Tafuta

Imani ya Kanisa inapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwani hii ni huduma ya Injili ya Upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake. Imani ya Kanisa inapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwani hii ni huduma ya Injili ya Upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Tano ya Pasaka Mwaka A: Huduma ya Upendo!

Liturujia ya Neno la Mungu inatutafakarisha kuwa, “Kristo ni Njia, Ukweli na Uzima” Katika kipindi hiki cha furaha ya ufufuko, tunaendelea kualikwa kuimarisha imani yetu kwa Kristo. Yeye ni njia, Daraja la kutufikisha kwa Mungu, yeye ni ukweli, yaani ufunuo halisi wa Mungu na yeye ni uzima, Yesu ndiye chanzo cha uhai usio na mwisho. Haishii hapa duniani; yeye anatupa ushindi dhidi ya kifo na kutuhakikishia kuishi na Mungu milele baada ya maisha haya. Injili ya huduma

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Familia ya Mungu, ni Dominika ya 5 ya Pasaka mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu inatutafakarisha kuwa, “Kristo ni Njia, Ukweli na Uzima” Katika kipindi hiki cha furaha ya ufufuko, tunaendelea kualikwa kuimarisha imani yetu kwa Kristo. Yeye ni njia, Daraja la kutufikisha kwa Mungu, yeye ni ukweli, yaani ufunuo halisi wa Mungu Baba na yeye ni uzima, Yesu ndiye chanzo cha uhai usio na mwisho. Haishii hapa duniani; yeye anatupa ushindi dhidi ya kifo na kutuhakikishia kuishi na Mungu milele baada ya maisha haya. Imani hii thabiti kwa Kristo haipaswi kuwa imelala, haipaswi kufichwa bali yapaswa kuonekana katika maisha yetu ya kila siku, katika majitoleo ya huduma (diakonia) kwa waliosahaulika, maskini, wajane, yatima, wazee, wagonjwa na walio katika changamoto mbalimbali kama ilivyoishi Jumuiya ya Wakristo wa kwanza baada ya Sherehe ya Pentekoste. Matokeo ya kuiishi vyema Imani yetu kwa Kristo kama wabatizwa ni kuwa mawe hai, tunashiriki kila mmoja kama kiungo hai katika mwili wa Kristo kulijenga Hekalu la Mungu yaani Kanisa.

Mashemasi ni kielelezo cha Injili ya Huduma ya Upendo
Mashemasi ni kielelezo cha Injili ya Huduma ya Upendo   (@Vatican Media)

Somo la Injili: Ni kutoka katika Injili ya Yohane 14:1-12. Somo la Injili Takatifu ni sehemu ya hotuba ndefu ya Kristo katika karamu ya mwisho kabla ya kuingia katika mateso, na kifo chake inayoanzia sura ile ya 13 ya Injili hii ya Yohane. Kristo anaongea kwa mara ya mwisho na Mitume wake waliokuwa na hofu, upweke na huzuni. Kwa nini Mitume hawa walikua na hofu na huzuni? Kwanza, Kristo alikua amekwishawaambia kwamba mmoja kati yao angemsaliti, yaani Yuda Iskarioti (Yn 13:21, 26), pili, Yesu aliwaambia kuwa anakwenda mahali ambapo wao hawawezi kwenda kwa wakati huo, jambo lililowafanya wahisi upweke na kukata tamaa (Yn 13:36) na tatu Yesu alitabiri kuwa Petro angemkana mara tatu (Yn 13:38.) Katika mazingira haya ya taharuki, Yesu anaanza sura hii ya 14 kwa neno la faraja, “Msifadhaike mioyoni mwenu”. Injili hii imegawanyika kimsingi katika sehemu kuu tatu, na ningependa tuujadili mafundisho kadhaa kwenye mgawanyiko huu ambao ndio unatupa msingi wa kuyaelewa Masomo mawili ya Dominika hii, yaani somo la kwanza na somo la pili kama ifuatavyo:

Kristo Yesu ni faraja ya watu wake
Kristo Yesu ni faraja ya watu wake   (@Vatican Media)

Fundisho la kwanza: Kristo anawafariji na kuwatia moyo wafuasi wenye hofu, huzuni na upweke, anatufariji nasi pia katika nyakati zote za upweke, huzuni na mashaka yetu. Sehemu ya kwanza ya Injili hii ya leo inaanzia aya ya 1-4. Na Kristo anaanza hapa kuwa kuwapa moyo Mitume wake kwamba, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mwaminini Mungu, niaminini nami pia”. Kama nilivyodokeza hapo Mwanzo kwamba, wanafunzi wa Kristo walikufa moyo baada ya Kristo kuwaambia kuwa anaondoka kati yao, na kule anakokwenda, hawawezi kufika. Lakini pia alishawadokeza juu ya matukio mawili, tukio la usaliti wa Yuda na tukio la Petro kumkana. Mitume wana hofu, wana huzuni na kujisikia wapweke sana. Anawaambia, Mwaminini Mungu, niaminini nami pia, ishara ya wazi ya Umungu wake. Kwamba kama walivyokuwa na imani kwa Mungu, vivyo hivyo walipaswa kuwa na imani kwake yeye aliyetumwa na Mungu, mwenye Umungu mmoja sawa na Baba. Naye yupo katikati yao. Ndugu mpendwa, neno kufadhaika katika lugha ya kigiriki tarassō, lina maana ya kutikiswa kama vile bahari inavyotikiswa na mawimbi mazito na dhoruba. Neno hili limetumika tena katika ile sura ya 11:33 Kristo alipofadhaika mbele ya kaburi la Lazaro, na ile sura ya 13:21 alipofadhaika akijua Yuda atamsaliti. Hapa wanafunzi wanafadhaika wakijua wanampoteza Bwana, mwalimu na rafiki yao Yesu. Sisi pia katika maisha yetu ya kila siku tunakutana na dhoruba na mfadhaiko kama huu waliokuwa nao mitume wa Yesu. Tunapatwa na mtikisiko mkubwa katika maisha yetu ya kila siku kwa nyakati mbalimbali.

Roho Mtakatifu analiongoza Kanisa katika Neno, Sakramenti na Huduma
Roho Mtakatifu analiongoza Kanisa katika Neno, Sakramenti na Huduma   (@Vatican Media)

Sisi leo tunafadhaika sana pale tunapopoteza vitu vinavyotupa usalama kama vile kupoteza kazi, kupoteza ndugu, wazazi na wapendwa wetu (kifo), au kupoteza heshima, kushindwa katika mipango yetu, katika masomo, katika biashara, kupoteza vyeo na hadhi mbele ya watu. Tunahisi kama dunia yetu inaporomoka, kama ulimwengu wote umetuangukia. Tunafadhaika tunaposalitiwa hata na watu tuliowapenda, watu tuliowasaidia na kuwajali na kula nao pamoja, tunaishia kuumizwa na kuvunjika moyo. Tunafadhaika kuhusu maisha ya baadaye. Maswali kama, “Je, nitaweza kusomesha wanangu?” “Je, nitapona ugonjwa huu?” Ninazeeka sasa, maisha haya ya uzee na au kustaafu yatakuwaje? Nimebadilishiwa utume, sasa maisha yatakuwaje? Je, nikiondoloewa kwenye ofisi hii itakuwaje tena? Je nikiondoka leo, familia yangu itabakije, watoto wataishije, hatma yangu itakuwaje, nk. Kumbe, kutokujua kitakachotokea kesho kunatufanya tuwe na anxiety au wasiwasi wa kupitiliza. Kristo aliye daima katikati yetu, anatupa moyo, usifadhaike moyoni, mwamini Mungu, niamini mimi pia, nipo pamoja nawe, ninatembea daima nawe, sikuachi kamwe. Imani ni dawa dhidi ya hofu, huzuni, upweke na mashaka. Imani ya mitume kwa Kristo itageuka kuwa nguvun ajasiri, kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyempokea siku ya pentekoste na baadaye wataanza maisha mapya pasi na hofu na mashaka yoyote tena, ingawa watapitia bado tena dhoruba na mitikisiko mingi. Nasi pia imani thabiti inatusaidia kushinda hofu, huzuni, upweke na mashaka yetu.

Muhimu: Neno, Sakramenti na Injili ya Huduma
Muhimu: Neno, Sakramenti na Injili ya Huduma   (@Vatican Media)

Fundisho la Pili: Kristo Yesu anatuahidi uhakika wa makao ya milele, kesho ya maisha yetu ipo mikononi mwake, licha ya mateso na hofu zote sasa. Kristo katika sehemu hii ya kwanza anaendelea kwa kuwaambia wanafunzi wake kwamba, “Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi...Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu, ili nilipo mimi nanyi muwepo. Katika tamaduni za Wayahudi, kawaida kijana aliyetaka kuoa, baada ya kumchumbia bi Arusi, alipaswa kwanza kurudi nyumbani kwa Baba yake.  Uko aliandaa makazi mapya (menō), chumba kipya ambacho kimsingi kiliungana na nyumba ya Baba yake. Na mara makazi yalipokuwa tayari alirudi kumchukua bi Arusi, katika muda na saa ambayo haikufahamika. Hivyo bi Arusi naye alipaswa kujiandaa na kujiweka tayari kwa ujio wa Bwana Arusi (Tunafahamu simulizi ya wanawali kumi). Hivyo Kristo, Bwana arusi, kwa mateso, kifo na ufufuko wake na kupaa kwake mbinguni, anakwenda kwa Baba, kutuandalia makao ya milele. Kurudi kwake, hapa mwinjili Yohane alimaanisha kwa nafasi ya kwanza, kurudi Yesu kwa mitume wake baada ya ufufuko wake siku ya tatu, kwa nafasi ya pili, ni ujio wa Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste na tatu ni ujio wake mara ya pili mwisho wa nyakati. Atakuja kulichukua kanisa, bi arusi wake, nasi twapaswa kujiandaa kwa ujio wake huo.

Kristo Yesu Ni Njia, Ukweli na Uzima
Kristo Yesu Ni Njia, Ukweli na Uzima   (@Vatican Media)

Ndugu mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo anatuhakikishia makazi ya milele, ambapo tutaishi katika ushirika naye pamoja na Baba na Roho Mtakatifu. Maisha ya hapa duniani ni ya mpito tu. Tunajua kuwa makao yetu ya kudumu (menō) hayategemei mambo ya dunia hii bali ipo kwa Mungu pekee. Kristo akiwa anatuandalia makao, anatualika nasi tusilale kiroho, viuno vyetu viwe vimefungwa na taa zetu zapaswa daima kuwa zimewaka. Tukitambua hilo, tutafanya kazi kwa moyo, kwa juhudi na maarifa lakini tukiwa na matazamio ya kujenga na kuwekeza katika makazi yetu ya kudumu mbinguni. Lakini pia Kristo anatupa moyo kwamba hata mateso na kifo sio mwisho. Tunapojua kuwa Yesu ameandaa mahali, kifo kinakuwa ni kuhama tu kutoka kwenye chumba cha muda, au nyumba ya kupanga ya wageni hapa duniani na kuelekea kwenye makazi ya kudumu yenye amani katika uzima wa milele. Hii inatupa faraja ya kweli hasa tunapoomboleza, au kupitia katika magumu na hofu.

Kristo Yesu ni Ufunuo wa Huruma, Upendo na Msamaha wa Mungu
Kristo Yesu ni Ufunuo wa Huruma, Upendo na Msamaha wa Mungu   (@Vatican Media)

Fundisho la tatu: Kristo si tu anatuonesha njia ya kwenda kwa Baba, bali yeye ndiye hiyo Njia, Ukweli na Uzima. Sehemu ya pili ya Injili hii ya inaanzia ile aya ya 5-11. Ndani yake kuna swali la Mtume Thomaso kuhusu njia (5-7) na ombi la Mtume Philipo kuhusu utambulisho wa Mungu (8-11). Mtume Thomaso alikua ni kati ya mitume wa Yesu ambaye alitaka kujua mambo lakini kwa ushahidi zaidi. Tunaona hata baada ya Yesu kufufuka hakuamini hata alipoambiwa na mitume wenzake mpaka pale Kristo alipomtokea. Hivyo anamwuliza Yesu, “Sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia?” Thomaso alijua Kristo alizungumzia makazi yale kama eneo la kijeografia, asielewe kuwa Kristo alizungumzia makao ya mbinguni. Kristo anamjibu kwa kumwambia, mimi ndimi njia, ukweli na uzima. Yesu haoneshi tu njia, bali yeye ndiyo hiyo njia, daraja la kutupeleka kwa Mungu, ndiye ukweli yaani ufunuo wa Mungu Baba na ndiye uzima, ndiye anayetoa nguvu ya kwenda katika njia hiyo. Kumbe aliyemwona Kristo, huyo amemwona Baba, kama anavyomjibu pia Mtume Philipo (8-11), aliyemwomba Kristo kuwaonesha Baba. Mtume Filipo naye alifikiri Mungu angejifunua kwao kama ilivyokuwa katika Agano la kale, katika tokeo au theophany, kwa namna ya ajabu ya miujiza ya kutisha. Lakini Kristo anamkumbusha kuwa yeye ndiye ufunuo, ndiye picha halisi ya uso wa Baba wa milele. Na kazi zote alizozitenda, zilikua na lengo la kuwasaidia ili wanafunzi nasi sote pia kuwamini ya kuwa yeye alitoka kwa Mungu.

Changamoto za maisha na utume wa Kanisa zinatatuliwa kwa Sala na Neno
Changamoto za maisha na utume wa Kanisa zinatatuliwa kwa Sala na Neno   (@Vatican Media)

Ndugu mpendwa, mashaka ya Thomaso ndiyo mashaka yetu ya kila siku. Kuna nyakati katika maisha tunakua njia panda, hatuoni wala hatuelewi tufanye nini na tutokeje pale tulipo kuendelelea mbele. Unapohisi hujui unakoenda kimaisha (kitaaluma, ndoa, wito mwingine wowote au hata maisha ya kiroho), hatuna haja ya kupata majibu yote ya kesho. Tunahitaji tu kuimarisha uhusiano wetu na Kristo Yesu katika ulimwengu uliojaa kila aina ya udanganyifu na mashaka, yeye aliye ukweli, ufunuo halisi wa Mungu Baba. Yeye ndiye ukweli usiobadilika, kinyume na mambo mengine ya ulimwengu huu ambayo yaweza kutupa uhakika usiodumu milele. Kristo kama daraja anatuunganisha sisi na Mungu, alikua sawa na sisi, anafahamu mahangaiko yetu, anafahamu huzuni zetu, anafahamu mapigano yetu dhidi ya dhambi na udhaifu wetu, na hivyo kama kuhani mkuu anatuombea kwa Mungu. Kisha yeye ndiye uzima, anatuimarisha, anatulisha kwa Neno na Sakramenti zake ili daima tuwe imara, tuwe hai na wenye uzima tele, uzima wa sasa, na uzima wa milele. Yeye mchungaji wetu mwema anatuambia, “mimi nilikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tena. Kristo anatenda kazi katikati yetu, na kwa kazi hizo anatualika sote tumwamini. Sehemu ya mwisho ya Injili hii yaani aya ya 12 inatusaidia kuelewa vyema somo la kwanza na somo la pili katika dominika hii ya leo. Kristo anawahikikishia mitume wake kuwa, “Yeye aniaminiye mimi, njia, ukweli na uzima, kazi nizifanyazo mimi naye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Ni baada ya Pentekoste (Kristo alipokuja kwao tena kwa njia ya Roho Mtakatifu) tunaona mitume wanazitenda kweli kweli kazi hizi za Kristo bila hofu na mashaka tena. Na matokeo yake yanaonekana wazi katika jumuiya ya wakristo wa Mwanzo.

Kesho Yetu iko mikononi mwa Mungu
Kesho Yetu iko mikononi mwa Mungu   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 6:1-7. Katika somo la kwanza kutoka katika kitabu hiki cha Matendo ya Mitume, Mitume wanawachagua Mashemasi saba, wanawaombea na kuwawekea mikono ili kutimiza huduma ya upendo kwa Kanisa la mwanzo. Hapa tunaona inawekwa rasmi ofisi hii ya ushemasi (diakonia) au huduma katika Kanisa la mwanzo. Katika somo hili tunapata fundisho la nne katika dominika hii ya 5 ya Pasaka. Fundisho la nne: Kristo Yesu anatupa nguvu ya kutusukuma kuona, kuguswa na kutatua changamoto kwa wakati na kwa usahihi. Anatuonesha njia ya kupata utatuzi wa changamoto zetu. Kwa nini mitume wanawachagua mashemasi hawa? Mitume waliwachagua mashemasi kutokana na manung’uniko ya Wayahudi wa Kiyunani, yaani Wayahudi walioishi nje ya Palestina, kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Hivyo wanawachagua mashemasi saba ambao walikua nao ni Waebrania wayunani, wanawakea mikono, kuwapatia nguvu ya Roho Mtakatifu, na wanatumwa kufanya huduma ya upendo (diakonia). Mitume na Mashemasi (kama Stefano na Filipo) wanaeneza Injili na kuhudumia maelfu ya watu. Uteuzi wa Mashemasi ni mfano wa kazi kubwa ya upanuzi wa ufalme wa Mungu ambayo Yesu aliisema, kazi hii ya huduma inavuka mipaka ya utamaduni (Wayahudi na Wayunani), wote wanathaminiwa na kuhudumiwa kwa usawa.

Imani ni dawa dhidi ya hofu, huzuni na machungu moyoni
Imani ni dawa dhidi ya hofu, huzuni na machungu moyoni   (@Vatican Media)

Ndugu mpendwa, Neno la Kristo Yesu linatusukuma daima katika kuona, kuamua kwa usahihi na kutenda kwa wakati, katika kutatua changamoto mbalimbali tunazokumbana nazo katika mazingira yetu, katika familia, jamii na utume wetu. Roho Mtakatifu anatupa nguvu ya kuwa wamoja, kushirikiana kwa pamoja kwa karama na vipaji mbalimbali kama ilivyokuwa jumuiya hii ya wakristo wa kwanza. Kristo aliye njia, ukweli na uzima anavunja kuta za matabaka kati yetu, ya kikabila, lugha, utaifa nasi tunakua jumuiya moja (koinonia) inayosali pamoja na kushirikishana katika hali zote. Je, katika familia zetu, jumuiya, parokia zetu, katika jamii yetu, tunaona changamoto, kuamua kwa usahihi na kutenda kwa wakati katika kuzipatia changamoto hizo majibu? Tunashirikisha wengine ili kwa pamoja tuweze kutatua changamoto zetu, au ni kila mmoja anapambana kivyake vyake kupata utatuzi? Mitume walimshirikisha Mungu kwa sala, na wakawateua mashemasi wale na kuwawekea mikono. Sisi tunamshirikisha Mungu changamoto zetu ili atuoneshe yeye njia ya kufikia suluhisho au tunaanza kwanza kwa nguvu zetu wenyewe? Mitume hawakupotezea, hawakufumbia macho malalamiko ya wajane, walichukulia kwa uzito na hata leo tuna ofisi hii muhimu katika Kanisa, ofisi ya Mashemasi. Sisi mara ngapi tunafumbia macho changamoto mbalimbali? Mara ngapi tunafumbia ukweli, kwa kujidanganya au kudharau kuwa matatizo na chngamoto hizo hazipo? Pengine katika ofisi zetu, katika utume wetu, katika familia zetu, katika parokia zetu. Tunaona, tunaguswa, kuamua kwa usahihi na kutenda kwa wakati? Neno la Mungu litusukume katika kuzitenda kweli kazi za Mungu. Tuwe nasi njia, kwa kusema ukweli ili tuweze kuleta matunda mema kwa wengine, turejeshe furaha na matumaini kwa waliokata tamaa, kwa waliosahaulika na kudharauliwa.

Mitume wakawa wakidumu katika Ekaristi, Neno na Sala
Mitume wakawa wakidumu katika Ekaristi, Neno na Sala   (@Vatican Media)

Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka 1 Pet 2:4-9. Katika somo la pili, Mtume Petro anamtaja Yesu kama “Jiwe lililo hai” na “Jiwe kuu la pembeni.” Kwa nini Mtume Petro anawaandika wakristo hawa maneno haya? Barua hii iliandikwa kwa Wakristo waliokuwa wanaishi kama wageni na wapitaji katika mikoa mbalimbali ya Dola ya Roma (kama Galatia, Kapadokia, na Bithinia). Walikuwa wakipitia mateso, kudhulumiwa, na kudharauliwa na jamii iliyowazunguka kwa sababu ya imani yao mpya kwa Kristo. Petro anatumia mfano wa “Jiwe lililokataliwa” ili kuwafariji; anawaambia kuwa kama Kristo alikataliwa na watu lakini akawa mshindi, wao nao wakikataliwa wasivunjike moyo. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka wao wamekuwa uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu na watu wa milki ya Mungu, nao wamekuwa warithi wa ahadi za Mungu. Fundisho la tano: Kwa njia ya ubatizo wetu, sisi tu wa thamani kubwa sana mbele za Mungu. Mtume Petro aliwaandikia wakristo hawa ambao wakati huu walikua wakipita mateso makubwa na kudharauliwa kwa sababu ya imani yao. Kwa kuwa kwao wakristo, walionekana wasio na thamani yoyote katikati ya jamii ile ya warumi. Mtume Petro anawakumbusha kuwa wao ni wenye thamani kubwa hata kama ulimwengu ukiwakataa. Ndugu mpendwa, Kristo leo anatupa moyo nasi sote kutambua daima thamani yetu kama wakristo, tuliokombolewa kwa damu ya thamani kubwa sana ya Kristo na tukafanywa kuwa warithi wa Ahadi za Kristo kwa njia ya ubatizo wetu. Kumbe nasi pia, Dunia inaweza kutukataa, kutupuuza, au kutuona hatufai (kama vile jiwe lilivyokataliwa na wajenzi). Huenda kuishi kwetu imani, kusema ukweli, na kuishuhudia imani yetu kwa matendo ikatugharimu pia wakati fulani. Lakini somo hili pia linatupa nafasi ya kutafakari, mimi thamani yangu ninaipata wapi? Hatuna haja ya kutafuta thamani yetu katika mambo ya ulimwengu huu. Thamani yetu ya kweli haipo katika vyeo, haipo katika fedha, haipo katika mali, haipo katika umaarufu, bali ipo kwa Kristo mwenyewe. Tunapoikataa thamani hii, tunaipoteza njia itupelekayo kwenye ukweli na uzima wa milele.

Waamini wanapaswa kuwa ni mawe hai katika ujenzi wa Kanisa
Waamini wanapaswa kuwa ni mawe hai katika ujenzi wa Kanisa   (@Vatican Media)

Fundisho la sita: Tunaalikwa kuwa mawe hai ndani ya mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Mtume Petro anatufundisha kuwa sisi tu mawe hai, na tumejengwa ili tuwe nyumba ya Roho kwa njia ya Yesu Kristo. Kuzitenda kazi za Kristo kama alivyotufundisha Kristo katika aya ya mwisho ya somo la Injili Takatifu ni kuwa mawe hai katika Hekalu la Mungu. Tunakuwaje mawe hai? Kwanza, Kwa njia ya vipaji na karama mbalimbali tulizojaliwa Roho Mtakatifu, sisi tunakuwa hayo mawe hai katika Kanisa la Mungu. Tunakuwa mawe hai katika familia zetu, tunakuwa mawe hai katika jumuiya zetu, tunakuwa mawe hai katika ulimwengu mzima. Licha ya tofauti zetu, bado tunajenga jengo moja. Neno la Kristo linatusaidia kuishi pamoja kwa umoja na upendo licha ya tofauti zetu. Tofauti zetu si chanzo cha uadui, wivu na chuki bali ni ishara na chanzo cha mshikamano na umoja ndani ya Kristo. Pili, Jiwe kwa kawaida halijijengi lenyewe; huwekwa mahali pake na mjenzi. Tunakuwa mawe hai tunapokubali kuwa Kristo ndiye anayetuongoza. Hii ina maana ya kuacha kutegemea akili zetu wenyewe na kuanza kufanya maamuzi kulingana na neno lake yeye aliye Njia, ukweli na uzima wetu.

Waamini wanakuwa hai wanaposhiriki: Ekaristi, Neno na Matendo ya Huruma
Waamini wanakuwa hai wanaposhiriki: Ekaristi, Neno na Matendo ya Huruma   (@Vatican Media)

Tatu, Tunakuwa hai tunaposhiriki Sakramenti (hasa Ekaristi na Kitubio) na kusoma Neno la Mungu. Haya ndiyo yanatupa damu na uhai wa kiroho ili tusiwe wakristo wa jina tu, bali wakristo wenye nguvu ya Mungu ndani yetu. Jiwe hai lina kazi; linabeba uzito wa jengo na kulinda waliomo ndani. Nne, Tunakuwa mawe hai tunapoanza kubeba mizigo ya wengine (kama tulivyoona kwa mashemasi katika somo la kwanza). Unapokuwa na huruma, unaposamehe, na unapotetea haki, unadhihirisha kuwa wewe ni jiwe lenye uhai, si jiwe baridi lisilo na hisia. Mwisho, Ili jiwe likae vizuri kwenye jengo, lazima lichongwe ili kutoa sehemu zenye ncha kali. Mungu anatumia changamoto za maisha, mapungufu yetu, na hata watu wanaotukwaza kutuchonga ili tuweze kutoshea vizuri katika mpango wake. Tunakuwa mawe hai tunapokubali mchakato huu wa kutakaswa tabia zetu. Hitimisho: Katika Dominika hii, Kristo anatualika kuacha mioyo yetu isifadhaike. Badala yake, tujijenge juu yake yeye aliye jiwe la msingi, tuyashike mafundisho yake ambayo ndiyo Ukweli, na tushiriki huduma ya upendo (Njia) ili hatimaye tushiriki makazi aliyotuandalia yaani uzima wa milele.

Tafakari D 5 Pasaka
01 Mei 2026, 15:08