Tafuta

2026.05.07 Askofu wa Jimbo Springfield, Illinois akiwa karibu na Picha ya Padre Augustine Tolton. 2026.05.07 Askofu wa Jimbo Springfield, Illinois akiwa karibu na Picha ya Padre Augustine Tolton.  (©Courtesy of the Diocese of Springfield, Illinois)

Madhabahu kwa heshima ya Mtumishi wa Mungu Padre Tolton

Jimbo la Springfield,Illinois,Marekani,lilitangaza mipango ya kujenga madhabahu kwa ajili ya Mtumishi wa Mungu Padre Augustine Tolton,ambaye historia yake ya kushinda ubaguzi wa rangi na migawanyiko katika wakati wake inaendelea kuwa chanzo cha msukumo wa kukuza amani na umoja.Mpango huo utarejesha Kanisa la kihistoria la Mtakatifu Boniface huko Quincy,ambapo Padre Tolton aliadhimisha Misa yake ya kwanza baada ya kuwekwa Daraja la Upadre 1886.

Sr. Christine Masivo, CPS  na Angella Rwezaula– Vatican.

Kanisa Katoliki la Springfield, Illinois nchini Marekani linajiandaa kumheshimu mmoja wa watu wake maalum sana kwa kujenga madhabahu ya kitaifa kwa ajili ya Mtumishi wa Mungu Padre Augustine Tolton, Padre wa kwanza Mweusi anayetambuliwa kwa umma nchini Marekani kwa kushinda mivutano ya rangi na migawanyiko iliyoikumba nchi hiyo katika karne ya 19 na kuishi maisha kamili huku akihudumia Kanisa na waamini wake, na licha ya ubaguzi alipendwa na wengi. Sasa historia ya maisha yake na ushuhuda wake unatarajiwa kuwafikia watu wengi zaidi kwa sababu Jimbo la Springfield, Illinois, mahali alipokulia na kuhudumu, tarehe 29 Aprili 2026 lilitangazwa kwamba wanapanga kujenga Madhabahu kwa heshima yake katika Kanisa la Mtakatifu Boniface, katika jiji la Quincy.

Madhabahu ya Padre Augustine Tolton
Madhabahu ya Padre Augustine Tolton   (©Courtesy of the Diocese of Springfield, Illinois)

Madhabahu ya kihistoria kwa mtu wa kihistoria

Kanisa hilo lina umuhimu mkubwa wa kihistoria kwa sababu hapo ndipo Padre Tolton aliadhimisha  Misa yake ya kwanza nchini Marekani baada ya kupewa Daraja la Upadre mjini  Roma mnamo 1886. Askofu Thomas J. Paprocki alielezea mpango huo kama wenye malengo makubwa na muhimu. Kanisa hilo, ambalo limebaki bila kutumika tangu 2020, linahitaji matengenezo makubwa kutokana na uharibifu wa ukungu na miaka bila kupasha joto au uingizaji hewa mzuri. Gharama za ukarabati zinatarajiwa kuzidi dola milioni 5, huku fedha za ziada zikihitajika kuunda uzoefu mpana wa hija unaohusiana na maisha ya Padre Tolton huko Quincy.

Mjue Padre Augustine Tolton
Mjue Padre Augustine Tolton   (©Courtesy of the Diocese of Springfield, Illinois)

Kutoka Utumwani hadi upadre

Historia Padre Tolton ni ya uvumilivu, imani na ujasiri wa ajabu. Alizaliwa utumwani huko Brush Creek, Missouri, mnamo 1854, alitoroka utumwani akiwa mtoto wakati mama yake, Martha Jane Tolton, alipokimbia kuvuka Mto Mississippi na watoto wake wakati wa Vita vya wenyewe kwa wenyewe kutafuta usalama nyuma ya Muungano. Hatimaye familia hiyo iliishi Quincy, ambapo kijana Augustine Tolton alikutana na ubaguzi lakini akaendelea kuvumilia na kutiwa moyo. Katika Shule ya Mtakatifu  Boniface, wazazi weupe walipinga uwepo wake, na kumlazimisha kuhama baada ya mwezi mmoja tu. Hata hivyo, Mapadre na Watawa katika Parokia ya Mtakatifu  Petro  iliyokuwa karibu walitambua imani yake ya kina na kuhimiza ndoto yake ya kuwa Padre.

Siku ya Uwasilishaji wa Mpango wa Madhabahu ya Padre Tolton
Siku ya Uwasilishaji wa Mpango wa Madhabahu ya Padre Tolton   (©Courtesy of the Diocese of Springfield, Illinois)

Pia alikabiliwa na mgawanyiko wa kidini, kwani alipokuwa na umri wa miaka 24 alifungua shule ya kwanza ya watoto Weusi huko Quincy lakini alikabiliwa na upinzani kutoka kwa Waprotestanti Waafrika-Wamarekani ambao walikataa kuwapeleka watoto wao huko kwa kuwa alikuwa Mkatoliki. Wakati ambapo hapakuwapo na  seminari ya Marekani iliyokubali vijana weusi kuwa mapadre, washauri wa Kanisa walipanga Tolton asomee Roma. Huko, alifanikiwa kitaaluma na kiroho na akawekwa daraja la Upadre mwaka 1886 katika Basilika ya Mtakatifu Yohane Lateran. Ingawa alikuwa na matumaini ya kuhudumu kama mmisionari barani Afrika, mamlaka ya Kanisa badala yake walimrudisha nchini Marekani kuhudumu huko  Quincy.

Huduma katikati ya mivutano

Padre Tolton alijulikana haraka kama Padre mwenye kipaji na mchungaji mwenye huruma ambaye aliwavutia Wakatoliki weusi na weupe. Akihudumu katika Kanisa la Mtakatifu Yoseph, Parokia ya utume  iliyounganishwa na Mtakatifu Boniface, alifanya kazi bila kuchoka kuwaunganisha waamini licha ya mgawanyiko wa rangi wa wakati wake.Padre Steven Arisman, Mwenyekiti wa Kamati ya Madhabahu ya Padre Augustine Tolton na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Francis Solanus huko Quincy, katika mahojiano na Vatican News, alisema kuwa Padre Augustine Tolton “alishinda migawanyiko yote ya wakati wake na alifanya hivyo kwa amani, matumaini na upendo.” Zaidi ya hayo, Mtumishi wa Mungu Tolton "hakupata  ugumu mkubwa wa mgawanyiko wa rangi tu, bali pia wivu wa kipadre, kwa sababu ya mafanikio yake" Padre Arisman alielezea. "Alipendwa sana kama padre na mchungaji katika eneo hili. Kulikuwa na mapadre wengi ambao hawakupenda sana ukweli kwamba alipendwa zaidi yao."

Madhabahu mpya ya Padre Augustine Tolton
Madhabahu mpya ya Padre Augustine Tolton   (©Courtesy of the Diocese of Springfield, Illinois)

Katika suala hili, Padre Tolton alikabiliwa na unyanyasaji na ubaguzi kutoka kwa mapadre wa Ujerumani kutoka parokia ya karibu. Akitafuta amani na fursa pana za huduma, baadaye alihamia Chicago, ambapo aliwahudumia Wakatoliki Weusi katika Parokia ya Mtakatifu Monica upande wa Kusini mwa jiji.  "Alishughulikia kila aina ya mgawanyiko na kila aina ya ugumu katika maisha yake kwa amani, utulivu, na uvumilivu kama huo. Hilo linatufundisha jinsi ya kumtazama Kristo kama msingi wa kile tunachofanya na sisi ni nani," Padre Arisman alisema. Kwa Padre Arisman, tunachojifunza kutokana na historia ya Padre Tolton leo hii ni “uvumilivu wake katika kukabiliana na majaribu makubwa, uvumilivu katika shida kubwa, na uvumilivu katika tumaini hilo kwamba Yesu ndiye anayetuokoa.” Historia yake ni “umoja na Kristo, ambaye ni Wokovu wetu, lakini pia  jinsi ya kuishi kwa amani na kila mmoja, jinsi ya kutafuta njia ya kushinda migawanyiko na mivutano ili tuweze kupata msingi wa pamoja.” Alifariki huko Chicago mwaka 1897 akiwa na umri wa miaka 43 tu  baada ya kupatwa na kiharusi cha joto, lakini ushuhuda wake kwa imani na hadhi uliacha matokeo ya  kudumu kwa Kanisa la Marekani.

Sababu za mchakato wa Utakatifu wake

Leo hii,  kujitolea kwa Padre Tolton kunaendelea kukua kwa kasi. Historia na ushuhuda wa Padre Tolton unaendelea kuwaunganisha watu. Askofu Joseph N. Perry, Msaidizi  Mchakato wa  kuwa Mtumishi wa Mungu, alifichua kwamba miujiza 40 inayowezekana inayohusishwa na maombezi ya Padre Tolton tayari imechunguzwa. Katika hafla ya uzinduzi wa madhabahu huko Quincy kulikuwa na watu kutoka matabaka yote ya maisha, wakiwemo wanasiasa wa eneo hilo na wawakilishi wa Kiprotestanti na Wakatoliki. Viongozi wa Kanisa wanaamini kwamba madhabahu hayo itaongeza ufahamu wa maisha yake na hali yake ya kiroho. Mipango ni pamoja na bustani za kukakaa na kufanya tafakari, maeneo ya ukumbusho na maeneo ya kielimu yanayofuatilia safari ya maisha ya Padre Tolton kutoka utumwa hadi upadre wake. Kwa Wakatoliki wengi, madhabahu huwakilisha zaidi ya mpango wa urejesho. Ni heshima kwa mtu aliyeshinda kukataliwa, ubaguzi wa rangi na ugumu kwa imani usioyumba na ambaye njia yake kuelekea utakatifu inaendelea kuhamasisha kizazi kipya.

Padre Augustine Tolton
Padre Augustine Tolton

Askofu Thomas John Paprocki wa Jimbo la Springfield huko Illinois alibariki mbamba la ukumbusho wakati wa hafla hiyo. Askofu Joseph Perry, Askofu msaidizi mstaafu wa Chicago, na mwakilishi wa jimbo na Mchakato wa kutangazwa utakatifu wa  Padre Tolton, pia alikuwepo. Padre Arisman alisisitiza jinsi ambavyo Padre Tolton "anavyotufundisha kweli kuungana" na akabainisha kuwa hata kamati ya kujenga madhabahu ni tofauti sana. "Tuna watu wa asili nyingine za imani. Tuna watu ambao si wa imani yoyote, lakini wanapenda historia ya Tolton."

Mfahamu Padre “Gus”

Kwa Padre Arisman, ujenzi wa Madhabahu ni fursa kwa historia ya Mtumishi wa Mungu Tolton kwenda zaidi ya Quincy na Marekani na kuwatia moyo watu wengi zaidi kumjua na kumgeukia katika maombi. “Jambo moja ninalowaambia watu wakati wote ni kwamba, mfahamu Padre “Gus” mwema, kama alivyoitwa. Utakuwa na rafiki mzuri kwa maisha yako yote,” alisema. “Ni rafiki mzuri na mtu wa siri, mtu ambaye unaweza kumgeukia kwa maombezi, mwongozo na msukumo katika historia yake.”

Madhabahu ya Mtumishi wa Mungu Padre Tolton
Madhabahu ya Mtumishi wa Mungu Padre Tolton   (©Courtesy of the Diocese of Springfield, Illinois)

Sala kwa maombezi ya Padre Augustine Tolton

Ee Mungu, tunakushukuru kwa ajili ya mtumishi na kuhani wako, Padre Augustus Tolton, aliyefanya kazi kati yetu katika nyakati za utata, nyakati ambazo zilikuwa nzuri na za kinzani. Huduma yake ilisaidia kuweka msingi wa kukuza imani ya Kikatoliki katika wakati wetu. Tunasimama katika kivuli cha huduma yake. Maisha yake yaendelee kututia moyo na kutujaza ujasiri na matumaini ambayo yaunde uinjilishaji mpya kwa ajili ya Kanisa tunalolipenda. Baba wa Mbinguni, huduma ya mateso ya Padre Tolton inaakisi huzuni zetu; tunaziona kupitia mateso na kifo cha Mwanao. Kama ni mapenzi yako, Ee Mungu, mtukuze mtumishi wako, Padre Tolton, kwa kutoa neema ninayoomba sasa kupitia maombezi yake…(taja ombi lako) ili wote wajue wema wa kuhani huyu ambaye kumbukumbu yake ni kubwa katika Kanisa alilolipenda. Kamilisha ulichoanza ndani yetu ili tuweze kufanya kazi kwa ajili ya utimilifu wa ufalme wako. Si kwa ajili ya utukufu wetu, bali utukufu wako Ee Mungu, kupitia Yesu Kristo, Mwanao na Bwana wetu; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, wewe ni Mungu wetu, unayeishi na kutawala daima na Milele. Amina.

Askofu akionesha Picha ya Padre Augustine Tolton Mtumishi wa Mungu
Askofu akionesha Picha ya Padre Augustine Tolton Mtumishi wa Mungu   (©Courtesy of Father Arisman)

Hati miliki

2010 Askofu Joseph N. Perry
Francis Kardinali  George, OMI
Jimbo Kuu Chicago.

Ili kuripoti neema zozote za kiroho au kimwili zinazopatikana kupitia maombi kwa jina la Padre Tolton,tafadhali andika: 

Ofisi ya Kardinali, Askofu Mkuu Chicago
835 North Rush Street
Chicago, Illinois 60611

Ili kuomba kadi ya maombi ya kutangazwa Mtakatifu kwa Padre Augustus Tolton, piga simu au andika:

AskofunJoseph N. Perry
Phone: 312.534.8376
3525 South Lake Park Avenue
Chicago, Illinois 60653

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

07 Mei 2026, 11:00