Tafuta

Kardinali Stephen Brislin,Askofu Mkuu wa  Johannesburg na Rais w SACBC. Kardinali Stephen Brislin,Askofu Mkuu wa Johannesburg na Rais w SACBC. 

Kardinali Brislin amjibu Trump:Papa Leo XIV,anazungumza kwa niaba ya Kanisa lote

Kardinali Stephen Brislin alikataa vikali matamshi ya Rais wa Marekani Trump kuhusu nafasi za Papa Leo XIV,akisisitiza kwamba Papa anawakilisha sauti ya umoja wa Kanisa Katoliki,si maslahi ya kibinafsi au ya kisiasa.Alifafanua kwamba uchaguzi wa Papa uliongozwa na Roho Mtakatifu na wala si swala la kijiografia.Viongozi wa Kanisa Katoliki Kusini mwa Afrika pia walilaani matumizi mabaya ya taswira za kidini na kuonya dhidi ya hatari za harakati za kisiasa zinazofifisha mpaka kati ya imani na nguvu

Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Wakati Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa katika Ziara yake ya Kitume Barani Afrika kuzitembelea nchi za Algeria, Cameroon, Angola na Guinea ya Ikweta, jumbe za kumuunga mkono zinaendelea kufuatia na maandishi yaliyoandikwa na Rais wa Marekani Bwana Donald Trump, dhidi ya Mafundisho ya Baba Mtakatifu. Kwa njia hiyo Kardinali Stephen Brislin, Askofu Mkuu wa Johannesburg na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika (SACBC), alielezea matamshi ya hivi karibuni ya Raisi  huyo kuwa ni ya kusikitisha sana.

Kupinga vikali kwa tafsiri za kisiasa

Akijibu madai kwamba kuchaguliwa kwa Papa kuliathiriwa na utambulisho wake wa Marekani na hesabu za kisiasa, Kardinali Brislin alipuuza vikali mapendekezo hayo. Alisisitiza kwamba mkutano mkuu katika Kikanisa cha Sistine uliongozwa kikamilifu na sala na Roho Mtakatifu, si na shinikizo la kisiasa au kitaifa. Kulingana na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides,  linabainisha kuwa Kardinali alisisitiza na kusema kuwa Makardinali walichagua kiongozi anayeweza kuongoza Kanisa kupitia changamoto za kimataifa na kuwahudumia watu katika mataifa yote, bila upendeleo au mshikamano wa kisiasa. Ni katika mkutadha wa ujumbe ulitolewa na Rais wa Marekani dhidi ya Mafundisho ya Baba Mtakatifu Leo XIV.

Sauti ya Papa kama Sauti ya Kanisa

Kardinali Brislin alizidi kufafanua kwamba, mafundisho ya Papa si maoni ya kibinafsi bali yanaonesha msimamo thabiti na wa pamoja wa Kanisa Katoliki. Nafasi hizi ni pamoja na utetezi kwa wahamiaji, hatua za haraka kuhusu mgogoro wa tabianchi, kutetea ukweli katika enzi ya akili unde (AI), taarifa potofu, na upinzani mkali dhidi ya vita na kuongezeka kwa hatua za kijeshi. Kwa kusisitiza jambo hili, Brislin alisisitiza mwendelezo wa mafundisho ya Kikatoliki na uhuru wake kutoka kwa ajenda za kisiasa zinazobadilika. Alisema, Baba Mtakatifu ni sauti ya maadili na kiroho yenye mizizi katika mafundisho ya tangu kale ya mijadala ya kisiasa ya kisasa.

Kulaani Matumizi Mabaya ya Kidini na Ibada ya Sanamu za Kisiasa

Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika lililaani vikali picha iliyotengenezwa na AI inayomwonesha Rais wa Marekani Donald Trump kama Yesu Kristo na kuongezeka kwa utaifa wa Kikristo, ukielezea kama upotoshaji mkubwa wa imani ya Kikristo. Na Askofu Thulani Victor Mbuyisa alisisitiza kwamba taswira kama hizo ni za kukufuru, kwani zinapunguza Fumbo  la Umwilisho na kwa uwongo zinahusisha utambulisho wa kimungu na mtu wa kisiasa. Alionya zaidi kwamba itikadi zinazowainua viongozi hadi hadhi ya karibu ya kimungu zinaharibu Injili kwa kuchanganya ibada ya kidini na tamaa ya kisiasa, akithibitisha kupinga kwa Kanisa jaribio lolote la kudanganya imani kwa ajili ya madaraka au kukuza ibada ya watu mashuhuri wa kisiasa.

Wito wa amani na uwazi wa maadili

Licha ya ukosoaji na mivutano, Kanisa linabaki thabiti katika dhamira yake. Baraza la Maaskofu katoliki(SACBC) lilisisitiza kwamba kejeli au mashambulizi ya kisiasa hayatanyamazisha kujitolea kwake kutangaza amani, haki, na ukweli.

Wakirudia ujumbe wa Papa Leo XIV, viongozi wa Kanisa walitoa wito mpana kwa mamlaka za kimataifa, kukataa ibada ya sanamu ya utajiri na madaraka, kugeuka kutoka kwenye migogoro, na kukubali huduma kama kipimo cha kweli cha nguvu. Katika ulimwengu unaokabiliwa na migogoro inayoongezeka, wanasisitiza kwamba uwazi wa maadili na uadilifu wa kiroho ni muhimu zaidi kuliko hapo awali.

BRASLIN KUUNGA MKONO PAPA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here

17 Aprili 2026, 09:50