Tafuta

Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Tano Kipindi Pasaka Mwaka A: Yesu Ni Njia, Ukweli Na Uzima

Wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu. Shemasi ni mhudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Mashemasi ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara.

Na Padre Octavian O. Hinju, JUCo, - Morogoro, Tanzania.

Huduma ya kitume sharti ijengwe katika utu wema, upole na ukarimu ili kuendelea kumwiga Kristo Yesu Mfufuka anayeendelea kwa nyakati zote kujisadaka kwa ajili ya watu wa Mungu alio wakomboa kwa: Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Huduma ya ushemasi ni kielelezo cha Kanisa linalo kua na kuenea kote ili kuendelea kuwafikia watu wote kwa njia ya huduma ya upendo unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu hata katika magumu, changamoto na upinzani: Unyofu katika huduma na utumishi. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Mashemasi ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha ya wakfu!Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya Pasaka Mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Masomo ya Dominika hii yana mthibitisha Kristu aliye upendo wa Mungu kuwa kwetu ni njia inayotupeleka mbinguni kwa Baba, ukweli utakao tuweka huru na uzima wa roho zetu.

Mitume walikuwa wakidumu katika Ekaristi, Neno na Sala
Mitume walikuwa wakidumu katika Ekaristi, Neno na Sala   (@Vatican Media)

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Dominika ya tano ya Kipindi cha Pasaka ambapo katika hofu na mashaka, wasiwasi na huzuni, Kristo Mfufuka anatufariji na anatukumbusha kuwa Yeye ndiye njia pekee ya kutupeleka kwa Baba. Faraja ya Bwana Mfufuka iendelee kukoleza chachu ya Injili na shauku ya kuendelea kumtangaza na kumshuhudia kwa watu wote, Yeye aliyeshinda dhambi na mauti. Kristo Mfufuka ni upendo halisi wa Mungu anaye tutokea tena na tena ili aambatane nasi siku zote katika safari ya Imani yetu kuelekea Galilaya mji wa ufufuko “lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba, anawatangulia kwenda Galilaya. Mtamwona huko kama alivyowaambia (Mk. 16:7.) Bwana Mfufuka ndiye hakika ya safari yetu hasa huku bondeni kwenye machozi, tunapo hangaika kutafuta wapi pa kukanyaga kwenye ulimwengu huu mamboleo unao endelea kuzongwa zongwa na vita, kinzani na machafuko. Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye anatambulika pia kama Balozi wa amani, anasisitiza kuwa njia pekee ya kupata amani ya kweli ni kupitia huyo Kristo aliye fufuka ambaye mara kadhaa alipowatokea Mitume aliwapa zawadi ya amani, basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa (Yoh. 20:21-23).

Mitume wakawachagua Mashemasi, ili wawe ni vyombo vya Injili ya huduma
Mitume wakawachagua Mashemasi, ili wawe ni vyombo vya Injili ya huduma   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume 6:1-7. Somo hili linaelezea hali ilivyokuwa katika Jumuiya ya Kanisa la Mwanzo ambapo changamoto za kitume zilitatuliwa kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu. Ni ukumbusho kwamba hata katika kuzitenda kazi za Bwana changamoto na vikwazo ni sehemu ya utume huo; ila ni kwa namna gani tunatatua changamoto hizo ndicho kipimo cha ukristu wetu. Kwa upande wao, Mitume walimwomba Roho Mtakatifu naye aliwategemeza kwa kipawa cha Hekima na Saburi hata wakaweza kutatua shida iliyowakabili. Sisi nasi katika shida mbalimbali hasa zile zinazo hitaji Hekima na utambuzi tusisite bali tumwombe ili daima aendelee kutenda kazi ndani mwetu. Kwa msaada na maongozi ya Roho Mtakatifu, Mitume wao walimaliza shida zao kwa kuwapa Madaraka Mashemasi saba wa kwanza waliowachagua ili kushughulikia mahitaji msingi ya watu fukara ili wao waendelee kuhubiri Neno la Mungu na kusali. Tendo hili la kuwapa madaraka mashemasi saba wa kwanza linatoa somo kwetu sote kuishi na kutambua utendaji wa Roho Mtakatifu ndani ya watu wengine, pili, tunaitwa kutopenda sana kung’ang’ania vitu. Mitume wanatufundisha kukasimisha madaraka kwa watu wengine ili pawepo na ufanisi na kazi zitendwe kwa ubora uliokusudiwa. Mitume walitambua kwamba, Madaraka ni huduma kwa watu wa Mungu hivyo tusione soni kukiri wazi kuwa tumezidiwa na kuelemewa bali tuombe msaada kutoka kwa watu wengine. Huu ni unyenyekevu mkubwa unaogusa na kufurahisha Moyo Mtakatifu wa Yesu Mfufuka. Nasi tukitaka kutimiza wajibu wetu vizuri, na pia ili basi tuweze kuimba pamoja na Mzaburi katika wimbo wa mwanzo yaani ‘Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu, machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake’ (Zab.98:1-2), ni lazima tushirikiane katika kazi mbalimbali za ujenzi wa Kanisa kuliko kumwachia mtu mmoja.  Ni katika ushirika matendo makuu ya Mungu hudhihirika wazi wazi, ‘Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao’ (Mt. 18:20).

Mitume wakawa wakidumu katika Neno la Mungu
Mitume wakawa wakidumu katika Neno la Mungu   (@Vatican Media)

Somo letu la Pili ni kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote, 2:4-9. Mtume Petro anaendelea na mahubiri yake mara baada ya ufufuko wa Bwana. Anawaimarisha watu akiwahamasisha kumwongokea Kristo Yesu kwa Maji na Ubatizo na kwa kuwekea mikono na Mitume. Katika somo hili tunamsikia Petro akitumia mifano dhahiri inayopatikana katika mazingira ya Kiyahudi ili waweze kuelewa ujumbe wa Kristo Mfufuka. Mtume Petro, anafundisha kuwa Kristo ndilo lile jiwe lililo hai na imara litoalo uzima wa milele na yeyote mwenye kumsadiki Kristo anasadiki juu ya uzima wa milele. Itakumbukwa kwamba hata baada ya kutenda miujiza na maajabu mengi bado Wayahudi walikataa kumwamini Kristo Yesu, hawa ndio wale waashi walio msulubisha Kristo. Kumbe hata sisi, zipo nyakati kwa kushindwa kwetu kulisikia, kulitafakari Neno la Mungu na kulitenda tumeshiriki moja kwa moja katika kazi ya kumsulubisha Kristo. Hii ni kutokana na mienendo isiyofaa ya maisha yetu na kukumbatia dhambi na uharibifu kiasi cha kufananishwa na waashi wanaolikataa jiwe safi lifaalo kwa ujenzi mzuri wa ufalme wa Mungu. Kristo ndiye Mhandisi na jiwe la ujenzi wa roho zetu; tusali isitokee hata mara moja tukamkataa kwa kudanganywa na fahari za ulimwengu huu; kama anavyotuonya hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI anaposema hivi “yamkini tumeishi kana kwamba Mungu hayupo, basi na tuanze sasa kuishi tukijua kuwa Mungu yupo.  Tutambue kuwa wakristo ambao ni Taifa jipya la Mungu, kwa Sakramenti ya Ubatizo waliifia dhambi na kufufuka pamoja na Kristo Yesu, wanashiriki uhai wa huyo Kristo Bwana wetu na wanarithi fadhili za Taifa la Mungu katika Agano la Kale. Hivyo basi yafaa sana kumsifu Mungu kwa maneno ya Mzaburi ambaye alipoyatafakari matendo makuu ya Mungu alisali akasema hivi, ‘mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe (Zab.33:1-3.)

Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha Huduma ya Upendo
Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha Huduma ya Upendo   (@Vatican Media)

Injili inayobeba na kutamatisha tafakari yetu ya siku ya leo ni kutoka kwa Mwinjili Yohane 14: 1-12. Yohane anaelezea bayana mambo yaliyo wasibu na kuwafadhaisha Mitume. Anasema kwamba Mitume wa Yesu walifadhaishwa sana na mambo matatu: Mosi ni uhaini wa Yuda Iskarioti. Huyu alikuwa ni Mtume wa kuaminika sana aliyebeba dhamana ya kutunza mfuko wa hazina. Hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyewahi kufikiria kuwa Yuda angelitenda alilolitenda. Tukio hili la uhaini na usaliti halina maana ya kutufunza kuto kumwamini mtu bali tutambue kuwa wakati mwingine wasaliti ni wale tunaokula nao sahani moja mezani petu. Tusali tusije tukajikuta katika hali kama hii. Jambo la pili lililo watatiza ni mkano wa Mtume Petro ambaye alikuwa ni mwandamizi wa Kristo ‘Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda (Mt. 16:18). Kama Mzee miongoni mwa Mitume pengine ilitarajiwa kuwa Mtume Petro atakuwa mfano na mwenye kuwatia moyo mwenzake, kwa tendo la kumkana Yesu wengi walipoteza tumaini. Na jambo la tatu lililowanyong’onyeza Mitume ni Kristo kuwaaga. Saa yake ya kupaa Kwenda kwa Baba ilikuwa karibu mno hivyo ilimpasa kuwaandaa juu ya tukio hilo. Hili liliwafanya wapoteze dira na muelekeo na mioyo yao kujawa huzuni na simanzi. Huenda pengine walio wengi walianza kuwaza kurudia kazi zao za zamani yaani uvuvi. Akifahamu kinacho wasonga, Kristo anajitabaisha kwao kuwa Yeye ni njia, ukweli na uzima. Mababa wa Kanisa wanatafsiri sehemu hii ya Injili ya Yohane yaani 14:1-12 ‘Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima’ kama ufunuo wa Umungu wake Kristo na jukumu lake la pekee kama Mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu. Kristo Mfufuka anajieleza kwetu sio tu kama mwongozo wetu bali kama kielelezo cha ukweli wa Mungu, njia ya wokovu, na chanzo cha uzima wa milele. Kama njia: Mungu Baba mara nyingi amesisitiza kwamba Yesu ndiye ‘mlango’ au njia ya pekee ya kwenda kwa Baba. Yeye ndiye njia pekee tunayotembea siku zote kupitia kuiga mfano wa maisha yake na ni njia inayo tuongoza kwa Baba, njia inayotuhitaji kuungana naye badala ya kufuata tu sera na sheria zetu wenyewe.

Kristo Yesu Ni Njia, Ukweli na Uzima
Kristo Yesu Ni Njia, Ukweli na Uzima   (@Vatican Media)

Tena Yesu ni ukweli naye anaonekana kwetu kwa hakika kama “Ukweli halisi” aliyefanyika mwili, kinyume na udanganyifu wa ulimwengu. Anajitambulisha kuwa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; ambaye huwaweka wanadamu huru, na kumfanya Yeye kuwa ndiye msingi wa maarifa yote ya kiroho na kimwili yaliyo sheheni ukweli wa milele. Yesu ni uhai kwani anatazamwa kama chanzo cha uzima tele wa kiroho na ule wa milele. Mababa wa Kanisa kama vile Mtakatifu Augustino katika ufafanuzi wake juu ya sehemu hii ya Injili ya Yohane anaeleza kwamba kwa sababu Kristo ndiye uzima (na nuru), kuambatana naye huleta uzima wa milele na kushinda kifo cha kiroho. Mababa wa Kanisa wanaendelea kuthibitisha na kuhitimisha ukweli huu wanaposema kwamba: Hakuna njia nyingine ya kumfikia Mungu Baba isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye aliteswa, akafa ili kulipia dhambi na kufufuka ili kutoa uzima. Kumbe, huduma ya kitume sharti ijengwe katika utu wema, upole na ukarimu ili kuendelea kumwiga Kristo Mfufuka anayeendelea kwa nyakati zote kujisadaka kwa ajili ya watu wa Mungu alio wakomboa kwa Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Huduma ya ushemasi kama ilivyo kuwa kwa Jumuiya ya kwanza ya waamini wa Kanisa la mwanzo ni kielelezo cha Kanisa linalo kua na kuenea kote ili kuendelea kuwafikia wote kwa njia ya huduma ya unyenyekevu hata katika magumu, changamoto na upinzani: maisha yetu yajengwe katika unyofu wa huduma na utumishi. Tunapo endelea kufurahia zawadi ya ufufuko wa Bwana tusali kuomba neema ya kumtambua Yeye kama njia ukweli na uzima kupitia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hii ni Sakramenti ya upendo wa kimungu kwa wanadamu. Tunapo mpokea Yesu, hatuna tena haja ya kumuomba atuoneshe Baba maana twaamini kuwa kwa kumwona Yeye tumemwona Baba; hivyo kujipatia nguvu ya kuweza kumfuata yeye aliye njia, ukweli na uzima. Tumsifu Yesu Kristo.

Njia Ukweli na Uzima

 

01 Mei 2026, 15:52