Kenya:Wahitimu Katoliki wa Kitanzania,“Wajukuu wa Nyerere,”wapongezwa!
Na Sr. Scolastica Tesha,CSG,–Nairobi, Kenya.
Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma katika vyuo mbalimbali nchini Kenya walikutana hivi karibuni Dominika tarehe 8 Machi 2026, katika ukumbi wa Don Bosco Utume jijini Nairobi kwa ajili ya sherehe maalum ya Misa ya pamoja ya kumshukuru Mungu, kuimarisha umoja wao na wakati huo huo kuwapongeza wanafunzi wanaohitimu mwaka huu 2026 na shukrani kwa mafanikio ya wanafunzi hao pamoja na kuwaombea wanapoanza hatua mpya ya maisha yao ya kitaaluma na kijamii mahali watakapotumwa. Mkutano huo uliwaleta pamoja vijana wanaojiita “Wajukuu wa Nyerere,” jina linaloashiria dhamira yao ya kuendeleza maadili na misingi ya Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
"Inafurahisha vijana kujiita Wajukuu wa Nyerere"
Katika tukio hilo awali ya yote ilikuwa ni Misa iliyoongozwa na Padre Albert Mugisha, AJ, kutoka Shirika la Mitume wa Yesu, akishirikiana na mapadre wengine wa Kitanzania wanasoma na wanaohudumu nchini Kenya. Baada ya misa, Profesa na Padre Richard N. Rwiza, alipata nafasi kuzungumza na wanafunzi na wageni waliohudhuria hafla hiyo ya pamoja, ambapo katika hotuba yake, aliwashukuru wanafunzi kwa kuenzi urithi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuhimiza mshikamano miongoni mwao. “Inafurahisha kuona vijana mkijiita Wajukuu wa Nyerere. Hii inaonesha kuwa mnathamini urithi wa kiongozi aliyesisitiza utu, mshikamano na huduma kwa jamii,” alisema Profesa Rwiza.
Padre Rwiza alisisitiza kuwa "elimu ni chombo cha kuwajenga wasomi kuwa watu wa unyenyekevu na kuwahudumia wengine na sio kuwa na majivuno kwa elimu waliyopata kupitia masomo yao." Kwa njia hiyo alihimiza akisema: “Msisahau mlikotoka, kumbukeni wale waliowasaidia kufikia elimu ya juu hasa majimbo yenu, familia zenu na mashirika yaliyochangia katika safari yenu ya elimu. Hii ni sehemu ya kuwa watu wa shukrani.” Profesa Rwiza zaidi aliwahimiza wanafunzi wote kuwa na mshikamano na ushirikiano, akisisitiza kwamba Nyerere alikuwa kiongozi wa watu wote, aliyethamini mshikamano wa jamii na (Pan-Africanism ) uafrika. “Nyerere aliishi kwa unyenyekevu na hakuwahi kujivuna au kuwadharau wengine, licha ya kuwa msomi. Msomi wa kweli hapaswi kujitutumua au kuwaona wengine kama nyanya mbichi. Kumbukeni shirika lenu, jimbo lilioawatuma, na familia zenu iliyowasaidia kufika hapa. Shirikianeni na wenzenu kwa kufuata mfano wa Mwalimu Nyerere; tuungane kwa upendo, mshikamano na mshirikiano miongoni mwa Watanzania na Wafrika wote,” alisema Profesa Rwiza.
Juhudi za kudumisha mshikamano miongoni mwa watanzania,Kenya
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki ( AMECEA,) Padre Anthony Makunde, Katika hotuba yake aliwapongeza wanafunzi kwa kuonyesha mshikamano na umoja, akiwapongeza pia viongozi wa TASAKE kwa juhudi zao za kudumisha mshikamano na ushirikiano miongoni mwa Watanzania waliopo Kenya. Padre Makunde alitoa mfano wa mwaka 1999 alipokuwa nchini Italia, wakati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, alipofariki walivyoungana na watanzania kumuombea na kuomboleza kifo chake. “mwaka 1999, tulikusanyika kama Watanzania wote kumuombea na kuomboleza kifo cha Baba wa Taifa. Huo mshikamano ndio mfano wa kile tunachopaswa kuendelea kudumisha leo,” alisema.
Padre Makunde aidha alisisitiza kuwa Umoja na mshikamano ni nguzo muhimu kwa Watanzania waliopo mbali na nyumbani, na kuwataka wanafunzi kutumia hata njia za kisasa kama makundi ya simu ili kudumisha umoja wao. Padre Makunde vile vile alieleza kuwa alishangazwa kusikia jina lililochaguliwa na wanafunzi, “Wajukuu wa Nyerere,” akisema ni jina lenye uzito mkubwa na linalomwendea Mwalimu Nyerere. Aliwahimiza wanafunzi kuiga maisha, falsafa, kauli na misimamo ya Nyerere: “Jina hili ni kubwa sana. Ningependa muige mfano wa Mwalimu Nyerere kwenye kauli, misimamo, falsafa na maisha yake yote. Mienendo yenu iwe ishara ya kuenzi urithi wake,” alisema Padre Makunde.
Sherehe hiyo ya kuwapongeza wahitimu wa vyuo mbalimbali vinawakutanisha Watanzania nchini Kenya, ikiwemo chuo kikuu cha Tangaza, Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) (Catholic University of Eastern Africa), chuo cha Don Bosco Utume (Don Bosco Technical Institute Utume) na Taasisi ya Mitume wa Yesu (Apostles of Jesus Institute). Wahitimu walipongezwa kwa kukata keki na kufungua shampeni kama ishara ya furaha na mafanikio yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Kikundi cha wajukuu wa Nyerere, Ndugu Costantini Mayunga kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marianist, alipata nafasi ya kuwashukuru wanachama kwa niaba ya viongozi waliochaguliwa, akisisitiza mshikamano na kuahidi kushirikiana kwa pamoja. Pia aliishukuru Chuo cha Don Bosco Utume kwa kutoa mazingira mazuri ya kufanyia sherehe yao. Kwa upande wake Mlezi wa kundi hilo, Padre Oleseriani ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Kikatoliki cha Africa Mashariki, (CUEA)aliwapongeza viongozi waliotangulia kwa juhudi zao za kuwaleta pamoja wanafunzi wa Kitanzania chini ya mwavuli wa "Wajukuu wa Nyerere", akisema "juhudi hizo zimekuwa daraja la kuimarisha mshikamano wao wakiwa nje ya Tanzania."
Ni jukwaa linalowaleta pamoja Watanzania bila kujali kama ni wanafunzi
Sherehe hiyo pia ilihudhuriwa na Rais wa Chama Cha Wanafunzi Watazania waliko Kenya(TASAKE), Purity Moshi, ambaye aliwapongeza viongozi wapya na kuwahimiza wanafunzi na wafanyakazi wa Kitanzania waliopo Kenya kujiunga na TASAKE ili kuendeleza umoja na ushirikiano wao.“ "Ni muhimu Watanzania waliopo Kenya kupendana, kushirikiana na kujumuika pamoja. Umoja wetu ndiyo nguvu yetu,” alisema Bi Moshi. Alimtambulisha pia msaidizi wake Malim aliyeshiriki naye katika sherehe hiyo, akisisitiza kuwa TASAKE "ni jukwaa linalowaleta pamoja Watanzania wote, bila kujali kama ni wanafunzi au wafanyakazi." Sherehe hiyo ilihitimishwa kwa wito wa kuendelea kudumisha maadili ya umoja, upendo na mshikamano yaliyokuwa msingi wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huku wanafunzi wakiahidi kuendeleza urithi huo kupitia elimu, falsafa yake ya ujamaana na mshikamano.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.