Kenya,Nairobi-AfriConnect 2026:”Kubaki Msalesian katika Ulimwengu wa Sauti Nyingi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Wakati muhimu wa ushirika wa bara, ambapo sauti, tamaduni na uzoefu viliungana ili kufufua kujitolea kuwasiliana kwa uhalisi, ubunifu, na uaminifu kwa karama ya Shirika la Don Bosco, ndiyo ilikuwa msingi Mkuu wa Mkutano wa “AfriConnect 2026,” wa Kanda ya Mawasiliano ya Kijamii ya Shirika la Mtakatifu Don Bosco, wajulikanao Wasalesian uliofanyika kuanzia tarehe 1-3 Mei 2026, kwa kuwaona pamoja wawakilishi wa Kanda mbili za Afrika, washirika, na wakurugenzi wa mawasiliano, wa Shirika hilo ambao “walikusanyika kwa roho ya ushirika ili kubadilishana uzoefu na kuimarisha mtandao wa mawasiliano ya kijamii wa Shirika la Kisalesian, barani Afrika huko Nairobi nchini Kenya.”
"Mawasiliano ni utambulisho wetu"
Haya yote yamo katika taarifa kutoka Ukurasa wa Shirika la Mawasiliano ya Kisalesian (ANS) kwa kubainisha kuwa katika Mkutano huo: “Vipindi vikuu vya mkutano vilikuwa: "Mawasiliano ni Utambulisho Wetu: Kubaki Msalesian katika Ulimwengu wa Sauti Nyingi," "Kufafanua Upya Utambulisho na Jukumu la Mawasiliano ya Kijamii," na "Usimamizi wa Migogoro na Mawasiliano: Njia ya Msalesian." Mada hizi zote ziliwawezesha washiriki kupata maarifa zaidi kuhusu dhamira inayobadilika ya mawasiliano ya Msalesian leo hii. Aidha katika ripoti yao ya mwisho wa Mkutano huo, inaeleza kwamba: “Katika kukamilisha michango hii, Dk. Nicholas Oduor, Profesa na mtaalamu wa vyombo vya habari, aliongoza kikao chenye nguvu kuhusu: "Fursa na Changamoto za Uinjilishaji wa Kidijitali," akiwaalika washiriki, kushiriki kwa kina na nafasi za kidijitali kama nafasi muhimu kwa dhamira ya leo hii.”
"Muda wa maombi,malezi na mazungumzo"
Pamoja na hayo, pia kulikuwa na “muda uliopangwa kwa ajili ya maombi, malezi, na mazungumzo katika kila siku ya mkutano huo.” Kuanzia hafla ya ufunguzi na mawasilisho ya mada hadi majadiliano ya kikundi, mawasilisho ya wajumbe, na vikao vya ushirikiano, programu hiyo ilikuza ushiriki hai na ubadilishanaji wenye maana.” Kwa njia hiyo ratiba ya siku tatu hizo hata hivyo zilisisitiza kwamba: “Kivutio cha siku ya pili kilikuwa ni ziara ya alasiri katika Jumuiya mbalimbali za Kisalesian zilizopo jijini Nairobi na hivyo, “Wajumbe walitembelea: “Bosco Boys Kuwinda,” “Bosco Boys Langata,” mahali ambapo Padre Fidel Orendain alibariki studio mpya iliyoanzishwa kwa ajili ya "AfriConnect"—Don Bosco Utume, “Don Bosco Boys Town,” na hatimaye “Don Bosco Youth Education Services.”
"Mawasiliano si chombo tu ni usemi wa utume..."
Kwa msisitizo zaidi uzoefu huo uliwapa washiriki wa mkutano halisi na kazi za Kisalesian za ndani na kuimarisha shukrani zao kwa utume katika uwanja huo. Mkutano ulimalizika kwa uundaji wa maazimio na hatua za kufanya kwa pamoja kwa siku zijazo, “ukithibitisha tena kujitolea kwa wawasilianaji wa Kisalesian kufanya kazi kwa umoja, taaluma, na ubunifu wa uinjilishaji.” Zaidi ya mkutano uliopangwa, “tukio hilo likawa uzoefu halisi wa bara la ushirika, likisisitiza kwamba mawasiliano si chombo tu, bali ni usemi muhimu wa utume wa kisalesian miongoni mwa vijana.” Mkutano huo jijini Nairobi “uliwakilisha ishara kali ya matumaini, ushirikiano, na kujitolea upya katika kujenga uwepo wa kisalesian uliounganishwa zaidi na wenye mwelekeo wa dhamira barani kote Afrika.”
Washiriki wa Mkutano
Washiriki wa Mkutano huo walijumuisha Padre Jacques Nagalo (AOS), Padre Oscar Medah (AON), Laurent Minani (AGL), Clarence Watts (AFM), Padre Philemon Chacha (TZA), Samuel Job (ANN), Padre Andrew Reut (ZMB), Padre Sebastian Koladiyil (AFE), Padre Guy Mulaisa (AFC), Padre Guy André Abena (ATE), Shemasi Kibrom Hagos Awala (AET), na Padre Sathish Paul (RMG), ambao walisindikizwa na Mshauri Mkuu wa Mawasiliano ya Kijamii, Padre Fidel Orendain. Mkutano huo ulihuishwa na kuongozwa na Padre Orendain mwenyewe, ambaye alihudumu kama mzungumzaji mkuu wakati wa mkutano huo wa siku tatu.
Mambo ya kujua kuhusu Akili Unde(AI)
Katika Ulimwengu uliotawaliwa na teknolojia za kidijitali, kama hii ya Akili Unde (AI) pamoja na mambo mengine yaliyo muhimu, inatumika kuboresha mtiririko katika utengenezaji wa programu za utangazaji, uboreshaji wa sauti na tathimini ya ubora wa picha, kutumia kwa ufanisi wigo wa masafa katika usambazaji wa televisheni na radio lakini vile vile kuzalisha vipindi vipya kwa kufufua taarifa za zamani na pia kulenga taarifa kwa ajili ya walengwa au mtu mmoja mmoja. Akili Unde pia inatumika kufukua maudhui kutoka katika hifadhi za nyaraka nyingi za kale, kuyaandaa maudhui kwa ajili ya kusambazwa kimataifa na kuzalisha huduma kama vile maelezo kwenye sauti, kuhamisha maandishi kwenda kwenye sauti na ishara, kwa haraka na kwa usahihi kuliko ambavyo ingefikiwa hapo awali. Pamoja na hayo mazuri lakini pia kuna hatari ya kutumiwa vibaya.
"Hadhi ya Watoto na vijana katika enzi ya Akili Unde"
Kama Shirika la Don Bosco(Salesian) linalojikita juu ya mafundisho ya vijana, ni vema kukumbusha hata yale ambayo Papa Leo XIV alisema kunako tarehe 13 Novemba 2025, mjini Vatican wakati akikutana na washiriki wa Mkutano kuhusu: “Hadhi ya Watoto na vijana katika enzi ya Akili Unde, (The dignity of children and adolescents in the age of Artificial Intelligence), ulioandaliwa na Mfuko wa Utafiti na Utafiti kuhusu Utoto na Ujana. Papa Leo XIV aliwashukuru kwa uwepo wao na kwa michango yao muhimu. “Hili lenyewe ni zoezi muhimu katika kulinda uhalisi na muunganiko wa binadamu, ambalo lazima liongozwe kila wakati na heshima kwa utu wa binadamu kama thamani ya msingi. Ni kwa kuchukua mbinu ya kielimu, kimaadili na uwajibikaji pekee ndipo tunaweza kuhakikisha kwamba akili ude inatumika kama mshirika, na si tishio, katika ukuaji na maendeleo ya watoto na vijana. Matumizi ya Akili Unde yanaibua maswali muhimu ya kimaadili, hasa kuhusu ulinzi wa heshima na ustawi wa watoto wadogo.”
Watoto na vijana wako katika hatari kubwa ya udanganyifu wa AI
Watoto na vijana wako katika hatari kubwa ya kudanganywa kupitia mifumo ya kimashine(algoriti) za Akili Unde(AI)ambazo zinaweza kushawishi maamuzi na mapendeleo yao. Ni muhimu wazazi na waelimishaji wafahamu mienendo hii, na kwamba zana zitengenezwe ili kufuatilia na kuongoza mwingiliano wa vijana na teknolojia.” Papa aidha alitoa wito kwamba “Serikali na mashirika ya kimataifa yana jukumu la kubuni na kutekeleza sera zinazolinda heshima ya watoto wadogo katika enzi hii ya AI.) Papa alisisitiza tena kwamba “Hii inajumuisha kusasisha sheria zilizopo za ulinzi wa data ili kushughulikia changamoto mpya zinazotokana na teknolojia zinazoibuka, na kukuza viwango vya maadili kwa ajili ya maendeleo na matumizi ya AI. Papa alisisitiza kwamba “hata hivyo kulinda heshima ya watoto wadogo hakuwezi kupunguzwa kwa sera pekee; pia inahitaji elimu ya kidijitali. Kama mtangulizi wake alivyowahi kusema kuhusu mpango wa ulinzi ulioendelezwa na vyama vitatu vikubwa vya Wakatoliki nchini Italia, watu wazima, lazima wagundue upya wito wao kama "wasanii wa elimu" na kujitahidi kuwa waaminifu wake.” “Kiukweli ni muhimu kuandika na kutekeleza miongozo ya maadili, lakini hiyo haitoshi. Kinachohitajika ni juhudi za kila siku za kielimu zinazoendelea, zinazofanywa na watu wazima ambao wenyewe wamefunzwa na kuungwa mkono na mitandao ya ushirikiano.”
Kukaribia ulimwengu wa kidigitali
Mchakato huu unahusisha kuelewa hatari ambazo matumizi ya AI na ufikiaji wa kidijitali wa mapema, usio na kikomo na usiosimamiwa unaweza kusababisha kwa mahusiano na maendeleo ya vijana. Ushauri wa Papa Leo XIV anabainisha kwamba, “Ni kwa kushiriki tu katika ugunduzi wa hatari hizo na athari kwenye maisha yao binafsi na kijamii, ndipo watoto na vijana wanaweza kusaidiwa katika kuukaribia ulimwengu wa kidijitali kama njia ya kuimarisha uwezo wao wa kufanya maamuzi yenye uwajibikaji kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya wengine. Kuhusu hilo Papa alisema kuwa “ni zoezi muhimu katika kulinda uhalisi na muunganiko wa binadamu, ambalo lazima liongozwe kila wakati na heshima kwa utu wa binadamu kama thamani ya msingi. Ni kwa kuchukua mbinu ya kielimu, kimaadili na uwajibikaji pekee ndipo tunaweza kuhakikisha kwamba akili ude inatumika kama mshirika, na si tishio, katika ukuaji na maendeleo ya watoto na vijana.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.