Tafuta

Tafakari Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Mtakatifu Exupery anasema Kisima ni chemchemi ya maisha. Tafakari Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Mtakatifu Exupery anasema Kisima ni chemchemi ya maisha.  (ANSA)

Tafakari Dominika ya Tatu ya Kipindi Cha Kwaresima Mwaka A: Kiu ya Uzima wa Milele

Kisima ni chemchemi ya maisha. Mwanamke katika Injili ya leo licha ya kubahatika kukutana na wanaume wengi lakini bado aliendelea kukabiliana na ukame na kiu ya upendo wa kweli. Kumbe, imani kwa Yesu na Kanisa lake, Maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; Kufunga na Matendo ya huruma ni mambo yanayozima kiu ya dhamiri nyofu. Jangwa la maisha ya binadamu linaweza kustawi na kushamiri ikiwa kama litamwagiliwa na chemchemi ya Neno la Mungu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya Tatu ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kiliturujia katika Kanisa. Mtakatifu Exupery anasema Kisima ni chemchemi ya maisha. Mwanamke katika Injili ya leo licha ya kubahatika kukutana na wanaume wengi katika maisha yake, lakini bado aliendelea kukabiliana na ukame na kiu ya upendo wa dhati na kweli. Kumbe, imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, Maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; Kufunga na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni mambo yanayozima kiu ya dhamiri nyofu. Jangwa la maisha ya binadamu linaweza kustawi na kushamiri ikiwa kama litamwagiliwa na chemchemi ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kadiri ya mapokeo ya Kanisa, dominika hii linafanyika takaso la kwanza la wakatekumeni watakaobatizwa katika Liturujia ya mkesha wa Pasaka, na kupokea uzima mpya rohoni mwao kwa kuondoleo ya dhambi. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafundisha kuwa; “Ubatizo Mtakatifu ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho na mlango unaowezesha kuzipata Sakramenti nyingine. Kwa njia ya Ubatizo tunafanywa huru toka dhambi na tunazaliwa upya kama watoto wa Mungu, tunakuwa viungo vya Kristo na tunaingizwa katika Kanisa na tunafanywa washiriki katika utume wake: Ubatizo ni sakramenti ya kuzaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu”, na Yesu Kristo ndiye Chemichemi ya uzima wa milele na Wokovu wa wote (KKK 1213). Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inatupa ujumbe wa matumaini, ikisema; “Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu. Uniangalie na kunifadhili, maana mimi ni mkiwa na mteswa” (Zab. 25:15-16). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu, wewe ndiwe asili ya rehema zote na mema yote. Umeonyesha kuwa dawa ya dhambi ni kufunga, kusali na kuwapa maskini. Utusikilize kwa wema sisi tunaokiri unyonge wetu, ili tunaponyenyekea moyoni, utuinue daima kwa huruma yako.”

Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa   (ANSA)

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Kutoka (Kut 17: 3-7). Ni manung’uniko ya Israeli kwa kukosa maji walipokuwa jangwani baada ya kukombolewa kutoka utumwani Misri. Kwa manung’uniko yao walimkosea Musa na Mungu, wakasahau mema yote aliyowatendea kwa mkono wake, wakatenda dhambi. Licha ya makosa yao, Mungu aliwasamehe dhambi zao, akatenda muujiza, akawapa maji, hata kama hawakustahili. Maji haya ni ishara ya ubatizo wetu unaotuondolea dhambi zetu na kutupatia uzima pasipo mastahili yetu kwa njia ya Yesu Kristo, anayetuongoza kuelekea nchi yetu ya ahadi, yaani mbinguni, kwa kuisikiliza sauti yake kama zaburi ya wimbo wa katikati inavyosema; “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu; Kama vile huko Mriba, hapo waliponijaribu baba zenu, wakanipima, wakayaona matendo yangu. Njoni tumwimbie Bwana, tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, tumfanyie shangwe kwa zaburi. Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba. Kwa maana ndiye Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho yake, na kondoo wa mkono wake.” (Zab. 95:8-9, 1-2, 6-7). Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 5:1-2, 5-8). Ujumbe wake ni kuwa Mungu alitupenda tangu mwanzo, hata tulipokuwa adui kwake kwa kutenda dhambi alituletea wokovu bila mastahili yetu, akajipatanisha nasi kwa njia Yesu Kristo Mwanae wa pekee, akatupa na zawadi ya Roho Mtakatifu ambaye anatuwezesha kumpenda na kumwita Baba. Ni kwa upendo wake, Yesu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu, akatuletea uzima wa kimungu ndani mwetu tunaoupokea kwa njia ya ubatizo. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa maji ya ubatizo ni alama ya maziko ya mkatekumeni katika mauti ya Kristo ambamo anafufuka pamoja naye ambaye ni kiumbe kipya. Hivyo ubatizo unatujalia kuzaliwa kwa mara ya pili, kwa maji na Roho Mtakatifu ambako bila kuzaliwa kwa namna hiyo, hakuna kuingia katika ufalme wa Mungu (rej. KKK 1214-1215).

Jangwa la maisha ya kiroho linaweza kurutubishwa kwa Neno na Sakramenti
Jangwa la maisha ya kiroho linaweza kurutubishwa kwa Neno na Sakramenti

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 4:5-42). Ni simulizi la mwanamke Msamaria kukutana na Yesu katika kisima cha Yakobo. Fundisho kuu ni hili; Yesu Kristo ni chemchemi ya maji ya uzima wa milele, ambaye katika Pasaka yake amewafungulia watu wote chemchemi ya ubatizo kwa mateso yake, ndio ubatizo ambao Yeye alipaswa kubatizwa nao. Damu na Maji vilivyotoka ubavuni mwake ni ishara ya Ubatizo na Ekaristi, sakramenti za uzima mpya ambazo kwazo kumekuwa na unawezekano wa kuzaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu ili kuingia katika Ufalme wa Mungu. Hivyo ubatizo tunaobatizwa nao ulitoka katika msalaba wa Kristo, ulitoka katika mauti yake (rej. KKK 1225). Ni katika muktadha huu Mama Kanisa katika sala ya utangulizi anasali hivi; “Yeye alipomwomba mwanamke Msamaria ampe maji, alikwisha mjalia paji la imani. Ndivyo alivyopenda yule mwanamke aone kiu ya imani hata akamwashia moto wa mapendo ya Mungu ndani yake”. Kumbe tukio la Yesu kukutana na Mwanamke Msamaria katika kisima cha Yakobo, lina ufunuo mkubwa katika fumbo la wokovu wetu. Kisimani zamani kulikuwa ni mahali ambapo watu walikutana kwa nia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana kutafuta wachumba na wachumba kukutana (rej. Mwa 26:15-25, 29:1-14, Kut 2:15-21). Tukizingatia katika lugha ya kibibilia, Nabii Hosea anaieleza Israeli kama mwanamke aliyeposwa na Mungu, lakini alikosa uaminifu, akawa msaliti, akajiingiza katika ukahaba, akawa kama kahaba, akajikahabisha kwa kuabudu miungu ya mataifa mingine. Hivyo Mwanamke Msamaria anasimama badala ya Israeli na jamii yote ya wanadamu iliyomwasi Mungu kwa dhambi zake. Yesu alikuja kutupatanisha na Mungu, akituongoza hatua kwa hatua, ili kutambua makosa yetu, kuyakiri na kuomba msamaha, kama alivyomuongoza mwanamke msamaria, hata akatambua na kukiri dhambi zake, akasamehewa, akapata, wongofu na uponyaji wa ndani, akaanza maisha mapya.

Kristo Yesu ni chemchemi ya maji ya uzima wa milele
Kristo Yesu ni chemchemi ya maji ya uzima wa milele   (AFP or licensors)

Hali hii inajidhihirisha kwa jinsi alivyoweza kumtambua Kristo Yesu hatua kwa hatua kama ifuatavyo: Kwanza alimtambua kama mwanaume Myahudi; “Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kutoka kwangu Msamaria” (Yn 4:9). Pili kama Bwana: “Bwana huna chombo cha kuchota maji, na kisima ni kirefu” (Yn 4:11). Kisha kama Nabii baada ya Yesu kumfunulia madhaifu yake; “Bwana naona ya kuwa u-nabii” (Yn 4:19). Na mwisho kama Masiha; “Najua ya kuwa yu aja Masiha aitwaye Kristo”. Yesu akajifunua kwake: “Mimi ninayesema nawe ndiye” (Yn 4:25-26). Naye anamkiri Kristo, kuwa ni Masiha, aletaye uzima mpya, uzima wa kiroho unaojidhihirisha kwa kumwabudu Mungu katika roho na kweli, akawa mmisionari, akawatangazia watu wa kijiji pake habari za Yesu, nao wakamwamini. Nasi tumwombe Kristo, chemchemi ya maji ya uzima, atutakase uovu wetu, na atujalie neema ya kusameheana kama anavyotuombea mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akisali; “Ee Bwana utujalie kwa ajili ya sadaka hizi tujitahidi kuwasamehe jirani zetu, maadam tunakuomba utusamehe sisi dhambi zetu wenyewe”. Kisha atujalie nguvu za kuendelea kutenda mema kwa kutulisha Mwili wake na kukata kiu yetu kwa Damu yake kama anavyotuombea mama Kanisa katika sala baada ya komunyo akisali; “Tumepokea amana ya fumbo la mbinguni. Nasi tumeshiba mkate wa mbinguni tukingali bado hapa duniani. Tunakuomba kwa unyenyekevu, ee Bwana, hayo tuliyopokea katika fumbo tuyatimize kwa matendo.” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

06 Machi 2026, 16:46