Tafakari Dominika ya Nne ya Kipindi Cha Kwaresima Mwaka A: Kipofu Anaona na Kuamini
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Ulemavu katika Agano la Kale ulihesabiwa kuwa ni kielelezo cha uwepo wa dhambi. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa yule mtu aliyezaliwa kipofu tangu tumboni mwa mama yake. Watu wakamuuliza Kristo Yesu ni nani aliyekuwa ametenda dhambi kiasi cha mtu yule kuzaliwa kipofu. Ulemavu ulihesabiwa kuwa ni kielelezo cha dhambi, kiasi hata cha kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Walitengwa na kuwekwa nje ya Hekalu, huku wakiendelea kuomba kila siku ya maisha yao! Yule mtu aliyezaliwa kipofu bila kupepesapepesa macho akakiri na kutangaza wazi kwamba, ndiye yeye aliyezaliwa kipofu sasa anayo furaha ya kuona, amekuwa huru: kiroho na kimwili na anamshuhudia Kristo Yesu kuwa kweli ni Nabii wala hana tena woga ndani mwake! Imani imemwezesha kuwa jasiri na kwake Kristo Yesu amekuwa ni chemchemi ya: Imani, mapendo na matumaini mapya, kwa kumrejeshea tena utu na heshima yake, siku ya Sabato na sasa kwa jeuri anamtolea ushuhuda wa nguvu. Mtu aliyezaliwa kipofu ni changamoto ya kuangalia mambo kwa jicho la imani, ili kuondokana na giza na hivyo kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Hii ni changamoto ya toba na wongofu wa ndani. Kipofu akabahatika kuona, kuelewa na hatimaye kuamini: “Nina amini Bwana.”
Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya furaha” – Domenica Laetae. Maneno ya wimbo wa mwanzo yaweka wazi maudhui haya yakisema hivi; “Furahi Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mpendao. Furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake” (Isa. 66:10-11). Tunaalikwa kufurahi kwa kuwa tumekaribia siku za kuadhimisha fumbo la wokovu wetu – mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo – Pasaka. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umeleta kwa namna ya ajabu upatanisho wa wanadamu kwa njia ya Neno wako. Tunakuomba utujalie wakristu bidii ya kujiweka tayari kwa ibada na imani, kuadhimisha sikukuu ijayo.” Katika dominika hii linafanyika takaso la pili la wakatekumeni watakaobatizwa usiku wa Pasaka. Ni katika muktahda huu ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika alama tatu za ubatizo: maji, mafuta matakatifu na mwanga. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inaeleza uhusiano uliopo kati ya ubatizo na ufufuko kuwa kwa Sakramenti ya ubatizo “Yesu anamwingiza Mkristo ndani yake Yeye, ambaye, kwa ubatizo wake, anatanguliza kifo chake na ufufuko wake.” Baada ya “kuzama katika maji, Roho Mtakatifu anaruka juu yetu toka mbinguni, na tukikubalika na sauti ya Baba, tunakuwa watoto wa Mungu”. Hivyo “mkristo anapaswa kuingia katika fumbo hili kwa unyenyekevu na toba, ashuke katika maji pamoja na Yesu ili apande pamoja naye, azaliwe kwa maji na kwa Roho, ili awe mwana mpendwa wa Baba, aenende katika maisha mapya. Ndiyo kusema kwa ubatizo, tunazikwa kaburini pamoja na Kristo, na kufufuka pamoja naye; tunashuka pamoja naye, ili tuweze kuinuka pamoja naye; tunapanda pamoja naye, ili tuweze kutukuzwa pamoja naye (rej. KKK 537).
Somo la kwanza ni la kitabu cha kwanza cha Samweli (1Sam. 16:1b, 6-7, 10-13a). Ni simulizi la Mungu kumchagua Daudi na kupakwa kwake mafuta ili awe mfalme wa Israeli. Samweli alipotumwa alifikiri kuwa Eliabu, mtoto wa kwanza wa Yese, mrithi wa baba yake, angefaa kuwa mfalme. Lakini Mungu ambaye “haangalii kama binadamu aangaliavyo”, aliutazama moyo wa Daudi katika udogo wake, ambaye katika kuchunga kondoo, alijifunza kumtegemea Bwana aliye mchungaji mwema, akapata kibali machoni pake, akamteua akapakwa mafuta akawa mfalme. Kupakwa mafuta kwa Daudi kukawa alama na ishara ya kupokea na kushirikishwa ufalme, ukuhani na unabii wa Kristo mchungaji mwema kwa kila mkristo anapobatizwa (rej. KKK 783-786; 1241). Ni katika mukatadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; Kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele” (Zab. 23). Na kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, wakatekumeni walitakiwa kuikariri na kuisali zaburi hii kwani ina vielelezo vya sakramenti tatu za kumuingiza mtu katika maisha ya Ukristo; Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi” (rej. KKK 1233). Ubatizo ni “sakramenti ya kuzaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu” kwa maongozi ya Yesu Kristo kuelekea uzima wa milele – “kando ya maji ya utulivu huniongoza”; Mafuta ya wakatekumeni kumfukuza shetani, na mafuta ya Krisima Takatifu kwa Kipaimara (rej. KKK 1237) – “Umenipaka mafuta kichwani pangu”, na kuinjongea komunyo ya Takatifu, Ekaristi, kupokea malisho ya uzima wa milele, Mwili na damu ya Kristo (rej. KKK 1244) – “Waandaa meza mbele yangu.”
Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Efe. 5:8-14). Fundisho ni kuwa kwa njia ya ubatizo, kwa ishara ya vazi jeupe tunampokea na kumvaa Kristo, mwanga halisi, tunakufa kuhusu dhambi na kufufuka naye, na mshumaa uliowashwa kutoka mshumaa wa Pasaka uliashiria kwamba Kristo sasa anatuangaza na kutufanya Nuru ya ulimwengu (rej. KKK 1243). Hivyo hatupaswi kuishi katika giza, bali katika mwanga, kuacha maisha ya kipagani na ibada zake ambazo zinakuwa zimegubikwa na matendo maovu na ya giza (rej. Mdo 19:23-41), na kuishi maisha ya kikristo kwa kujibidisha kusali na kushiriki ibada zake, zinazoangazwa na nuru ya Kristo zikituelekeza katika uzima wa milele. Nuru hii ya Kristo inapaswa iangaza maisha yetu ya kila siku, mahali popote. Ni kwa kufanya hivyo tunakuwa tunaishi katika neema za ufufuko, hatujalala usingizi wa mauti. Ndiyo maana Mtume Paulo asema hivi; “Amka, wewe usinziaye, ufufuke katika wafu, na Kristo atakuangaza.”
Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 9:1-41). Ni simulizi la Yesu kumponya aliyezaliwa kipofu, hatua kwa hatua. Kwanza anamwonea huruma na kumwendea, kisha akatema mate, akatengeneza tope, akampaka machoni kwa hiyo tope, akamwambia aende kunawa katika kisima cha Siloamu. Naye akaenda, akanawa, akarudi anaona. Maana ya Siloamu ni aliyetumwa. Kristo Yesu ni Siloamu yetu, kisima chetu, aliyetumwa na Mungu kutuletea wokovu. “Basi kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu”, ndiye Kristo Yesu. Kipofu, alipoponywa aliona mwanga, ishara ya uzuri, furaha, utakatifu na uzima. Akatoka katika giza, ishara ya ubaya, masikitiko, dhambi na kifo. Hivi vitu viwili, mwanga na giza haviwezi kuwa mahali pamoja kwa wakati mmoja. Uwepo wa kimoja huondoa kingine. Kuchagua mwanga ni kuchagua maisha, kuwa upande wa Mungu, unakuwa huru, huogopi, hofu inakutoka, na kuchagua giza ni kuchagua kifo, kuwa upande wa shetani, kuishi kwa hofu na mashaka. Kuwa upande wa Mungu ni kumsikiliza na kumfuata Kristo, nuru na mwanga wa kweli. “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu; Yeye anifuataye hataenda gizani kamwe bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yn. 8:12). Hali hii inajidhihirisha katika majibizano kati ya kipofu aliyeponywa na mafarisayo. Yeye alipoulizwa na mafarisayo wenye hila jinsi alivyoponywa, alieleza bila kuogopa jinsi Yesu alivyomponya, na kukiri kwa ushujaa na ujasiri kuwa Yesu ni Nabii, hana dhambi, ni mtakatifu. Lakini mafarisayo wakiwa gizani kwa hofu na mashaka walimwambia, “wewe umezaliwa katika dhambi tupu nawe unatufundisha sisi?”
Hata sisi tunaweza kuwa kama Mafarisayo tukikaza shingo na kwa kiburi na majivuno tukaendelea kuishi katika giza la dhambi. Ili kuepuka hali hiyo tujibidishe kutoka gizani na kuingia katika mwanga wa Kristo kwa kutambua madhaifu yetu, kuyakiri na kuyatubu kwa kukubali kwenda kunawa katika bwawa la sakramenti ya upatanisho. Sala yetu daima hii; Bwana nipate kuona. Tukifanya hivyo kwa unyenyekevu na toba ya kweli, Yeye ni mwenye huruma, atatusamehe na kutujalia wokovu na uzima wa milele. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakutolea kwa furaha dhabihu ziletazo wokovu wa milele. Tunakuomba sana utusaidie kuziheshimu kwa moyo wote na kuzitoa vema dhabihu hizi kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha kwa kusali; “Ee Mungu, unayemtia nuru kila ajaye ulimwenguni humu, tunakuomba uitie mioyo yetu nuru ya neema yako, tuweze kuwaza daima yakupendezayo wewe Mwenyezi na kukupenda kweli”. Na hii ndiyo hamu ya mioyo yetu. Tumsifu Yesu Kristo!