Tafuta

Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Mfufuka ambayo jamii ya kwanza ya Wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli. Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Mfufuka ambayo jamii ya kwanza ya Wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli. 

Tafakari Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Mashuhuda wa Ufufuko!

Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Mfufuka ambayo jamii ya kwanza ya Wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu ya Fumbo la Pasaka na Fumbo la Msalaba Rej. KKK 638. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kwa wafu. Hiki ni kielelezo cha ushindi wa Msalaba; Upendo usiokuwa na upeo; nguvu ya sadaka ya hali ya juu kabisa. Huu ni ushindi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na nguvu za giza na kwamba, kifo hakina tena sauti ya mwisho. Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Mfufuka ambayo jamii ya kwanza ya Wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu ya Fumbo la Pasaka na Fumbo la Msalaba Rej. KKK 638. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba.

Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni Mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko.
Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni Mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko.

Pasaka ni chemchemi ya: imani, maisha na matumaini mapya na kwamba, Kristo Yesu ndiye amani yetu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli mashuhuda wa Fumbo la Pasaka, maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Mfufuka awe ni chemchemi ya amani duniani na faraja kwa wale wote wanaoteseka na kunyanyasika kwa vita, njaa na magonjwa na athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia. Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yasaidie kuimarisha imani, matumaini na mapendo kama ilivyokuwa kwa Maria Madgalena na wale wanawake wengine waliowahi asubuhi na mapema siku ya kwanza ya juma. Rej. Mt 28: 1- 10. Simoni Petro na yule mwanafunzi ambaye alipendwa sana na Kristo Yesu walikuwa bado hawajalifahamu Fumbo kuu la Ufufuko wa wafu, lakini “akaona na kuamini.” Rej Yn 20: 1-10. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Yesu Mfufuka, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo thabiti. Ni mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni Manabii wenye ujasiri katika hija ya maisha yao huku bondeni kwa machozi. Tujitahidi kuongozwa na Roho Mtakatifu na kamwe tusimezwe na malimwengu.

Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu
Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu

Huu ni mwaliko wa kuendelea kuwa ni mashuhuda amini na hai wa Fumbo la Pasaka kwa kutambua kwamba, kila Mbatizwa ni Mtume mmisionari na hivyo anashiriki kikamilifu katika: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuadhimisha Fumbo la Pasaka ya Bwana kwa mioyo iliyotakasika na kupyaishwa kwa neema na baraka za Roho Mtakatifu, tayari kuyapyaisha na kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu na mwanga wa Injili ya Kristo Mfufuka. Wimbo wa Aleluiya Kuu unaosikika katika kipindi hiki cha Pasaka ni wimbo wa sifa, shangwe, utukufu na heshima kwa Kristo Mfufuka, aliyeshinda dhambi na mauti. Ni wimbo unaomtukuza Mungu mkuu; na ni wimbo wa wenyeheri unaotoa mwaliko wa ushiriki katika Pasaka ya milele, kiini cha Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana. “Surrexit, yaani Amefufuka.”

Wakristo Wanapaswa kuwa ni Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka
Wakristo Wanapaswa kuwa ni Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka   (Vatican Media)

Tunasoma katika Maandiko Matakatifu “Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.” Mt 28:7. Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni kiini cha imani na matumaini ya Mama Kanisa. Huu ni ushuhuda na ukweli amini juu ya Kristo Yesu kuhusu maisha na utume wake hapa duniani. Kwa hakika, Kristo Yesu ndiye Mwana wa Baba wa milele; Shuhuda wa huruma, upendo na msamaha wa Baba kwa mwanadamu aliyetopea katika dhambi. Kristo Yesu ndiye lile Hekalu lililobomolewa na hatimaye, kusimamishwa kwa muda wa siku tatu. Rej Yn 2:18-19. Kristo Yesu ndiye lile Jiwe lililokataliwa na waashi, wakamkana Mkuu wa uzima ambaye Mungu amemfufua kwa wafu. Rej Mdo 3:15. Kristo Mfufuka ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Nyakati zote ni zake na kwamba, Kristo Mfufuka anaendelea kuwa kati ya waja wake kwa njia ya Roho wake Mtakatifu, Sakramenti za Kanisa; Kwa Neno lake linaposomwa, kutafakariwa, kutangazwa na kushuhudiwa. Rej Yn 14:19. Mababa wa Kanisa wanakiri na kusema, Sherehe ya Pasaka ni mwanzo wa Kanisa la huduma ya haki, amani na upatanisho; hili ni Kanisa linalosimikwa katika upendo, umoja na mshikamano na kwa hakika Pasaka ya Bwana ni udongo wenye rutuba nzuri katika mchakato wa ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Heri ya Pasaka ni mwaliko kwa waamini kuwa watu wapya na hatimaye kuanza kutembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka, tayari kupyaisha imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Pasaka ya Bwana 2026
04 Aprili 2026, 10:33