Tafakari Dominika ya Tatu ya Pasaka Mwaka A: Jinsi ya Kumtambua Kristo Mfufuka!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa inawazamisha waamini katika hija ya kiroho ya wanafunzi wa Emau. Mtume Petro aliyekuwa mwoga kupindukia, leo anatoa ushuhuda wa Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Hii ni kiri ya imani kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo Yesu; na ni mwaliko kwa waamini kuambata na kuchuchumilia utakatifu wa maisha baada ya kukomboleo na Kristo Yesu kutoka katika minyororo ya Ibilisi, Shetani; kwa kuzingatia haki, kutenda mema sanjari na kujitahidi kumwilisha matunda ya Roho Mtakatifu katika uhalisia wa maisha ya Mkristo! Rej. Gal 5: 19-20. Kristo Yesu ni utimilifu wa Torati na Unabii, mwaliko kwa waamini kuendelea kumtambua Kristo Mfufuka katika: Neno, Sakramenti, Sala na katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, tayari kumtangaza na kumshuhudia, kama walivyofanya wale Wafuasi wa Emau. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 15 hadi 18 Aprili 2026 anatembelea nchini Cameroon kama mjumbe na shuhuda wa matumaini, hasa kwa vijana wa kizazi kipya; ili kuragibisha na kukoleza mchakato wa haki, amani na upatanisho, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Cameroon kuendelea kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na hali ya kuheshimiana. Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Cameroon inanogeshwa na kauli mbiu: “Umoja Katika Kristo.” Hii ni kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika kauli mbiu yake ya Kiaskofu “In Illo unum uno” Yaani: “Ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa mintarafu Zaburi ya 127. Baba Mtakatifu Leo XIV analitaka Kanisa kuwa ni chombo cha matumaini, haki, amani na upatanisho.
Mwinjili Luka 24:13-35, anamwonesha Kristo Mfufuka anayejitokeza na kuandamana na wafuasi wa Emau. Kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, Wafuasi wa Emau walikuwa ni kati ya wafuasi 70 waliotumwa na Kristo Yesu kwenda kuhubiri. Ni wafuasi waliochoka na kujikatia tamaa baada ya kushuhudia Kashfa ya Fumbo la Msalaba yaani: Mateso na Kifo cha Kristo juu ya Msalaba. Hili ni tukio ambalo lilizika imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo Yesu, Masiha na Mkombo wa Ulimwengu. Huyu ni Masiha ambaye hakujibu matarajio na wala hakuwa na vigezo vya kuwa ni Masiha. Mara Kristo Mfufuka anajitokeza kati yao na kuanza kuandamana nao katika safari ya kurejea tena Emau. Njiani anawafafanulia Maandiko Matakatifu kama utimilifu wa Torati ya Musa na Unabii juu ya mateso na kifo chake cha Msalaba. Na hatimaye, anatambulika kwao katika “Kuumega Mkate” yaani wafuasi wa Kristo Yesu wanamtambua katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kifo, Ufufuko na Maisha; ni mambo ambayo wafuasi wa Emau walikuwa wakijadiliana njiani baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu wao. Ni watu waliokuwa wamechanganyikiwa kutokana na Kashfa na upuuzi wa Msalaba, uliozika: Imani na matumaini yao yote. Wanafunzi hawa walishindwa kujenga imani yao kwa Kristo Yesu ambaye amateswa, amekufa na kushindwa vibaya, kiasi kwamba amezikwa pamoja na matumaini yao yote! Yesu, Mwalimu na Mkombozi aliyewafufua wafu na kuwaponya wagonjwa akashindwa kujiokoa mwenyewe hadi kuishia kwenye Kashfa ya Msalaba. Walishindwa kuamini ilikuaje Mwenyezi Mungu akashindwa kumwokoa Yesu kutoka kwenye ukatili mkubwa wa kifo. Kumbe kwao, Msalaba wa Kristo ulikuwa ni Msalaba wa mawazo yao kuhusu Mungu; Kifo cha Kristo kilikuwa ni kifo cha yule waliyedhani pengine ni Mungu. Wanafunzi hawa ndio waliokufa na kuzikwa kaburini kutokana na kushindwa kwao kulifahamu Fumbo la Msalaba.
Wafuasi wa Emau kwa kukutana na Kristo Mfufuka wanapata mabadiliko makubwa katika maisha, wito na utume wao. Lakini ikumbukwe kwamba, Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu si imani iliyozaliwa ndani ya Kanisa, lakini Kanisa limezaliwa katika imani kwa Kristo Mfufuka anayeendelea kuwafunda wafuasi wake kumwamini hata kama bado hawajamwona. Kanisa halina budi kuendelea kumtambua, kumwamini na kumsadiki Kristo Mfufuka anayeliuhisha kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kama walivyofanya wanafunzi wa Emau, kwa kujikita katika Ibada na uchaji kwa Mungu; Upendo na mshikamano kwa jirani; hii ni imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwani Mwenyezi Mungu anaangalia moyo wa mtu na kukataa unafiki!
Fumbo la Ekaristi Takatifu ni: Sakramenti ya Sadaka, Shukrani, Kumbukumbu na uwepo. Ni tendo la shukrani na masifu kwa Baba wa milele. Hii ni kumbukumbu ya Sadaka ya Kristo Yesu na ya mwili wake. Uwepo wa Kristo Yesu unajidhihirisha kwa nguvu ya Neno lake na Roho Mtakatifu. Imani ya kweli ni ile inayomwilishwa katika matendo ya huruma na upendo kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wengine bila ubaguzi. Imani ya kweli inawasaidia waamini kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu na wala si kama adui wa kufutiliwa mbali kutoka katika uso wa dunia. Kwa hakika, imani ya kweli inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea: Utu, heshima pamoja na haki msingi za binadamu na kwamba, imani inakua na kuchanua katika unyenyekevu. Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo, tayari kurejea tena katika maisha kwa furaha, ujasiri na imani thabiti, bila kusita kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao, ili aweze kuwakirimia mwelekeo mpya wa maisha. Upendo unaomwilishwa katika maisha ni amana ya mwamini kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mara ngapi waamini wanakatishwa tamaa kwa kukataa kuamini kwamba, ukuu na nguvu ya Mungu havijioneshi kwa nguvu, vitisho na mamlaka, bali katika upendo, msamaha na maisha tele! Wanafunzi walimtambua Yesu kwa kuumega mkate, katika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, changamoto na mwaliko wa kuvunjilia mbali mambo yote yanayofisha macho yao na hivyo kuufanya moyo wao kushindwa kuvunjilia mbali mawazo mgando na maamuzi mbele, kwa hakika watashindwa kuufahamu Uso wa Mungu! Katika usiku wa giza nene, hali ya kuchanganyikiwa na kukatisha tamaa, Kristo Yesu anajitokeza na kuanza kuandamana nao, ili waweze kumgundua kwamba yeye ni njia, ukweli na uzima.
Yesu Mfufuka anatumia fursa hii kugeuza hali yao ya kukata tamaa kuwa ni chemchemi ya maisha na yale matumaini ya kibinadamu yanapotoweka kama ndoto ya mchana, matumaini ya Kimungu yanayochukua nafasi ya kuanza kung’aa, kwani kile ambacho hakiwezekani kwa binadamu, kinawezekana mbele ya Mungu. Pale mwanadamu anapogusa sakafu ya kushindwa na udhaifu wake ndipo pale anapoanza kuzama katika mawazo ya kufikiria na kudhani kwamba yeye ni bora kuliko wengine na anaweza kujitegemea na kujitosheleza mwenyewe; na kwamba, ni sehemu muhimu sana ya ulimwengu, hapo ndipo Mwenyezi Mungu anapomnyooshea mkono wake kiasi cha kugeuza usiku wa giza kuwa ni mapambazuko angavu na cheche za furaha zinaanza kuchanua, kifo chake kinageuka kuwa ni ufufuko na kuanza kuchapa miguu tena kurejea Yerusalemu, yaani kurejea tena katika chemchemi ya maisha na kutambua ushindi wa Msalaba. Ushuhuda wa Mitume wa Kristo Yesu, kutoka kutokuamini kwao hadi kuamini. Mitume walipoteza kabisa matumaini, wengine wakaanza kurudi tena kuendelea kufanya kazi zao waliozokua wanafanya kabla ya kuitwa na Kristo Yesu; anapowatokea, wanaondolewa hofu na wanajawa na furaha kubwa. Wanafunzi wa Emau walisafiri na Yesu lakini hawakumtambua. Walimtambua katika kuumega mkate na mara baada ya kumtambua wanapata nguvu mpya na wanaondoka mara kurejea Yerusalemu, hofu na mashaka vikaondoka nao wakaamini tena.
Imani ya Mitume hawa ndio imani yetu sisi leo hii ya kwamba, Kristo ni mzima, amefufuka kutoka wafu, wajibu wetu ni kumwamini, kufurahi na kuwashirikisha wengine furaha hii ya Injili. Wafuasi wa Emau baada ya kukutana, kuzungumza na kutembea na Yesu Kristo Mfufuka, wanarejea wakiwa wamesheheni furaha, imani na matumaini kedekede, tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka aliyewafufua kutoka katika makaburi yao ya kutoamini na kujikatia tamaa. Kwa kukutana na Kristo Mfufuka wakapata nafasi ya kufafanuliwa utimilifu wa Maandiko Matakatifu, Sheria na Unabii na hatimaye, kufahamu kwa kina na mapana maana ya Kashfa ya Fumbo la Msalaba. Kwa mang’amuzi ya Fumbo la Msalaba wakaweza kufikia ukweli wa Ufufuko kiini cha maisha na matumaini mapya. Ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu kuna haja kwa waamini kusubilisha mawazo yao yanayomwonesha mungu kuwa ni muweza wa yote na mwenye nguvu!