Tafuta

2026.03.19Kenya: Uzinduzi wa kitabu cha taalimungu  ya sinodi ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Hekima Kenya, Machi 18,2026 2026.03.19Kenya: Uzinduzi wa kitabu cha taalimungu ya sinodi ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Hekima Kenya, Machi 18,2026 

Kenya:Uzinduzi wa kitabu cha Taalimungu ya sinodi ya Kiafrika

Uwazi mkubwa kwa upendo wa Mungu unaohitajika katika kiini cha sinodi,si kwa maslahi binafsi bali kwa msingi wa Mungu.Wito wa haki,upendo na utunzaji ambapo sinodi inashirikishwa kama safari ya ujumuishaji na kukutana.Haya yalijitokeza katika Uzinduzi wa kitabu cha Taalimungu ya Sinodi ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Hekima Kenya,tarehe 18 Machi 2026.

Sr. Christine Masivo, CPS, na Angella Rwezaula – Vatican.

Sinodi sasa inahitaji uhalisia. Ni kile kilichosisitizwa kwa kina na wawasilishaji tofauti katika uzinduzi wa kitabu chenye kichwa: “Taalimungu ya Sinodi ya Kiafrika” katika Chuo Kikuu cha Hekima jijini Nairobi, Kenya, tarehe 18 Machi 2026 ambapo walisisitiza kuwa kuna haja ya kubadilisha mjadala uliofanywa kuhusu Sinodi na kuutekeleza. Pia kuna pengo katika dhana ya sinodi kutojulikana vizuri na washiriki wa Kanisa. Sinodi lazima ikite mizizi kutoka mashinani ili kuweza kuzaa matunda yake na yaweze kuhisiwa.

Uzinduzi wa Kitubu kuhusu Sinodi Afrika
Uzinduzi wa Kitubu kuhusu Sinodi Afrika

Kwa kutumia methali ya Kiafrika "Mti mrefu una nguvu kama mizizi yake," kazi hiyo  ya kuchochea mawazo iliyohaririwa na Agbonkhianmeghe E. Orobator,  pamoja na wachangiaji wengine inahitaji kuchukuliwa hatua sasa. Katika tukio la kutia moyo la uzinduzi wa kitabu hicho walichunguza uelewa unaobadilika wa Sinodi katika Kanisa, huku wakisisitiza  umuhimu wa tamaduni, wa kusikiliza, na ushirikishwaji katika kuunda mustakabali unaoendeshwa na utume.

Kuna haja ya juhudi za ushirikiano na uthibitisho

Kwa mujibu wa Dk. Stephen Eyowa, SJ, Mkuu wa Kitivo cha  Taalimungu katika Chuo cha Hekima, alisema, "Sinodi inahusiana sana na utamaduni wa Kiafrika." Kuna haja ya wakati mwafaka wa kukuza Taalimungu ya Kiafrika, hasa katika nyanja za kitaaluma na kikanisa kuhusu Sinodi.

Kitabu kuhusu Sinodi Afrika
Kitabu kuhusu Sinodi Afrika

Kitabu hiki kiliwasilishwa kwa kutaka kumsaidia Mwafrika kuzungumza kwa sauti yake katika Kanisa la Ulimwengu, badala ya kutegemea mifumo ya kiitikadi iliyoingizwa. Kuipatia Kanisa barani Afrika rasilimali muhimu za kutafakari na kufufua fursa za uchungaji. Hii inawapatia  washirika nafasi na msingi wa kufanya kazi pamoja huku ulimwengu wetu ukikabiliwa na matatizo, na vile kitabu hicho kinaakisi mada ya “Ubuntu” kama Mwafrika na hivyo uzinduzi wa kitabu hicho  ulikumbusha umuhimu wa kufanya kazi pamoja. Kati ya washiriki tofauti waliodhuria waliweza kusisitiza kwamba "Sinodi ni tembea pamoja, na sio chaguo."

Dk Uwineza SJ:Kitabu hiki ni matokeo ya Mpango wa Sinodi ya Afrika

"Taalimungu  ya Sinodi Afrika”  si jina tu bali ni maono," alisema hayo Dk. Marcel Uwineza SJ. Hii ni wazi kuwa ni wito wa uongofu kwa Kanisa barani Afrika na ulimwenguni, uingiliaji kati unaohitajika na sauti ya kinabii katika kuunda Kanisa la baadaye. Alirudia kwamba, "Kitabu hiki kinatoka Afrika hadi ulimwenguni, kikitoa hali ya kiroho ya ulimwengu uliojeruhiwa unaohitaji uongofu wa kiroho." Hivyo Sinodi katika Kanisa ni fumbo la Mungu na si la kihierarkia bali linaanzia kwenye ubatizo.

Sinodi si mahali pa kwenda bali ni mchakato wa safari

Sinodi ina sifa ya kusikiliza, kupambanua, na kuamini. Sinodi si mahali pa kwenda bali ni safari," ambayo ni tofauti bila kujitenga; hivyo, sinodi si jambo la hiari, alisisitiza Dkt. Uwineza SJ. Aidha alisema kuwa "mustakabali wa Kanisa unategemea mizizi, na Afrika ndiyo mizizi hiyo." Ulimwengu sasa unaitazama Afrika katika mtazamo wa uinjilishaji wake.

Askofu Saldarriaga,SJ: Kuna hatari ya kuzungumzia Sinodi bila hatua

Kwa upande wa Askofu Rodrigo Mejía Saldarriaga,SJ, mwanzilishi mwenza katika Chuo Kikuu cha Hekima katika uzinduzi huo, alisema, "Faida ya sinodi ni kwamba iko katika maandalizi; ni kuwa sherehe na kukaa pamoja." Sinodi lazima kuuishi na inahitaji mabadiliko ya mawazo, mtazamo, na vitendo. Alielezea masikitiko yake kwamba Sinodi inazungumziwa, lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Alibainisha kuwa safari ya Sinodi inapaswa kubadilishwa kwa ajili ya malezi ya kipadre, muundo mzima unapaswa kurekebishwa katika muktadha wa Sinodi, na Baraza la Maaskofu Katoliki linapaswa kualikwa ili kuchangia Kanisa zima.

Wakati wa uzinduzi wa Kitabu kuhusu Sinodi
Wakati wa uzinduzi wa Kitabu kuhusu Sinodi

Sr Veronica Rop,ASE, mchango wa watawa wa kike,bado hawana sauti Afrika

Kwa upande wa Dk. Sr. Veronica Rop,ASE, alichangia kitabu hicho kuhusiana na mchango wa wanawake waliowekwa wakfu katika eneo la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki(AMECEA). Alifuatilia misingi ya maisha ya kitawa tangu wamisionari wa mwanzo waliofika barani Afrika na kufanya kazi kubwa kuhusu elimu, afya, na huduma ya kichungaji, na kazi yao imeonekana.

Sr Veronica akitoa mchango wake
Sr Veronica akitoa mchango wake

"Masista hawana sauti kanisani,  ya kuchangia kama roho ya Sinodi inavyoita,"alisema Sr Veronica. "Labda ni kutoka na utamaduni wa Kiafrika kwa mwanamke kuonekana hivyo na asisikilizwe." Watawa wa kike  wanapaswa kupewa sauti na nafasi ya kutekeleza yale waliyojifunza, na kizazi kipya kinapaswa kutumia nafasi ya kidijitali na kuwa wamisionari katika nafasi yao wenyewe. Tunaomba kuthaminiwa na kutembea kwa kujiamini na kuelewa sisi ni nani kama wamisionari. "Bila wanawake Watawa, tungekuwa nini Afrika?" aliuliza swali

David Kaulemu, SJ, Sinodi huchangamotisha na huambatana na uongofu wa kiroho

Naye David Kaulemu, SJ, mchangiaji mwingine na mshiriki kutoka Zimbabwe, alishirikisha mchango wake kulingana na mchakato wa sinodi kama “safari ya kazi iliyoanza.” Sinodi huchangamotisha  na huambatanisha uongofu wa kiroho. Inalenga msingi wa kitaalimungu na wajibu wake kwa mafundisho ya Kanisa na tamaduni ya Kikristo, ikitoa wito wa kupyaishwa na kuruhusu washiriki wote kuchangia ndani ya Kanisa. Wachangiaji walipongeza kitabu, hicho kama vile Dkt. Kaulemu, SJ, alivyobainisha kuwa; hii inahitaji uwajibikaji wa kiroho na upendo katika kusafiri pamoja kwa njia mpya katika Kanisa, ulimwengu, na Roho Mtakatifu.  

Uzinduzi wa Kitabu kuhusu Sinodi Afrika
Uzinduzi wa Kitabu kuhusu Sinodi Afrika

Dk. Anthony Egan, SJ: kuna haja ya mazungumzo katika roho ya uhuru na utambuzi

Kwa upande wa mzunguzaji mwingine Dk. Anthony Egan, SJ, ambaye alibainisha kuwa mazungumzo, utambuzi, na uaminifu ni muhimu sana na vinahitajika sana katika safari hii ya sinodi. "Kuna haja ya mazungumzo katika roho ya uhuru na utambuzi sahihi kutoka kwa Roho na kwa uaminifu wa kweli kutoka  pande zote ambao ni muhimu kwa manufaa ya wote. Kwa hivyo utambuzi unahitajika badala ya udanganyifu."

Wakati wa Uzinduzi wa Kitabu kuhusu Sinodi Afrika
Wakati wa Uzinduzi wa Kitabu kuhusu Sinodi Afrika

Dk Chikoje:Sinodi inasisitiza mawasiliano kwa jamii na ushirika kuhusiana na Utatu

Dk. Chijoke alishirikisha  mchango wake kulingana na mawasiliano ya kisasa, akisisitiza kwamba sinodi inasisitiza mawasiliano ambayo ni muhimu kwa jamii na ushirika kuhusiana na Utatu. Alibainisha kuwa uwajibikaji wa mtu binafsi hujikita katika hekima ya jamii na huleta kila kitu pamoja. Pia alisisitiza ushiriki wa vijana katika nafasi ya kidijitali na kuwapatia vijana na wanawake sauti ambayo haiwaogopi na sio kuwakandamiza. Lakini badala yake wawe katika jumuiya, ambayo ni mwili mmoja.

Uzinduzi kuhusu Sinodi Afrika
Uzinduzi kuhusu Sinodi Afrika

Dk. Marcel SJ:Wengi hawajuhi Sinodi ni nini, mabadiliko huja na upinzani

Dk. Marcel SJ alisema, "Niliona kwamba kuna upinzani mwingi kwa sababu wengi hawaelewi Sinodi ni nini; mabadiliko huja na upinzani." Sinodi ni njia ya msingi ya kuwa na Mungu, Mungu akielekea ubinadamu na ubinadamu ukiitikia,” alisema. Katika mchango wake alibainisha uwazi mkubwa kwa upendo wa Mungu unaohitajika katika kiini cha sinodi, si kwa maslahi binafsi bali kwa msingi wa Mungu. Wito wa haki, upendo, na utunzaji ambapo sinodi inashirikiswa kama safari ya ujumuishaji na kukutana.

Maswali wakati wa uzinduzi wa kitabu kuhusu Sinodi
Maswali wakati wa uzinduzi wa kitabu kuhusu Sinodi

Kanisa lina asili ya Kihierarkia

Mababa wa Kanisa waliishi sinodi na Kanisa linafanana na sinodi. Kanisa lina asili ya kihierarkia, likiwaita watu kuwa wa jumuiya, badala ya kihierarkia, likihama kutoka mamlaka hadi huduma. "Sinodi inawaalika wote kutoka katika kutengwa hadi kujumuishwa, na sinodi ina matumaini kwa ulimwengu wa kisasa unaowahusisha wale wanaokutana mezani, hasa wanawake," alisema. "Imekuwa safari ya sinodi katika kuandika kitabu hiki, na ni mfano mzuri wa sinodi ya uzoefu wa sinodi bora kabisa."

Uzinduzi wa kitabu kuhusu Sinodi Afrika
Uzinduzi wa kitabu kuhusu Sinodi Afrika

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

 

19 Machi 2026, 10:37