Tafuta

Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, naye ni Mungu kweli pamoja na Baba na Mwana. Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, naye ni Mungu kweli pamoja na Baba na Mwana.  

Tafakari Dominika ya Sita Kipindi Cha Pasaka Mwaka A: Roho Mtakatifu Mfariji

Kulingana na Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, naye ni Mungu kweli pamoja na Baba na Mwana. Yeye si nguvu tu, bali ni Nafsi hai inayotoka kwa Baba na Mwana, inayowaongoza, kuwafariji, na kuwatakatifuza waamini, na anahusika kikamilifu katika kazi ya uumbaji na ukombozi (Rej KKK. Na. 683-686). Roho Mtakatifu tunaye ahidiwa leo, Yeye ni Mungu kamili, mwenye akili, hisia, na mapenzi, si nguvu isiyo na utu!

Na Padre Octavian O. Hinju, JUCo, - Morogoro, Tanzania.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Sita ya Mwaka A wa Pasaka. Baba Mtakatifu Leo XIV anaadhimisha Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, tarehe 8 Mei 2026 kwa kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, yaliyoko Jimbo kuu la Napoli, Kusini mwa Italia mahali: Pa upendo wa Mungu unaotoa joto kwa wale waliovunjika na kupondeka mioyo; ni mahali ambapo imani na upendo vina tamalaki. Ilikuwa ni tarehe 8 Mei 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV alipokabidhiwa dhamana ya: Kuongoza, Kufundisha na Kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Siku ya Sala maalum kwa ajili ya Bikira Maria wa Pompei. Kumbe, hija hii ya kitume inapania pamoja na mambo mengine, kuiweka huduma na utume wa kichungaji unaotekelezwa naye kama Khalifa wa Mtakatifu Petro chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Pompei na kwamba, katika maisha na utume wake, anaendelea kufuata nyayo za Papa Leo XIII, ambaye pamoja na mambo mengine, ni Kiongozi wa Kanisa aliyejibidiisha kuweka msingi wa Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu Rozari Takatifu pamoja na yeye mwenyewe kumtangaza Mwenyeheri Bartolo Longo, Mtume wa Rozari Takatifu kuwa ni Mtakatifu “Aleluya, Mkinipenda mtazishika amri zangu, nami nitamwomba Baba naye atawapa msaidizi mwingine ili akae nanyi milele; ndiye Roho wa ukweli atakayewaongoza katika kweli yote” (Yn. 14:15-17), huu ndio ujumbe wa Kristu kwetu sisi unao tufikia kwa njia ya masomo ya siku ya leo.  Ni maneno mepesi lakini yenye maana nzito; kwamba kupenda ni kulishika, kuliishi na kuliruhusu Neno la Mungu ligeuze mwenendo na matendo yetu. Na ni katika pendo hili aminifu, Mungu anakaa kwetu “naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli” (Yn.  1:14). Ni Furaha angavu inayo tualika kuingia katika kilindi cha Imani yetu: ndiyo Pasaka ya Bwana, Aleluya! Aleluya!

Roho Mtakatifu ni Bwana na Mleta Uzima
Roho Mtakatifu ni Bwana na Mleta Uzima   (@Vatican Media)

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 6 ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa. Ni Dominika inayo tupatia ukweli kwamba kipindi cha Pasaka kinaelekea ukingoni. Dominika ya tarehe 17 Mei 2026 tutaadhimisha Dominika ya Kupaa Bwana Mbinguni Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni na Dominika itakayofuata yaani tarehe 24 Mei 2026 ni Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume sanjari na Siku ya Waamini Walei Ulimwenguni wanaotumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wa maisha yao; Ni siku inayofunga wiki saba za Kipindi cha Pasaka. Hii ni Sherehe muhimu inayoadhimisha kushuka kwa Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwa Kanisa, ikifuatia siku 50 baada ya Pasaka, na pia inatumika kama Siku ya Waamini Walei. Ndio maana dhamira ya masomo ya dominika hii imebebwa na ahadi ya Yesu aliyowapa Mitume, Ahadi ya ujio wa Zawadi ya Roho Mtakatifu; Kristo Yesu anawaambia “Mkinipenda mtazishika amri zangu, nami nitamwomba Baba naye atawapa msaidizi mwingine ili akae nanyi milele; ndiye roho wa ukweli atakayewaongoza katika kweli yote. (Yoh. 14:15-17). Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Kulingana na Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, naye ni Mungu kweli pamoja na Baba na Mwana. Yeye si nguvu tu, bali ni Nafsi hai inayotoka kwa Baba na Mwana, inayowaongoza, kuwafariji, na kuwatakatifuza waamini, na anahusika kikamilifu katika kazi ya uumbaji na ukombozi (Rej KKK. Na. 683-686). Roho Mtakatifu tunaye ahidiwa leo, Yeye ni Mungu kamili, mwenye akili, hisia, na mapenzi, si nguvu isiyo na utu ndani mwake. Ndiye apataye utukufu. Ndio kusema kwamba anaabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana, kama tunavyo kiri katika ungamo la Imani yetu kuu katika kanuni ya Nicea-Konstantinopoli.

Roho Mtakatifu ni chachu ya umoja, upendo na mshikamano
Roho Mtakatifu ni chachu ya umoja, upendo na mshikamano   (@Vatican Media)

Huyo Roho Mtakatifu ndiye anaye tutakatifuza yaani Yeye hutuletea Zawadi ya kimungu kwa njia ya mapaji saba; Hekima, Akili, Shauuri, Nguvu, Elimu, Ibada na Uchaji wa Mungu (Isaya 11:2). Roho Mtakatifu ni Mwezeshaji; Huwawezesha waamini kuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi na kuwaunganisha na Kristo. Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani ya Kanisa na katika mioyo ya waamini kama mwalimu na mwongozo wa kweli. Nao Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano wanamtambua Roho Mtakatifu kama roho ya kanisa. Kwamba ndiye nguvu ifanyayo kazi, nguvu inayohuisha Kanisa, Roho Mtakatifu ndiye aliyoetumwa ili kulitakasa, kuliongoza katika ukweli, na kuliunganisha kanisa. Mtaguso unakazia nafasi ya Roho katika kusambaza karama za daraja na karama kwa waamini wote, akiliongoza Kanisa katika safari inayolenga utume na hija katika historia ya ukombozi.Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Somo la kwanza, ni kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume 8:5-8,14-27. Somo hili linatoa picha ya jinsi Imani ya kikristo ilivyo anza polepole kisha kukua ikaanza kuenea kote kuanzia Yerusalemu hata pande zote za ulimwengu. Imani ilienea kwa njia ya sadaka ya uhai na maisha na uthubutu wa watu wa Mungu. Mwito na mwaliko unao tuangukia sisi sote ni ule wa kuyasadaka maisha yetu kwa ajili ya Injili kama wamisionari kwa mfano wa Filipo katika somo letu la kwanza. Mwenyezi Mungu aliithibisha Imani kwa miujiza na maajabu mbalimbali yaliyo tendwa kupitia Mitume.

Roho Mtakatifu ni Mfariji na chanzo cha baraka na neema
Roho Mtakatifu ni Mfariji na chanzo cha baraka na neema   (@Vatican Media)

Katika Kristo Mfufuka, waamini wanaendelea hata sasa kuunganishwa kuwa kitu kimoja kwa sababu wote wamepata Zawadi moja yaani Roho Mtakatifu. Umisionari ni kazi msingi ya Kanisa linalo kua na kukomaa katika Kristu. Lakini waamini sharti watambue kuwa Roho Mtakatifu ndiye mfanyaji wa kwanza wa utume wa kanisa hivyo wote waliompokea amewapa kuwa wamisionari. Kuwa Mmisionari wa kweli ni kuwa Jasiri na Hodari kulitangaza neno la Mungu kama Nabii Isaya alivyopata kusema “Haya, tokeni katika Babeli, Kimbieni kutoka kwa Wakaldayo; Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya, Yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, BWANA amewakomboa watu wake, aleluya” (Is. 48:20) katika wimbo wetu wa mwanzo siku ya leo.Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Itakumbukwa kwamba kwa sakaramenti ya ubatizo tumeitwa na kutumwa, basi tumwombe huyo Roho ili akae nasi na kututakasa kwa ajili ya kazi hiyo ili tunapoianza safari ya kimisionari ndani mwetu na katika mazingira ya kanisa mahalia ikazae matunda kusudiwa kama anavyo Sali Mtakatifu Yosefu Allamano kuwa “utakatifu kwanza kisha umisionari”, na kwa enzi kuu tumpigie Mungu kelele za shangwe nchi yote (Zab. 66:1).

Roho Mtakatifu ni chanzo cha ujasiri katika kutangaza Injili
Roho Mtakatifu ni chanzo cha ujasiri katika kutangaza Injili   (@Vatican Media)

Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1 Pet.3:15-18). Ujumbe wa Somo hili ni kuhusu gharama ya ufuasi wetu kwake Kristu Mfufuka. Petro Mtume anaelezea bayana kweli ya Injili ya kwamba katika kumfuasa Kristu kuna magumu na changamoto zinazo kuja kutokana na ufuasi wetu, Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe (Lk. 9:23-25). Ni wazi kuwa katika kuifanya kazi ya Bwana tutakumbana na vita na madhulumu mengi ila tusikate tamaa wala kuogopa bali tuwe Jasiri katika Imani kwa ilivyokuwa kwa Mt. Ignasi wa Antiokia ambaye allitwa pia Theophirus katika madhulumu dhidi ya kanisa alisimama imara akimtegemea Mungu siku zote. Katika sura ya kwanza ya barua yake kwa Warumi aliandika hivi “kwa njia ya mateso na kifo dini kinacho nikabili mbele yangu, nina tumaini kuuona uso wako wewe Ee Mungu, na hata nimepewa zaidi ya nilivyoomba; kwa maana natumaini kuwasalimu kama mfungwa katika Kristo Yesu, ikiwa ni kweli mapenzi ya Mungu nihesabiwe kuwa nastahili kufika mwisho. Kwa maana mwanzo umepangwa vema, ikiwa nitapata neema ya kushika fungu langu bila kizuizi hata mwisho. Kwa maana ninaogopa upendo wako, usije kunidhuru. Maana ni rahisi kwako kutimiza upendalo; lakini ni vigumu kwangu kumfikia Mungu, ikiwa umeniacha.”

Roho Mtakatifu ni Mungu kweli pamoja na Baba na Mwana
Roho Mtakatifu ni Mungu kweli pamoja na Baba na Mwana   (@Vatican Media)

Hakuogopa kufa kwa vile alimwamini Yeye aliye mhubiri. Hata marafiki zake na waumini wa Roma waliokuwa na ushawishi walipo panga kumzuia asikiendee kifo dini aliwazuia ndipo akasali akisema hivi, “Kwa maana si nia yangu kuwapendeza ninyi, bali nimpendezavyo Mungu kama vile mnavyompendeza yeye. Kwa maana wala sitapata nafasi nyingine namna hii ya kumkaribia Mungu; wala nyinyi, ikiwa sasa mtanyamaza, hamtastahiki heshima ya kazi iliyo bora zaidi. Kwa maana kama ukinyamazia kunihusu, mimi nitakuwa wa Mungu; lakini mkiupenda mwili wangu, itanibidi tena kukimbia. Salini, basi, msitafute kunipa kibali chochote kikubwa zaidi ya kwamba nitolewe dhabihu kwa Mungu wakati madhabahu ingali imetayarishwa; ili mkiwa mmekusanywa pamoja katika upendo, mwimbieni Baba sifa kwa njia ya Kristo Yesu, ya kwamba Mungu ameniona mimi, kama Askofu wenu, kuwa nastahili kutumwa kutoka mashariki hadi magharibi. Ni vema kutoka katika ulimwengu kwenda kwa Mungu, ili nifufuke tena katika Yeye. Mimi ni nafaka ya mbingu na nisagwe na meno ya Wanyama wakali ili niweze kumpatia Kristu mkate safi wa mbinguni. Kama alivyo hubiri Mtume Petro, Mt. Ignasi wa Antiokia kwa mwangaza wa somo letu la pili ametuonyesha wazi kuwa mateso na masumbufu ya maisha ni njia ya kupata utukufu. Basi sisi nasi yatupasa kuvumilia magumu yote kwa ajili ya Imani katika Kristo aliyefufuka.Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Injili inayoongoza tafakari yetu siku ya leo ni kutoka kwa Mwinjili Yohana 14:15-21. Kristo Yesu leo anatuambia kwamba kuzishika amri zake ni Ishara ya kumpenda.

Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu
Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Mtume Paulo alipo yatafakari hayo alisema hivi “Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria (War. 13:10). Leo Kristu anapojiandaa kupaa Kwenda kwa Baba anatuandaa nasi kupokea Zawadi ya kimungu yaani Roho Mtakatifu awe kwetu ni msaidizi wa daima kwa wale wote wanao hubiri Injili yake kwa mataifa. Mtu akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutafanya makao yetu kwake (Yoh. 14:23), kumbe yeyote mwenye kupokea na kusadiki ukweli huo atapendwa na Mungu Baba, na kwa njia ya kifo na ufufuko wa Yesu, anapewa tuzo ya uzima wa milele.Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu tunayeahidiwa tunawezesha kuupata urafiki wa milele na Baba wa mbinguni. Huyu ni Roho wa ukweli, Yeye ndiye Roho wa uzima, chemchemi ya maji yanayobubujika kutoa uzima wa milele. Kwa njia yake Baba huwapa watu uzima, waliokufa kwa sababu ya dhambi, mpaka atakapoifufua miili yao inayokufa katika Kristo. Roho Mtakatifu anakaa ndani ya Kanisa na ndani ya mioyo ya waaminifu kama hekalu lake la kudumu. Anasali ndani yao na kushuhudia ndani yao juu ya kufanywa wana. Analiongoza Kanisa katika kweli yote na kulipatia umoja na ushirika na katika huduma za kitume. Analijalia karama mbalimbali za daraja na, huliongoza kwa njia yake ya upendo, na kulitajirisha kwa matunda yake. Kwa nguvu ya Injili analiwezesha Kanisa kukua na kulifanya upya daima, na kuliongoza katika muungano kamili na Bwana-arusi wake yaani Kristu. Kwa njia ya Roho kanisa humwambia Kristu Bwana-arusi wake ‘njoo.’ Kwa njia hii Kanisa linajidhihirisha kuwa ni watu ambao umoja wao una chimbuko lake katika umoja wa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tunapoendelea kuyatafakari hayo tusali tukisema “Roho mkuu mfariji mwema, mwenye kila kitu chema uje kutuangazia na imara kututia, tusikie mafundisho, tuyashike mapaka mwisho. Amina.

09 Mei 2026, 16:56