote yule, bali kufuata maongozi na ufunuo wa Mungu, mwenye uwezo na mamlaka yote juu ya mwili na roho ya mwanadamu. Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema; “Bwana ni nguvu za watu wake, naye ni ngome ya wokovu kwa Kristo wake. Uwaokoe watu wako, uwabariki urithi wako, uwachunge, uwachukue milele (Zab. 28: 8-9). Hivyo tuwe na hofu ya Mungu na sio ya mwanadamu yeyote. Lakini hofu yetu ya Mungu, sio kwa sababu ya ukatili au ubaya wake, bali ni hofu ya heshima inayosimikwa katika upendo wake kwetu sisi. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Bwana, utujalie kuliheshimu na kulipenda daima jina lako takatifu; kwa maana huachi kamwe kuwaongoza wale uliowaimarisha katika upendo wako.”
Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Yeremia (Yer 20:10-13). Ni ushuhuda wake jinsi maadui na rafiki zake walivyokuwa wanapanga mashitaki juu yake, kupitia kuhani Pashhur, ili amshawishi mfalme atoe hukumu ya kifo juu yake kwa sababu ya kukemea maovu yao na kutanga adhabu juu yao na juu ya Yerusalemu kama wasipoongoka kutubu. Yeremia anasema hivi: “Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake.” Yeremia alipata madhulumu na mateso mengi sana hata kunusurika kuuwawa. Hiyo, alikata tamaa, akataka kuacha kuhubiri, akimlalamikia Mungu kwa kumpa kazi ngumu kiasi hiki hata kuilaani siku aliyozaliwa. Lakini alipojitafakari, aliamua kubaki mwaminifu kwa Mungu na kumtegemea Yeye. Ndiyo maana anasema; “Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.” Kisha akajikabidhi mikononi mwa Mungu na kuomba akisema; “Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo yao, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.” Ni kweli mji wa Yerusalemu ulivamiwa, kuta zake zikabomolea, hekalu likanajisiwa, na watu wengi walichukuliwa mateka uhamishoni Babeli, naye Yeremia akaachwa Yerusalemu. Lakini baadaye alishurutishwa kwenda Misri ndipo alipokufa kwa kuuawa. Hii inatufundisha kuwa wajumbe wa Mungu wanapitia mateso mengi na makali. Lakini, licha ya kuwa wanapitia mateso mengi. Daima mwisho wao ni tuzo ya uzima wa milele mbinguni. Hivyo hatupaswi kuacha kuishuhudia imani yetu hata tukipatwa na mateso ya namna gani, kwani Mungu daima yupo nasi mpaka utimilifu wa dahari. Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, fedheha imenifunika uso wangu. Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, na msikwao kwa wana wa mama yangu. Maana wivu wa nyumba yako umenila, na launu yao wanaokulaumu zimenipata. Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, wakati ukupendezao; Ee Mungu kwa wingi wa fadhili zako unijibu, katika kweli ya wokovu wako. Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema, kwa kadiri ya rehema zako unielekee. Walioonewa watakapoona watafurahi; Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe. Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji, wala hawadharau wafunga wake. Mbingu na nchi zimsifu, bahari na vyote viendavyo ndani yake” (Zab. 68:7-9, 13, 16, 32-34).
Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 5:12-15). Ni ufafanuzi na maelezo jinsi dhambi, adhabu zake, mateso na mahangaiko, vyote hivi vilivyoingia duniani. Kwamba ni kwa njia ya Adamu wa kwanza dhambi iliingia duniani, pamoja na mateso yote, kifo kikawa adhabu yake. Lakini kwa njia ya Adamu wa pili, yaani Yesu Kristo, neema na baraka za Mungu zimeletwa duniani, nazo ni nyingi kiasi cha kuishinda dhambi na adhabu yake. Mtume Paulo anatumia lugha ya biashara ya kununua na kulipa akisema kuwa Yesu alikuja duniani kulipa deni ambalo sisi binadamu hatukuwa na uwezo wa kulilipa. Ni kwa mateso na kifo chake, akaleta wokovu uliozidi uovu wa dhambi ya mwanadamu, kwa dunia nzima. Kwa hiyo wema wake ulizidi ubaya wa dhambi za watu wote duniani, hata akawa sababu ya wokovu wetu. Sisi tunapomshuhudia Kristo, tunaueneza wokovu kwa ulimwengu wote, na tukitenda dhambi, tunaongeza mateso yake. Na Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 10:26-33). Kuna mambo makuu matatu ambayo Yesu anayatilia msisitizo. Kwanza ni kutokuogopa mtu yeyote yule katika kuitangaza habari njema ya wokovu, Injili, ambayo inapaswa kutangazwa wazi wazi bila kuficha cho chote na bila kuogopa cho chote. Yesu anasema hivi; “Msiogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” Jukumu hili la kuitangaza Habari Njema, linamhusu kila mbatizwa, kwa kuwa njia ya ubatizo, Waamini wakristo wote wanakuwa wameunganika na Kristo na kufanywa kuwa Taifa la Mungu, na hivyo wanashiriki kazi ya Kristo ya kikuhani, kinabii na kifalme, wanaitwa kutekeleza, kila mmoja kadiri ya hali yake, utume ambao Mungu amelikabidhi Kanisa kwa njia ya Mitume (rej. KKK 871). Hivyo “wana wajibu wa kukiri mbele za watu Imani ambayo wameipokea kwa Mungu kwa njia ya Kanisa na kushiriki utendaji wa kitume na wa kimisionari wa taifa la Mungu” (KKK 1270), mmoja mmoja au wakiungana katika vyama, ili ujumbe wa Mungu wa wokovu ujulikane na kupokelewa na watu wote duniani (rej. KKK 900).
Jambo la pili ni sababu ya kutokuogopa, nayo imesimikwa katika thamani ya kila mtu binafsi, ambayo haiwezi kulinganishwa na kitu cho chote. Mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na anakusudiwa kuishi maisha ya umilele mbinguni na ni Mungu peke yake mwenye uwezo na mamlaka ya juu ya mwili na roho ya mwanadamu (re. KKK 225, 356-361). Mwanadamu, kwa kujaliwa roho isiyokufa ni kiumbe peke yake duniani ambacho Mungu amekitaka kwa ajili yake chenyewe. Tangu kutungwa mimba kimekusudiwa heri ya milele (KKK 1703). Yesu anasema hivi; “Je! mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi”. Lakini pia tusiogope kwa kuwa kumshuhudia Kristo sio jitihada na juhudi za kibinadamu tu. Bali ni kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu atutiaye nguvu na neema za Mungu. Hii ni ahadi ya Yesu mwenyewe aliposema; “Mtapokea Roho Mtakatifu na kuwa mashahidi wangu...hata miisho ya dunia” (Mdo 1:8). Hivyo tusiogope, kukata tamaa wala kutafuta kulipiza kisasi kwa wanaotudhumulu kwa ajili ya Injili, bali tufurahi na kushangilia kwa kuwa tuzo letu ni kubwa mbinguni (rej. Mt 5:12). Yesu mwenyewe anasema hivi: “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.” Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, pokea sadaka hii ya kutupatanisha nawe na kukusifu. Utujalie itutakase tupate kukutolea mapendo safi ya mioyo yetu.” Na katika sala baada ya komunyo anasali; “Ee Bwana, sisi tuliolishwa Mwili na Damu takatifu ya Mwanao, tunaomba rehema yako ili ibada hii tunayofanya mara nyingi ituletee kweli ukombozi”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!