Tafakari Jumamosi Kuu: Kitovu Cha Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, Kesha la Pasaka ni kilele cha siku kuu tatu za Pasaka ambazo Kanisa huziadhimisha kuanzia Alhamisi kuu, Ijumaa kuu, kilele chake katika usiku Mtakatifu. Baada ya kuadhimisha: Mateso na Kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, katika usiku huu mtakatifu, tunaadhimisha Ufufuko wake kutoka wafu kama alivyosema. Tunamshangilia, “Kristo Mfufuka, tumaini la Ufufuko na Uzima wetu” Ufufuko wa Bwana wetu Yesu ni msingi wa Imani yetu, kama anavyotuambia Mtume Paulo, “Kama Kristo asingalifufuka basi Imani yenu ni bure” (1 Kor 15:14). Tunamshangilia Kristo aliyetoka mzima kaburini, usiku ambapo Kristo alikata minyororo ya dhambi na mauti akatoka kuzimu ameshinda. Tunashangilia utimilifu wa Ahadi ya Mungu, Ahadi ya kuwaletea taifa lake ukombozi wa milele kwa njia ya sadaka ya Mwanaye mpenzi Bwana wetu Yesu Kristo, baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva. Nasi tunashiriki mateso kifo na ufufuko wa Kristo kwa njia ya ubatizo wetu. Tunapokea zawadi kubwa ya ukombozi kutoka katika utumwa wa dhambi na kuanza safari ya mpya ya maisha ndani ya Kristo Mfufuka.
Kesha la Pasaka: Mama wa Mikesha Yote ya Kanisa: Siku ya Jumamosi kuu huanza katika ukimya, ni siku Yesu aliyokuwa amelala kaburini. Lakini mambo huanza kubadilika jioni, tunapoingia katika Kesha hili la Pasaka. Katika giza, siku inayotangulia ufufuko wa Bwana yaani Jumamosi usiku, Wakristo wanakusanyika katika mkesha, ni kesha la Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama wa Mikesha yote. Mtakatifu Augustino aliliita Kesha hili la Pasaka kuwa “Mama wa mikesha yote” kwa sababu katika usiku huu, Kanisa lipo macho kusubiria ufufuko wa Kristo Bwana wetu.” Tunatafakari kwa kina historia nzima ya ukombozi wetu, tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi siku hii Takatifu ambapo Kristo alifufuka kutoka wafu, siku ya tatu baada ya mateso na kifo chake. Tunakutanika kusubiria na kushangilia utimilifu wa ahadi ya Yesu kwamba siku ya tatu atafufuka (Mt. 16:21-23; Mk 8:31; Lk 9:21-22). Ni kweli alifufuka kama alivyosema nasi tumekusanyika kushangilia ufufuko wake, ushindi wake dhidi ya kifo na mauti na tunda la ukombozi uliotokana mateso, kifo na ufufuko wake. Tunaposhangilia ufufuko wa Kristo, tunashangilia upya wa maisha yetu pia, ambapo kwa njia ya ubatizo wetu nasi sote tulizaliwa upya kama watoto wa nuru kutoka katika utumwa wa dhambi.
Mpangilio wa Kiliturujia katika Mkesha wa Pasaka: Makesha ya Sherehe ya Pasaka yanaadhimishwa tofauti kabisa na maadhimisho mengine ya Liturujia. Mkesha huu kwa namna ya pekee umegawanyika katika sehemu kuu nne nazo ni; Liturujia ya Mwanga, Liturujia ya Neno, Liturujia ya Ubatizo na Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Katika mkesha huu, Siku hii takatifu, ningependa tutafakari kwa kina mpangilio huu mzima wa Kiliturujia katika sehemu hizi kuu nne, ambao utatusaidia kuelewa vyema ni nini maana ya Pasaka ya Bwana, adhimisho hili kubwa katika Imani yetu. Sehemu ya kwanza: Liturujia ya Mwanga/ Mwanzo wa Adhimisho. Sehemu hii ya kwanza ya huanzwa kwa ibada ya kubariki moto nje ya Kanisa au mahali panapofaa, waumini wote wakikusanyika pamoja kuuzunguka moto huu mpya, wakati huu taa zote zikiwa zimezimwa. Kusanyiko hili ni Ishara ya Kanisa linalowaalika wanawe waliotawanyika popote duniani wakusanyike ili kukesha na kusali, kama kumbukumbu ya Pasaka ya Bwana, wakijiandaa kusikiliza Neno lake na kutukuza Mafumbo yake. Moto huu mpya maana yake ni nini? Moto huu katika Agano la Kale unatukumbusha uwepo wa Mungu katikati ya watu wake, Mungu aliyewaongoza wana wa Israeli jangwani kwa nguzo ya moto, wakiwa safarini kuelekea Nchi ya Ahadi. Katika Agano Jipya, Moto huu ni ishara ya Kristo Mfufuka, Nuru ya Ulimwengu na Mwanga wa Mataifa ambaye kwa Fumbo Takatifu la Pasaka, ameshinda giza la dhambi na mauti, na kwa njia yake, amefanya uumbaji mpya wa taifa jipya la watu wa Mungu. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu, moto wa upendo wa Mungu unawashwa tena ndani ya mioyo yetu, nasi tunashiriki fumbo hili la Pasaka kwa njia ya Ubatizo wetu. Moto pia ni Ishara ya utakaso. Kristo Mfufuka anatakasa mioyo, fikra, mawazo, akili na matendo yetu, nasi tunaanza maisha mapya ndani yake yeye aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili yetu.
Mshumaa wa Pasaka: Mara baada ya moto huu mpya kubarikiwa, Mshumaa wa Pasaka huanza kupambwa kwa Ishara mbalimbali kabla haujawashwa bado katika moto ule mpya. Maneno ya sala ya kubariki Mshumaa huu yanatualika nasi sote tuwake daima tamaa ya Mbinguni kwa Adhimisho hili takatifu la Ufufuko wa Bwana. Mshumaa huu kwa namna ya pekee, unapambwa kwa Ishara mbalimbali ambazo huambatana na maneno yanayosemwa na Kuhani. Kuhani huchora Ishara ya Msalaba, Ishara ya ukombozi wetu juu ya Mshumaa, huku akisema, “Kristo Jana na Leo (hapa akichora mstari wa wima), Mwanzo na Mwisho (akichora mstari wa mlalo). Kisha anachora herufi Alfa, herufi ya kwanza katika lugha ya Kigiriki juu ya Msalaba, na kisha Omega (herufi ya mwisho ya lugha Kigiriki) chini ya Msalaba. Hii inamaanisha kuwa Kristo Yesu ndiye Mwanzo na Mwisho wa vitu vyote. Yeye alikuwepo kabla ya ulimwengu kuumbwa na atakuwepo milele. Ni dhihirisho la Umungu wake (Ufunuo 22:13). Kisha kuhani huandika namba ya mwaka husika (2 0 2 6). Ukitazama katika Mshumaa wa Pasaka, basi huandikwa mwaka husika, mfano mwaka huu utaandikwa 2026, namba moja moja katika kona nne za Msalaba ulio katika Mshumaa. Anapochora namba zote hizi husema maneno kwa mpangilio wa kila namba. “Nyakati ni zake (2) na Karne pia (0), Utukufu ni wake, na Enzi pia (2) kwa karne zote za milele (6), Amina. Nini maana ya maneno haya? Hii inatukumbusha kuwa Kristo Yesu hayuko kwenye vitabu vya historia tu, bali yupo hai na anatawala sasa hivi, katika wakati wetu huu tulio nao sasa. Kila sekunde ya maisha yetu iko chini ya ulinzi wake, sasa na hata milele yote. Kisha kuhani huweka madonda matano ya Kristo katika mshumaa (hujulikana kama chembe tano za ubani). Hizi zinawakilisha Madonda Matano Matakatifu ya Yesu (mikononi mawili, miguuni mawili, na ubavuni moja). Kuhani husema, “Kwa majeraha yake matakatifu na matukufu, atulinde na kutuweka salama, Kristo Bwana wetu, Amina. Madonda haya yanatukumbusha kwamba, ingawa Yesu amefufuka, alama za majeraha yake zimebaki kama ushuhuda wa upendo wake mkuu na ushindi wake dhidi ya dhambi na mauti.
Kuwasha Mshumaa wa Pasaka: Baada ya Mshumaa huu kupambwa kwa alama hizi mbalimbali, Kuhani atauwasha Mshumaa katika moto mpya akisema, “Mwanga wa Kristo aliyefufuka kwa utukufu utuondolee giza moyoni na akilini.” Kisha ataimba Mwanga wa Kristo nasi sote tunaitika, tumshukuru Mungu. Kisha maandamano huanza kuelekea kwenye mlango mkubwa wa Kanisa. Padre au Shemasi husimama na kuuinua Mshumaa na kuimba tena “Mwanga wa Kristo, nasi tunaitika tumshukuru Mungu. Na hapa sote tunawasha rasmi mishumaa yetu kutoka katika Mshumaa wa Pasaka, yaani Kristo Mfufuka. Maandamano na mishumaa yetu inayowaka: Baada ya kuwasha mishumaa yetu, maandamano kuingia Kanisani huanza, yakiongozwa na Mshumaa wa Pasaka. Maandamano haya yanafananishwa na safari ya wana wa Israeli walipotoka utumwani Misri kuelekea nchi ya ahadi. Kama vile walivyoongozwa na nguzo ya moto usiku, waamini wanaongozwa na Mshumaa wa Pasaka (Kristo) kuelekea uzimani. Hii ni ishara kwamba kwa dhambi sisi sote tulikua gizani na kwa ufufuko wa Kristo Yesu, sisi sote tunatoka katika giza la dhambi na mauti kwa kuupata mwanga wetu kutoka kwa Kristo. Ni kwa njia ya Ubatizo sisi sote tunakabidhiwa mwanga huu wa Kristo Yesu ili tupate kuulinda na kamwe tusitembee gizani tena, na kwa mwanga huo tuweze mwisho wa maisha yetu kumlaki Bwana.
Mbiu ya Pasaka: Tukiwa na mishumaa yetu, tukiongozwa na mwanga wa Kristo tunaingia Kanisani na kisha huimbwa Mbiu ya Pasaka. Mbiu ya Pasaka (kwa Kilatini Exsultet) ni wimbo mkuu wa sifa na ushindi unaoimbwa mara baada ya Mshumaa wa Pasaka kuwekwa kwenye kinara chake madhabahuni. Ni moja kati ya nyimbo nzuri na za kale zaidi katika Liturujia ya Kanisa. Wimbo huu ni tangazo la ushindi wa Kristo, Kristo aliyemshinda Shetani, aliyeshinda dhambi na mauti. Yaeleza namna dhambi ilivyoingia katika historia ya mwandamu, mwanzo wa safari mpya ya ukombozi na utimilifu wa safari hiyo katika Fumbo hili Takatifu sana la Pasaka. Mbiu hii yaeleza thamani ya sadaka ya Kristo ilivyoleta ukombozi wa milele kwa taifa jipya la Mungu. Yaeleza sifa ya Mshumaa, Mshumaa unaomwakilisha Kristo mwenyewe. Lakini tutasikia pia hata nyuki waliotengeneza nta ya Mshumaa ule wakitajwa, Ishara kwamba ulimwengu wote unashiriki kumtukuza Mungu kwa fumbo hili Takatifu. Mbiu hii itarudia mara kwa mara maneno “Huu ndio usiku” (Haec nox est) ikisisitiza kuwa usiku wa Pasaka ni usiku mtakatifu sana kwa sababu ndio usiku ambapo Kristo alishinda dhambi na mauti kwa kufufuka kwake. Kwa mbiu hii, sehemu ya kwanza ya Liturujia ya Mwanga huitimishwa na kuingia rasmi katika sehemu ya pili ya Liturujia ya Neno.
Sehemu ya pili: Liturujia ya Neno: Katika Kesha hili ambalo ni Mama wa Mikesha yote, yanatolewa masomo tisa, yaani saba ya Agano la Kale na mawili ya Agano Jipya (Waraka na Injili), ambayo kimsingi yote yanapaswa kusomwa. Isipokuwa kama kuna sababu nzito ya kichungaji za kupunguza idadi ya masomo, basi na yapunguzwe masomo ya Agano la Kale. Lakini yapaswa kufahamika daima kuwa, masomo yote haya 9 ya Neno la Mungu ni sehemu msingi sana ya kesha hili la Pasaka. Msisitizo wa kwanza ukiwa ni muhimu yote yakasomwa. Katika Masomo yote ya sherehe hii, kanisa halichoki kutueleza maana ya usiku huu kwamba ni safari kutoka katika hali ya upotevu na kuingia katika hali ya uzima wa kimungu. Masomo haya yatueleza kwa mpangilio tangu uumbaji, anguko la wazazi wetu wa kwanza, mpango wa Mungu wa kumkomboa tena mwanadamu aliyeanguka na utimilifu wake katika Kristo Bwana wetu. Kila baada ya somo, huimbwa zaburi na kisha kuhani husoma sala kabla somo jingine. Hebu tutazame kwa kifupi masomo haya yote. Somo la Kwanza: (Mwanzo 1:1-2:2): Simulizi la somo hili laelezea Habari nzima ya uumbaji wa Mwanadamu hapo mwanzo. Somo hili latupa picha juu nafsi tatu za Mungu yaani, Baba Mwana na Roho Mtakatifu zadhihirika katika uumbaji, na hivyo hivyo katika safari nzima ya ukombozi wa mwanadamu. Kumbe kazi ya uumbaji ni kazi ya utatu mtakatifu, na kazi ya ukombozi hali kadhalika. Pia latueleza namna Mungu mwema alivyoumba kila kitu chema na kizuri na kilele cha uumbaji huu ni uumbaji wa Mwanadamu, aliye sura na mfano wa Mungu mwenyewe (Mwanzo 1:26). Pasaka yatukumbusha juu ya thamani kubwa ya mwanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu kati ya viumbe vingine vyote. Tutunze sura na mfano huu wa Mungu ulio ndani yetu kwa kutamani kuishi daima maisha matakatifu.
Somo la Pili: (Mwanzo 22:1-18.) Baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza, Mwenyezi Mungu, kwa mapendo makubwa alianzisha upya safari ya ukombozi wa mwanadamu kwa kumwita Ibrahimu, akafanya naye maagano na kumpatia Ahadi. Katika somo hili, Ibrahimu anaamriwa na Mungu kumtoa mwanaye wa pekee Isaka kama sadaka. Ni Ishara ya utii wa imani na uaminifu wa Ibrahimu kwa Mungu. Badala ya Isaka, Mwenyezi Mungu anatoa mwanakondoo. Hii ni alama ya Mungu Baba kumtoa Mwanae wa pekee Yesu Kristo Bwana wetu, Mwanakondoo wa kweli, atakayetolewa sadaka kwa ajili ya dhambi zetu. Tunamshukuru Mungu kwa upendo na uaminifu wake wakati wote. Somo la tatu: (Kut 14:15-15:1.) Kitabu cha kutoka, kinaeleza mwanzo wa safari ya taifa la Israeli kutoka utumwani Misri kuelekea nchi ya Ahadi. Katika somo hili, sura hii ya 14-15 Mwenyezi Mungu anawavusha Waisraeli katika Bahari ya Shamu kwa namna ya ajabu, na kwa kuvuka kwao bahari hii wanaanza safari mpya ya maisha. Somo hili katika kesha hili la Pasaka lina maana kubwa sana kwetu. Mtume Paulo anafananisha tukio hilo na Sakramenti ya Ubatizo, kwamba, kukombolewa kwa taifa la Israeli kutoka utumwani Misri na kuvuka kwao Bahari ya Shamu ni mfano wa Ubatizo wetu, ambao sote tuliokolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti na kuanzishiwa safari mpya ya maisha, kama wana wa Mungu. Kwa namna ya pekee, katika mkesha huu watabatizwa wakatekumeni, wataanza safari mpya ya maisha huku nasi sote tukirudia Ahadi zetu za Ubatizo.
Somo la nne: (Isa 54:5-14.) Mwenyezi Mungu alinena na watu wake kwa vinywa vya Manabii. Licha ya taifa lake mara kwa mara kushindwa kuwa waaminifu kwa Agano ambalo alifanya nao, bado Mungu hawaachi. Bado anaendelea kuwapenda na anatamani bado kudumisha na kurejesha kila wakati uhusiano wake na taifa lake teule. Anajifananisha na mume anayempokea mke aliyekuwa ameachwa (taifa la Israeli walioasi kila wakati), akiahidi amani na usalama usioisha. Ndio wito wa Mungu wa kila siku kwetu sisi sote. Mungu yu tayari kutupokea, anatupenda upeo, na kututafuta kila wakati tunaposhindwa kuwa waamifu kwake. Somo la tano: (Isa 55:1-11). Somo la tano ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya 55:1-11 ni mwaliko wa upendo wa Mungu kwa kila mwenye kiu ya kiroho kuja kupokea neema ya wokovu ambayo ni zawadi ya bure, ikionesha kuwa vitu vya ulimwengu, mali, vyeo, utajiri, anasa haviwezi kuitosheleza roho. Ni Neno la Mungu pekee (aliye Chakula cha Uzima) linaloweza kutupa uzima wa kweli. Kupitia somo hili, Kanisa linatukumbusha kuwa Neno la Mungu lina nguvu kama mvua inavyostawisha nchi; halirudi bure bali linatupa uhai mpya na kuthibitisha Agano la Milele ambalo Mungu amelifanya nasi kupitia ushindi wa mwanae dhidi ya dhambi na mauti.
Somo la sita: Bar 3:9-15, 32-4:4. Mwenyezi Mungu katika Maandiko Matakatifu anajifunua kwetu kama Hekima, akitualika sote kuitafuta hekima hiyo, kwani ndiyo uzima wetu. Na hekima hii ya kweli haipatikani katika mambo ya uliwengu huu, bali yatoka kwake yeye aliye chanzo cha hekima yote. Nabii Baruku anawaonya Waisraeli kuwa waliteseka utumwani kwa sababu waliiacha chemchemi ya Hekima, walimwacha Mungu. Katika muktadha wa Pasaka, somo hili linaashiria kuwa Kristo ndiye Hekima ya Mungu aliyekuja kuishi nasi; hivyo, kufufuka kwake kunatupa mwanga wa kuijua njia ya kweli kuelekea uzimani na kutuhimiza kushika amri zake kwa furaha kama watu waliokombolewa. Somo la saba: Eze 36:16-28. Somo hili ni hitimisho muhimu la masomo ya Agano la Kale kwa sababu linatoa ahadi ya utakaso, wongofu na mageuzi ya ndani. Mungu anawaahidi watu wake kuwanyunyizia maji safi ili kuwatakasa na uchafu wao wote, na kuwapa moyo mpya wa nyama badala ya moyo mgumu wa jiwe, huku akiweka Roho wake ndani yao ili waweze kufuata amri zake. Katika Mkesha wa Pasaka, somo hili ni ishara ya moja kwa moja ya Sakramenti ya Ubatizo na neema ya Ufufuko wa wafu, ambapo Kristo Yesu hatutakasi tu kwa nje, bali anatuumba upya kiroho na kutufanya kuwa wana wa Mungu wenye uwezo wa kuishi maisha ya utakatifu. Somo hili lahitimisha mpango wa masomo ya Agano la kale.
Kuimba Utukufu: Baada ya kusikia masomo yote saba ya Agano la Kale pamoja na sala, mishumaa ya Altareni huwashwa, Kuhani anaanzisha kuimba utukufu nasi sote tunaimba na kushangilia. Kengele zote zinagongwa, taa zote zinawashwa, maua na mapambo yote ya Kanisa sasa yanaonekana wazi. Ni nini maana ya kuimba Utukufu? Utukufu iliyoimbwa juu mbinguni wakati wa kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ikiashiria ujio wa Mwanga mkubwa ulimwenguni, Masiha na Mkombozi wetu, sasa inaimbwa tena tukishangilia utimilifu wa kazi ya ukombozi kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Baada ya utukufu husomwa somo la kwanza katika Agano Jipya, somo la Waraka. Somo la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 6:3-11. Mtume Paulo anatupa matokeo ya Fumbo kuu la Pasaka, ambalo kila mmoja tunashirikishwa kwa njia ya ubatizo wetu. Anatufundisha ni nini maana ya kuunganika na Kristo. Tumebatizwa katika mauti ya Kristo, kusudi kama vile Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo nasi sote tuishi katika upya wa uzima. Pasaka inatukumbusha kuwa na sisi pia tulikufa kwa sababu ya dhambi na tunaishi tena pamoja na Kristo Yesu. Katika Mkesha huu, Kanisa linajipatia watoto wapya, wakatekumeni ambao kwa kipindi kirefu walikua wakijiandaa kwa ajili ya Ubatizo wao. Baada ya somo la Waraka sote husimaa na Kuhani anaaza kuimba Aleluya mara tatu kwa shangwe, akiinua sauti yake kila mara kidogo zaidi na wote wanarudia kuimba. Kisha huimbwa zaburi ya 118, wakati watu huitika Aleluya. Katika shangilio hili tunamshukuru Mungu kwa kuwa fadhili zake ni za milele. Amedhihirisha hilo katika historia ya ukombozi wa taifa lake, tangu uumbaji hata ukombozi. Kisha husomwa somo la Injili ikifuatiwa na mahubiri. Somo la Injili ya Mathayo 28:1-10.
Katika somo la Injili, Mwinjili Mathayo anaelezea tukio la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka wafu ambapo wanawake waliokwenda kaburini wanaambiwa na Malaika juu ya ukweli mkuu wa Imani yetu. Kristo aliyeteswa, aliyekufa Msalabani amefufuka kama alivyosema. Somo hili la Injili Takatifu latufundisha kuwa; Kwanza: Ufufuko wa Kristo ni Ushindi wa Uzima dhidi ya Mauti. Injili inaanza kwa kuelezea tetemeko kuu la nchi na malaika akivingirisha jiwe. Hii inaashiria kuwa hakuna kizuizi cha kidunia au cha kifo kinachoweza kumzuia Mungu. Ujumbe wa malaika ni wa wazi “Hayupo hapa; kwani amefufuka“. Hii inatufundisha juu ya nguvu ya Mungu anayeweza kubadili mauti yetu na kutupa uzima na matumaini mapya ya uhai. Kwa kufufuka kwake alitutoa sote katika makaburi yetu ya dhambi, udhaifu, kukata tamaa, hofu na mashaka, na kutuwekea roho mpya kwa njia ya ubatizo wetu. Pili: Ufufuko wa Kristo unatuondolea hofu na mashaka. Malaika anawaambia wanawake, "Msiogope ninyi." Huu ni ujumbe wa faraja kwa waamini wote; Ufufuko wa Yesu unaondoa hofu ya kifo na kutupatia matumaini mapya. Tunapata nguvu kwamba, hata katika mateso na kifo bado kuna ushindi na matumaini mapya. Tatu: Ufufuko wa Kristo ni wito wa kuwa mashuhuda, kuwa mitume. Baada ya kuona kaburi wazi, wanawake wanapewa agizo la kwenda haraka kuwaambia wanafunzi wake kuwa amefufuka na atawatangulia Galilaya. Hii inatufundisha kuwa furaha ya Pasaka haipaswi kubaki ndani yetu tu, bali ni lazima ishirikishwe kwa wengine na ionekane katika maisha yetu ya kila siku. Matokeo ya Pasaka ni nguvu ya kuishi maisha mapya ya ushuhuda. Nne: Pasaka ni kukutana na Kristo Mfufuka kila siku ya maisha yetu. Wanawake walipokuwa njiani kutoa habari, Yesu mwenyewe anakutana nao na kuwasalimu. Hii inasisitiza kuwa Pasaka si hadithi ya kale tu, bali ni tukio la kukutana na Bwana aliye hai katika maisha yetu ya kila siku. Tunakutana naye kila siku ya maisha yaetu katika Neno lake, katika sala, katika sakramenti zake, na katika nafsi za wanaoteseka. Tuombe neema ya kumtambua daima Kristo kila mara anapokutana nasi. Baada ya homilia fupi hufuata sehemu ya tatu, Liturjia ya ubatizo.
Sehemu ya Tatu: Liturujia ya Ubatizo.Baada ya Liturujia ya Neno, hufuata sasa Liturujia ya Ubatizo. Ubatizo wetu ni tunda la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa kuwa ni kwa njia hiyo sisi sote tunashiriki katika Fumbo la Pasaka, tunakufa na kufufuka pamoja na Kristo kama anavyotufundisha Mtume Paulo. Sehemu hii huanza kwa kubariki Maji ya Ubatizo na kuwakaribisha wale wanaobatizwa katika Jumuiya ya waamini. Maji yana nafasi ya pekee sana katika historia ya ukombozi wetu. Kuanzia wakati wa uumbaji (Mwa 1:1), maji katika gharika ya Nuhu (Mwa 7:12), Maji katika Bahari ya Sham (Kut 14:15-15:1), na maji katika Mto Yordani (Josh 3:6). Maji yamekuwa ni ishara ya mabadiliko kutoka kifo kwenda katika uzima wa milele. Mshumaa wa Pasaka unatumbukizwa katika Kisima chenye Maji ya Ubatizo na Roho Mtakatifu anavuviwa katika maji tukimwomba Kristo mfufuka maji yale yalete uzima mpya kwa wale watakaobatizwa humo. Nasi sote tunapata nafasi ya kukiri tena Imani yetu kwa Kristo Mfufuka kwa kurudia ahadi zetu za ubatizo. Ufufuko wa Kristo ukitukumbusha kila mara juu ya ubatizo wetu. Tunakiri nia yetu ya kutorudi tena katika maisha ya kale, maisha ya dhambi na kuahidi kuendelea kuishi katika upya wa maisha. Kanisa hivyo katika usiku huu mtakatifu linajipatia Watoto wapya wanaobatizwa, wakishiriki nao katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Tunaalikwa kuwaombea ili waendelee kuwa imara na kukua katika Imani yao.
Sehemu ya Nne: Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Sehemu ya mwisho katika adhimisho la Kesha hili la Pasaka, Mama wa Mikesha yote, ni Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya shukrani kwa Mungu (Eucharistein) kwa zawadi ya ukombozi wetu uliofumbatwa katika fumbo la msalaba wa Kristo. Nasi kila tunapoadhimisha sadaka hii ya Kristo tunatoa shukrani kwa Mungu na kukumbuka ukarimu huu mkubwa wa Kristo Yesu kutoa uhai wake kwa ajili ya uzima wetu. Pasaka yatukumbusha daima kuwa ni watu wa shukrani kwa Mungu kwa zawadi hii kubwa ya ukombozi lakini pia kwa neema na baraka zake nyingi anazotujalia katika maisha yetu. Pia tunaposherekea ukarimu huu wa Kimungu nasi tunalikwa kujitoa sadaka ya kwa ajili ya wengine. Ekaristi Takatifu inatuunganisha katika umoja na ushirika. Tunapoadhimisha Ekaristi Takaifu, tunaingia katika ushirika na Kristo kwa kuwa tunakutanika pamoja kuadhimisha mauti yake mpaka ajapo, kama alivyowaamuru Mitume kufanya kila wakutanapo. Kumbe, nasi katika adhimisho hili la Ekaristi Takatifu tunaingia katika ushirika na Kristo. Yupo nasi katika Neno lake, kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu yupo nasi daima katika maumbo ya mkate na divai. Tunapompokea Kristo anakaa ndani mwetu nasi tunakaa ndani mwake, anatupa uzima wa Roho zetu. Hitimisho: Katika Mkesha huu, tumshangilie Mungu ambaye ametimiza ahadi yake ya ukombozi wa milele kwa mwanadamu ambaye hapo mwanzo alikufa kwa sababu ya dhambi. Tuombe neema ya kuipokea zawadi hii ya ukombozi ili nasi tuishi maisha mapya, kwa kufa na hatimaye kufufuka pamoja na Kristo Yesu.