Tafuta

Yerusalemu ya Zamani. Yerusalemu ya Zamani. 

Mtawa ashambuliwa Yerusalemu,mshukiwa wa shambulio akamatwa

Mtawa,mtafiti katika Shule ya Kifaransa ya Utafiti wa Biblia na Akiolojia,alishambuliwa katika eneo la Mlima Sayuni.Tukio hilo,lililolaaniwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Israeli na ambalo mwanamume wa miaka 36 alikamatwa,ni sehemu ya muktadha wa vurugu unaotia wasiwasi.

Vatican News

Padre Olivier Poquillon, mkurugenzi wa Shule ya Kifaransa ya Utafiti wa Biblia na Akiolojia huko Yerusalemu, alitoa maoni yake  Aprili 30  kwenye jarida la X kuhusu shambulio la mtawa lililotokea Aprili 28, 2026,  karibu na eneo la Kaburi la Mfalme Daudi kwenye Mlima Sayuni. Tendo hilo aliliita kuwa Ni “pigo la chuki, changamoto ya kawaida.” Mtawa huyo wa Kifaransa mwenye umri wa miaka 48, mtafiti katika Shule ya Kifaransa ya Utafiti wa Biblia na Akiolojia huko Yerusalemu, alifukuzwa barabarani na mtu aliyemsukuma chini kisha akampiga teke. Video iliyotolewa na Polisi pia inaonesha michubuko upande wa kulia wa uso wa mtawa huyo.

Ukatili dhidi ya mapadre

Polisi wa Israeli walitangaza Aprili 29, kukamatwa kwa mwanamume mwenye umri wa miaka 36 anayeshukiwa kumshambulia mtawa huyo, na kuongeza kwamba wanachukulia "kwa uzito sana" kitendo chochote cha vurugu "kinachochochewa na nia inayowezekana ya ubaguzi wa rangi na kuelekezwa dhidi ya mapadre." Akisubiri upelelezi wa mahakama katika shambulio hilo, Padre Poquillon aliwashukuru "watu waliokwenda kuwaokoa wakati wa shambulio hilo, wanadiplomasia, wasomi, na wote waliotoa msaada."

Kulinda Uhuru wa Kuabudu

Katika siku za hivi karibuni, mkurugenzi wa Shule ya Kifaransa ya Utafiti wa Biblia na Akiolojia alilaani "shambulio lisilo na maana" dhidi ya mtawa huyo, "akilaani vikali" kilichotokea. Wizara ya Mambo ya Nje ya Israeli, katika chapisho kwenye X, ililiita "kitendo cha aibu," ikihakikisha kwamba Israeli bado imejitolea "kulinda uhuru wa dini na uhuru wa kuabudu kwa imani zote." Mtu aliyekamatwa kwa shambulio hilo "anaendelea kuzuiliwa," Wizara ya Israeli ilisema, ikisisitiza "sera thabiti dhidi ya vurugu na azimio la kuwashtaki haraka wahusika." "Vurugu dhidi ya watu wasio na hatia, na hasa dhidi ya wajumbe wa Jumuiya za kitawa, hazina nafasi katika jamii yetu," taarifa hiyo ilisisitiza.

Uadui unaongezeka

Kitivo cha Kibinadamu cha Chuo Kikuu cha Kiebrania cha Yerusalemu pia kilionesha "mshtuko na lawama kubwa" kuhusu shambulio hilo katika taarifa. "Hili si tukio la pekee, bali ni sehemu ya mtindo wa kutia wasiwasi wa kuongezeka kwa uadui dhidi ya Jumuiya  ya Kikristo na alama zake," Kitivo kilisema. Mwanzoni mwa mwezi Aprili, jeshi la Israeli liliwaondoa wanajeshi wawili kazini baada ya kuharibu sanamu ya Yesu katika kijiji cha Debl, ​​kusini mwa Lebanon, kitendo kilichosababisha kulaaniwa sana.

MTAWA KUSHAMBULIWA YERUSALEMU

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

01 Mei 2026, 11:48