Tafuta

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mashirika ya Kitawa Jimbo kuu la Arusha yamenogeshwa na kauli mbiu “Tushirikishane Kutangaza Injili ya Kristo kwa Watu Wote Hasa Wasiomjua Kristo.” Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mashirika ya Kitawa Jimbo kuu la Arusha yamenogeshwa na kauli mbiu “Tushirikishane Kutangaza Injili ya Kristo kwa Watu Wote Hasa Wasiomjua Kristo.”  (@Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 25 ya Umoja wa Mashirika ya Kitawa Jimbo Kuu la Arusha

Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yanapaswa kushirikiana katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, lakini hususan kwa wale ambao hawajabahatika kumfahamu Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hiki ndicho kipaumbele katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Watawa Wanaofanya Utume wao Jimbo kuu la Arusha, Tanzania.

Na Frt. Simeon M. Leiyan, - Jimbo Kuu Katoliki Arusha

Ujenzi wa umoja katika tofauti anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, ni mchakato unaosimikwa katika fadhila ya: Unyenyekevu, uhuru wa ndani pamoja na kupokea utambuzi kwa kuheshimu wito wa kila mwanashirika. Mama Kanisa anaendelea kuwahamasisha watawa kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na la Kimisionari kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika: Neno la Mungu, Maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa; Unyenyekevu na Uhuru wa ndani, daima wakitafuta kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao na yale ya waamini kwa njia ya karama ya Shirika lao. Mama Kanisa katika maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa anapenda kukazia majiundo makini na endelevu kwa watawa; umuhimu wa kujenga na kudumisha maisha ya umoja na udugu wa kibinadamu; maisha ya kiasi; ukimya na matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kuwawezesha watawa kukaza macho yao kwa Uso wa Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Watawa waoneshe bidii, juhudi na mwamko wa kutaka kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kilio cha walimwengu, ili kuwajibu kwa wakati muafaka, vinginevyo, wanaweza kujikuta wakiwa wamepoteza mwelekeo na utambulisho wao wa Kikristo! Kanuni ya Mtakatifu Benedikto: Sala na Kazi “Ora et Labora” ni mwongozo unaowasaidia Wabenediktini katika maisha na utume wao kuwa ni watu wanaofanya kazi kwa: Bidii, juhudi na maarifa ili waweze kujipatia mahitaji yao msingi pamoja na kuendelea kumwilisha matunda ya kazi hizi katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa njia ya kazi za mikono na akili zao wanamtukuza Mwenyezi Mungu, aliye asili ya wema na ukarimu wote. Hii ni changamoto pia kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuhakikisha kwamba, yanajiwekea sera na mikakati ya kujitegemea na kulitegemeza Kanisa mahalia. Maisha ya taamuli yaendelee kupyaishwa ndani ya Kanisa kutokana na uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na watu wake, hata pale ambapo kumekuwepo na changamoto kubwa na hali ya kutaka kukata tamaa.

Askofu mkuu Isaac Amani Massawe akiongoza Ibada ya Misa Takatifu
Askofu mkuu Isaac Amani Massawe akiongoza Ibada ya Misa Takatifu

Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, maisha ya taamuli yataendelea kupyaishwa ili kuwawezesha watawa kuutafuta Uso wa Mungu, ili waweze kuona na kuguswa na mahangaiko ya binadamu katika ulimwengu mamboleo! Ni katika muktadha wa umuhimu wa maisha na utume wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yanapaswa kushirikiana na kushikamana katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, lakini hususan kwa wale ambao hawajabahatika kumfahamu Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hiki ndicho kipaumbele katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Watawa Wanaofanya Utume wao Jimbo kuu la Arusha, Tanzania. Maadhimisho haya yamenogeshwa na kauli mbiu “Tushirikishane Kutangaza Injili ya Kristo kwa Watu Wote Hasa Wasiomjua Kristo.” Huu ndio mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: Kiroho na kimwili. Umoja huu ulianzishwa na Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha. Maadhimisho haya ni wakati wa kutangaza na kushuhudia ushirika wa upendo unaokita mizizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; chemchemi ya wema na uzuri unaoweza kuleta nguvu mpya, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Wito wa maisha na utume wao wa kitawa, uwawezeshe kujisikia kuwa ni washiriki wa mradi mkubwa wa upendo wa Mungu unaowafungamanisha na kuwaunganisha wote ili kuwa wamoja. Watambue kwamba, kila mmoja wao anashiriki kikamilifu katika kutekeleza mradi huu kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa njia ya mshangao wa historia ya miito yao.

Watawa wa Mashirika mbalimbali washikamane kutangaza Injili ya Kristo
Watawa wa Mashirika mbalimbali washikamane kutangaza Injili ya Kristo

Ni muda muafaka wa kuishi na kuendelea kupyaisha ushiriki katika mashirika yao kwani kuna hatari kubwa ya kuweza kumezwa na uchoyo pamoja na ubinafsi na hivyo kufyekelea mbali ushirika wa kijumuiya. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kuna ushiriki mkamilifu kwa kutambua kwamba, kila mtawa ni sehemu ya mradi huu mkubwa, ili kuweza kuiishi zawadi hii kuna umuhimu wa kujenga umoja unaovuka kinzani za kitawa! Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa umoja huu kunako mwaka 2000 imeadhimishwa na Askofu mkuu Isaac Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania ambaye amewataka watawa kutembea katika njia ya: Imani, Matumaini na Mapendo kwa Ujasiri na Unyenyekevu. Amewapongeza kwa maisha na utume wao Jimbo kuu la Arusha. Bila shaka sifa na ushuhuda wa maisha yao vimekuwa na mvuto kwa wasichana kutaka kujiunga na mashirika yao. Umoja huu uwe ni fursa ya kufahamiana zaidi na hivyo kufundishana na kushirikishana mbinu bora za uinjilishaji, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati mintarafu roho na karama za Mashirika yao. Watawa waweke tumaini imara kwa Kristo Yesu, wakisukumwa na imani na mapendo thabiti kwa Mungu na jirani zao. Watawa waupende Msalaba ambao ni tumaini la utukufu ujao; wawe na shauku ya kutaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia, ili kusudi ushuhuda wao uonekane mbele ya watu wote na Baba yao aliye mbinguni apate kutukuzwa. Rej. Mt 5:16. Na hatimaye, "Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikra zenu" Rom 12: 2a.

Watawa wa Mashirika mbalimbali wanaofanya utume wao Arusha
Watawa wa Mashirika mbalimbali wanaofanya utume wao Arusha

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania, anawataka watawa kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Wanayo haki na nyajibu zao wanazopaswa kutekeleza kwa kushirikiana na kushikamana na watu wa Mungu katika ujumla wao. Wawe mstari wa mbele katika: utume, maisha na ujenzi wa Makanisa mahalia kwa njia ya karama na mapaji yao, lengo likiwa ni kushiriki kikamilifu katika utume wa Makanisa mahalia kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni wakati wa kuondokana na ubinafsi kwa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa Kanisa la nyumbani, ili kuzamisha ndani mwao dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Ni muda muafaka wa kujipambanua katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa mahalia. Askofu mkuu mstaafu Lebulu anawataka watawa kuzamisha mashauri ya Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao katika: Ufukara, utii wa Kiinjili na Usafi kamili. Wakazie daima maisha ya kijumuiya ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Wajitahidi kushiriki na kunogesha maisha na utume wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo hususan katika Nchi za Afrika na kwa namna ya pekee katika Ukanda wa Nchi za AMECEA ambako dhana ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo inapewa kipaumbele cha pekee kama sehemu muhimu sana ya shughuli za kichungaji. Itakumbukwa kwamba, Jubilei hii, ilipaswa kuadhimishwa Mwezi Desemba 2025, lakini ikasogezwa mbele, ili kutoa nafasi kwa watawa wengi kuweza kuhudhuria.

Watawa Jubiei 25 Arusha
05 Mei 2026, 16:03