Tafuta

Vita vinavyoendelea  kuharibu miundo mbinu Nchi za Mashariki ya kati Vita vinavyoendelea kuharibu miundo mbinu Nchi za Mashariki ya kati  (ANSA)

Lebanon:Maaskofu wa Melkite walalamikia uharibifu wa majengo

Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Kimelkite nchini Lebanon walielezea wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti kwamba Israeli inabomoa majengo ya kiraia na ya Kitawa katika sehemu za kusini mwa Lebanon chini ya udhibiti wake.Baraza la Maaskofu Katoliki la Kigiriki la Kimelkite nchini Lebanon limehimiza serikali ya Lebanon na Umoja wa Mataifa kulinda mali za raia na taasisi za kitawa kusini mwa Lebanon,likitaja kijiji cha Yaroun,ambapo,wanajeshi wa Israel waliharibu nyumba ya watawa.

Na Sr. Christine Masivo CPS -Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki la Kigiriki la Kimelkite nchini Lebanon lililaani vikali taarifa za kuendelea kwa ubomoaji wa majengo ya kiraia na kitawa katika maeneo ya kusini mwa Lebanon yaliyo chini ya udhibiti wa Israeli. Maaskofu hao walieleza kuwa matukio hayo yaliacha “jeraha kubwa katika dhamiri ya kitaifa na kibinadamu,” hasa kwa kuwa yalifanyika baada ya wakazi wa maeneo hayo kuhamishwa kutokana na hali ya vita. Kwa mujibu wa shirika la habari Katoliki la Kitaifa (NCR)lilieleza kwamba kijiji cha Yaroun kimetajwa kuwa moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi. Kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo, wanajeshi wa Israeli walibomoa nyumba ya watawa ya Wamelkite pamoja na majengo mengine ya kiraia.

Israeli yajitetea dhidi ya madai

Jeshi la Israel lilikanusha kulenga kwa makusudi taasisi za Kitawa. Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi tarehe 2 Mei 2026, jeshi hilo lilisema kuwa wakati wa operesheni za kuharibu miundombinu ya Hezbollah katika kijiji cha Yaroun, jengo moja liliharibiwa bila wao kutambua mara moja kuwa lilikuwa linahusiana na Kanisa. Jeshi hilo liliongeza kuwa lilichukua hatua kuzuia uharibifu zaidi mara baada ya kutambua uhusiano wa jengo hilo na taasisi ya kidini. Aidha, lilidai kuwa eneo hilo lilikuwa limetumiwa zamani na wapiganaji wa Hezbollah kurusha makombora kuelekea Israel. Hata hivyo, viongozi wa Jumuiya ya Kikristo katika Yaroun wamepinga maelezo hayo. Adib Ajaka, mmoja wa viongozi wa Jumuiya hiyo, alisema picha zilizotolewa na jeshi la Israel zilikuwa za jengo tofauti lililokuwa karibu na nyumba ya watawa, na kusisistiza kuwa nyumba ya watawa yenyewe ilibomolewa kabisa.

Wito kulinda maeneo ya kidini na raia

Maaskofu wa Melkite waliitaka serikali ya Lebanon pamoja na Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa mali za raia na taasisi za kidini zinapewa ulinzi wa haraka. Walisisitiza kuwa maeneo ya ibada na taasisi za huduma za kijamii havipaswi kugeuzwa maeneo ya mapigano au kuharibiwa wakati wa vita. Shirika la Kikatoliki la Ufaransa, L’Oeuvre d’Orient, pia lililaani tukio hilo, likilitaja kama “kitendo cha makusudi cha kuharibu mahali pa ibada” pamoja na juhudi za kuzuia wakazi kurejea katika makazi yao kusini mwa Lebanon.

Mvutano wa kisiasa na vita

Mvutano kati ya Israel na Hezbollah umeendelea kuathiri maisha ya maelfu ya wananchi wa Lebanon. Israel ilichukua udhibiti wa baadhi ya maeneo ya mpakani kusini mwa Lebanon katika vita vya hivi karibuni dhidi ya kundi hilo linaloungwa mkono na Iran. Ingawa makubaliano ya kusitisha mapigano ya siku 10 yalitangazwa Aprili 17 mjini Washington na baadaye kuongezwa kwa majuma matatu, mashambulizi na hali ya taharuki bado vinaendelea. Wizara ya Afya ya Lebanon imesema kuwa watu 2,696 wameuawa huku wengine 8,264 wakijeruhiwa tangu kuanza kwa vita hivyo. Wakati huo huo, mjadala wa kisiasa umeibuka kuhusu uwezekano wa mkutano kati ya Rais wa Lebanon Joseph Aoun na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu nchini Marekani. Pendekezo hilo limezua upinzani mkubwa kutoka kwa Hezbollah na washirika wake ambao wanapinga mazungumzo ya moja kwa moja na Israel.

Kanisa kusisitiza utu na amani

Katika mazingira haya ya vita na migawanyiko, Kanisa la Melkite linaendelea kutoa sauti ya kutetea utu wa binadamu, haki za raia na heshima ya maeneo ya kidini. Maaskofu hao wameonya kuwa kuharibiwa kwa nyumba, makanisa na taasisi za huduma ni pigo kubwa kwa matumaini ya amani na maridhiano. Kwa waamini wengi wa Lebanon, ujumbe wa Kanisa unabaki kuwa mwaliko wa kulinda maisha, kuheshimu utu wa kila mtu na kutafuta njia za mazungumzo badala ya uharibifu na vita.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

07 Mei 2026, 11:40