Tafuta

2026.03.09 Tanzania-Dodoma:Siku moja ya kuombea amani ya dunia iliyoandaliwa na wanawake wa Baraza la Makanisa ya Kikristo Tanzania(CCT). 2026.03.09 Tanzania-Dodoma:Siku moja ya kuombea amani ya dunia iliyoandaliwa na wanawake wa Baraza la Makanisa ya Kikristo Tanzania(CCT). 

Tanzania:Mamia ya Wanawake Dodoma Waungana kuombea Amani ya Dunia!

Tukio hilo lilihudhuriwa na wanawake kutoka makanisa mbalimbali yanayounda Baraza la Makanisa ya Kikristo Tanzania(CCT,)huku lengo kuu likiwa ni kuwakutanisha waamini kwa pamoja kuombea amani ya dunia,Taifa la Tanzania na jamii kwa ujumla.Askofu Kibozi:“Mkabidhi Kristo changamoto na mizigo ya maisha.”Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule,alikuwa mgeni rasmi.Bertha Msaki,Mwenyekiti wanawake wa CCT,aliishukuru serikali kwa ushirikiano wake.

Thadei Aloyce Tesha na Sr Scholastica TeshaCSG, - Dodoma.

Mamia ya wanawake kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo walikusanyika katika Parokia ya Kizota, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma nchini Tanzania, ili Kuombea Amani Duniani kote katika tukio lililoandaliwa na wanawake wa Baraza la Wakristo Tanzania(CCT).  Kwa kukumbuka kuwa mwanzo mwa mwezi Machi unajikita na maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani ifikapo kila tarehe 8 Machi ya kila mwaka, tukio hilo lilifanyika tarehe 6 Machi 2026 huku likibeba ujumbe mzito wa "kuhimiza amani, mshikamano na maadili mema katika jamii".

Wanawake Wakristo waombea amani ya Dunia, huko Dodoma Tanzania
Wanawake Wakristo waombea amani ya Dunia, huko Dodoma Tanzania

Kujenga jamii yenye maadili, upendo na mshikamano

Kupitia maadhimisho hayo, wanawake waliweza kujadili nafasi yao katika kujenga jamii yenye maadili, upendo na mshikamano. Shughuli zilianza kwa maandamano ya amani yaliyoanzia eneo la Chinangali kuelekea Parokia ya Kizota. Katika maandamano hayo, wanawake kutoka madhehebu tisa yanayounda Baraza la makanisa nchini Tanzania ( CCT ) walishiriki kwa wingi wakiwa wamevalia sare zao za umoja. Walionekana wakitembea kwa utulivu huku wakibeba mabango yenye ujumbe wa amani, upendo na mshikamano kwa jamii.

Wanawake wana nafasi kubwa katika kuhamasisha amani katika jamii

Baadhi ya mabango hayo yalikuwa na ujumbe unaohamasisha umoja na utulivu katika jamii, huku washiriki wakisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa. Maandamano hayo yalivutia hisia za wakazi wa maeneo hayo ambao walijitokeza kushuhudia tukio hilo. Wakazi wengi walieleza kufurahishwa na hatua ya wanawake kuonesha mshikamano wao katika kuombea amani ya dunia na taifa kwa ujumla. Kwa mujibu wa waandaaji wa tukio hilo, maandamano hayo yalilenga "kuonesha kwa vitendo kuwa wanawake wana nafasi kubwa katika kuhamasisha amani katika jamii."

Wanawake Wakristo waombea amani ya Dunia
Wanawake Wakristo waombea amani ya Dunia

Kukusanyika katika Parokia ya Kizota

Baada ya maandamano hayo, washiriki walikusanyika katika Parokia ya Kizota ambako walipokelewa na viongozi mbalimbali wa dini na jamii. Miongoni mwa viongozi waliokuwepo ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Mhashamu Wilbroad Henry Kibozi, pamoja na viongozi wengine wa makanisa akiwemo Askofu Antony Muliyashimba na Bertha Msaki, mwenyekiti wa wanawake wa CCT.

Askofu Kibozi:Mkabidhi Kristo changamoto na mizigo ya maisha

Akizungumza katika mkutano huo, Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu Katoliki Dodoma, Mhashamu Kibozi aliwataka "wanawake kuendelea kuwa mfano bora katika jamii kwa kuzingatia maadili mema na kuwalea watoto katika misingi ya heshima, upendo na uwajibikaji." Alisisitiza kuwa "wanawake wana mchango mkubwa katika malezi ya familia na ustawi wa jamii kwa ujumla." Katika tafakari yake, Askofu Kibozi alinukuu maneno ya Yesu Kristo yanayosema: “Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha.” Akifafanua ujumbe huo, alisema pumziko la kweli linapatikana kwa Yesu Kristo na akawahimiza wanawake kumkabidhi Kristo changamoto na mizigo ya maisha yao. Aidha, aliwahimiza "wanawake kuendelea kuombea amani ya nchi ya Tanzania pamoja na viongozi wake ili taifa liendelee kuwa na utulivu, mshikamano na maendeleo."

Askofu Kibozi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma akitoa tafakari
Askofu Kibozi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma akitoa tafakari

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma:"Dini zimekuwa mchango mkubwa kuimarisha maadili katika jamii"

Katika muktadha huyo naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule, alikuwa mgeni rasmi. Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kulinda na kudumisha amani nchini akieleza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote. Alisema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini, zikiwemo zile zilizo chini ya CCT, katika kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kwa mujibu wake, "taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha maadili katika jamii pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo." Aidha, alibainisha kuwa "ushirikiano kati ya serikali na taasisi za dini ni muhimu katika kujenga jamii yenye maadili mema na mshikamano.

Mwenyekiti wa CCT

Awali Bertha Msaki, mwenyekiti wao akisoma risala ya wanawake wa CCT, aliishukuru serikali kwa ushirikiano wake katika masuala mbalimbali ya kijamii na maendeleo. Hata hivyo, alitoa ombi la "kuimarishwa kwa ushirikiano huo hasa katika ujenzi wa ofisi za CCT. Alieleza kuwa tayari eneo limetengwa katika mtaa wa Miyuji kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo, hivyo aliomba serikali ya mkoa kutoa ushirikiano ili mradi huo uweze kukamilika kwa manufaa ya taasisi hiyo na jamii kwa ujumla. Kwa mujibu wa Msaki, uwepo wa "ofisi hizo utasaidia kurahisisha uratibu wa shughuli za taasisi hiyo pamoja na kuimarisha huduma zake kwa jamii."

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Tanzania, Rosemary Senyamule
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Tanzania, Rosemary Senyamule

Baadhi ya shuhuda za washiriki

Baadhi ya wanawake walioshiriki katika maadhimisho hayo walieleza kuwa tukio hilo limekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha maisha yao ya kiimani na kijamii. Vaileti Joseph, mmoja wa washiriki, alisema "mkutano huo umempa hamasa mpya ya kuendelea kushiriki katika shughuli za kanisa na jamii. " Alieleza kuwa kupitia mafundisho aliyoyapata ameweza "kujitambua zaidi katika nafasi yake kama mwanamke ndani ya familia na jamii."

"Wanawake wana jukumu kubwa la kujenga jamii yenye maadili mema"

Kwa upande wake, Prisca Nmagoha alisema, "tukio hilo limemkumbusha kuwa wanawake wana jukumu kubwa katika kujenga jamii yenye maadili mema". Alisisitiza kuwa "wanawake wanapaswa kuwa mfano bora hasa katika malezi ya watoto ili kuhakikisha kizazi kijacho kinakua katika misingi ya maadili." Naye Valerian Moshi alisema wanawake ni nguzo muhimu katika familia na jamii, hivyo wanapaswa kutumia nafasi yao vizuri katika kuhamasisha amani, upendo na mshikamano.

"Juhudi za kudumisha amani zinahitaji ushirikiano wa kila mmoja"

Maadhimisho hayo ya Siku ya Kuombea Amani Duniani yameacha ujumbe muhimu kwa jamii kwamba juhudi za kudumisha amani zinahitaji ushirikiano wa kila mmoja. Wanawake wametajwa kuwa na nafasi ya kipekee katika kujenga jamii yenye upendo, maadili na mshikamano. Kupitia maombi, mshikamano na ushirikiano kati ya taasisi za dini, serikali na wananchi, inaaminika kuwa jamii inaweza kuendelea kuwa na utulivu na maendeleo endelevu. Kwa ujumla, maadhimisho hayo yameonesha kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika kuhamasisha amani na maadili mema katika jamii, hivyo juhudi zao zinapaswa kuungwa mkono ili kuendelea kujenga taifa lenye utulivu na mshikamano.

Asante kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

08 Machi 2026, 10:08