Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 5 ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A: Kristo Yesu Ni Njia, Ukweli Na Uzima

Ujumbe umekijika katika nafasi ya Mashemasi katika huduma za Kanisa, waamini kama mawe hai za kuujenga mwili wa Kristo yaani Kanisa, na Yesu Kristo mwenyewe akiwa ndiye Njia, Ukweli na Uzima. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake, aleluya” (Zab 98:1-2). Maajabu haya ni Ukombozi na kujaliwa maisha na uzima wa milele!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya Pasaka mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Ujumbe umekijika katika nafasi ya Mashemasi katika huduma za Kanisa, waamini kama mawe hai za kuujenga mwili wa Kristo yaani Kanisa, na Yesu Kristo mwenyewe akiwa ndiye Njia, Ukweli na Uzima. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake, aleluya” (Zab 98:1-2). Maajabu hayo ni ukombozi na kujaliwa uzima wa kweli kwa njia ya Yesu. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Tunakuomba utusikilize kwa wema sisi wanao, ili katika kumwamini Kristo tupate uhuru wa kweli na urithi wa milele.”

Kristo Yesu Ni Njia, Ukweli na Uzima
Kristo Yesu Ni Njia, Ukweli na Uzima   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 6:1-7). Ni simulizi la kuanzishwa na kuwekwa kwa huduma ya ushemasi katika Kanisa la mwanzo, kama sehemu ya kutatua changamotomo zilizojitokeza katika jumuiya ya kwanza ya wakristo. Hii ilitokea kwa kuwa kadiri idadi ya waamini ilivyozidi kuongezeka, changamoto zilijitokeza kama vile ubaguzi, hivyo kukawa na manung’uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma za mahitaji ya kila siku. Ndipo mitume walipoamua wachaguliwe watu wema, wenye kujaa Roho Mtakatifu na hekima, kuchukua jukumu la kuwahudumia wajitaji katika jumuiya, hasa maskini na wajane ili mitume waendelee kuhubiri Neno na kudumu katika sala zaidi. Huu ukawa mwanzo wa huduma ya kishemasi katika Kanisa kama Katekisimu ya Kanisa Katoliki inavyofafanua ikisema kuwa; Ushemasi ni daraja ya pekee na ya kudumu ya hierarkia katika kanisa. Sakramenti ya Daraja huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo, aliyejifanya shemasi, yaani mtumishi wa wote. Hivyo wao hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo. Katika kusimikwa kuwa shemasi mtu mwanaume huwekewa mikono na askofu peke yake, kuashiria muungano wa pekee alionao na Askofu, katika kazi zake za utumishi, “diakonia.” Mashemasi wanaimarishwe kwa kuwekewa mikono tangu enzi za mitume, ili waweze kutekeleza huduma ya kishemasi katika Kanisa, katika maisha ya kiliturujia na kichungaji, na katika kazi za kijamii na za mapendo. Hivyo ni kazi ya Shemasi kumtumikia Askofu na Padre katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi, kugawa Komunyo Takatifu, kusimamia ndoa na kuibariki, kutangaza Injili na kuhubiri, kuongoza mazishi na kujitoa kwa huduma mbalimbali za mapendo (KKK 1554-1571).

Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa
Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa   (@Vatican Media)

Ujumbe kwetu sisi kwa nyakati zetu, ni kuwa ili tuweze kutimiza nyajibu zetu vizuri, ndani ya Kanisa, ushirikaino ni wa lazima. Sio vizuri na haipendezi mtu mmoja kulimbikiziwa mamlaka na majukumu. Hivyo ili ujumbe wa Injili usonge mbele na ulete manufaa kwa wote katika jumuyiya, lazima wawepo wanaojikita katika sala na kuhubiri na wengine katika kusimamia na kutoa huduma zingine za kila siku kwa wahitaji. Ni kwa kufanya hivyo sifa na utukufu wa Mungu utadhihirika kwa watu wote kama zaburi ya wimbo wa katikati inavyosema; “Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe. Mpigieni Bwana vigelegele enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Mshukuruni Bwana kwa kinubi, kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu. Huzipenda haki na hukumu, nchi imejaa fadhili za Bwana. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa” (Zab. 33:22, 1-2, 4-5, 18-19).

Mitume wakadumu katika Neno na Sala
Mitume wakadumu katika Neno na Sala   (@Vatican Media)

Somo la pili ni kutoka Katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 2:4-9). Ujumbe ni kuwa Yesu Kristo ni jiwe hai, ni mzima, hafi tena. Licha ya kuwa alikataliwa na waashi, watu walio wake, Wayahudi hata wakamtoa asulubiwe na kuuwawa kifo cha msalabani. Mbele za Mungu Yeye ni mteule wake mwenye heshima kuu. Hivyo wote wanaomwamini na kumfuata nao wanafanywa kuwa mawe hai ya kuujenga mwili wake yaani Kanisa, wanashiriki ukuhani wake mtakatifu, ili watoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Tena hawatatahayarika kamwe. Lakini wale wanaokataa kumsadiki wataangamizwa milele katika hukumu ya mwisho. Kwa Ubatizo sisi nasi tumekuwa sehemu ya uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu. Hivyo tunapaswa kuzitangaza fadhili zake yeye aliyetuita tutoke gizani kuingia katika nuru yake ya ajabu, ili tuje kushirikishwa uzima wake milele mbinguni.

Ni Muhimu kugawana kazi na majukumu kadiri ya karama za Roho Mtakatifu
Ni Muhimu kugawana kazi na majukumu kadiri ya karama za Roho Mtakatifu   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mwinjili Yohane (Yn. 14:1-12). Ni wosia wa Yesu alioutoa siku ya Alhamisi Kuu katika karamu ya mwisho. Kristo Yesu baada ya kuwapa wanafunzi wake fundisho kuu la kutumikiana kwa upendo na kuwaambia habari za kuondoka kwake na yatakayompata baada ya mmoja wao kumsaliti, na utabiri wake kuwa Petro atamkana, wanafunzi wake walijawa na wasiwasi na mashaka makubwa hata pengine kukata tamaa. Ni katika mazingira haya Yesu anawafariji akiwaambia; “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi”. Kisha anawapa matumaini akiwaambia; “Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia, maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia.” Mtume Tomaso anaweka wazi mashaka yake sio tu kutokujua njia bali pia anakoenda Yesu. Hivyo anamuuliza; “Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?” Ndipo Yesu akatamka huu ufunuo mkuu wa nyakati zote; “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Hii ndiyo habari njema na ya furaha inayotupa amani na utulivu katika mioyo yetu na pia inatupa nguvu na ujasiri wa kuendelea kukabiliana na changamoto na magumu katika kumfuata Kristo aliye Njia, Ukweli na Uzima.

Kwa Hakika Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima!
Kwa Hakika Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima!   (@Vatican Media)

Filipo hakuweza kuelewa ukuu wa huu ufunuo hivyo alitoa ombi akisema; “Bwana tuonyeshe Baba nasi yatutosha." Yesu akaweka wazi uhusiano uliopo kati yake Yeye na Mungu Baba akisema; “Aliyeniona mimi amemwona Baba.” Yesu, Mungu mwana yumo ndani ya Baba na Baba yu ndani yake. Huu ni ufunuo wa uhusiano uliopo kati ya Mungu Baba na Mungu Mwana. Kisha akahitimisha kwa kusema; “Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.”Ni ujumbe wa matumaini na wenye kututia nguvu na kutupa moyo. Tukijikabidhi kwake Kristo kwa imani tutaweza kufanya mambo makubwa zaidi kwani daima Mungu atasikiliza sala zetu na kutekeleza yale tunayoomba kwa imani katika kweli na haki. Ndiyo maana Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 2614, inasisitiza kusema; “Yesu anapowaaminisha wanafunzi wake fumbo la sala kwa Baba, anawafunulia kile ambacho sala yao na yetu lazima kiwe, baada ya kuwa amerudi kwa Baba katika ubinadamu wake uliotukuka. Kilicho kipya sasa ni kuomba kwa jina lake. Imani ndani yake inawaingiza wafuasi kumjua Baba, kwa sababu Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Imani huzaa matunda yake katika mapendo: kushika neno lake, amri zake, kukaa naye ndani ya Baba, ambaye ndani yake anatupenda hata kukaa ndani yetu. Katika agano hili jipya, hakika ya kusikilizwa maombi yetu, ina msingi juu ya sala ya Yesu.”

Kristo Yesu akawaambia niendako mwaijua njia!
Kristo Yesu akawaambia niendako mwaijua njia!   (@Vatican Media)

Basi tujitahidi kuyaweka yote chini ya maongozi ya Kristo na kujiaminisha kwake, tukijua kuwa tutayashinda yote na kuingia katika uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu, umetushirikisha umungu wako mkuu katika kuishiriki sadaka hii takatifu. Tunakuomba utujalie tuufuate kwa mwenendo mwema ule ukweli wako kama tunavyoujua”. Na baada ya Komunyo anahitimisha akisali; “Ee Bwana, tunakuomba uwe na sisi taifa lako. Na kama ulivyotujalia mafumbo haya ya mbinguni, utufikishe kwenye uzima, utuondoe katika maisha ya zamani na kutuweka katika maisha mapya”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari Dominika 5 ya Mwaka A
01 Mei 2026, 08:34