Dominika ya Nne ya Pasaka: Siku ya 63 ya Kuombea Miito Ndani ya Kanisa
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Familia ya Mungu, ni Dominika ya 4 ya Pasaka mwaka A wa Kanisa, Dominika ya “KRISTO MCHUNGAJI MWEMA” Katika Dominika hii kila mwaka, Mama Kanisa anatualika kusali kuombea miito Mitakatifu katika Kanisa, yaani Ndoa Takatifu, Daraja Takatifu na Utawa. Kristo Mchungaji Mwema kwa njia ya Ubatizo na kwa njia ya miito hii Mitakatifu katika Kanisa, ametushirikisha sisi sote wajibu huu wa kuwa Wachungaji wa Kundi lake, akitualika kumtumikia kwa upendo, sadaka, utakatifu na Haki. Kama yeye alivyo kilelezo chetu, aliyejitoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake, akatufungulia mlango wa Mbinguni ili tuupate uzima wa milele, tuombe nasi sote neema ya kuisikia daima sauti yake, na kuishi kiaminifu miito yetu, ili nasi tuweze kuwaongoza wengine kwa Mungu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo wa XIV kwa ajili ya Siku ya 63 ya Kuombea Miito Mitakatifu ulimwenguni unajikita katika kauli mbiu, “Ugunduzi wa Ndani wa Zawadi ya Mungu.” Baba Mtakatifu Leo wa XIV katika Dominika hii ya kuombea Miito Mitakatifu katika Kanisa, anasisitiza kuwa wito si jambo la nje tu, bali ni ugunduzi wa zawadi ya bure ya Mungu inayochipuka ndani kabisa ya moyo wa mwanadamu. Baba Mtakatifu anatoa wito kwa kila mwamini, na kwa namna ya pekee sana kwa vijana, kujifungamanisha na Kristo Yesu kila mara katika utulivu, sala na tafakari ya kina ya moyo, ili kuweza kuisikia sauti yake na kumfuata kwa uaminifu. Ni sauti inayomwita kila mmoja wetu katika njia ya kipekee ya kuuendea utakatifu.
Akitutafakarisha kutoka kwa Mwinjili Yohane sura ya 10, Baba Mtakatifu Leo XIV anatumia picha ya Yesu, Mchungaji Mwema anayevutia na kubadilisha maisha ya wale wote walio tayari kumfuata. Anasema kuwa, “Maisha yanakuwa na maana na uzuri wa kweli pale tunapomfuata Kristo Yesu, kwani wito si mzigo bali ni mpango wake wa upendo na furaha anaotushirikisha kila mmoja wetu.” Baba Mtakatifu anahimiza parokia, familia, na jumuiya za kitawa kuunda mazingira yanayoruhusu miito kuchanua, tukifahamu kuwa sote tunatembea pamoja kama Jumuiya. Anasisitiza umuhimu wa kusindikizana kidugu kwa sala kila mara ili kusaidia wale wanaopokea wito wa Mungu kuweza kuukubali kwa furaha na ujasiri. Masomo yetu yote katika Dominika hii yanatuelekeza katika kutafari juu ya Kristo Mchungaji mwema, na wajibu wetu sisi aliopenda kutushirikisha kila mmoja kadiri ya wito wake, wito huu wa kulichunga Kundi lake.
Somo la Injili: Ni kutoka katika Injili ya Yohane 10:1-10. Katika somo hili la Injili Takatifu, Kristo Mchungaji Mwema anajitambulisha kwetu kama Mlango, anasema, “Mimi ndimi mlango wa Kondoo”. Tunaweza kujiuliza swali msingi, kwa nini Kristo anajitambulisha kama Mlango mwanzoni kabisa mwa sura hii ya 10 ya Injili ya Yohane? Fundisho hili la Kristo ni mwendelezo wa sura ya 9:1-41, sehemu ya Injili tuliyoisikia katika Dominika ya nne ya Kwaresma mwaka A, ambapo Bwana wetu Yesu Kristo mara baada ya kumponya yule mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa kwake siku ya Sabato, aliingia katika mvutano mkubwa sana na Mafarisayo. Matokeo yake walimfukuza yule aliyekuwa hapo mwanzo kipofu, kwa kuwa alikiri wazi kwamba ni Kristo yESU ndiye aliyemponya. Wakati Mafarisayo walimfukuza Kipofu huyu (mfano wa Kondoo aliyepotea), Bwana wetu Yesu Kristo Mchungaji Mwema anamtafuta bado mtu yule na kumpatia uponyaji kamili. Kristo hakumpatia tu uponyaji wa nje, bali anamfungulia mlango na njia ya Mbinguni, anampatia uponyaji wa ndani wa kiimani na kiroho. Mafarisayo walishindwa kutimiza wajibu huu wa kuwaleta watu kwa Mungu, wa kuwasaidia watu kupata uhuru na uponyaji kutoka katika vifungo mbalimbali vya shetani. Hawa Kristo anawafananisha na wezi na wanyang’anyi, ambao hawakuwajali kabisa kondoo.
Katika somo hili kwa namna ya pekee katika Dominika hii ya Mchungaji mwema, ningependa tutafakari pamoja mambo matano yafuatayo: Fundisho la Kwanza: Maana ya Mchungaji katika Agano la Kale na Agano jipya, Mchungaji alikuwa ni nani? Katika mazingira, tamaduni na Historia ya Taifa la Israeli katika Agano la Kale, dhana hii ya Mchungaji haikua jambo jipya. Kwanza: Mwenyezi Mungu kama Mchungaji Mkuu wa Kundi lake. Mahusiano ya taifa la Israeli na Mwenyezi Mungu yalijengeka katika misingi ya kichungaji, Mwenyezi Mungu akijitambulisha na kujidhihirisha katika Agano la Kale kama Mchungaji wa Kundi lake yaani Nyumba ya Israeli (Eze 34:15). “Kama mchungaji atafutavyo kundi lake, siku ile alipo kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza” Picha hii ya Mungu tunaiona pia katika zaburi ya 23, Mfalme Daudi anaposema, “Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu” Kumbe Mwenyezi Mungu kwa nafasi ya kwanza ndiye Mchungaji Mkuu wa Taifa lake Teule. Zaburi ya 81 hali kadhalika inamwita Mungu, “Ee Mchungaji wa Israeli, usikie, Wewe unayemwongoza Yusufu kama kundi.” Hapa Mungu anaonekana kama kiongozi wa taifa zima.
Pili: Viongozi wa wanadamu kama Wachungaji. Katika Agano la Kale, Wafalme na Viongozi wa kidini waliitwa wachungaji. Katika wote hao tunawaona Musa na Daudi kama Mifano ya wachungaji wa Kundi la Mungu, Musa akiwakilisha Manabii na Daudi akiwakilisha Wafalme. Wote wawili katika historia yao walikuwa wachungaji wa mifugo halisi kabla ya kuitwa kuchunga watu wa Mungu. Hii ilifundisha kuwa uongozi wa kweli unahitaji moyo wa unyenyekevu na utumishi. Katika Agano la kale tunaambiwa walikuwepo pia wachungaji wabaya. Manabii kama Ezekieli (sura ya 34) na Yeremia (sura ya 23) waliwashutumu viongozi wa Israeli kwa kuwa wachungaji wabaya ambao walijilisha wenyewe badala ya kundi, na kuwaacha kondoo watawanyike. Waliposhindwa kuifanya kazi hiyo Mwenyezi Mungu aliwakataa na kuahidi kuwa yeye mwenyewe atalichunga kundi lake (Eze 34:15).
Tatu: Kristo Mchungaji Mwema Katika Agano Jipya. Bwana wetu Yesu Kristo katika sura yote ya 10 ya Injili ya Yohane anajitambulisha kwetu kama Mchungaji Mwema, anayeutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake, anayewajua kondoo wake nao wamjua, anayewatafuta na kuwaleta katika kundi moja kondoo wote hata wale ambao si wa zizi lake, anayewapa uzima wa milele kondoo wake, asiyekubali kamwe kumpoteza hata kondoo mmojawapo na anayewalinda kondoo wake dhidi ya maadui. Ni utimilifu wa ile Ahadi ya Mungu kwamba, “Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu” katika kitabu cha Nabii Ezekiel 34:15. Katika somo tulilosikia, sura ya 10:1-10, Kristo anajitambulisha kwetu kama Mlango wa kondoo. Kwa namna ya pekee sisi tuliobatizwa ndio kondoo katika zizi lake, ndio Taifa jipya la Mungu katika Agano jipya, Kundi moja, chini ya Mchungaji mmoja Yesu Kristo. Kwa ubatizo na kwa miito binafsi kila mmoja anakabidhiwa na Kristo wajibu huu wa kuwa Mchungaji wa Kundi la Mungu. Fundisho la Pili: Bwana wetu Yesu Kristo Mchungaji Mwema ndiye Mlango pekee wa kutupeleka kwa Baba. Baada ya kuelewa maana ya Mchungaji katika Maandiko Matakatifu, Katika somo hili la Injili Takatifu dominika hii ya 4 ya Pasaka, Bwana wetu Yesu Kristo anajitambulisha kama “Mlango wa Kondoo”. Katika aya ya saba na ya tisa anasema, “Mimi ndimi mlango” Katika tamaduni za Wayahudi ambao walikua ni jamii ya wafugaji, fundisho hili lilieleweka bayana. Katika mazingira ya vijijini huko nyikani, zizi la kondoo mara nyingi lilikuwa ni ukuta wa mawe au miiba uliowazunguka kondoo.
Zizi hili halikuwa na mlango wa mbao kama ilivyo wakati wa sasa; badala yake, mchungaji mwenyewe alilala kwenye upenyo mdogo wa kuingilia zizini. Yeye alikuwa ndiye mlango na hakuna aliyeweza kuingia au kutoka bila kupita juu yake. Hali kadhalika, alikua ndiye mlinzi wa zizi, hakuna mbwa mwitu au wevi ambao wangeweza kuingia zizini na kuwadhuru kondoo, bila kumdhuru yeye kwanza. Ndugu mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo ndiye Mlango wa kweli wa kuingia katika uzima wa milele. Ndiye mlango wa kweli wa kuingia ulipo ulinzi na usalama wa kweli. Kama vile kondoo walivyokuwa salama ndani ya zizi, pasi na hofu na mashaka dhidi ya mbwa mwitu, wevi na wanyang’anyi ndivyo nasi tutakavyokuwa na amani na usalama ikiwa tupo chini ya ulinzi mara wa Kristo Mchungaji wetu mwema. Ametoa maisha yake kwa ajili yetu, ili sisi tusiishi tena kamwe katika hatari, hofu na mashaka. Kwa kuwa amesimama daima mlangoni, tuna Imani, nguvu, ujasiri na matumaini makubwa hata pale magumu yanapotupata, tunajua Kristo Mchungaji wetu anayajua yote, na hataruhusu yatujie ili kutuharibu, ili kutuangamiza na kutuangusha chini, bali katika hayo, utukufu wa Mungu udhihirike kama ilivyokuwa kwa yule mtu aliyezaliwa kipofu na kuponywa na Kristo. Kwa kuponywa kwake, nguvu na ukuu wa Mungu ulidhihirika ndani ya Kristo. Kristo anafahamu kwanza changamoto zetu hata kabla hazijatupata kwa kuwa yeye yu daima mlangoni. Hatoruhusu tupatwe na magumu, tubebe msalaba mzito kuliko nguvu zetu.
Fundisho la tatu: Tunaishi katika ulimwengu wenye kelele na sauti nyingi, tuisikie sauti ya Kristo Mchungaji Mwema. Katika tamaduni za Wayahudi, wachungaji walipokuwa huko nyikani mbali na nyumbani, waliweka mifugo yao katika zizi moja. Katika zizi moja la kijiji, makundi mengi ya kondoo yalichanganywa pamoja usiku. Asubuhi, kila mchungaji alitoa mlio au sauti yake ya kipekee. Kondoo walitoka na kumfuata mchungaji wao tu, wakitofautisha sauti yake na ile ya wageni. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Dominika hii anatoa wito kwa kila mwamini, na kwa namna ya pekee sana kwa vijana, kujifungamanisha na Kristo kila mara katika utulivu, sala na tafakari ya kina ya moyo ili kuweza kuisikia sauti yake na kumfuata kwa uaminifu. Ni sauti inayomwita kila mmoja wetu katika njia ya kipekee ya kuuendea Utakatifu. Ndugu mpendwa, kama vile makundi mbalimbali ya kondoo walivyokuwa katika zizi moja, ndiyo uhalisia wa maisha yetu ya kila siku hapa duniani. Tupo katika ulimwengu uliosheheni sauti nyingi za kila aina, mitandao ya kijamii, watsup, Instagram, tiktok, biashara, marafiki, kazi, changamoto za kila namna, kote huko tunasikia sauti mbalimbali zikituita. Ipo sauti ya Kristo Mchungaji wetu mwema, na zipo sauti nyingine za wageni. Sauti nyingi za wageni, hizi mara nyingi hutuambia kuwa furaha inapatikana kwenye mamboya kidunia, fedha pekee, umaarufu, anasa, starehe za kidunia, mali, nguvu, madaraka nk. Katika mchanganyiko huo ni lazima tujifunzi kuisikia sauti ya Mchungaji wa kweli, Bwana wetu Yesu Kristo. Kujifunza kuitambua sauti ya Mchungaji kunatusaidia kuchuja ni ushauri gani wa kuufuata na upi wa kuupuuza ili nisipotee, ni yapi yaliyo mambo ya muhimu katika maisha na ni yapi yasiyo ya muhimu, ni yapi ya kufuata na ni yapi ya kuachana nayo, ni nani anasema ukweli na anayeniongoza kwenye kweli, ni yupi tapeli na dalali wa Imani yangu, ni mambo yapi ya muda niachane nayo na ni yapi ya umilele nijifungamanishe nayo. Dominika hii inatualika kujitahidi kila wakati, hata katikati ya mchanganyiko huu kuisikia daima sauti ya Kristo na kuifuata.
Ni katika ukimya, sala, Neno la Mungu na Tafakari kama alivyotualika Baba Mtakatifu Leo XIV tutaweza kutofautisha kati ya sauti ya Kristo Mchungaji Mwema katikati ya mawimbi ya sauti nyingi za ulimwengu. Yawezekana kuna watu, vitu au mifumo inayokuja kwa sura ya upole lakini lengo lake ni kuchinja na kuharibu, kuharibu familia zetu, kuharibu Watoto wetu, kuharibu Imani yetu, kuharibu mahusiano yetu, kuharibu jamii yetu, kuharibu amani, furaha na utulivu wetu wa ndani. Roho Mtakatifu anatupa uwezo wa kusema “Hapana” kwa vitu vinavyoonekana vizuri kwa nje lakini havina sauti ya Kristo Yesu ndani yake. Kama kondoo walivyokataa kumfuata mgeni, na sisi tunajifunza daima kuwa macho tuwapo na nguvu ya Mungu ndani mwetu. Fundisho la nne: Kristo Mchungaji Mwema ana uhusiano wa karibu nasi Kondoo wake, anatujua na kumwita kila mmoja kwa jina. Katika Tamaduni za Wayahudi, Mchungaji hakuwa mfanyakazi aliyekaa mbali; aliishi na kondoo wake mchana na usiku. Aliwapa majina kulingana na tabia zao au alama zao. Uhusiano huu ulikuwa wa karibu kiasi kwamba mchungaji alijua hata hali ya kila kondoo, alijua yupi alikuwa mgonjwa, yupi alikuwa dhaifu, yupi alikua imara. Ndivyo Mwenyezi Mungu anavyotujua sisi. Hayupo mbali nasi, bali yupo karibu kabisa na sisi. Anatuita kila mmoja kwa jina lake. Ndugu mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo Mchungaji Mwema anatufundisha kuwa, mbele za Mungu, wewe sisi ni wa thamani kubwa. Mwenyezi Mungu anatujua binafsi na amekuita binafsi kwa jina lako. Hivyo kila wakati unapopitia changamoto ambazo hakuna anayezielewa, kumbuka kuwa Kristo Mchungaji wako anakujua, anakuelewa. Amekuchunguza, anajua jinsi ulivyo. Yeye anajua alama zako na tabia zako, anajua udhaifu wako na nguvu zako, na anakupenda hivyo ulivyo. Kumbe hatuhitaji kuvaa masks au kujifanya tuko sawa mbele za Mungu. Katika sala zako za kila siku, unaweza kuwa mkweli. Ikiwa umevunjika moyo, mwambie; ikiwa una hasira, mwambie. Yeye ni mchungaji anayeishi nawe mchana na usiku, si Mungu wa mbali asiyeguswa na maumivu yako, bali ni Mungu aliye daima karibu nawe. Ikiwa Mchungaji wetu anatujua kwa majina, na sisi tunaitwa kuwa wachungaji wa wenzetu (katika ngazi ya familia, kazini, au kanisani).
Je, tunawajua kondoo wetu kwa majina, tabia zao, alama na mienendo? Ukaribu wangu na familia yangu upoje, ninawafahamu kiasi gani Watoto wangu, mwenzangu wa ndoa, mwenzangu katika jumuiya, kwa tabia, kwa karama na vipaji vyao, kwa udhaifu na kwa nguvu zao, mabadiliko ya tabia na mienendo yao? Kristo anatukumbusha wajibu wetu wa kuwa karibu na kondoo, kuwafahamu kwa kina na kuwasaidia walio wagonjwa na dhaifu. Hatuwezi kufanikiwa iwapo tupo mbali na kondoo wetu. Wazazi mpo mbali na Watoto, mnaonana na Watoto wakati wa likizo tu na tena kwa muda mchache kwa sababu ya kazi na majukumu. Muda mwingi Watoto wapo tuition na Masomo ya ziada, hakuna muda wa kuhudhuria kwa kina mafundisho ya katekisimu, hakuna muda wa kuchanganyikana na Watoto wenzao, hawana muda kujifunza kazi za mikono, kazi za nyumbani. Sisi pia wachungaji tupo mbali na kondoo wetu kwa kuyapa kipaumbele mambo mengine ya kijamii kuliko mambo ya kiroho, makazini waajiri wapo mbali na wafanyakazi kwa sababu tu ya tofauti za vyeo, mishahara, majukumu. Kristo, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alikuja Katikati yetu, akawa sawa na sisi. Anatutuma nasi kuwa wachungaji wema, kuwa karibu na kondoo.
Fundisho la tano: Tofauti kati ya Mchungaji Mwema na Mchungaji wa Mshahara, mimi nipo Kundi gani? Bwana wetu Yesu Kristo katika somo hili la Injili Takatifu anatofautisha aina mbili za wachungaji. Aina ya kwanza ya Mchungaji ni yule asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mvivi naye ni mnyang’anyi. Yesu hapa alikuwa akiwasema Mafarisayo waliomfukuza yule kipofu katika sura iliyotangulia (Yn 9). Hawa walikuwa wachungaji wa mshahara au wevi waliotumia dini kwa maslahi yao wenyewe badala ya kuwaongoza na kuwasaidia kondoo waliopotea kuiona njia na mlango wa kuupata uhuru wa kweli, wa kumjua na kumwamini Mungu. Kristo anatulika kujifanana naye, yeye aliye Mchungaji wa kweli. Ndugu mpendwa, tunaishi katika ulimwengu uliojaa changamoto kubwa sana katika uchungaji, kuanzia ngazi ya mtu binafsi. Wapo wanaotumia Madaraka au nafasi zao vibaya. Kristo leo anatufundisha kuwa makini na viongozi (wa kiroho, kijamii, au hata kazini) ambao wanatumia nafasi zao kwa ajili ya ubinafsi, sifa, au fedha. Kiongozi wa kweli, kama Kristo, yuko tayari kupoteza ili kondoo wake wapate faida. Kristo anatualika na kutupa ujasiri wa kutambua na kutofuata Wachungaji wa mshahara ambao hukimbia kondoo wao shida zinapotokea, au pale wanapotimiza maslahi yao.
Huenda katika familia, katika kanisa, katika jamii yetu tumekua watu wa mshahara. Je, mimi hapa nilipo ni mwajiriwa au ni Mchungaji? Huenda nimewapa watoto wangu watu wa mshahara wanisaidie kuwalea kwa kuwa mimi pia ni mtu wa mshahara, sina nafasi, majukumu ni mengi, visingizio vingi, huenda mimi kama Padre wakati fulani ninajijali zaidi, sitaki kuchoka, sitaki kuumia, ninatafuta urahisi, ninakwepa majukumu na kuwasahau Kondoo niliokabidhiwa na Mungu. Katika jamii, katika uongozi, katika kazi, nimekuwa mwoga kusimamia ukweli. Kristo anatuhimiza kuwa na ujasiri wa kimaadili. Wakati mwingine kufuata ukweli kutakufanya uonekane asiye mtiifu kwa mifumo iliyopotoka. Fundisho hili linatuhusu kwa kutuonyesha kuwa ni heri kufukuzwa na wevi na kupokelewa na Mchungaji Mwema kuliko kubaki salama zizini mwa viongozi na wachungaji batili. Mchungaji mwema anawaongoza kundi lake kwenye malisho, yeye anajua ni wapi yalipo malisho mabichi, anajua wapi yalipo maji ya utulivu. Katika ulimwengu uliojaa kila aina ya njaa na kiu, ni Kristo pekee anayeweza kutuonesha ilimo hazina ya kweli, yalipo malisho bora na ya kutosha, ulimo uzima wa roho zetu. Si hivyo tu, yeye anatembea daima mbele yetu, yu tayari kuzikabili daima hatari zote kwa ajili yetu. Katika maisha ya kila siku, anatufundisha kuwa kiongozi bora ni yule anayeonyesha njia kwa matendo yake mwenyewe, akitupa ujasiri wa kufuata nyayo zake kuelekea kwenye mafanikio ya kiroho. Kwa njia ya Roho Mtakatifu Kristo ametupa sisi uhai na uzima tele.
Somo la 1: Ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 2:14a, 36-41. Baada ya kupokea Roho Mtakatifu, Petro na mitume wengine wanahubiri kwa ujasiri kuwa Yesu, aliyesulubiwa, ndiye Kristo na Bwana. Wanawaambia viongozi na watu kuwa hakuna wokovu katika mwingine yeyote. Watu waliosikiliza walichomwa mioyo yao na kuuliza, “Tutendeje ndugu zetu?” Hii inaonyesha nguvu ya neno la Mungu linapotangazwa na mwitikio wa kondoo kuisikia sauti ya Mungu kupitia wahubiri. Somo hili la kwanza linatufundisha kuwa kumsikiliza Kristo Mchungaji Mwema kunapaswa kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha yetu (toba) na kutupa ujasiri wa kutangaza ukweli wa imani yetu bila hofu. Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka 1 Pet 2:20b-25. Katika somo la pili, Mtume Petro anatukumbusha juu ya wito wetu wa kufuata nyayo za Kristo. Katika kutubu na kubatizwa kama ilivyokuwa kwa wasikilizaji wa hotuba ya Mtume Petro katika somo la kwanza, tulichagua kumfuata Kristo ambaye aliteswa kwa ajili yetu. Mtume Petro anatufundisha kuwa, Yesu hakuwa Mchungaji wa maneno tu, bali wa vitendo. Alituachia mfano wa jinsi ya kuishi kwa uvumilivu, unyenyekevu, na upendo, hata tunapokutana na dhuluma au changamoto. Hitimisho: Tumwombe Kristo atupe neema ya kuisikia daima sauti ya Kristo Mchungaji mwema katikati ya sauti nyingi katika ulimwengu huu. Atupe nguvu ya kuitika daima wito wake, na kuishi daima kwa kufuata nyayo zake katika upya wa maisha kama wabatizwa, kama wana wa Mungu.