Tafuta

Wanafunzi wa Emau walimtambua Kristo Mfufuka katika Neno la Kuumega Mkate. Wanafunzi wa Emau walimtambua Kristo Mfufuka katika Neno la Kuumega Mkate.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Tatu ya Pasaka: Neno la Mungu na Ekaristi

Tunaalikwa kukutana na kumtambua Kristo katika kuumega Mkate – Ekaristi Takatifu, baada ya kupata ufafanuzi na maelezo yanayomhusu Yeye katika Neno la Mungu. Tendo hili linatupa furaha kubwa isiyo na kifani kwani “Ekaristi ndio jumla na muhtasari wa imani yetu: Namna yetu ya kufikiri hulingana na Ekaristi, na Ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yetu ya kufikiri” (KKK 1327.) Kristo Yesu ni utimilifu wa Torati na Unabii, kiini cha maisha mapya ya imani.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 3 ya Pasaka Mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Tunaalikwa kukutana na kumtambua Kristo katika kuumega Mkate – Ekaristi Takatifu, baada ya kupata ufafanuzi na maelezo yanayomhusu Yeye katika Neno la Mungu. Tendo hili linatupa furaha kubwa isiyo na kifani kwani “Ekaristi ndio jumla na muhtasari wa imani yetu: Namna yetu ya kufikiri hulingana na Ekaristi, na Ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yetu ya kufikiri” (KKK 1327). Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Mpigieni Mungu kelele za shangwe nchi yote, imbeni utukufu wa jina lake. Tukuzeni sifa zake, aleluya” (Zab. 66:1-2). Ni kwa tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, watu wako na waone furaha siku zote kwa ajili ya kutiwa nguvu mpya roho zao. Kwa vile sasa wanafurahi kwa kurudishiwa ile heshima ya kuwa wana wako, waitazamie ile siku ya kufufuka kwao, wakitumaini kupewa pongezi.” Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 15 hadi 18 Aprili 2026 anatembelea nchini Cameroon kama mjumbe na shuhuda wa matumaini, hasa kwa vijana wa kizazi kipya; ili kuragibisha na kukoleza mchakato wa haki, amani na upatanisho, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Cameroon kuendelea kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na hali ya kuheshimiana. Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Cameroon inanogeshwa na kauli mbiu: “Umoja Katika Kristo.” Hii ni kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika kauli mbiu yake ya Kiaskofu “In Illo unum uno” Yaani: “Ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa mintarafu Zaburi ya 127. Baba Mtakatifu Leo XIV analitaka Kanisa kuwa ni chombo cha matumaini, haki, amani na upatanisho.

Wanafunzi wake walimtambua katika Neno na Kuumega Mkate
Wanafunzi wake walimtambua katika Neno na Kuumega Mkate   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2:14, 22-28). Ni mafundisho na ushuhuda wa mtume Petro juu ya fumbo la Pasaka, mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo – kuwa aliteswa, akasulibiwa msalabani, akafa na akazikwa, Mungu akamfufua siku ya tatu kutoka wafu, ishara ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Hivyo Yeye amekuwa tumaini la ufufuko wetu katika heri ya mbinguni. Kristo Yesu alikuwa mwanadamu kama sisi, isipokuwa hakutenda dhambi. Ubinadamu wake ulijidhihirisha katika mateso na kifo chake. Yeye ni mwana wa Mungu na ni Mungu; miujiza, ishara na maajabu aliyofanya yanashuhudia u-mungu. Ni kwa hila tu, viongozi wa wayahudi walimkataa Yeye na ujumbe wake, wakamtoa kwa Warumi asulibiwe. Pilato alitoa hukumu ya mwisho. Lakini ni wayahudi ndio waliodai asulubiwe. Ndiyo maana Yesu mwenyewe alimwambia Pilato; “Yule aliyenitoa kwako ana dhambi kubwa zaidi” (Yn 19:11). Lakini, wote wanaoamini katika mateso, kifo na ufufuko wake, Mungu atawapatia uzima wa milele mbinguni pamoja naye. Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe. Nimemwambia Bwana, ndiwe Bwana wangu; Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu. Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, naam, mtima wangu umenifundisha usiku. Nimemweka Bwana mbele yangu daima, kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, nao utukufu wangu unashangilia, naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini. Maana hutaiacha kuzimu nafsi yangu, wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. Utanijulisha njia ya uzima; mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume, mna mema ya milele” (Zab. 16: 1-2, 5, 7-11.)

Utambulisho wa Kristo Mfufuka: Neno, Sakramenti, Sala na Matendo
Utambulisho wa Kristo Mfufuka: Neno, Sakramenti, Sala na Matendo   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 1:17-21). Ni ushuhuda wake kuwa Mungu ni Baba yetu mwema na mwenye haki, alimtuma Mwana wake wa pekee kuja kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Kwa kuwa tumekombolewa kwa damu ya thamani, damu ya Kristo, yatupasa kuishi kitakatifu tukiyatazama yaliyo juu Kristo aliko, ili nasi tuweze kufika aliko yeye Mkombozi wetu. Mtume Petro, akitumia lugha ya kisheria ya Warumi ya kuwekwa huru mtumwa kwa yeye kujilipia au kulipiwa fedha, kitu au vitu vya thamani kama fidia, anasema kuwa sote tulikuwa watumwa, Shetani alikuwa Bwana wetu na dhambi minyonyoro iliyotufunga. Na kwa kuwa hatukuwa na kitu chochote chenye thamani ya kuwa fadia yetu ili tuachwe huru, tumewekwa huru kwa fidia ya damu azizi ya Yesu, na kufanywa watoto wa Mungu. Hivyo tujiepushe na mambo yanayoweza kuturudisha katika utumwa wa shetani. Tuizingatie haki na kutenda mema kwa kumwilisha ndani mwetu matunda ya roho ambayo ni; upendo, furaha, amani, mshikamamo, uvumilivu, unyenyekevu, utii na uchaji kwa Mungu (Gal. 5:22-23), na kuyatupilia mbali matendo ya mwili ambayo ni; chuki, fitina, ufisadi, ibada ya sanamu, uadui, ugomvi, kijicho, hasira, ubinafsi, utengano, mafarakano, wivu, ulevi, ulafi, uzinzi na uasherati (Gal. 5:19-20).

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 24:13-35). Ni simulizi la Yesu Mfufuka kuwatokea wafuasi wawili wa Emau, nao kumtambua katika kuumega mkate. Ilikuwaje? Ilikuwa hivi; Kifo cha Kristo kiliwafanya wafuasia wake wapoteze imani juu yake, kwa sababu walitegemea awe ni Masiha, mfalme mwenye nguvu na uweza wote na asingeweza kufa kifo cha aibu msalabani. Baada ya kifo chake na kusikia habari za kufufuka kwake nao hawakuami, wakaanza kutawanyika kurudi vijijini kwao. Katika safari yao Yesu aliwatokea na kuambatana nao, kisha kuwauliza juu ya walichokuwa wanajadiliana. Nao wanamweleza kinaganaga habari zake Yesu aliyefundisha na kutenda miujiza mingi, jinsi alivyotiwa mikononi mwa Mayahudi na kuuawa msalabani, nao walimshangaa kuona kuwa hakufahamu kilichokuwa kinaendelea. Nao hawakutambua kuwa waliyekuwa wanamweleza ndiye Yeye Yesu Mfufuka. Baada ya wao kumueleza Yesu kile kinachomhusu kadiri ya uelewa wa kibinadamu. Yesu mwenyewe aliwaeleza tukio lile lile kadiri ya mpango wa Mungu jinsi lilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu. Na walipofika mwisho wa safari yao wakamsihi akae pamoja nao kwa kuwa kumekuchwa. Jioni ile walimkaribisha chakula bila kujua Yeye ndiye Kristo Mfufuka. Na wakati wa kula, Kristo Mfufuka alirudia tendo alilolifanya siku ya Alhamisi Kuu katika mlo wa Kipasaka, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, na akawapa. Ndipo macho yao yalipofumbuliwa, wakamtambua, naye akatoweka mara. Hili tukio linatufundisha kuwa mkate alioubariki na kuumega, uligeuka kuwa Ekaristi Takatifu, Mwili wake halisi, ukawakilisha uwepo wake halisi, naye asingeweza kuwepo katika hali zote mbili, umbo la mwili wake wa kibinadamu na katika Ekaristi Takatifu kwa wakati mmoja, hivyo alitoweka katika uhali wa mwili wake halisi, akabaki nao katika hali ya mkate, Ekaristi takatifu.

Kristo Mfufuka ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini
Kristo Mfufuka ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini

Tukio hili ni ushuhuda wa wazi wa kinachotokea katika kila adhimisho la Misa Takatifu. Tukio hili lilianza kwa liturujia ya Neno na kisha kuumega mkate, Ekaristi Takatifu, tukio linalowafanya wafuasi wawili wa Emau waweze kumtambua Kristo Mfufuka. Hivyo, liturujia ya Ekaristi, lazima itanguliwe na liturujia ya Neno ambayo ni maandalizi kwa ajili ya Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Hivyo tukitaka kushiriki vyema na kikamilifu maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni lazima tushiriki vizuri kwanza liturujia ya Neno. Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 1346-1347 inafafanua hivi hili fundisho; “Liturujia ya Ekaristi huendelea kadiri ya muundo huo wa msingi ambao umehifadhiwa karne zote...katika mambo makuu mawili yanayounda umoja wa msingi wa kusanyiko: liturujia ya Neno, pamoja na masomo, homilia, na maombi ya wote; liturujia ya Ekaristi, pamoja na kuleta mkate na divai, kushukuru - konsekrasio na komunyo. Hivyo, liturujia ya Neno na liturujia ya Ekaristi huunda umoja zikifanya ibada moja tu. Kwa kweli meza iliyoandaliwa kwa ajili yetu katika Ekaristi kwa upande mmoja ni ile ya Neno la Mungu na kwa upande mwingine ni ile ya Mwili wa Bwana. Hili ni tendo lile lile la mlo wa Pasaka wa Yesu Mfufuka pamoja na wafuasi wake ambapo walipokuwa wakitembea aliwafafanulia Maandiko, na akiketi pamoja nao mezani alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.”

Kristo Mfufuka ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo
Kristo Mfufuka ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo   (@Vatican Media)

Mwaliko kwetu ni kuwa kunapotokea shida au matatizo katika familia, ndani ya kanisa katika ngazi mbali mbali: Jimbo, parokia, kigango, jumuiya, shirika au taasisi yoyote ile, wapo wanaojitenga na kuanza kuwanyooshea wengine vidole. Hatupaswi kujitenga na jumuiya zetu wakati wa matatizo na majaribu bali kuungana pamoja na kutafuta suluhu kwa pamoja. Tushirikishane pale magumu yanapotukabili ili kumruhusu Yesu kuwa pamoja nasi atusaidie kufanya mang’amuzi sahihi na kupata suluhisho linalojenga. Kwani Yeye anasema; “wakutanapo wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo katikati yao”. Tukifanya hivyo tutastahilishwa kuingia katika furaha ya milele mbinguni. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana tunakuomba upokee dhabihu za Kanisa lako linalofanya shangwe. Na kama ulivyolifanya lifurahi sana sasa, ulijalie pia furaha ya milele”. Na katika sala baada ya Komunyo anasali; “Ee Bwana, tunakuomba utuangalie kwa wema sisi taifa lako. Utujalie tufufuke na miili mitukufu, sisi ambao umependa kutufanya wapya kwa mafumbo haya ya milele.” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D3 Pasaka

 

17 Aprili 2026, 12:20