Congo DR:Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu kuhudumia wenye HIV
Na Sr. Dorothée Sindani, RSCJ.
Ulimwengu wetu umeathiriwa na kujeruhiwa huku baadhi ya watu wakiishi na Virusi vya ugonjwa wa Ukimwi kwa ukimya, wakiwa na hofu ya kukataliwa na aibu juu ya afya yao, wakilemewa na mawazo ya watu wengine wanavyo watazama. Kutambua hali ya afya ya kuwa na Virusi vya wa Ukimwi (HIV/VUU kunamaanisha mateso ya kimwili na kunyanyapaliwa, ndiyo sababu wengi wa waliothiriwa mara nyingi huendelea kukaa kimya, wakificha hali yao kwa kuogopa kukataliwa na familia zao na jamii zao. Kwa kutoa msaada wa kimatibabu na mwongozo wa kiroho kupitia kundi la "Marafiki wa Sophie", masista wamebadilisha hali yao ya kukata tamaa kuwa mwanzo mpya.
Dhamira ya huruma na uwepo kamili
Wakiongozwa na karama la Shirika la Masista wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ishara ya upendo wa huruma ya Yesu, masista hawa huwakaribisha watu wanaoishi na na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi bila kuwahukumu. Kupitia ishara rahisi za kila siku na kuwasikiliza kwa makini, wao huwakumbusha kwamba ugonjwa haubainishi thamani ya mtu. Masista huwasaidia kwa kuhifadhi heshima yao ya kibinadamu kwa wagonjwa, kwa kutoa msaada wa kimaadili na kimwili kwa watu wazima na watoto ambao bado hawajui hali yao.
Usaidizi wa kiroho, kimaadili, kisaikolojia na kimwili
Kikundi cha “Marafiki wa Sophie” kilianzishwa rasmi mwaka 2019, lakini muda mrefu kabla ya hapo, Sr Marie-Pascaline Ekosoni, RSCJ, alikuwa tayari ametoa msaada wake kwa familia iliyoathiriwa na Virusi vya ugonjwa wa Ukimwi. “Mtu anapokataa hali yake, anaweza kuteseka kutokana na matatizo ya kisaikolojia” alisema Sr Marie-Pascaline. Hivyo basi kuepuka hili, Sr Marie-Pascaline huwasikiza wagonjwa na lengo la kuimarisha kujithamini na ustahimilivu wa wagonjwa wanapokabiliana na ugonjwa huu.
Kikundi hiki kimepewa jina la mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mtakatifu Madeleine Sophie Barat, wakiwa na nia ya kuwaona na kuwahudumia wagonjwa kama marafiki wa Mtakatifu wa kukaribishwa ndani ya familia ya kweli ya kiroho, isiyo na unyanyapaa. Mbali na usaidizi wa kiroho, kimaadili na kisaikolojia, Masista hutoa msaada wa kimwili (maziwa, unga wa mahindi, sukari, mchele na kadhalika), ambao hutolewa kwa upendo, huwapa wagonjwa fursa ya kubaki katika hali nzuri na kutoteseka na njaa, wakati wa matibabu.
Kutoka katika mateso hadi kutoa ushuhuda wa matumaini
Bi. Nouchka mwenye umri wa miaka thelathini na tano, mwanachama wa "Marafiki wa Sophie", alikubali kuelezea historia yake. Alizaliwa na Virusi vya ugonjwa wa Ukimwi baada ya kuambukizwa na mama yake, ambaye alikufa miaka michache baada ya kuzaliwa kwake, alikuwa wa pili kati ya ndugu watatu. Wote waliambukizwa lakini bila ufahamu wowote wa hali yao. "Hatukujua hali yetu", alisema, lakini alikumbuka kwamba watu kijijini walikuwa wakisema kwamba ‘mama wa watoto hawa alikufa kwa Virusi vya ugonjwa wa Ukimwi.
Kwa bahati mbaya, mtoto mdogo hakuishi. Kukataliwa na familia yake na jamii kulimuacha na majeraha makubwa. Kwa sababu ya kuachwa kwake, Bi. Nouchka alipata shida kubwa, ambayo ilimfanya aache matibabu na kuzama katika msongo wa mawazo. "Sikutaka tena kuishi," alisema. Kama wengine wengi, aliona hali yake kama ya aibu, mzigo usiowezekana kubeba, hisia ambayo ni ya kawaida kwa watu wengi wanaoishi na Virusi vya ugonjwa wa Ukimwi.
Hali inayorejesha maisha
Kukutana kwa Bi. Nouchka na Sr Marie-Pascaline Ekosoni kulibadilisha wakati muhimu maishani mwake. Alipokelewa kwa heshima na wema, akasikilizwa bila kuhukumiwa au kulaaniwa, Bi. Nouchka polepole alipata tumaini tena. "Kukutana na Sr. Pascaline ilikuwa wakati wa mwanga wa matumaini. Nilipata nguvu na kuamua kuishi", alielezea. Kwa msaada huu, aliweza kugundua sura ya Kanisa inayotoa huduma, kuinua mtu tena na kumpa matumaini. Mchakato wa uponyaji haukuwa rahisi. Bi. Nouchka alikiri kwamba alipitia wakati wa hasira na uasi. "Nilikuwa nimefikia hatua ya kumlaani Mungu, na hasa mama yangu, nilipoelewa jinsi maambukizi yalivyotokea. Kwa sababu angepaswa kutulinda", alisema.
Leo ni mama wa mtoto wa kiume wa miaka mitatu, ambaye hana Virusi vya Ukimwi kutokana na matibabu na mwongozo mwema. Ingawa Baba yake mtoto huyo alimkataa na kumtelekeza, Bi. Nouchka anaendelea na safari yake kwa ujasiri na heshima. Alikataa kuishi kwa aibu. "Hali hii si kikwazo kwangu tena," alisema. Amejitolea kuongeza uelewa, kwa sasa anahusika katika kuwatia moyo wengine kutumia dawa zao mara kwa mara na kuwajibika katika mahusiano ya kibinadamu, ili kulinda maisha yao na maisha ya wengine.
Amekuwa sauti kwa wasio na sauti, akiwashukuru wale waliomrejeshea tumaini. "Ninamshukuru Sr Marie-Pascaline Ekosoni na Marie-Jeanne Elonga na Masista wote wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kunikaribisha. Nimeelewa kwamba Moyo wa Yesu huwakaribisha kila mtu, na kwamba wakati mwingine, tunakosa ujasiri wa kurudi kwenye moyo huu tunaoutamani. Nimerejesha nafasi yangu katika jamii. Leo, natembea nikiwa nimeinua kichwa changu. Wale wanaonikubali kama nilivyo sasa ni sehemu ya familia yangu”.
Wito wa kukubalika na huruma
Uzoefu wa Bi. Nouchka ni uthibitisho kwamba hakuna mtu anayetambuliwa na ugonjwa wake. Katika ulimwengu huu uliobarikiwa na uliojeruhiwa, upendo unaoishi kwa njia halisi, kukubalika bila masharti na huruma kunaweza kubadilisha majeraha kuwa njia za matumaini. Kukubalika bila masharti ndio tiba ya kwanza. "Nina nia ya kuongeza uelewa kwa maelfu ya watu na ninapigania ulimwengu usio na Ugonjwa waVirusi vya Ukimwi", Bi. Nouchka alihitimisha.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.