Tafakari Dominika ya Tatu ya Pasaka Mwaka A: Ufafanuzi wa Neno & Ekaristi Takatifu
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, ni Dominika ya 3 ya Pasaka mwaka A wa Kanisa. Kristo Mfufuka anaendelea kujidhihirisha kwa wafuasi wake kwa nyakati mbalimbali. Katika Dominika ya Tatu ya Pasaka mwaka A wa Kanisa, Kristo anajidhihisha kwa wanafunzi wawili wa Emau. Ni wafuasi waliokuwa wamekata tamaa, waliojawa na huzuni na hofu kufuatia Mateso na kifo cha Yesu. Wakiwa njiani, wakitokea Yerusalemu, Kristo Mfufuka anaingia katikati ya safari yao, ijapokuwa hawakuweza kumtambua. Kisha “Anawafunulia Maandiko Matakatifu nao Wanamtambua katika Kuumega Mkate.” Kutaniko lao na Kristo haliwaachi vile vile walivyokuwa. Wanaondoka mara usiku ule ule, wakiwa na furaha, nguvu, ari na matumaini mapya kurejea Yerusalemu. Wanafunzi hawa ndio sisi katika safari yetu ya Maisha. Tunapata nafasi ya kukutana na Kristo katika Misa Takatifu. Anajifunua kwetu katika Neno lake na kutuimarisha katika Ekaristi Takatifu. Tukishakutana na Kristo, hatuwezi kubaki palepale. Ni lazima nasi turudi Yerusalemu kwa ujasiri, tukitoka kwenye upweke, mashaka, huzuni na hofu yetu ili kuwatangazia wengine kuwa Bwana amefufuka kweli! Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 15 hadi 18 Aprili 2026 anatembelea nchini Cameroon kama mjumbe na shuhuda wa matumaini, hasa kwa vijana wa kizazi kipya; ili kuragibisha na kukoleza mchakato wa haki, amani na upatanisho, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Cameroon kuendelea kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na hali ya kuheshimiana. Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Cameroon inanogeshwa na kauli mbiu: “Umoja Katika Kristo.” Hii ni kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika kauli mbiu yake ya Kiaskofu “In Illo unum uno” Yaani: “Ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa mintarafu Zaburi ya 127. Baba Mtakatifu Leo XIV analitaka Kanisa kuwa ni chombo cha matumaini, haki, amani na upatanisho.
Somo la Injili Ni Injili Kama Ilivyoandikwa na Luka 24:13-35. Katika Dominika hii ya tatu ya Kipindi cha Pasaka mwaka A wa Kanisa, Mama Kanisa anatupa nafasi ya kutafakari kutoka kwa Mwinjili Luka juu ya simulizi la wanafunzi wawili wa Emau. Simulizi hili tulilisikia pia katika siku ya Jumatatu ya Pasaka (Luka 24:13-35). Katika simulizi hili, Bwana wetu Yesu Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi hawa wawili waliokuwa safarini kutoka Yerusalemu kuelekea Emaus baada ya mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Simulizi hili kimsingi tunalipata tu kutoka kwa Mwinjili Luka pekee, ingawa Mwinjili Marko pia anataja kwa kifupi sana tukio linalofanana na hilo katika sehemu ya mwisho ya Injili yake, inayoitwa “Nyongeza ya Marko/ The Markan Long Ending” (Mk 16:12-13). Hapo tunaambiwa kuwa kuwa, “Yesu aliwatokea watu wawili katika namna nyingine walipokuwa wakitembea kwenda shamba.” Lakini swali msingi tunaweza kujiuliza ni kwamba, kwa nini tunapata nafasi ya kutafakari sehemu hii ya Injili Takatifu katika Dominika hii ya tatu ya Pasaka? Katika somo hili la Injili Takatifu ningependa tutafakari pamoja mafundisho manne ambayo yatatusaidia kuelewa ujumbe mzima ambao Mama Kanisa anatupatia katika Dominika hii ya tatu ya Pasaka mwaka A kama ifuatavyo: Fundisho la Kwanza: Tunawaona wanafunzi wawili, wakiwa njiani na waliokata tamaa, ndio mimi na wewe katika safari yetu ya kiroho, safari ya maisha. Somo la Injili Takatifu linaanza kwa kutueleza kuwa, wawili miongoni mwa wafuasi wa Kristo walikuwa njiani wakienda katika kijiji kimoja jina lake Emau. Safari hii tunaweza kuiona kama safari tu ya kawaida lakini Mwinjili Luka ana mengi sana ya kutufundisha katika simulizi hili. Wanafunzi hawa wawili waliondoka kutoka Yerusalemu ambapo ndipo Kristo alipoteswa na kufa Msalabani, wakielekea Kijiji cha Emau umbali takribani maili saba, wakiwa na hofu, mashaka, huzuni, na hauku wakiwa wamekata tamaa kabisa na kupoteza matumaini. Kwa nini walikua na huzuni, kwa nini walikua na hofu, mashaka na kukata tamaa? Tunaambiwa wafuasi hawa (Mmoja aitwaye Kleopa na mwingine hatajwi kwa jina) walikuwa na Matumaini makubwa sana kwa Kristo, walimtegemea kama Masiya, Mwokozi atakayewakomboa Israeli, sasa alikwisha hukumiwa, akateswa na kufa msalabani. Lakini huzuni kubwa zaidi ni kwamba hata kaburini hakuwamo tena kama walivyopewa habari na wale wanawake kadha wa kadha waliokwenda kaburini. Si kwa bahati mbaya Mwinjili Luka anataja hapa umbali wa safari (yaani maili 7, umbali takribani kilometa 11 hivi), na hizi sehemu mbili, yaani Yerusalemu na Emau, kama tutakavyozijadili hapo baadaye kidogo.
Mwanafunzi huyu wa pili ni nani? Ndugu mpendwa, Mwinjili Luka anamtaja mwanafunzi mmoja kwa jina katika Safari hii aitwaye Kleopa, lakini mwanafunzi mwingine hatajwi kwa jina. Hii inatukumbusha kuwa, safari hii ya wanafunzi ya Emau ndiyo safari yetu ya kila siku ya kiroho mimi na wewe. Mwinjili Luka kwa kutokumtaja jina mwanafunzi wa pili, anatualika kila msomaji wa Neno la Mungu kuchukua nafasi hiyo ya mwanafunzi wa pili wa Yesu. Wanaondoka Yerusalemu, tunaweza kusema, waliukimbia mji wa Yerusalemu. Yerusalemu ulikuwa mji wa Mungu, ulikua mji wa Ahadi, ilikuwa jumuiya ya waamini, na ndipo pia wanafunzi wengine walipobaki, ingawa nao pia walijifungia ndani kwa hofu. Nini maana ya safari hii ya Yerusalemu kwenda Emaus? Kuondoka kwa Wanafunzi hawa kutoka Yerusalemu ni ishara kwamba walitoka ilipokuwa jumuiya ya waamini, lilipokuwapo Hekalu mahali patakatifu pa sala, wanaupa kisogo Mji Mtakatifu wa Mungu, mji wa Ahadi, wanakimbia kutoka alikotesekea na kufa Bwana wao, wanakimbia kutoka jua lilipochomozea na wanakimbilia jua lilipozamia huko kijijini Emaus, kutoka kwenye mwanga na nuru kwenda kwenye giza. Ndio maana Mwinjili Luka hapa anaitaja Yerusalemu na Emau ingawa maana nyingine muhimu zaidi ya jina Emaus tutaiona pia hapo baadaye kidogo. Ndugu mpendwa, kama nilivyotangulia kusema, Injili hii inatuhusu kabisa mimi na wewe.
Kuna nyakati katika safari yetu ya kiroho tunakuwa kama hawa wafuasi wawili wa Emau. Wanafunzi hawa walisema “Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayeikomboa Israeli." Kumbe wao walitaka na walitegemea kwa hakika Mkombozi wa Kisiasa atakayewaondoa Warumi waliowakandamiza. Lakini Mungu alikuwa na mpango mkubwa zaidi kwao, mpango ambao ungetimia kwa njia ya Mateso na Kifo cha Yesu Msalabani. Sisi pia mara nyingi tunaweka masharti kwa Mungu, “Nikisali hivi, nipate kazi hii” au “Nikiomba hivi Mungu anitoe kwenye changamoto hizi” nk. Mpango wa Mungu pale unapokuwa tofauti na matarajio yetu (kama Msalaba wa Yesu), tunakata tamaa tukidhani ameshindwa. Katika maisha yetu, tunapopata matatizo makubwa, changamoto kubwa, mara nyingi tunaweza pia kugeuzia mgongo Kanisa na kwenda kutatufa miujiza, tukageuzia mgongo sala na tafakari, tukageuzia mgongo Ibada na Misa Takatifu, tukamgeuzia mgongo hata Kristo Yesu ambaye alisulibiwa nje kidogo ya Mji wa Yerusalemu. Tunaweza kuachana na jumuiya zetu ndogondogo, na kukimbilia katika mambo ya kidunia, tukatoka kwenye nuru na kukimbilia kwenye giza tukijaribu kutafuta maana nyingine ya maisha kama huyu mwanafunzi mwenzangu Kleopa wa Emau, kwa kuwa wa pili ndiye mimi. Kuna hatari ya kutafuta maana ya maisha katika mambo ya kidunia, upweke, ulevi, anasa, uraibu au hata hata kurudia maisha na tabia zetu za zamani tukijaribu kutafuta faraja ya muda. Kwa kufanya hivyo tunaondoka kwenye nuru na kuingia katika giza.
Fundisho la Pili: Kristo Mfufuka anaingia katika safari yao, anawafunulia Maandiko Matakatifu. Kristo anaingia katika safari yetu ya maisha. Katika Somo hili la Injili tunaambiwa, wanafunzi hawa wakiwa njiani wakizungumza na kuulizana wao kwa wao habari za mambo hayo yaliyotokea, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa, wasimtambue. Akawaambia, ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Katika hali hiyo ya kukata kwao tamaa, hofu, mashaka, huzuni, hasira, Kristo anaingia katikati yao na anatembea nao. Wanafunzi wa Kristo ni wazi kabisa hawakuyaelewa mafundisho ya Kristo, aliyewaambia mara kwa mara utabiri juu ya kuhukumiwa, kuteswa, kufa na kufufuka kwake. Hata hivyo, Kristo hawaachi peke yao, anawafunulia Maandiko, yote yaliyonenwa juu yake kutoka Musa hadi manabii wote, akionesha kuwa ilimpasa kuteseka ili kuingia katika utukufu wake. Licha ya hayo bado hawakumtambua. Tukio hili la wanafunzi hawa wa Yesu kutokumtambua Kristo alipoingia katikati yao ni ishara ya upofu wa kiimani, upofu wa kiroho. Wanafunzi walitarajia kumwona Yesu kama mshindi wa kijeshi au kimuujiza. Walipomwona mgeni wa kawaida tu barabarani, hawakumfikiria kuwa ni Yeye. Kumbe nasi pia katika safari ya maisha yetu, safari yetu ya kiroho, mara nyingi tunamtafuta Mungu katika mambo makubwa na ya ajabu. Tunatamani kumwona Mungu aliye kati yetu katika miujiza mikubwa, huku tukimsahau katika mambo madogo madogo ya kawaida kabisa ya kila siku, katika kazi zetu, katika sala, katika Neno lake, katika Jumuiya inayosali, katika marafiki zetu wanaotujia wakati wa changamoto, au hata katika nafsi za wanaokuja kwetu kama wahitaji, maskini, wagonjwa, wageni nk.
Kristo Yesu anapoingia katikati yao anawauliza swali moja, “Ni maneno gani mnayosemezana hivi mnapotembea?” Yesu anawauliza Mnazungumza nini? Si kwa sababu hajui, bali ili kuwapa nafasi ya kutoa machungu, hofu, na majonzi yaliyokuwa yamejaa mioyoni mwao. Hii inatufundisha kuwa Kristo ni msikilizaji mkuu ambaye anataka tushiriki naye mahangaiko yetu ya kila siku. Kristo anakuja kwetu kila siku, anataka tumweleze yote yanayotusibu kama hawa wanafunzi walivyomwelezea Yesu masikitiko, hofu, huzuni, kukata kwao tamaa. Kristo anakuja kwetu kila saa ya maisha yetu. Anatupa nafasi ya kumweleza yale yote tunayopitia katika maisha, huenda ni misiba, changamoto za maisha, migogoro ya familia, ni kukata tamaa, udhaifu wetu, mahangaiko yetu ya kila siku katika maisha nk. Ni kweli zipo nyakati tunapitia na hatuoni kabisa tumaini tena. Mara kwa mara katika misiba, katika changamoto kubwa tunaweza kuona namna huzuni inavyojaza mioyo yetu, wakati mwingine tunashindwa kuelewa Neno lolote. Kristo anataka tuseme naye, anatusikiliza.
Fundisho la Tatu: Wanafunzi wanamwalika Yesu nyumbani, anawafungua macho yao katika Ekaristi. Kristo akiisha kuwafunulia maandiko, wanakaribia katika kijiji kile cha Emau, naye akafanya kama alitaka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakimwambia, kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa na mchana unakwisha. Kristo akaingia ndani na kukaa nao. Alipokuwa ameketi, mwinjili Luka anarudia maneno yale yale Kristo aliyoyatamka katika Karamu ya mwisho, alipoiweka rasmi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Alitwaa mkate, akaubariki akaumega akawapa. Na na hapo tunaambiwa yakafumbuliwa macho yao. Kama nivyotangulia kusema hapo mwanzo, si kwa bahati mbaya Mwinjili Luka anatupatia maelezo yote haya. Wafuasi hawa kumkaribisha Yesu nyumbani kwao kunatafsiriwa kama tendo la ukarimu, utayari katika kupokea. Wanafunzi walimkaribisha Yesu wakisema, “Kaa nasi, kwa kuwa kunakuchwa.” Tunaweza kusema, kama wafuasi wale wasingemkaribisha, Yesu angeendelea na safari na wasingepata fursa ya kumtambua. Kisha tukumbuke kuwa simulizi hili linatuhusu mimi na wewe katika maisha yetu ya kila siku. Nipo tayari kumkaribisha Yesu nyumbani kwangu, kwa maana ya kwanza, rohoni mwangu? Mara ngapi nimemwacha akapita? Mara ngapi nimemfukuza? Mara ngapi amekuta nina mambo mengi, hakuna nafasi? Ndugu mpendwa, baraka kubwa za Mungu na ufunuo mkubwa mara nyingi hupatikana kupitia ukarimu. Tunapofungua milango ya mioyo yetu au nyumba zetu kusaidia wengine, tunatengeneza mazingira ya Kristo kujifunua kwetu na kuingia katikati yetu. Haijalishi tumekata tamaa kiasi gani, haijalishi tuna huzuni kiasi gani, haijalishi tumekuwa kwenye giza muda mrefu kiasi gani, haijalishi tumeshashindwa mara ngapi, tunapompa Kristo nafasi, tunapomsihi kama hawa wafuasi, “Bwana kaa pamoja nasi, ni usiku sasa” Kristo hasiti kuingia ndani mwetu na kuwasha moto mpya. Anafanya makazi ya kudumu ndani mwetu.
Tukumbuke daima kuwa Kristo atakuja kwetu kwa namna za kawaida kabisa kama nilivyotangulia kusema. Huenda kwa mwaka mzima nimewafukuza na kuona kama maskini waliofika kwangu kuomba ni wasumbufu, kisha nikafikiri Kristo anatafutwa na kupatikana Kanisani katika Ekaristi. Mara kadhaa yawezekana nimekwepa kufanya matendo ya huruma kwa wagonjwa, yatima, maskini, wazee, kwa sababu nina shughuli nyingi, siwezi kuacha kazi zangu nikaenda kuona wagonjwa, nikaenda kutembelea wafungwa, nikaenda kuwafariji waliofiwa. Nimeacha mara kwa mara kuhudhuria ibada ya Misa Takatifu na kupokea Sakramenti za kanisa. Sina nafasi ya kusoma Maandiko Matakatifu, muda wangu wa ziada ni mitandano ya kijamii, ni matukio mengine nayapa kipaumbele zaidi. Humu tunamzuia Kristo kuingia ndani mwetu.Kristo Yesu akiisha kuingia anaketi nao chakulani, na anapoumega mkate, basi macho yao yalifunguliwa, wakamtambua. Ndugu mpendwa, Macho ya wafuasi hawa hayakufumbuliwa kwa Neno pekee walipokuwa njiani, wala kwa kuumega mkate pekee. Ilikuwa ni mchakato, kwanza Neno lilichoma mioyo yao, kisha Ekaristi ikafungua macho yao. Hii ndiyo siri ya Misa Takatifu, iliyogawanywa kwa namna ya pekee katika Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Tunahitaji sehemu zote mbili. Neno la Mungu huandaa akili na moyo, lakini Ekaristi inatupa mguso wa moja kwa moja na Mungu. Bila Neno, Ekaristi Takatifu inaweza kuwa desturi tu na bila Ekaristi, Neno linabaki kuwa maarifa tu ya kichwani. Kumbe, Ekaristi Takatifu inatupa namna mpya ya kuona kama anavyotuambia Mt. Thomasi wa Aquino kwamba, yafichikayo machoni, imani huyaona. Katika maisha ya kawaida, tunaona tu mkate na divai altareni; lakini kwa macho ya kiimani yaliyofumbuliwa na Ekaristi, tunamwona Kristo Mfufuka.
Ekaristi Takatifu inatupa uwezo wa kuona uwepo wa Mungu katika mambo ya kawaida kabisa ya maisha yetu. Wafuasi hawa mara tu walipomtambua, Yesu alitoweka mbele yao. Tukio hili la kutoweka mbele yao maana yake ni nini? Yesu hakuhitaji tena kuonekana kwa macho ya nyama kwa sababu sasa alikuwa ndani yao kupitia Ekaristi waliyoipokea. Alitoweka machoni lakini alibaki ndani mwao, akafungua macho ya mioyo yao, wakamtambua sasa si kama mpita njia, bali Kristo Mfufuka. Kumbe nasi tunamtambua Kristo anayeishi katikati yetu katika Neno lake, katika Ekaristi na sakramenti nyingine za kanisa, katika nafsi ya Padre, na katika nafsi za wanaoteseka. Ingawa kwa macho hatumwoni, ila yu nasi siku zote mpaka ukamilifu wa dahari. Mitume walishangaa kwa nini mioyo yao haikuwaka ndani mwao wakati Kristo aliposema nao njiani. Kumtambua Kristo ni neema. Tunahitaji msaada wa Kimungu ili tuweze kuyaelewa maandiko. Waliyajua maandiko lakini hawakuyaelewa bado mpaka pale Kristo alipofungua akili zao. Kumbe Injili hii inatukumbusha nasi kuwa mara nyingi Mungu anazungumza nasi kupitia matukio ya kila siku, lakini tunakuja kushtuka baadaye kuwa “Mungu alikuwa hapa, nami sikujua.” Tumwombe Kristo afungue akili na mioyo yetu, ili tumtambue anaposema nasi.
Fundisho la Nne: Matunda ya kukutana na Kristo ni kutoa ushuhuda, Mitume wanarudi Yerusalemu. Wafuasi hawa baada ya kufumbuliwa macho wakaondoka saa ile ile kutoka Emaus wakarejea Yerusalemu. Kama nilivyotangulia kusema, maana nyingine ya muhimu sana ya kiteolojia ya jina Emaus katika lugha ya Kiebrania ni “I-may'uhs” yaani “chemchemi ya maji ya moto.” Hii inadhihirisha jinsi mioyo ya wanafunzi ilivyopata moto na uchangamfu wa imani baada ya kukutana na Neno la Mungu na kumtambua Kristo Mfufuka katika Ekaristi Takatifu wakiwa katika karamu kule Emaus. Tunaambiwa wakaondoka, saa ile ile wakarejea Yerusalemu, hawakujali umbali, hawakujali giza, hakujali tena hofu, hakujali tena uchovu. Hapa tunakuja kutambua kwa hakika kuwa Mwinjili Luka alikua na maana kubwa zaidi ya safari ya kawaida kwa wasomaji wake ambao ndio sisi leo. Ndugu mpendwa, Injili hii inatufundisha kuwa kila mara tukikutana na Kristo katika Ekaristi na Neno, tunapata nguvu ya ajabu ya kuanza upya. Yale matatizo yaliyotufanya tukimbie Yerusalemu yetu, tunayajia kwa ujasiri mpya wa kuyatatua. Kama nilivyoeleza maana ya kwanza, Emau ulikuwa mji wa kujificha na kukimbia matatizo kwa hawa wafuasi. Lakini Yerusalemu ulikuwa mji wa hatari na msalaba, mahali ambapo Yesu aliteswa na kuuwawa. Walirudi kwenye jumuiya, walikusanyika tena kama Kanisa la wakristo wa kwanza, ambao baada ya Pentekoste walipokea Roho Mtakatifu na kumtangaza Kristo kwa nguvu bila woga. Kumbe, nasi pia katika Ekaristi Takatifu, Kristo anawasha moto ndani mwetu, anaondoa ubaridi na giza ndani ya mioyo yetu. Kipimo cha kama tumempokea Yesu sawasawa katika Misa ni shauku yetu ya kila siku ya kusema mema juu ya Mungu na wenzetu. Tunapotoka katika Misa Takatifu na kubaki na kinyongo, masengenyo, witu au uvivu wa kiroho, basi huenda hatujamtambua bado katika kuumega mkate. Ekaristi inapaswa kuwasha moto ndani mwetu wa kuwatumikia wengine na kuwa mashuhuda wa uwepo wa Mungu katika maisha ya wengine walio na hofu na mashaka.
Somo la 1: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume 2:14, 22-28. Mitume wa Yesu baada ya Pentekoste walianza kwa nguvu kumtangaza Kristo Mfufuka pasi na hofu na mashaka tena. Hapa tunamwona Petro akitoa hotuba yake ya kwanza baada ya Pentekoste. Petro, ambaye awali alimkana Yesu kwa hofu, sasa anasimama mbele ya umati mkubwa kusema ukweli. Anahubiri bila woga kwamba, Yesu aliyeteswa, akafa msalabani amefufuka kama ilivyotabiriwa katika Maandiko Matakatifu. Ni tumaini la ufufuko wetu na heri ya Mbinguni. Kama vile Yesu alivyowafafanulia wale wanafunzi Maandiko njiani, Petro naye anawafafanulia watu Maandiko ili waelewe maana ya mateso na ufufuko wa Yesu. Kutaniko letu na Kristo katika Ekaristi litupe nguvu ya kusema ukweli bila kuogopa, na kusimama katika kweli ya imani yetu. Somo la Pili: Ni Waraka 1 Pet 1:17-21. Katika somo la pili, Mtume Petro anatukumbusha kuwa hatukukombolewa kwa vitu vinavyoharibika kama fedha na dhahabu, bali kwa damu ya thamani, kama ya mwanakondoo asiye na mawaa, wala doa, yaani, ya Kristo. Somo hili linatufundisha kujithamini kwa kutambua nguvu na thamani ya ukombozi wetu. Ikiwa Mungu alilipa gharama kubwa kiasi hicho yaani Damu ya thamani kubwa ya Mwanae wa pekee ili kukukomboa, maana yake wewe ni wa thamani sana mbele zake. Hakuna dhambi au hali ya kukata tamaa inayopaswa kukufanya ujione hufai. Kumbe Pasaka ni wito wetu wa kila siku wa kujitahidi kuishi maisha matakatifu, kutenda haki, kuhurumia, kupenda, kuthamini wengine, kujitoa sadaka, kusamehe, ili tuweze kuungana Kristo, yeye aliyetoa uhai wake kwa ajili yetu sisi rafiki zake baada ya maisha yetu ya hapa duniani. Hitimisho: Tumwombe Kristo aifungue daima mioyo yetu, atufunulie Maandiko kwa nguvu ya Roho wake Mtakatifu, na aiwashe mioyo yetu anaposema nasi, nasi tupate ujasiri wa kuutangaza ufufuko wake.