Tafuta

Akili unde huiga mawasiliano ya binadamu na kwa sababu hii lazima itumike kwa uangalifu na kwa uwajibikaji. Akili unde huiga mawasiliano ya binadamu na kwa sababu hii lazima itumike kwa uangalifu na kwa uwajibikaji. 

Seoul:Watawa watafakari kuhusu maadili na imani ya AI

Jumuiya za kitawa nchini Korea Kusini zilishiriki katika hotuba maalum kuhusu akili Unde (AI),zikitaka hekima, uwajibikaji na kujitolea kwa hadhi ya binadamu.

Padre  Mark Robin Destura, RCJ na Sr Christine Masivo - Vatican 

 

"Akili Unde huiga mawasiliano ya binadamu, na kwa sababu hiyo, lazima itumike kwa uangalifu na kwa uwajibikaji," hii ilikuwa mojawapo ya dhana zilizoanzishwa na Padre James Bang Jong-woo katika hotuba maalum kuhusu akili unde na maadili nchini Korea Kusini. Hotuba hiyo, iliyofanyika tarehe 24 Februari 2026, katika Kanisa Kuu la Wafransiskani la Jeongdong huko Seoul, Korea Kusini. Padre James, profesa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Korea, alitoa hotuba hiyo ya saa mbili, yenye kichwa: "Imani Katika Uso wa Teknolojia: Maadili ya AI." Karibu washiriki 250 walihudhuria tukio hilo, wengi wao wakiwa watawa, walionyesha shauku inayoongezeka ndani ya jamii za Kanisa katika kuelewa athari za kimaadili za teknolojia zinazoendelea kwa kasi.

AI tayari ni sehemu ya maisha ya kila siku

Kulingana na ripoti ya Catholic Times of Korea, wakati wa hotuba hiyo, Padre James alibainisha kuwa akili unde tayari imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Alisema, jumuiya nyingi za kidini tayari zinatumia zana za AI kwa ajili ya kutafuta data, kuunda maudhui, na kusaidia katika uinjilishaji. Hata hivyo, alionya kwamba AI pia ina hatari kwa sababu inaweza kuiga lugha na mawazo ya binadamu kwa njia ambazo zinaweza kufifisha tofauti kati ya akili ya binadamu na majibu yanayotokana na mashine. "Akili unde” huiga mawasiliano ya binadamu," alielezea, "na kwa sababu hii lazima itumike kwa uangalifu na kwa uwajibikaji."

Wasiwasi wa kimaadili na hatari halisi

Kulingana na ripoti, ili kuonesha hatari zinazowezekana, Padre James alirejea kesi ya Adam Raine, mvulana wa miaka 16 nchini Marekani ambaye inasemekana alikufa kwa kujiua baada ya mwingiliano wa muda mrefu na chatbot ya AI. Chatbot inadaiwa iliendeleza uhusiano wa karibu wa kihisia na kijana huyo na kuimarisha mawazo yake ya kujiua. Kesi hiyo ya kusikitisha, ambayo bado iko chini ya uchunguzi wa kisheria nchini Marekani, imeibua wasiwasi wa kimataifa kuhusu majukumu ya kimaadili yanayohusika katika kukuza na kutumia teknolojia za AI. Kwa Padre James, mifano kama hiyo inaangazia hitaji la haraka la kutafakari kimaadili. "Hatupaswi kukataa akili unde," alisema, "lakini lazima tuelewe jinsi inavyopaswa kutumika."

Kuimarisha utambuzi wa kiroho

Sr. Jung Yun-jin, katibu mkuu wa shirikisho la maandalizi, pia alihutubia mkutano huo, alibainisha kuwa maendeleo ya haraka ya teknolojia za kidijitali yanahitaji ufahamu wa kina wa kiroho. Alisema, "Lazima tutafakari jinsi tunavyoitikia mabadiliko haya na jinsi tunavyowasilisha ujumbe wa Injili kwa watu leo."

Teknolojia katika huduma kwa wanadamu

Katika mikutano mingine iliyotolewa na Padre James kuhusu mada hiyo, alisisitiza kwamba AI, kama maendeleo mengine ya kiteknolojia, inaweza pia kuonekana kama ishara ya uwezo wa ubunifu wa wanadamu. "AI ni ushahidi wa uwezo wa binadamu kushiriki kwa uwajibikaji katika kazi ya ubunifu ya Mungu," alisema. "Lakini lazima iwahudumie wanadamu na kuchangia kwa manufaa ya wote kulingana na mafundisho ya Kanisa." "Mashine ni zawadi ya ubunifu wa binadamu iliyotolewa na Mungu," alisema. "Lakini zinabaki kuwa unde  kwa kuundwa. Lazima tuhakikishe kwamba hazitunyimi kamwe uhuru na heshima yetu  kama viumbe wa Mungu."

17 Machi 2026, 12:46