Wakristo na Waislamu waungana nchini Pakistan kuombea amani
Na Kielce Gussie – Vatican.
Huku migogoro na vurugu zinazoendelea zikiashiria maisha ya kila siku katika mpaka kati ya Afghanistan na Pakistan, mkutano wa kidini katika "Kituo cha Amani" huko Lahore, nchini Pakistan, uliwaleta pamoja wawakilishi wa Jumuiya za Kikristo na Kiislamu katika Msikiti wa Badshahi, msikiti wa kifalme wa jiji hilo kuombea amani. Padre Asif Sardar, Msimamizi Mkuu wa Jimbo Kuu la Lahore, alielezea kwamba mkutano huo "ulikusudiwa kuwa ishara ya amani na umoja, haswa katikati ya vita kati ya Afghanistan na Pakistan.”
Dhamira ya pamoja ya amani
Kulingana na shirika la Kipapa la habari za Kimisionari Fides, Msimamizi Mkuu alielezea tukio hilo kama "ndoto" kwani aliweza "kushuhudia maelewano na amani kati ya jamii hizo mbili." Mkutano huo uliwaleta viongozi hawa wa Kiislamu na Wakristo wakati wa Kwaresima na Ramadhani na ulijumuisha chakula cha jioni cha waislamu, ambayo ni mlo wa kuvunja mfungo. Padre Sardar alielezea tukio hilo lilikuwa limetengwa kwa ajili ya kuthibitisha tena ushirika wa kiroho wa jumuiya hizo mbili na "kujitolea kwa pamoja kwa amani katika wakati huu mgumu ulioangaziwa na vita vinavyotuathiri moja kwa moja." Kuweka mkazo katika kufunga, sala, na hisani, alibainisha, kunamaanisha kushiriki mkate na wale ambao hawana, kukuza haki, amani, na maridhiano.
Wakati wa mkutano huo, Padre James Channan, wa Shirika la Wadominikani na Mkuu wa Kituo cha Amani huko Lahore, na imamu wa msikiti huo, Abdul Khabir Azad, walizungumzia ahadi hii ya "kuimarisha mizizi ya mahusiano kati ya Wakristo na Waislamu nchini Pakistan, na kuishi maadili ya pamoja ya kufunga, kutafakari, na kujitolea yaliyopo katika Ramadhani na Kwaresima," na "kuomba amani, kuinua maombi yetu pamoja kwa Mungu kwa ajili ya utulivu wa Pakistan na mwisho wa migogoro ya kimataifa." Padre huyo alisisitiza kwamba mkutano huu wa kidini ulikuwa mfano halisi wa kuheshimiana. "Tumetuma ujumbe wazi: imani inaweza kuwa daraja la umoja na si ukuta wa mgawanyiko."
Wito wazi
Hii haikuwa wakati pekee wa maombi na tafakari uliofanyika hivi karibuni nchini Pakistan. Jumuiya ya Wakatoliki pia iliongoza maandamano ya kuwasha mishumaa na mkesha wa maombi uliowekwa wakfu kwa amani katika mpaka kati ya Pakistan na Afghanistan. Waumini wa kidini, wa Kanisa la Mtakatifu Pio la Pietrelcina, na wanachama wengine wa jumuiya hiyo waliomba Vituo vya Msalaba. Padre Qaisar Feroz OFM Cap., Katibu Mtendaji wa Tume ya Mawasiliano ya Kijamii ya Mkutano wa Maaskofu Wakatoliki wa Pakistan, na Sr Azmat, Mkuu wa Shirika la Masista wa Kitume la Wakarmeli, waliongoza sherehe hiyo. Padre Feroz alisisitiza kwamba ujumbe ulikuwa wazi: wanalaani vurugu kati ya nchi hizo mbili na wanaendelea kutetea kusitisha mapigano kupitia mazungumzo. "Vurugu za msimamo mkali za Taliban ni itikadi mbaya," alisema, "Ahadi ya pamoja kutoka kwa waumini inahitajika ili kuizuia na kuibadilisha." Zaidi ya hayo, aliikumbusha jumuiya ya kimataifa kuhusu wajibu wake wa kusaidia kumaliza mgogoro na kuleta amani. Aliomba kwamba "amani iwe lengo na maslahi ya pamoja ya wanadamu wote."
Asante kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here