Tafuta

Papa  Leo XIV alitembelea Wazee huko Angola Papa Leo XIV alitembelea Wazee huko Angola  (ANSA)

Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV,Angola:Ziara ya Papa ni wakati usio na kifani kwetu!

Papa Leo XIV akitembelea nyumba ya wazee huko Saurimo,Georgina Mwandumba,mkurugenzi wa kituo hicho,alizungumza na Vatican News kuhusu wazee 74 waliokataliwa na familia zao kutokana na imani za kishirikina,akibainisha kuwa ziara ya Baba Mtakatifu inatoa fundisho kubwa kwa ajili ya jamii ya Angola

Na Dulce Araújo - Angola

"Kuwa mzee ni baraka kubwa. Ni vizuri kuchukua muda na kukaa na babu na bibi. Tuthamini maisha." Huu ndio ujumbe Georgina Mwandumba aliowaachia Waangola katika mahojiano yake na Vatican News, ambapo aliwasilisha nyumba ambayo amekuwa akiiongoza kwa miaka saba, miaka ambayo ilionekana kupita haraka kutokana na furaha ya kweli anayopata kufanya kazi na wazee. Kwa kupata mafunzo ya usaidizi wa kijamii tangu utoto wake, Gavana wa zamani wa Mkoa, Daniel F. Neto, alimtambua kama kuwa mtu anayefaa kusimamia nyumba hiyo, ambayo imekuwepo kwa miaka 14 na ni mali ya Serikali ya Angola.

Mahusiano mazuri na Kanisa

Bi. Mwandumba alisisitiza kwamba wana uhusiano mzuri na Kanisa, ambalo, mbali na kutoa msaada wa kiroho kwa wakazi, pia hutoa michango kusaidia katika shughuli. Michango ya kifedha pia hutoka kwenye vyama na wafadhili, lakini ni mchango wa kila mwezi wa serikali, ingawa ni chini ya kile kinachohitajika, ndiyo unaofanya Nyumba iendelee kufanya kazi. “Wazee hujikita na  kilimo katika ardhi iliyotupu kama burudani na kama njia ya kuchangia riziki yao. Lakini kila kitu wanachohitaji, kuanzia chakula hadi huduma ya afya, hutolewa na Nyumba hii ya wazee.” Kiukweli, “Kituo cha Afya cha Nyumba ya wazee huwahudumia pia wakazi wa vijiji vya karibu”.

Makazi ya wazee yamegawanyika  pande mbili, upande moja ni wa kike, na upande mwingine ni wa kiume. Nyumba hiyo ilipata mwonekano mpya kwa ajili ya  ziara ya Papa, na baadhi ya huduma ambazo mkurugenzi alikuwa ameomba kwa muda mrefu, kama vile kuunganishwa kwa  umeme  wa moja kwa moya wa Saurimo (badala ya Jenereta ) na maji ya bomba, vyote vilitekelezwa na hivyo kurahisisha maisha, alibainisha Bi. Georgina, ambaye tayari aliona hii kama baraka iliyoletwa na ziara ya Papa Leo XIV na kwa mngangao alisema: “hakika hii ni  baraka kutoka Mbinguni, na tayari tunafurahi!”

Ushirikina na kutelekezwa na familia

Nyumba hiyo iko kama kilomita 10 kutoka jiji la Saurimo. Wazee 74, ambapo  42 kati yao ni wanawake, wenye umri kati ya miaka 60 na 93, ingawa wakati mwingine wanaonekana wazee zaidi, baada ya kufikishwa kwenye kituo hiki katika hali mbaya ya kimwili.  Wazee hao huletwa na Polisi ambao, baada ya  kukimbilia usalama kutoka kwa jamaa zao wanaowanyanyasa na kuwatuhumu kuwa wachawi.

Hata hivyo, kwa maoni ya Georgina, hii inazidi kuwa kisingizio cha kuepuka kuchukua jukumu la kuwatunza wazee. Kwa hivyo, aliiomba jamii kuwathamini wazee na alibainisha kuwa ziara ya Papa kwa watu hao  "waliokataliwa" kuwa "fundisho kubwa." Hata alishirikisha uzoefu wake mwenyewe mzuri na babu na bibi yake. Wazee hawa wanafurahi katika Nyumba hiyo, wanaelewana, na wanahudhuria Misa pamoja, hata kama si wote ni Wakatoliki, lakini hakuna shaka wangependelea kuwa na familia zao, ambazo kwa bahati mbaya hata hawawatembelei, alifichua mkurugenzi huyo mwenye huzuni kidogo.

Ziara ya Papa Leo XIV katika nyumba ya wazee

Kwa hivyo, ziara ya Papa katika nyumba hiyo kunako tarehe 20 Aprili  2026, ilikuwa wakati wa furaha kubwa kwa wanaume na wanawake hao, ambao walikuwa kitovu cha umakini siku hiyo. Maandalizi ya kumkaribisha mgeni muhimu yaliendelea vizuri: wazungumzaji waliowakilisha wenzao, nyimbo, na matukio mengine mengi ya kushangaza. Nani alijua kwamba ziara hiyo inaweza pia kusababisha kuundwa kwa Kanisa ndani ya Nyumbani ya Wazee, ambapo kwa sasa msaada wa kiroho hautolewi na Padre wao bali na Mapadre wanaokuja kuadhimisha Ibada ya Misa ya Dominika katika chumba kidogo kilichopangwa kwa kusudi hili. Katika kituo hicho yenye pande mbili, ya Kike na Kiume na wakazi watatu au wanne katika kila chumba, mkurugenzi alionesha tumaini kuwa na wafanyakazi zaidi wa kuwatunza wazee hao.

Kwa sasa kuna Mkurugenzi, Msimamizi, Mfanyakazi wa kijamii, na Wafanyakazi wa jikoni na usafi. Hata hivyo, kinachomsumbua zaidi Bi. Mwandumba ni kukomesha desturi ya kipuuzi ya mashtaka ya kishirikina na matumizi yake kama kisingizio cha kuwaacha wazee. "Sisi ni waamini, tunakwenda Kanisani," alisema, "kuamini kwamba kuna kiumbe mchawi anayeweza kushinda baraka za Mungu ni kutoamini, si imani!" Alipoulizwa kuhusu uhusiano kati ya suala hilo na mada ya ziara ya Papa nchini Angola "Hija wa Matumaini, Upatanisho, na Amani" Georgina alibainisha kuwa: "amani lazima ianzie katika familia zetu."

Imesasishwa  saa  24 Aprili 2026 saa 11.25 na Sr Christina Masivo.

ANGOLA ZIARA YA PAPA/WAZEE

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

24 Aprili 2026, 11:26