Matunda halisi ya ziara ya Papa Leo XIV yataonekana katika amani tunayoijenga
Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.
Kutoka nchi ambayo bado inatamani amani ya kudumu, Askofu Eduardo Hiiboro Kussala alitoa ujumbe wa shukrani wa dhati kufuatia ziara ya hivi karibuni ya kitume ya Papa Leo XIV barani Afrika. Kama Askofu wa Jimbo la Tombura-Yambio na Rais wa Tume ya Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan na Sudan Kusini, alitafakari ziara hiyo kama ishara ya matumaini kwa bara lililo na majeraha makubwa na imani chanya. Kwa Askofu Hiiboro, uwepo wa Papa barani Afrika haukuwa wa ishara tu. Ulikuwa wakati uliozungumzia moja kwa moja uhalisia wa watu kutoa faraja katika muktadha ambapo amani inabaki dhaifu na safari ya kuelekea upatanisho inaendelea.
Mwendelezo wa kinabii wa ushuhud wa Kipapa
Askofu aliweka ziara hii katika historia pana ya mikutano ya kipapa na Afrika. Alikumbuka ishara yenye nguvu ya Papa Francisko wakati wa ziara yake ya 2023 nchini Sudan Kusini, alipopiga magoti na kubusu miguu ya viongozi wa kisiasa. Kitendo hicho, alibainisha, kilibadilisha diplomasia kuwa unabii, wito wa kimaadili wa uongofu na amani unaoendelea kusikika. Alielezea kwamba uzi huu wa kinabii unaendelea na Papa Leo XIV. Tangu mwanzo kabisa wa ziara yake, Baba Mtakatifu aliweka mwelekeo wazi, akiweka msingi wa ujumbe wake katika Heri za mlimani kutoka Injili ya Mathayo. Kwa kufanya hivyo, hakutoa maneno ya faraja tu bali pia njia halisi ya upya.
Heri za Mlimani ni kama ramani ya barabara ya amani
Katikati ya ujumbe wa Papa Leo XIV kuna ukweli rahisi lakini wa kina, "Heri wapatanishi." Kwa Askofu Hiiboro, maono haya ya Injili ni faraja na agizo. Inawapatia changamoto watu binafsi, viongozi, na mataifa yote kufikiria upyaishaji na uelewa wao wa nguvu, mafanikio, na amani. Alisisitiza, amani si tu kutokuwepo kwa migogoro. Ni tunda la haki, ukweli, na heshima kwa utu wa binadamu. Katika bara lenye imani nyingi lakini mara nyingi limelemewa na migogoro na ukosefu wa usawa, Heri za mlimani hutoa maono yanayobadilisha, yanayohitaji unyenyekevu, huruma, na kujitolea upya kwa manufaa ya wote. Askofu pia aliangazia nguvu ya Kanisa Barani Afrika, hasa vijana wake. Alisema vijana ni ishara ya matumaini na msingi ambao mustakabali wenye amani zaidi unaweza kujengwa juu yake.
Kutoka maneno hadi vitendo
Akitafakari urithi wa Mapapa wa hivi karibuni wakiwemo Papa Yohane Paulo II na Papa Benedikto XVI, Askofu Hiiboro alibainisha mwendelezo wa ujumbe wa ujasiri, upyaishaji, unyenyekevu na sasa kupitia Papa Leo XIV, wito wa kuishi Heri za mlimani. Lakini changamoto, alisisitiza, iko wazi. Wakati umefika wa kuhama kutoka kunena tu hadi utendaji. Kanisa lazima lirudishe sauti yake ya kinabii, liunde viongozi wa dhamiri, liandamane na vijana, na kukuza mazungumzo na makutano kama njia za amani. “Huu ndio utambulisho wetu. Hii ndio dhamira yetu,” alithibitisha, akiwahimiza wote kuishi kile wanachotangaza.
Wito wa kudumu wa mabadiliko
Ziara ya Papa imeshakamilika na sasa maana yake ya ndani inaanza kufunuka. Askofu Hiiboro alitukumbusha kwamba umuhimu wake wa kweli hautakuwa katika matukio yenyewe, bali katika athari yake ya kudumu. “Ziara hii itakumbukwa si tu kwa nyakati zake, bali kwa maana yake,” alihitimisha. “Matunda yake ya kweli yataonekana katika kile tunachokuwa.” Katika maneno haya kuna changamoto na tumaini kwamba mbegu zilizopandwa wakati wa ziara hii zitazaa matunda katika maisha yaliyobadilishwa, jamii zipatanishwe, na mustakabali ulioumbwa na amani.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.