Tafuta

Dominika ya Nne ya Kipindi cha Pasaka huitwa pia Dominika ya Bwana wetu Yesu Kristo Mchungaji Mwema. Hii ni Siku ya 63 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa Dominika ya Nne ya Kipindi cha Pasaka huitwa pia Dominika ya Bwana wetu Yesu Kristo Mchungaji Mwema. Hii ni Siku ya 63 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa  (@Vatican Media)

Dominika ya Kristo Mchungaji Mwema: Wito Ni Zawadi Kutoka kwa Mungu

Dominika ya Yesu Kristo Mchungaji Mwema inakwenda sanjari na Maadhimisho ya siku ya 63 ya Sala kuombea miito duniani inayo chagizwa na kaulimbiu isemayo “Kugundua tena kutoka ndani wito kama Zawadi ya Mungu.” Papa Leo XIV katika ujumbe wake kwa siku hii ya leo, anaangazia wito kama safari ya mtu binafsi, yenye uzuri na shauku ya ndani ya kumwamini Bwana Mfufuka. Anawatia moyo waamini kumsikiliza na kumfuata Kristo Bwana wetu aliye mchungaji wetu.

Na Padre Octavian O. Hinju, CP. -JUCo, Morogoro, Tanzania.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Nne ya Kipindi cha Pasaka. Dominika hii inatambulika pia kama Dominika ya Bwana wetu Yesu Kristu Mchungaji Mwema. Ni siku maalumu ya kuombea miito mitakatifu. Dominika hii ya Nne ya Pasaka iliwekwa rasmi na Mama Kanisa mnamo mwaka 1964 kwa idhini ya Mtakatifu Paulo VI kama siku rasmi ya kuombea miito katika Kanisa la kiulimwengu. Leo tunamtazama huyo aliye teswa, akafa na kufufuka, ambaye kwa upendo mkuu ametoa uhai wake kwa ajili ya kuwakomboa kondoo wake waliopotea; ndiye Kristo Mchungaji wetu Mkuu. Dominika ya mwaka huu 2026 inaongozwa na kaulimbiu isemayo “kugundua tena kutoka ndani wito kama Zawadi ya Mungu”. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa siku hii ya leo, anaangazia wito kama safari ya mtu binafsi, yenye uzuri na shauku ya ndani ya kumwamini Bwana Mfufuka. Anawatia moyo waamini kumsikiliza na kumfuata huyo Kristu Bwana wetu aliye Mchungaji wetu mwema. Huu ni wito kwa wenye Daraja takatifu na Maisha ya wakfu kuendelea kujisadaka maisha yao kwa kumwiga Kristu Bwana na Mwalimu (Yoh. 13:14-15). Msingi na mwelekeo wa Dominika hii ni kuendelea kuutazama wito mtakatifu pamoja na changamoto zake katika ulimwengu huu mamboleo kama zawadi tusiyo stahili tunayoipokea katika vyombo dhaifu “lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.

Wito ni zawadi adhimu kutoka wa Mungu
Wito ni zawadi adhimu kutoka wa Mungu   (@Vatican Media)

Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu (2 Kor. 4:7-10), Zawadi kutoka kwa Mungu. Katika mtazamo huu, hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI Katika hotuba yake ya kwanza kabisa siku alipo chaguliwa kuliongoza Kanisa la kiulimwengu, hotuba iliyosheheni unyenyekevu mkubwa, alisema, baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II aliyekuwa maarufu sana, wapendwa kaka zangu Makardinali wamenichagua mimi, mtu wa kawaida na mfanyakazi katika shamba la Bwana kuwa Papa, lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anatambua jinsi ya kuendeleza kazi yake hata kwa kutumia vyombo dhaifu kama mimi. Kwa mantiki hiyo, wito ni Zawadi kwa ajili ya viumbe dhaifu lakini wale tu walio wanyenyekevu wenye utayari wa kuongozwa na Roho wa Bwana. Mungu anatuita na anatuteua ili atustahilishe kuifanya kazi yake kwa wema na uaminifu. Kumbe, Dominika ya Yesu Kristo Yesu Mchungaji mwema, ni ukumbusho kuwa mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anateua viumbe dhaifu ila wanyenyekevu ili waendeleze kazi ya kitume kwa nyakati zote, “basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” (Mt. 28:19). Wenye Daraja takatifu na maisha ya wakfu sharti watambue kwamba ‘wito si jawabu lake mtu binafsi bali ni jibu la Kristo kwa kiu ya watu wake’, kama anavyo zungumza Mt. Yohane Paulo wa II, Papa. Katika Dominika hii tukumbuke kwamba miito mitakatifu ni jawabu la upendo wa Mwenyezi Mungu kwa maombi ya watu wake, ‘basi, tuteulie mfalme atutawale kama Mataifa yale mengine yote (1 Sam. 8:5). Ingawa zipo nyakati maombi yetu hayapendezi masikioni pa Mwenyezi Mungu, lakini haachi kutuhurumia na kutusikiliza maana “BWANA amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu, (Zab. 103:8-10).

Tafuteni na kumwilisha sifa kuu za Mchungtaji mwema kama alivyokuwa Yesu
Tafuteni na kumwilisha sifa kuu za Mchungtaji mwema kama alivyokuwa Yesu   (@Vatican Media)

Mungu, Baba na Bwana wa historia, daima anaendelea kutusikiliza kila tumuombapo. Katika mtazamo na shauku ile ile ya wazee wa taifa la Israeli walioomba kupewa mfalme, Mama kanisa Mtakatifu anarudia tena katika sala ya kolekta siku ya kutolewa kwa Sakramenti ya Daraja takatifu ya upadre; anaposali kwa niaba ya jamii nzima ya waamini akisema “Ee Mungu, uliye mchungaji wa milele, unaliongoza kundi lako kwa ulinzi wa daima. Ulijalie Kanisa lako, kwa wema wako mkuu, mchungaji ambaye atakupendeza kwa utakatifu na kutufaidia sisi kwa kutuchunga kwa bidii.”  Katika huruma na upendo wake, Mwenyezi Mungu kwa kinywa cha nabii anajibu hivi kwamba “Nitawapeni wachungaji wanipendao moyoni, watakaowalisha kwa maarifa na busara,” (Yer. 3:15). Kwa maneno haya kutoka kwa Nabii Yeremia, “Mungu anawaahidi watu wake kuwa hatawaacha bilaa mchungaji ili kuwakusanya pamoja na kuwaongoza.”  ‘Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, (Yer. 23:4).’ Kwa mantiki hiyo wito sio jambo la mtu binafsi bali Mungu mwenyewe anayeita watumishi wake ili wamtumikie, alisema maneno hayo Mtakatifu Yohane Paulo wa II. Yeyote anaye pokea mwaliko na wito sharti atambue kwamba yeye ni kiongozi na mchungaji wa watu wa Mungu. Anatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Amepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika pendo kuu na huruma ya Mungu.

Maadhimisho ya Siku ya 63 ya Miito Ulimwenguni
Maadhimisho ya Siku ya 63 ya Miito Ulimwenguni   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 2:14a, 36-41. Somo hili linamwonesha mchungaji mwema kama mtu na kiongozi jasiri kwa mfano wa Mtume Petro. Alisimama mbele za watu ili kutoa ushuhuda wa ufufuko wa Bwana. Petro aliwaonya na kuwataka kufanya toba na mageuzi ya ndani kuhusu mtindo wao wa maisha usiofaa; hivyo wachague kumuongokea mwenyezi Mungu, na wakate shauri kumsadiki Kristu waliyemsulubisha. Vilevile watubu na kupokea ubatizo ili wapate maondoleo ya dhambi na kumpokea Roho Mtakatifu. Katika wajibu wao wa kufundisha yaani “Officium docere,” wachungaji sharti wawe imara katika kumshuhudia na kumtangaza Kristo Mfufuka bila woga wowote. Katika kutimiza dhima hiyo, watambue kwamba hakuna yeyote anayejifanya mchungaji kwa ajili yake mwenyewe. Mosi, ni lazima ateuliwe na Kristu “si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana (Yoh. 15:16-17), pili ni sharti watumwe na yule aliye waita na kuwateua “basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” (Mt. 28:19).   Yeyote mwenye kupenda kutimiza mapenzi ya Baba “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka” (Yoh. 6:38); yaani mchungaji mwema kama ilivyo kwa Mvuvi wa watu anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo kama anavyo tanabaisha mwanataalimungu William Baclay kwani, mvuvi mzuri ana sifa za pekee ambazo ni muhimu ili kuwaleta wengine kwa Kristo.

Kristo Yesu Ni Kiongozi na Mlango wa Kondoo wake
Kristo Yesu Ni Kiongozi na Mlango wa Kondoo wake   (@Vatican Media)

Barclay ana unganisha kwa vitendo ustadi wa mvuvi na sifa anazohitaji zenye kubeba ndani mwake ushuhuda wa kiroho wa mkristu; Mosi awe na subira, mchungaji mwema katika kuwachunga na kuwaongoza watu wa Mungu ni lazima atambue kuwa njia ya haraka na pupa haizai matunda. Mchungaji mwenye busara daima husubiri wakati wa Mungu. Pili, ustahimilivu. Mchungaji ni lazima atambue kuwa kondoo wote si sawa. Wanazo sifa na tabia tofauti. Ustahimilivu utamfanya awachunge vema bila kumpoteza hata mmoja wao. Tatu, ujasiri; mchungaji mwema awe tayari kuondoka kutoka kwenye mazingira yampayo furaha ili kuingia katikati ya mbwa mwitu na kuwatafuta kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea. Nne, utambuzi na mang’amuzi sahihi. Hii itamsaidia mchungaji kutambua wakati sahihi wa kuzungumza au kukaa kimya. Kipi afanye ama kipi asikifanye kwa maslahi mapana ya kondoo anao wachunga. Tano; kubadilika kulingana na mazingira na mahitaji ya watu wa Mungu. Mchungaji mwema sio yule asiyekubali ushauri wa watu wengine na asiwe mwenye misimamo yenye kuua, kudogosha au kuumiza moyo na dhamiri za wale walioko chini yake. Awe tayari kusikiliza sauti ya Mungu inayo sikika kupitia wanadamu wengine. Sita, unyenyekevu ambayo ni mama wa fadhila zote. Mchungaji mwema awe daima tayari kuweka kando maslahi yake binafsi na kumtanguliza Kristu katika kila jambo analo tenda. Aepukane na ubinafsi ili afanyike kuwa daraja kwa ajili ya kuwaleta wote kwa Kristu, ‘ili litimizwe lile neno alilolisema, wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao (Yoh. 18:9).

Kanisa linawahitaji vijana watakaojitosa kimasomaso kutangaza Injili
Kanisa linawahitaji vijana watakaojitosa kimasomaso kutangaza Injili

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro Kwa Watu Wote (1Pet. 2:20b-25). Mtume Petro anaeleza kwamba katika kutubu na kubatizwa tulichagua kumfuata Kristo ambaye aliteswa kwa ajili yetu. Anatutaka sisi tulio wafuasi wake tutende mema na katika kuyatenda hayo yaliyo mema basi tusichoke, ‘tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio (Wagal. 6:9-10); kadhalika tuyavumilie mateso tukimwiga Kristu. Injili inayo tamatisha tafakari yetu siku ya leo ni kutoka kwa Mwinjili Yohane 10: 1-10. Mwinjili Yohane anatukumbusha ukweli kwamba Kristu Mfufuka pekee ndiye kiongozi na mlango wa kweli. Kama kondoo wa malishoye sharti tuingie katika mlango wa huyo mchungaji wetu shujaa. Nasi sote tuliobatizwa tutambue kwamba sisi ni kondoo katika zizi lake, “jueni kwamba BWANA ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; tu watu wake, na kondoo wa malisho yake, (Zab.100: 3); hivyo yatupasa tupitie kwa kristu katika kumfuata. Kumbe yeyote anaye chukua wajibu wa mchungaji mkuu sharti awe mwaminifu kwa kristu. Uaminifu wetu kwa Bwana Mfufuka ujijenge katika sala na tafakari ya Neno la Mungu.

Hii ni Siku ya 63 ya Sala kwa ajili ya kuombea Miito Mitakatifu
Hii ni Siku ya 63 ya Sala kwa ajili ya kuombea Miito Mitakatifu

Kwa njia ya sala sote tuna alikwa kusali na kuomba, kupitia Bikira Maria Msaada wa Wakristo, ili Kanisa liweze kupata vijana watakaojitoa kimasomaso kwa ajili ya huduma ya Neno, Sakramenti na Utume wa Kanisa. Kwa sala na matoleo yetu ya kibinadamu, vijana wawe wasikivu kwa sauti ya Mungu ili kila mmoja wao aweze kuitikia wito kadiri anavyojisikia kutoka katika undani wa maisha yake. Kanisa linawahitaji vijana watakaowasha moto wa Injili; vijana watakaoendeleza ari na mwamko wa kimisionari tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Familia, Kanisa dogo la nyumbani linaposali na kuombea miito, linaalikwa pia kuonesha mshikamano wa huruma na upendo kwa kuchangia katika mchakato wa kukuza na kuimarisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Na sasa kwa mfano wa hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI tunasali kuombea miito tukisema “Ee Baba, uamshe ndani ya waamini wako, miito mitakatifu ya Upadri na Utawa, ili kuimarisha Imani na kulinda uzuri wa maisha ya Kikristo. Tunakuomba, uweze kuwasha mioyoni mwa vijana wengi, ari ya kujitoa kwako, ili waweze kuwa watumishi wako waaminifu katika Kanisa lako. Tujalie Mapadre na Watawa wengi, watakatifu na wenye hekima, wanaojitoa kwa moyo mmoja kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, tunakuomba usikilize sala zetu, kwa njia ya Yesu Kristo, Mwanao, Bwana wetu. Amina.” Tumsifu Yesu Kristo.

Liturujia Mchungaji Mwema
25 Aprili 2026, 10:02