Wanamuziki,wamisionari na madaktari katika Misa ya Papa huko Kilamba
Na Claudia Torres – Kilamba, Angola
Papa Leo XIV alialiadhimisha Misa Takatifu huko Kilamba, yapata kilomita 30 kutoka mji wa pwani wa Luanda. Watu wapatao 100,000 walikusanyika kwa ajili ya liturujia Dominika tarehe 19 Aprili 2026, sio tu kutoka Luanda, bali kutoka Poland, Italia, na hata Uruguay. Mazingira yalikuwa ya kisherehe, ikiongozwa na kwaya ya ‘500 vozes’, chini ya uratibu wa Sekretarieti ya Liturujia Kitaifa, ikiwakilisha kwaya za Majimbo na Majimbo Makuu yanayojumuisha Baraza la Maaskofu wa Angola na São Tomé (CEAST). "Tuko hapa kupiga muziki wote unaowafanya watu wacheze," alisema mpiga kinanda Luis Muxinda, mmoja wa vijana wawili waliopiga kinanda kwa ajili ya Misa ya Papa. Kwake, ilikuwa mara ya kwanza kupiga kinanda katika hafla ya aina hii. "Hii ni fursa nzuri sana na ninahisi msisimko sana," alisema.
Wamisionari kutoka Uruguay na Poland
Kundi kubwa la mapadre waliketi katika safu za kwanza za viti, wakiwa wamevalia mavazi maalum ya Misa ya rangi nyeupe kwa ajili ya liturujia siku ya Dominika ya Tatu ya Pasaka. Miongoni mwao alikuwa Padre Andrés Algorta, mmisionari kutoka Uruguay ambaye ameishi Angola kwa miaka mingi, akifanya utume wake katika Parokia ya Mtakatifu Paulo huko Luanda. "Tunafurahi sana kwamba Papa yuko hapa pamoja nasi," alisema, akitoa shukrani kwa ukaribu wa Baba Mtakatifu na watu wa Benguela, mji wa pwani ambao umeathiriwa na mafuriko mabaya.
Katika hotuba yake kwa mamlaka ya Angola mnamo Aprili 18, Papa Leo XIV aliwakumbuka waathiriwa na wale waliopoteza makazi yao. "Papa alikuwa mkarimu sana kwa kujiunga na mateso yao. Nadhani wakati huo hakuwa karibu tu na wakaazi wa Benguela tu bali Waangola wote," alisema mmisionari huyo wa Uruguay.
Pia alikuwepo Sr Krystyna Zachwieja wa Shirika la Masista Wafransiskani wa Maria kutoka Poland ambaye anafanya utume wake wa kichungaji na pia kama mwalimu na vile vile katika malezi ya wanaojiunga katika Shirika lao huko Angola. "Kile tunachokishuhudia sasa ni jambo la ajabu," alisema kwa ujasiri kwamba ziara ya Papa itakuwa jambo la msaada sana wa upyaishaji katika uinjilishaji nchini Angola.
Madaktari katika Utume
Kulikuwa pia Sergio Facchini na Eleonora Biasotto, madaktari wa Watoto kutoka Italia ambao wanafanya utume wao kwa miaka miwili katika Hospitali ya “Mungu Mpaji” huko Luanda. Wanatoa huduma kwa watoto walio na utapiamlo ambao Eleonora alielezea kama suala "gumu" ambalo wakati mwingine huwaweka katika "hali ya utata sana." Licha ya changamoto, alisema, "tunajitahidi kufanya tuwezavyo.” "Kazi yetu," Sergio aliongeza, "inatuvuta karibu na wale waliotengwa hata katika hali hii ngumu tayari, na uwepo wa Papa, ambaye anataka kuwa karibu na watu hawa, unatupa nguvu na unatusaidia kuendelea na kazi yetu."
Padre Daniel Malamba Mmisionari wa Neno la Mungu wa Angola alisema ilikuwa chanzo cha furaha kwa Wakristo wa Angola kumkaribisha Papa kama "mhujaji wa amani na matumaini,” na akaongeza kusema kwamba watu bado wanahitaji "amani ya kijamii, amani ya moyo, na amani ya kuishi pamoja kikamilifu."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.