Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu ni chemchemi ya maji ya uzima. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu ni chemchemi ya maji ya uzima.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika ya Tatu ya Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Yesu Ni Maji ya Uzima

Liturujia ya Neno la Mungu inatutafakarisha kuwa, “Kristo Yesu ni Chemchemi ya Maji ya Uzima” Katika Dominika hii tunakutana na Mungu anayejibu kiu ya Mwanadamu anayemtafuta katika safari ya jangwani. Mtakatifu Exupery anasema Kisima ni chemchemi ya maisha. Mwanamke katika Injili ya leo licha ya kubahatika kukutana na wanaume wengi katika maisha yake, lakini bado aliendelea kukabiliana na ukame na kiu ya upendo wa dhati na kweli. Muhimu imani kwa Yesu.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 3 ya Kwaresma, mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu inatutafakarisha kuwa, “Kristo Yesu ni Chemchemi ya Maji ya Uzima” Katika Dominika hii tunakutana na Mungu anayejibu kiu ya Mwanadamu anayemtafuta katika safari ya jangwani. Mtakatifu Exupery anasema Kisima ni chemchemi ya maisha. Mwanamke katika Injili ya leo licha ya kubahatika kukutana na wanaume wengi katika maisha yake, lakini bado aliendelea kukabiliana na ukame na kiu ya upendo wa dhati na kweli. Kumbe, imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, Maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; Kufunga na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni mambo yanayozima kiu ya dhamiri nyofu. Jangwa la maisha ya binadamu linaweza kustawi na kushamiri ikiwa kama litamwagiliwa na chemchemi ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mwenyezi Mungu anajidhihirisha katikati ya kiu ya taifa lake teule, licha ya udhaifu wao, anawapatia maji na kutuliza kiu yao ya muda mfupi. Katika Agano jipya Kristo anajifunua kwetu kama Maji ya Uzima. Sisi taifa jipya la Mungu kwa njia ya Ubatizo, tunashirikishwa uzima wa milele wa Kimungu katika fumbo la Pasaka, si kwa mastahili yetu, bali kwa njia ya neema ya Roho Mtakatifu. Hivyo masomo yetu kuanzia Dominika hii ya 3, 4 na ya 5, yanatuekeza moja kwa moja kutafakari Fumbo Takatifu la Pasaka. Utaratibu huu wa masomo haya katika Dominika hizi tatu, tangu kale ulilenga katika maandalizi ya mwisho ya Wakatekumeni, ambao wanajiandaa kuzaliwa upya katika Ubatizo katika mkesha wa Pasaka. Katika Dominika hii, tumshukuru Mungu, ambaye hakumwacha mwanadamu apotee, bali kwa njia ya Kristo amefanya tena uumbaji mpya, katika Maji na Roho Mtakatifu. Tuwaombee Wakatekumeni wote katika safari na kiu yao ya kuzaliwa upya, ili washirikishwe uzima wa Kimungu na Kristo Mfufuka katika Ubatizo.

Ubatizo ni chemchemi ya maisha mapya
Ubatizo ni chemchemi ya maisha mapya   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Kutoka 17:3-7. Somo la kwanza kutoka katika kitabu hiki cha Kutoka ni simulizi la safari ya wana wa Israeli jangwani baada ya kuvuka Bahari ya Shamu, ambapo walipofika katika eneo lililoitwa Refidimu, walikutana na changamoto kubwa sana ya maji. Wakahofia kufa kwa kiu, wao pamoja na mifugo yao. Mwenyezi Mungu anatuliza kiu yao ingawa hawakustahili, Ishara ya Mungu asiyewaacha kamwe watu wake katika mahangaiko yao. Ningependa tutafakari somo hili kwa kuangazia mambo matatu muhimu yafuatayo: Jambo la kwanza: Taifa la Israeli wapo safarini, ni safari ya jangwani, ni safari ya kila mmoja wetu. Kitabu cha Kutoka, kimsingi kinaeleza mwanzo wa safari ya Taifa la Mungu kutoka utumwani Misri kuelekea katika nchi ya Ahadi. Laelezea namna Mwenyezi Mungu kwa upendo wake mkuu alivyowatendea mambo makuu katika historia hii ya kusisimua ya ukombozi wao kutoka Misri. Walianza safari mpya, kutoka utumwani, kuelekea pumzikoni katika nchi ya Ahadi, nchi iliyojaa maziwa na Asali. Mwenyezi Mungu mwenyewe aliwatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo ili awaongoze njia, na usiku ndani ya moto mfano wa nguzo ili kuwapa nuru wapate kusafiri mchana na usiku (Kut 13:21). Mungu aliyewatoa Misri alikuwa pamoja nao wakati wote, hadi kufikia nchi ya Ahadi.

Kristo Yesu ni chemchemi ya maji ya uzima mpya
Kristo Yesu ni chemchemi ya maji ya uzima mpya   (ANSA)

Ndugu mpendwa, safari ya wana wa Israeli kutoka utumwani Misri kuelekea nchi ya Ahadi ni safari ya kila mmoja wetu. Kwa dhambi sisi sote tulikuwa utumwani, ni utumwa wa dhambi na mauti. Kwa njia ya Ubatizo wetu, sisi sote tumeanza safari mpya ya maisha. Mwenyezi Mungu kwa mkono wake wenye nguvu ametukomboa kutoka katika nguvu za giza na vifungo vya shetani na kutufanya kuwa tena wana wateule, wana wa nuru. Anatembea daima mbele yetu, yupo pamoja nasi wakati wote, anatuangazia njia ili tutembee daima katika nuru yake kuelekea nchi yetu ya Ahadi, nyakati za giza yupo nasi, nayakati za mwanga yupo daima mbele yetu. Dominika hii ni ya pekee kwa Wakatekumeni, wanaojiandaa kupokea sakramenti ya Ubatizo katika mkesha wa ufufuko wa Bwana. Tunawaombea ili nao waimarike katika safari yao kuelekea kuzaliwa kwao upya katika ubatizo. Jambo la pili: Wakiwa jangwani wanakutana na changamoto, wanamnung’unikia Mungu, Ishara ya ukosefu wa imani. Baada ya Mwenyezi Mungu kwa mkono wake wenye nguvu kuwavusha watu wake Bahari ya Shamu, waliingia rasmi katika jangwa. Ni mazingira magumu, hapakuwa na chakula, hapakuwa na maji, hapakua na usalama. Lakini jambo moja kubwa walilopaswa kukumbuka ni kwamba, Mungu alikuwa mbele yao, aliwatangulia. Somo hili kutoka 17:3-7 walifika Eneo la Refidimu, hapo hapakua na maji. Wanafanya nini? Wasahau kama Mungu alikua mbele yao. Wanateta na Musa, “Tupe maji tunywe” (Kut 17:2). Musa anaona wazi kuwa watu hawa si tu walikua na kiu bali walikosa Imani kwa Mungu aliyewatendea mambo makuu huko kote. Wanadiriki hata kuona kana kwamba maisha ya Misri yalikua bora. Wanaona kama vile ulikua ni mpango wa Musa na Mungu kuwatoa Misri ili kuwaua wao na watoto wao na Wanyama wao kwa kiu. Je, Mungu aliyewaleta jangwani, siye aliyewapiga wazaliwa wa Misri? Siye aliyeipasua Bahari wakapita? Siye aliyewapa mana wakala jangwani?  Sasa wanataka kumpiga Musa kwa Mawe, Ishara ya ukosefu mkubwa wa Imani.

Kwa Ubatizo waamini wanashirikishwa Umungu wa Kristo
Kwa Ubatizo waamini wanashirikishwa Umungu wa Kristo

Ndugu mpendwa, kila mara tunaposoma simulizi la safari ya wana wa Israeli na namna walivyohusiana na Mungu aliyewatoa utumwani, tunaweza kuwashangaa tunasema, hivi hawa walikua ni watu wa namna gani? Kwa nini hawakuona mambo yote Mungu aliyowatendea, hawaoni wema wa Mungu, wanalalamika na kunung’unika kwa kila jambo. Lakini kiuhalisia safari ya maisha ya wana wa Israeli ndiyo safari ya maisha yetu sisi ya kila siku. Kila mmoja wetu Mungu amemwita katika njia yake ya maisha Ingawa sote tupo safari moja kuelekea uzima wa milele. Mungu anajua fika kuwa sio safari rahisi, lakini hatuachi, yupo mbele yetu daima. Nyakati mbalimbali tunapoona mambo yanakwenda ndivyo sivyo kama tulivyotarajia, huenda ni ndoa inapitia misukosuko, huenda ni wito wangu/wako kama padre, kama mtawa, kama kijana mwenye malengo mbalimbali, katika kazi, masomo, mahusiano, katika biashara mambo yanayumba. Mambo hayakwendi vile nilitarajia, tunafikiri Mungu hayupo pamoja nasi. Tunaona kama Mungu ametuhadaa, kana kwamba ulikua ni mpango wa Mungu tuteseke, au tupitie changamoto hizi. Tunaona kama Mungu tuliye naye sasa sio Mungu yule yule tuliyekuwa naye wakati mambo yalipokuwa shwari. Tunaona huyu Mungu tuliye naye katika bonde la changamoto, sio Mungu tuliyekuwa naye wakati tulipokuwa kwenye kilele cha mafanikio na furaha yetu. Tunaona kama Mungu hayupo hapa, kana kwamba Mungu hachukulii kwa uzito hali hii ninayopitia sasa. Ndugu mpendwa, Mungu aliyekuwa nawe katika kilele cha mlima ndiye Mungu uliye naye, niliye naye hata katika bonde sasa. Mungu aliyegawanya Bahari nikapita, aliyetengeneza njia, ndiye Mungu aliyenileta hapa kwenye jangwa tupu na kame. Ni Mungu huyu huyu yupo nawe katika ndoa inayoyumba, katika mahusiano yenye misukosuko, katika wito wako unapokata tamaa, katika mahangaiko yako ya kutafuta ajira, katika changamoto yako ya afya unayopitia, katika mtikisiko wa kiuchumi unaopitia sasa, katika biashara zako zinazozorota, na katika kila hali tunayopitia. Tazama mbele, anakwenda mbele yetu, anataka tumwamini, He is in control. Anataka tufike mwisho wa safari yetu salama tukiwa naye.

Mwenyezi Mungu anazima kiu ya Waisraeli
Mwenyezi Mungu anazima kiu ya Waisraeli

Jambo la Tatu: Mwenyezi Mungu anatutazama kwa huruma, anatuliza kiu yetu. Nini jibu la Mwenyezi Mungu kwa watu hawa waliokosa Imani? Mwenyezi Mungu haiibu kwa ukali, wala hawaadhibu licha ya udhaifu mkubwa wa taifa lake Israeli. Kinyume chake anamwamuru Musa kuichukua ile fimbo aliyoipigia Bahari ya Shamu nayo ikagawanyika, na akalipige lile Jabali katika Horebu, na hapo maji yalitoka na watu wakanywa. Mungu anamwambia Musa, “Tazama nitasimama mbele yako huko juu ya lile Jabali huko Horebu” Mwamba na Fimbo ya Musa ni Ishara ya uwepo thabiti wa Mungu kati ya watu wake. Maji yanayotiririka kutoka kwenye mwamba ni zawadi ya uhai ambayo iliwadumisha na kutuliza kiu ya Wana wa Israeli katika safari yao yote jangwani.  Ndugu mpendwa kama nivyotangulia kusema hapo mwanzo, kila mmoja wetu katika safari yake ya maisha, na hata sasa tuwapo katika safari yetu ya mfungo wa Kwaresma, kila mmoja wetu ana kiu yake. Zaweza kuwa ni changamoto kama nilivyoeleza hapo awali, migogoro, changamoto za afya, kukata tamaa, changamoto za kifamilia, changamoto za biashara, huenda ni masomo. Lakini si changamoto tu, tuna matamanio yetu mbalimbali, nia zetu nyingi ambazo tunatamani Mungu atende kitu kwa ajli yetu na kwa ajili ya wengine katika safari yetu. Hatupaswi kukata tamaa wala kunung’unika kipindi Mungu anapofanyia kazi sala zetu na maombi yetu. Mwenyezi Mungu pekee ndiye anayeweza kutuliza kiu zetu zote. Anatuamuru kama alivyomwamuru Musa, si kwa ukali, bali kwa sauti ya upole, katikati kabisa ya ukame na kiu ya maisha yetu, akiwa amesimama mbele yetu “Chukua fimbo yako, piga katika mwamba.”

Yesu anakutana na Mwanamke Msamaria: Kiu ya huruma ya Mungu
Yesu anakutana na Mwanamke Msamaria: Kiu ya huruma ya Mungu

Pale unapodhani hakuna tumaini tena Mungu ndipo anakuonesha ukuu na nguvu yake. Fimbo yetu kwanza kabisa ni Imani thabiti, fimbo yetu ni matumaini yasiyotetereshwa na hali tunazopitia, tukiamini kuwa Mungu ana nguvu kuliko hali yoyote ile hata kama ni ngumu na ya kutisha namna gani. Fimbo yetu ni Neno la Mungu, Neno lenye nguvu ya kupasua Bahari na kutengeneza njia, ya kupasua mwamba na kutoa maji, Fimbo yetu ni Sakramenti za kanisa, zinazotupa nguvu ya kuendelea kutembea katika njia yetu, hata kama ina miiba, hata kama ina miamba, hata kama ina nyoka wa kutisha, hata kama ina maadui wa kila namna. Inua fimbo yako sasa. Mwenyezi Mungu atasimama mbele yako. Hatupaswi kulalamika, hatupaswi kuona shaka, hatupaswi kuhangaika huku na kule kutafuta kutuliza kiu ya maisha yetu, bali kubaki katika Imani kwa Mungu mmoja. Kutaniko la Kristo na Mwanamke Msamaria katika somo la Injili lawakilisha taifa jipya la Israeli, ambalo mara kadhaa walimwacha Mungu wa kweli na kuabudu miungu wengine, kutafuta faraja na kitulizo cha kiu zao kutoka kwa miungu mingine kama Baali nk. Kristo anakutana na mwanadamu aliye na kiu ya kumtafuta Mungu, na anatuliza kiu yetu, yeye ndiye chemchemi ya uzima. Kristo anakutana nasi hata sasa.

Saa Sita ina umuhimu wa pekee katika maisha ya Mwanamke Msamaria
Saa Sita ina umuhimu wa pekee katika maisha ya Mwanamke Msamaria

Somo la Injili Ni Kama ilivyoandikwa na Yohane 4:5-42. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Yohane ni simulizi refu la kutaniko la Yesu na Mwanamke Msamaria katika mji wa Sikari karibu na kisima cha Yakobo. Ni eneo lililokaliwa na watu wa Mataifa, wapagani. Katika somo hili ningependa tutafakari kwa kina mambo matano yafuatayo ambayo ni msingi sana katika kuelewa ujumbe wa Injili hii ya leo, na kuona ni jinsi gani yanatugusa sisi pia katika maisha yetu ya kila siku, hususani katika safari yetu kuelekea Fumbo la Pasaka. Jambo la kwanza: Kutaniko la Kristo na Mwanamke Msamaria maana yake ni nini? Kwa nini saa sita, ina maana gani kwetu sisi. Bwana wetu Yesu Kristo akiwa safarini kuelekea Yerusalemu, alipita katika njia ambayo wengi hawakupenda kuitumia, kutokana na uadui uliokuwepo kati ya Wayahudi na Wasamaria. Wasamaria tukumbuke walikua ni mchanganyiko wa Wayahudi na Waashuru baada ya kupelekwa utumwani mwaka ule 722 BC. Huko walipoteza utambulisho wao wa kitaifa kama Wayahudi, na utambulisho wao wa kidini kwa kuwa waliabudu miungu mingi ya Wapagani katika Hekalu lililojengwa katika mlima Gerizimu. Hali hii katika maandiko matakatifu ilifananishwa na Mwanamke ambaye alikosa uaminifu kwa Mumewe, kwa kuwa Agano kati ya Mungu na watu wake lilikua kama Agano la ndoa Takatifu.

Waamini wanazaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu
Waamini wanazaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu   (@Vatican Media)

Hivyo Kutaniko hili ni kutaniko kati ya Mungu na taifa lake jipya, litakalotakaswa kwa maji na ubatizo na kwa roho Mtakatifu. Ni ufunuo wa Mungu anayevunja kuta na mipaka yote ya uadui kati ya watu, Mungu anayevunja ukuta wa ubaguzi wa kijinsia (rabi hawakupaswa kuzungumza na Wanawake hadharani). Ni Mungu anayemkaribia yeye aliyeonekana na jamii nzima kama mdhambi, (mwenye wanaume watano, aliyetengwa, akisimama kuwakilisha watu wa mataifa, waliotengwa, walioonekana hawana thamani, walioonekana wadhambi, wenye wanaume wengi, yaani wanaoabudu miungu mingine). Kumbe ni Mungu anayetutafuta kwanza sisi, licha ya udhaifu wetu. Huruma yake ni kubwa kuliko udhaifu na dhambi zetu. Lakini kwa nini saa sita? Mwanamke alikwenda saa sita kwa kuwa ulikua ni muda ambapo asingekutana na yeyote kutokana na picha mbaya aliyokua nayo kwenye jamii yake. Ni muda ambapo jua lilikua kali na Kristo alikua na kiu. Lakini tukumbuke si kiu tu ya maji, bali ni kiu ya kumtafuta mwanadamu, ndiyo kiu aliyoiona hata saa yake ilipotimia pale Msalabani, aliposema nina kiu “Sitio” Ilikuwa ni kiu bado ya kumtafuta na kumkomboa mwanadamu aliyepotea. Ndio maana anawaambia wanafunzi wake kwamba njaa na kiu yake ni kuyatenda mapenzi ya Mungu. Mwanamke huyu anatafuta muda ambapo alikua yeye peke yake, kwenda kutafuta maji na hapo anakutana na Kristo. Kumbe ni katika ukimya, Kristo anakutana nasi na kutuliza kiu ya mioyo yetu. Je, nina ukimya? Nina jitihada binafsi za kumtafuta Mungu, Mungu ambaye ana kiu kila siku ya kunitafuta na kukutana nami?

Kanisa la Ubatizo wa Bwana
Kanisa la Ubatizo wa Bwana

Jambo la pili: Maji haya anayozungumzia Kristo Kristo, maji ya uzima, maana yake ni nini? Kristo anakutana na mwanamke huyu msamaria Kisimani. Kwa tamaduni za wayahudi kisimani ilikua ni sehemu ambapo watu walipatia wachumba. Yakobo alikutana na mkewe Raheli katika kisima (Mwa. 29). Ni katika mazingira hayo, Yesu (Bwana Arusi) anakuja kisimani kukutana na mwanadamu (Bibi Arusi, wakati huu akiwakilishwa na mwanamke Msamaria/Mataifa) ili kuanzisha Agano Jipya la Upendo.  Yesu anasimama kwenye kisima cha kale ili kuonyesha kuwa Yeye ni mkuu kuliko Yakobo. Anatoa kitu kipya, Maji ya Uzima (Neema) ambayo hayahitaji “mtungi” wa juhudi za kibinadamu pekee, bali yanabubujika ndani ya roho. Maji haya ndiye Roho Mtakatifu tuliyempokea katika Ubatizo wetu. Kupitia maji ya Ubatizo, tunakufa na kufufuka pamoja na Kristo katika uzima mpya. Maji ya kawaida yanatuliza kiu kwa saa chache, lakini maji ya Yesu yanatuliza kiu ya milele ya mwanadamu. Ni hitimisho kuwa mwanadamu ana kiu moyoni mwake ambayo haiwezi kutulizwa na mambo ya ulimwengu huu, mambo ya muda na ya kupita tu bali kwa uzima utokao kwa Mungu, kama tulivyotafakari katika somo lile la kwanza. Jambo la tatu: Kwa nini hapa anatajwa Mume, “Yesu akamwambia, nenda kamwite Mume wako”, maana yake ni nini? Mahusiano ya Mungu na taifa lake teule yanaelezwa kama mahusiano ya ndoa kati ya Mume na Mke. Mwanamke huyu anajibu, “Sina Mume” Kristo anamwambia umesema vyema, kwa maana umekua na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako.”

Kutabarukiwa kwa Kanisa la Ubatizo wa Bwana
Kutabarukiwa kwa Kanisa la Ubatizo wa Bwana

Ndugu mpendwa, mume anayetajwa hapa sio tu mume, bali ni miungu wengi. Mwanamke huyu anawakilisha watu wa mataifa walioabudu miungu ya uwongo kama vile Baal na Ashteroth katika hekalu huko mlimani Gerizimu. Miungu hawa kimsingi hawakuweza kumpa mwanamke yule furaha ya kweli na uzima wa kudumu. Sisi sote tuliobatizwa, tulioshirikishwa uzima wa kimungu kwa njia ya Maji na Roho Mtakatifu hatupaswi tena kuwa na miungu mingine. Hatupaswi kutafuta uhai na uzima wetu nje ya Kristo aliye chemchemi ya uzima wetu. Huenda tumekua tukihangaika huku na kule tukitafuta faraja, usalama na uzima wa kweli katika mambo mengi, ambayo yamediriki hata kuchukua nafasi ya Mungu. Hayo twapaswa kuyaacha kwa kua ni Kristo pekee atulizaye hamu ya mioyo yetu. Jambo la nne: Saa anayoizungumzia Kristo Yesu, “Saa inakuja” ambapo waabuduo halisi watamwabudu Mungu katika roho na kweli, maana yake ni nini? Kabla ya Yesu, ibada ilitegemea maeneo ya kijiografia (Mlima Gerizimu kwa Wasamaria au Yerusalemu kwa Wayahudi). Waabuduo wa kweli ni wale wanaoelewa kuwa Mungu hafungwi na jengo au mlima. Hekalu la kweli sasa ni mwili wa Kristo. Nasi sote tuliobatizwa tunafanywa kwa namna ya pekee kuwa hekalu hilo la Roho Mtakatifu. Waabuduo wa kweli ni wale ambao mioyo yao imeguswa na Roho Mtakatifu. Ibada yao inatoka ndani ya nafsi, si kwa mazoea au kwa kufuata tu mapokeo na sheria za kidunia.

Maji Ni Uhai
Maji Ni Uhai   (ANSA)

Ni ibada hai inayochochewa na nguvu ya Mungu ndani ya mtu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ametoa moyo wa jiwe ulio ndani mwetu naye ameandika sheria yake ndani ya mioyo yetu ya nyama. Ni katika saa ya mateso yake msalabani, Kristo atalitimiza hilo. Mungu anatutafuta daima na anatualika ili tumwabudu katika roho na kweli. Nimefungua moyo wangu, ili ujazwe daima na neema za Mbinguni, ili niweze kuishi maisha yanayompendeza Mungu na ibada yangu ipate kibali mbele za Mungu? Huruma ya Mungu ni kuu, anatusukuma kila mara kuiendea, ili tupate uzima. Jambo la tano: Mwanamke anauacha mtungi wake, anakwenda mjini. Anakua mmisionari. Mwanamke Msamaria baada ya Kristo kujifunua kwake (Mimi ninayesema nawe ndiye), naye anamtambua kama na kumkiri, kwanza, anaacha mtungi wake. Mtungi ulikuwa chombo kilichomuunganisha na maisha yake ya zamani, maisha ya kiu isiyoisha, aibu ya kujificha kwa sababu ya dhambi na mahangaiko ya kila siku, ambayo kimsingi yalikua ndiyo kiu yake. Anapoacha mtungi, anaacha mzigo wa dhambi na mambo yote yaliyomuunganisha na maisha ya kale. Ameupata uzima ambao hauhitaji tena visima vya kidunia, amempata Kristo, chemchemi ya uzima. Pili anakwenda kutoa ushuhuda, anakuwa mmisionari. Huko anawaambia watu, “Njooni mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda. Matokeo yake, watu wengi katika Samaria walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke.

Maji ni bidhaa muhimu katika maisha
Maji ni bidhaa muhimu katika maisha   (AFP or licensors)

Ndugu mpendwa, kila anayekutana na Kristo, kila anayeitwa kuwa mfuasi anaacha maisha ya kale na kuanza maisha mapya. Mitume walivyoitwa na Kristo, waliacha kila kitu. Kama vile Petro na Yohane walivyoacha nyavu zao, na Mathayo alivyoacha meza ya ushuru, mwanamke huyu anaacha mtungi. Nasi kila tunapokutana na Kristo tunapaswa kuacha kabisa maisha ya kale. Tunapaswa nasi kuachana na mitungi yetu. Hatuwezi kuwa wamisionari wa kweli ikiwa bado tumeshikilia "mitungi" ya kale (tabia, aibu, hofu, tamaa, vinyongo, wivu, chuki, visasi, mashaka au usalama na faraja katika mambo ya kidunia). Tunapaswa kuwa huru ili tuweze kukimbia kwenda kuwajulisha wengine, matendo makuu aliyututenda Mungu. Katika kipindi hiki cha kwaresma tuombe neema ya kuacha mitungi yetu ili Kristo atakapofufuka tupate nasi nguvu na ujasiri wa kukimbia kwenda kumshuhudia katika ulimwengu. Somo la Pili: Ni Kutoka Katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Rum 5:1-2, 5-8. Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anatufundisha kuwa ni Mungu aliyeanza kutupenda sisi bila hata mastahili yetu. Hapo mwanzo tulikua wadhambi, lakini bado Mungu amedhihirisha kiu yake ya kuendelea kumtafuta Mwanadamu aliyepotea. Ukombozi huo unatimia kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Nasi sote kwa njia ya ubatizo, tunashirikishwa neema hiyo, uzima huo wa Kimungu. Roho Mtakatifu akaaye ndani mwetu anatuwezesha tumpende Mungu na kwa ujasiri tuweze kumwita Baba. Hitimisho: Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu ambaye ameanzisha na kukamilisha safari mpya ya ukombozi wa milele wa wanadamu wote. Tuombe neema ya kusikia sauti ya Mungu kila siku na kuwa tayari kukumbatia upya wa maisha ili nasi tustahilishwe kuupata uzima wa milele.

Kwaresima D 3
07 Machi 2026, 16:21