Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu ndiye Mchungaji mwema, yuko tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kondoo wake kama kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu ndiye Mchungaji mwema, yuko tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kondoo wake kama kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya 63 ya Kuombea Miito

Ujumbe wa Papa Leo XIV wa Siku ya 63 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa kwa Mwaka 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Utambuzi wa Zawadi ya Bure ya Mungu Inayochanua Ndani Kabisa ya Mioyo Yetu. Dominika ya Nne ya Kipindi Cha Pasaka inajulikana kama "Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema" kwa sababu yuko tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kondoo wake, kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 4 ya Pasaka mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Ni “Dominika ya Mchungaji Mwema”. Yesu ndiye Mchungaji mwema, nasi kondoo wa malisho yake. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV wa Siku ya 63 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa kwa Mwaka 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: "Utambuzi wa Zawadi ya Bure ya Mungu Inayochanua Ndani Kabisa ya Mioyo Yetu. Dominika ya Nne ya Kipindi Cha Pasaka inajulikana kama "Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema." Dominika tarehe 26 Aprili 2026 Papa Leo XIV anatoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 8 kutoka Jimbo Kuu la Roma. Hii ni Siku ya kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu ndiye Mchungaji mwema, yuko tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kondoo wake kama kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Kristo Mchungaji mwema anawasogeza kondoo wake ili kuwa karibu naye, ili hatimaye kuutambua uzuri na wema wake usiokuwa na mipaka, ili hatimaye kuweza kushiriki katika maisha na utume wake, ili kuakisi uzuri wake na kwamba, maisha ya ndani ni mahali muafaka kwa kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu katika nafasi mbalimbali kutengeneza mazingira bora zaidi yanayowezesha zawadi ya Mungu kukumbatiwa, kustawishwa, kulindwa na kuusindikizwa, ili iweze kuzaa matunda mengi. Ni katika tumaini hili Zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Nchi imejaa fadhili za Bwana. Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, aleluya” (Zab. 33:5-6). Na mama Kanisa Katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuelekeze kwenye furaha za mbinguni, kusudi sisi kondoo wako wanyonge, tufike huko alikotoka mchungaji wetu shujaa.” Ni siku ya kuombea Miito mitakatifu ndani ya Kanisa, tukiitikia mwito wa Yesu alivyoagiza akisema; “Mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke wafanyakazi katika shamba lake” (Mt 9:37.)

Kristo Yesu Ndiye Mchungaji Mwema
Kristo Yesu Ndiye Mchungaji Mwema   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha matendo ya Mitume (Mdo. 2: 14a, 36-41). Ni hotuba ya Mtume Petro siku ya Pentekoste ya kwanza lilipozaliwa Kanisa la kimisionari. Mtume Petro anawataka wayahudi kutambua ubaya wa kosa lao la kumtoa Yesu kwa Pilato ili auawe, ambaye amefufuka kutoka wafu. Kisha anawaonya wakate shauri la kumsadiki Yeye waliyemsulibisha; watubu na kupokea ubatizo kwa jina lake, ili wapate ondoleo la dhambi na kumpokea Roho Mtakatifu. Nasi kwa Sakramenti ya Ubatizo tumeondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote, na kumpokea Roho Mtakatifu, na kufanywa kuwa Makuhani, Wafalme, na Manabii. Kama Makuhani tunatupasa kumtolea Mungu sadaka na kuwatakatifuza watu wengine kwa sala zetu. Kama wafalme tumeshirikishwa katika utawala wa Mungu. Hivyo tunapaswa kuyatalawa maisha yetu kwa kuishi vyema na sio kutawaliwa na dhambi. Na kama manabii tunatupasa kumuhubiri Kristo kuwa Bwana na mfalme wa maisha yetu. Yeye ndiye kiongozi na mchungaji wa maisha yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu.  Ni katika tumaini hili Zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza katika njia za haki, kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata, siku zote maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele” (Zab. 23:1-6).

Kristo Yesu anatoa maisha yake ili kumkomboa mwanadamu kutoka dhambini
Kristo Yesu anatoa maisha yake ili kumkomboa mwanadamu kutoka dhambini   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 2:20b-25). Ni mausia kwa wakristo wa kipindi kile kuwa kutubu na kubatizwa tu haitoshi kwa uzima wa milele, wanapaswa kutenda mema na kuvumilia mateso,  kama Kristo Yesu alivyoteseka kwa wokovu wa watu wote. Nasi kwa ubatizo tulichagua kumfuata Kristo Bwana na Mwokozi wetu. Hivyo daima tubaki imara katika imani yetu hata katika mateso na taabu, tuvumilie, tukimtegemea Mungu. Mateso yasiwe chanzo cha kutufanya tutende dhambi. Bwana wetu Yesu Kristo ni kielelezo chetu ambaye pamoja na kwamba hakuwa na dhambi, alivumilia mateso yote ili aweze kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi, tulipokuwa tumepotea kama kondoo. Lakini kwa ubatizo tumeacha dhambi na kumrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.Tukumbuke kuwa hata katika mateso Yeye yupo pamoja nasi akituimarisha katika udhaifu wetu wa kibinadamu, tuweze kuyastahimili na kuyashinda mabaya.

Ni Siku ya 63 ya Kuombea Miito Ndani ya Kanisa
Ni Siku ya 63 ya Kuombea Miito Ndani ya Kanisa   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 10:1-10). Ni mafundisho ya Yesu kujifananisha na mlango wa zizi la kondoo. Sisi, tukiwa kondoo katika zizi lake, yatupasa kuisikiliza sauti yake na kumfuata Yeye ambaye ni njia, ukweli na uzima. Yeye ni kila kitu kwetu; ni mlango, ni mchungaji, ni njia, ni malisho, ni mlinzi na ni uzima wetu. Yeye anamfahamu kila aliye wake kwa jina lake, anajua mahitaji yake, madhaifu yake, magonjwa yake, mahangaiko yake, majeraha yake na tiba anayohitaji. Neno lake na Sakramenti, hasa Ekaristi Takatifu na Kitubio ndiyo malisho bora yanayotupa nguvu ya kutuwezesha kusonga mbele katika safari ya kuelekea nchi ya ahadi – Yerusalemu Mpya – Mbinguni, kwenye uzima wa milele. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha hivi; “Padre – Kristo Mwingine – anapoadhimisha sakramenti ya kitubio, hutekeleza huduma ya mchungaji mwema, anayetafuta kondoo aliyepotea, huduma ya Msamaria mwema, anayeponya majeraha, huduma ya Baba anayemngojea Mwana mpotevu na kumpokea anaporudi, na huduma ya hakimu mwenye haki asiyeangalia tofauti ya watu, na ambaye hukumu yake kwa pamoja ni ya haki na ya huruma. Kwa jumla padre ni ishara na chombo cha mapendo ya Mungu yenye huruma kwa mkosefu” (KKK 1465). Nayo Ekaristi Takatifu tunayopokea inatujengea umoja wa ndani na Kristo Yesu, inatupa uzima wa kimungu ndani mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu, ambao huhifadhi, hukuza na hufanya upya uzima wa neema itokanayo na ubatizo (KKK 1391-1392).

Utambuzi wa zawadi ya bure ya Mungu inayochanua ndani kabisa mioyo yetu
Utambuzi wa zawadi ya bure ya Mungu inayochanua ndani kabisa mioyo yetu   (@Vatican Media)

Kama ilivyokuwa katika Agano la Kale, viongozi wa kiserikali na kidini katika Israeli walichukuliwa kama wachungaji, yaani watu waliopewa mamlaka na Mungu ya kuwaongoza watu wake. Lakini wapo waliotafuta maslahi yao binafsi na kusababisha mateso na mahangaiko kwa watu wao. Mungu kwa kinywa cha Nabii Ezekieli aliahidi kuwanyang’anya mamlaka hayo na Yeye mwenyewe kuwa mchungaji wa watu wake (Ezekieli 34). Hawa Yesu anawaita wezi na wanyang’anyi, walizoea kuiba, kuua na kuharibu. Hivyo hatuna budi kujihadhari nao kwa kujikabidhi kwa Kristo Mchungaji wetu mwema. Ni katika tumaini katika sala baada ya komunio anasali hivi; “Ee Mchungaji mwema, ututazame kwa mapendo sisi kundi lako. Upende kutuweka katika malisho ya milele sisi kondoo wako uliotukomboa kwa damu takatifu ya Mwanao.” Mama Kanisa kwa upendo wake kwetu ametupatia sala ya “kutolea Moyo Mtakatifu wa Yesu binadamu wote” ili kwayo tujiweka chini ya Yesu Kristo Mchungaji wetu mwema. Basi na tuhimishe tafakari yetu kwa kujikabidhi kwa Kristo Yesu Mchungaji wetu tukisali;  “Ee Yesu mwema mno, Mkombozi wa binadamu wote, ututazame sisi tuliojinyekesha mbele ya altare yako. Sisi ni mali yako, twataka kuwa mali  yako; na tupate kuungana zaidi nawe. Kila mmoja wetu anajitoa leo kwa hiari yake kwa moyo wako mtakatifu. Wako watu wengi wasiokuja bado; wako na watu wengi waliokataa amri zako  wakakudharau. Ee Yesu mwema, uwahurumie  watu hao wote, uwavutie wote  katika Moyo wako Mtakatifu.

Siku ya 63 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa
Siku ya 63 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa   (@Vatican Media)

Ee Bwana, uwe mfalme, siyo tu wa waamini wasiojitenga  hata mara moja nawe, bali uwe pia  Mfalme wa wana  wapotevu  waliokuacha: uwafanyizie hao wote, wapate kurudi upesi  nyumbani kwa Baba, wasipotee kwa umaskini na njaa. Uwe mfalme wa watu waliodanganywa  kwa uwongo, au waliotengwa kwa fitina; uwarudishe katika bandari ya ukweli  na katika umoja wa imani, lipate upesi kuwa kundi  moja na mchunga mmoja. Ee Bwana, ulijalie Kanisa lako uhuru kamili pamoja na usalama; uyajalie mataifa yote mapatano na amani: ufanye pande zote za dunia, isikilike sauti  hii moja: Usifiwe Moyo wa Yesu, uliotuletea  wokovu: upate heshima na utukufu, milele na milele. Amina.” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Yesu Mchungaji Mwema

 

25 Aprili 2026, 08:56