Assisi:Maonyesho ya Masalia ya Mtakatifu Francis wa Assisi yatamatishwa
Vatican News
Dominika tarehe 22 Machi 2026, ilikuwa siku rasmi ya kuhitimisha heshima kwa masalia ya Mtakatifu Francis, yaliyowekwa wazi kwa mwezi mmoja kutoka Kanisa la chini ndani ya Basilika ya Mtakatifu Francis huko Assisi. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa masalia yake kuwekwa wazi, na takribani watu 370,000 kutoka pande mbalimbali za dunia walifika kutoa heshima. Heshima hii ya wazi ni moja ya matendo msingi yaliyopangwa kufanyika katika mwaka huu ambao inaadhimishwa kumbukizi ya miaka 800 tangu kifo chake.
Maelfu ya mahujaji walitembelea Assisi kutoka pande mbalimbali za dunia walifika kutoka heshima kwa masalia ya Mtakatifu Francis ambayo yaliwekwa wazi kwa mara ya kwanza miaka 800 tangu kifo chache.
Kardinali Zuppi: Tusikilize Ujumbe wa Amani
Misa ya kuhitimisha zoezi hili, iliadhimishwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Italia, Kardinali Matteo Zuppi, Askofu Mkuu wa Bologna, katika Basilika ya Mtakatifu Francis. Katika mahubiri yake, aligusia juu ya kipindi hiki ambacho kimetawaliwa na ubinafsi na migogoro, ambapo udanganyifu mbaya ni “kupingana na uovu kwa uovu,” Askofu Mkuu alisema, wakristo wanaitwa kwa “nguvu zisizo na silaha,” zilizozaliwa na Ufufuko, ambazo zinapinga kifo na kila kitu kinachoongoza. “Katika msimu huu unaoinua nguvu” alihimiza “tusikilize ujumbe wa amani. Ni kiasi gani cha hofu na jeuri ambavyo tayari vingeondolewa ikiwa tungesema tu, kwa nyuso zetu na maneno yetu, “amani iwe nanyi.””
Kujengea Njia ya kweli ya Amani
Kardinal Zuppi, aliendelea kukazia kiini cha ujumbe wa Kikristo. “Siyo nguvu ndizo zinazoongoza dunia,” alisema, “kwa sababu upendo ndiyo pekee unaoweza kubadilisha hili.
Akimrejea Mtakatifu Francis, Kardinali Zuppi alisisitiza umuhimu wake kwa wote. “ Yeye siyo wa mtu mmoja, ila ni wa watu wote,” na anafundisha “upendo ambao unaweza kumtambua kila mmoja kama ndugu. Ni upendo uliojaa unyenyekevu,” aliendelea, “upendo usiokata tamaa na kurudisha ulimwengu kwenye uhai, hadi kufikia hatua ya kupokonya silaha.”
Katika ulimwengu “uliosongwa na migogoro na migawanyiko,” alimwalika kila mmoja kuwa “mjenzi wa amani, na mashahidi wa kupokonya silaha, kwa kujenga daraja pale ambapo kuta zimejengwa na kurudia njia ya Injili inayotualika kufanya mazungumzo kuwa ulinzi pekee wa kweli wa amani.
Masalia ya Mtakatifu Francis:Faraja Kuu
Uzoefu wa Ibada ya umma yenyewe ulikuwa “faraja kuu” kwa maelfu ya mahujaji waliofika Assisi, alikazia Kardinali. Mbele ya masalia ya Mtakatifu Francis, watu wengi waling’amua “nguvu” na uwepo wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku,” aliongeza. Utakatifu “siyo ukamilifu, ila ni tafakari ya kina ya upendo wa Mungu katika umaskini wa maisha yetu.”
Tumekuwa “kama ndugu tuliomzunguka Francis,” alisema Padre Marco Moroni, Mkuu wa Konventi Takatifu ya Assisi, akirejelea maelfu ya mahujaji waliofika kutoa heshima kwa masalia ya Mtakatifu Francis. “Ndugu zaidi ya 370,000 walikusanyika hapa kutoka pande mbalimbali za dunia. Kusanyiko lililojaa roho ya udugu na sala, iliyotafuta kukutana, katika ishara ya umaskini na udhaifu wa mifupa, ujazo mkuu wa nguvu na maisha yaliyoongozwa na Roho Mtakatifu, ulioendelea kuzaa matunda. Padre Moroni aliwashukuru wote walioshikiri, kupanga na kufanikisha tukio hili ambalo ameeleza limefanikiwa zaidi ya matarajio yake.
Mtakatifu Francis anatuita kwake
Padre Giulio Cesareo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Konventi Takatifu ya Assisi, aliongeza: “Wengi waliniuliza kama nilitegemea ujio wa watu wengi hivyo, na nilijibu ndio. Sikuwa na mashaka kuwa watu wengi watakuja kukutana na Mtakatifu Francis.” “Ambacho sikutegemea ni umoja wa mahujaji waliojaa furaha na moyo wa ibada: ukimya, uvumilivu, na kuweka simu pembeni… na bado kuna masalia ya picha za fresco za mtakatifu Francis na Giotto,” aliongeza. “Maelezo pekee ni kwamba, hakuna aliyekuja kumuona Mtakatifu Francis, bali yeye aliye hai anatualika kuzungumzana na mioyo na akili zetu.” Padre Cesareo aliwashukuru wanamawasiliano na waandishi walioshirikiana na Konventi Takakatifu ya Assisi na kufikisha ujumbe wa tukio hili kwa watu.
Pumzi ya Upya
Mwezi huu wa maadhimisho ulikuwa ni wakati wa kuhuishwa na kuboresha mahusiano yaliyojikita kwenye sura ya mtakatifu Francis. Jumuiya ya mafrateri wafransisco iliwakaribisha ndugu kutoka Italia, na kutoka nchi nyinginezo kama Brazil, Marekani, Tanzania, India, Korea, na Mashariki ya Kati. Tukio hili pia ilikuwa fursa ya kutengeneza musiki na video iliyosindikiza heshima hii ya wazi “Su questo colle” (Juu ya mlima huu).
Kwa kuongezea, ukarabati wa kina ulifanyika kwenye Konventi Takatifu ili kuondoa vikwazo ambavyo vingezuia wageni kuona masalia haya yaliyowekwa wazi kwa wote. Hii ilibeba maana halisi ya tafakari ya Mtakatifu Francis, na roho iliyomwongoza katika safari ya wongofu na kuwa na matamanio ya kuwafikia wote, hasa walio pembezono na waliotengwa na jamii.
Safari Mwendelezo
Jioni, mara baada ya mahujaji wa mwisho kutoa heshima zao, masalia ya mtakatifu huyu yaliwekwa katika Kanisa kuu, mahali pa faragha ambapo ndugu wafransiskani walihudhuria kwa pamoja kuhitimisha zoezi hili la heshima za wazi.
Zaidi ya hayo, dhamira ya “Mtakatifu Fransis Anaishi” itaendelea kwa kipindi chote cha mwaka 2026. Itasindikiza matukio yote ya maadhimisho ya miaka 800 tangu kifo chake ikionesha uhai wa kudumu wa ujumbe wake na uwezo wa kuzungumza na wote.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.