Tafuta

Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV huko Angola:Papa akiwa katikati ya Skauti wa Angola Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV huko Angola:Papa akiwa katikati ya Skauti wa Angola  (@Vatican Media)

Ziara ya Papa Leo XIV yafufua matumaini nchini Angola

Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV nchini Angola imepokelewa kama ishara yenye nguvu ya ukaribu wa Mungu na watu wanaokabiliwa na changamoto kubwa za kijamii. Watawa na waamini pia wanaelezea ziara hiyo kama wakati wa neema,umoja na matumaini mapya.Kupitia maneno na uwepo wake,Baba Mtakatifu amewaalika Waangola kukumbatia upatanisho na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya mustakabali wa haki na amani.

Na Sr. Christine Masivo, CPS - Vatican.

"Hizi zilikuwa siku zenye nguvu zilizojaa furaha, imani, na shauku kwetu sote." Kwa maneno haya, Sr. Idalina Mareco wa Mabinti wa Maria Msaada wa Wakristo (FMA) alieleza  mazingira ambapo imani iliishi kwa njia inayoonekana na ya kijamii, yalijitokea wakati wa Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu  Leo XIV ya hivi karibuni barani Afrika kuanzia 13 hadi 23 Aprili 2026.

Ziara yenye kuakisi furaha na imani ni ujumbe unaozungumza na Moyo

Kwa wengi, uwepo wa Papa ulikuwa zaidi ya ishara. Kwa mujibu wa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, liliakisi kwamba, ziara ya Papa ilishuhudiwa kama ishara hai ya ukaribu wa Mungu na taifa linaloendelea kuvumilia majeraha yaliyosababishwa na umaskini, ukosefu wa haki, ukosefu wa ajira, na mgawanyiko wa kijamii. Hata hivyo, katikati ya hali halisi hizi, ziara hiyo ikawa chanzo cha nguvu mpya na kutia moyo. Sr Idalina akizungumza na Shirika la Fide, alisisitiza kwamba Baba Mtakatifu hakuogopa kutambua mapambano ya watu wa Angola. Badala yake, alizungumzia moja kwa moja hali halisi yao, akitambua maumivu yao na uwezo wao. Ujumbe wake uliendelea kuangazia utajiri wa watu, utu wao, ustahimilivu, na uwezo wa kujenga upya.

“Katika ujumbe wake wote, alitukumbusha juu ya rasilimali hizi," alibainisha, akiashiria wito wa Papa wa matumaini, amani, na maridhiano. Hizi si maadili ya kufikirika, bali ni mahitaji ya haraka kwa jamii inayotafuta uponyaji. Maneno ya Papa yaligusa kwa undani kwa sababu yalithibitisha kwamba hata katika mateso, kuna njia ya kusonga mbele yenye msingi wa umoja na uwajibikaji wa pamoja.

Kujenga mpango wa matumaini pamoja

Mojawapo ya wakati muhimu zaidi ya ziara hiyo ilikuja wakati wa hotuba ya Papa kwa viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia, na wanadiplomasia huko Ikulu ya Rais. Huko, alitoa mwaliko wazi na wa kushawishi kwamba, "Pamoja mnaweza kuifanya Angola kuwa mradi wa matumaini." Wito huu ulisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika sekta zote za jamii. Papa alisisitiza jukumu la Kanisa kama "chachu katika unga," likifanya kazi kimya kimya lakini kwa ufanisi kukuza haki na mshikamano. Alipinga mifumo inayoendeleza ukosefu wa usawa na akataka mfumo wa kuishi pamoja bila unyonyaji na ahadi za uongo. Cha kuvutia hasa ilikuwa msisitizo wa Papa Leo XIV wa kufikia pembezoni mwa wale wanaoishi pembezoni mwa miji na maeneo ya vijijini ya mbali. Jamii hizi, ambazo mara nyingi hupuuzwa, ndizo mahali ambapo moyo wa kweli wa taifa upo na ambapo mustakabali wake unaundwa.

Wakati wa neema na upyaishaji

Akirudia hisia hiyo , Sr. Laurinda Kinha wa Shirika la Don Bosco alielezea ziara hiyo kama "wakati wa neema." Kwake, kumkaribisha Papa ilikuwa fursa na uzoefu wa kiroho sana. Picha ya mchungaji akiwatembelea kundi lake ilikuwa na maana kubwa, haswa kwani hii ilikuwa miongoni mwa safari za kwanza za upapa wake. Alibainisha kuwa ziara hiyo ilileta faraja ya kweli kwa watu ambao wamekabiliwa na majaribu mengi katika miaka ya hivi karibuni. Muhimu zaidi, ilithibitisha tena utume na utambulisho wa Kanisa nchini Angola. Ilitumika kama ukumbusho kwamba Kanisa linabaki karibu na watu wake, likiandamana nao katika mapambano na matumaini yao.

Njia kuelekea upatanisho

Ziara ilipomalizika, matokeo  yake yanaendelea kufunuka katika mioyo ya waamini. Watu wa Angola wengi sasa wanatazamia kwa matumaini mapya kwamba ujumbe wa Papa utahamasisha upatanisho wa kweli ambao unaishi kila siku katika mahusiano yaliyo na msamaha, heshima, na mshikamano. Katika ulimwengu ambao mara nyingi unaonyeshwa na mgawanyiko, safari hii ya kichungaji inasimama kama ushuhuda wenye nguvu, kwamba Mungu hutembea na watu wake, na kwamba kupitia imani, hata majeraha makubwa zaidi yanaweza kuanza kupona.

USHUHUDA WA WATU WA ANGOLA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

27 Aprili 2026, 11:54