Tafuta

Maltempo Roma, ingenti danni sul Litorale Romano

Maaskofu Wakatoliki kusini mwa dunia watoa wito kuharakisha mpito wa nishati uliyo na haki

Maaskofu Wakatoliki wa Afrika,Asia na Amerika Kusini waanzisha "kampeni ya Makanisa ya Kusini mwa Dunia," na kuzisihi serikali kupitisha mkataba wa kimataifa ili kukomesha upanuzi wa mafuta ya visukuku na kuongoza mpito wa haki kuelekea nishati mbadala.

Mark Saludes,LiCAS na Sr. Christine Masivo,CPS,–Vatican.

Katika “Kampeni ya pamoja ya Makanisa ya Kusini mwa dunia kwa ajili ya makao yetu ya pamoja” iliyotolewa na vyombo vya Maaskofu wa bara vinavyowakilisha Kanisa Katoliki  Kusini mwa Dunia, pamoja na usaidizi kutoka kwa viongozi wa makanisa barani Ulaya na Oceania, walitoa wito kwa serikali kupitisha mkataba wa kimataifa ili kusimamisha upanuzi wa mafuta ya visukuku na kuongoza mpito wa haki kuelekea nishati mbadala.

Asia tayari wanaona mabadiliko ya tabianchi na mifumo ya kiuchumi isiyoendelevu

Katika hati iliyotumwa kwa Shirika la Habari za Kanisa barani Asia ( LiCAS News,) Maaskofu walisema jamii yote  Afrika, Amerika Kusini, na Asia tayari wanaona mabadiliko ya tabianchi  na mifumo ya kiuchumi isiyo endelevu. Kampeni hiyo inasema kwamba mabadiliko ya tabianchi "sio tu mgogoro wa kimazingira," bali pia "ni matokeo ya mifumo isiyo endelevu ya uzalishaji na matumizi na 'uchumi unaoua,'na kusababisha hali tatanishi yenye upana zaidi ambao "unatishia heshima na amani ya binadamu." Maaskofu walisisitiza ushahidi wa kisayansi unaounganisha ongezeko la joto duniani na matumizi endelevu ya mafuta ya visukuku. Hati hiyo inabainisha  kuchomwa kwa mkaa, mafuta, na gesi ndio "sababu kuu ya kuharibika kwa hivi karibuni."

Mafundisho  ya Kanisa Katoliki Kijamii

Walisisitiza mvuto wao katika Hati ya Mafundisho kijamii ya Kikatoliki, Maaskofu walihimiza serikali kupitisha mfumo wa kimataifa unaofungamana ili kuondoa mafuta ya visukuku huku wakilinda jamii zilizo katika mazingira magumu. "Wakiongozwa na chaguo la upendeleo kwa maskini na utunzaji wa uumbaji ulioelezewa katika Mafundisho ya Kijamii ya Kikatoliki," Maaskofu walitangaza "uungaji mkono wao usioyumba kwa mpito wa haki" na kutoa wito kwa serikali "kupitisha mkataba wa kuzuia kuenea na kuachana na mafuta ya visukuku kama sharti la kimaadili na kisiasa."

Kampeni hiyo ilipendekeza Mkataba wa Mafuta ya Visukuku ambao ungekamilisha Mkataba wa Paris kwa kushughulikia uzalishaji wa mafuta ya visukuku moja kwa moja. Ilitoa wito wa kukomesha uchunguzi mpya na uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta, na gesi, kwa usawa kuondoa shughuli zilizopo za mafuta ya visukuku, na kuhakikisha "mpito wa haki" wa kimataifa unaowalinda wafanyakazi na jamii. Viongozi wa Kanisa  pia walionya kwamba upanuzi unaoendelea wa mafuta ya visukuku unahatarisha kuzidisha mvutano wa kijiografia na kisiasa. Sera zinazokuza upanuzi mkali wa mafuta na gesi, hati hiyo inasema, zimechangia migogoro na kile inachokielezea kama "aina za ubeberu wa petroli."

Kanisa Katoliki la Ufilipino 

Kanisa Katoliki nchini Ufilipino limeibua wasiwasi kama huo kuhusu uhusiano kati ya mafuta ya visukuku na migogoro. Katika taarifa ya kichungaji ya tarehe 4 Machi 2026 Caritas Philippines ilionya kwamba mgogoro unaoongezeka katika Mashariki ya Kati unafichua matatizo makubwa ya kimuundo yanayohusiana na mfumo wa nishati wa kimataifa. Harakati ya  hatua za kijamii ya Kanisa ilisema mzozo huo ulionesha kwamba "uchumi wa mafuta ya visukuku unaendelea kuunda mgogoro wa kijiografia na kisiasa." Njia za kimkakati za nishati kama vile Mlango wa Hormuz, aliongeza, zimekuwa sehemu za kukabiliwa ambapo nguvu za kijeshi, maslahi ya kiuchumi, na utegemezi wa mafuta hukutana. Caritas Ufilipino  ilionya kwamba wakati "mafuta yanapoingiliwa na vita, matokeo yake huenea kote ulimwenguni - haswa kwa uchumi dhaifu kama Ufilipino." Kundi hilo lilisema nchi hiyo bado "inategemea kwa hatari makaa ya mawe, mafuta, na gesi kutoka nje," utegemezi ambao "unaunganisha utulivu wetu wa kitaifa na migogoro ambayo hatuwezi kudhibiti na kuwaweka watu wetu katika mshtuko wa masoko ya nishati duniani yanayoyumba."

Mstakabali wa tabianchi

Wakitazama  mbele mazungumzo ya kimataifa ya hali ya tabianchi  yanayokuja, Maaskofu wanahimiza serikali kuunganisha mipango ya kuondoa mafuta ya visukuku katika ahadi za kitaifa za hali ya hewa na kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa kuelekea mpito wa nishati uliopangwa. Kampeni hiyo ilifungwa kwa wito wa mshikamano wa kimataifa na hatua za pamoja. Maaskofu walisema wako tayari kusikiliza "kilio cha dunia na kilio cha maskini" na kuwaalika "watu wote wenye nia njema kujiunga na muungano wa kihistoria kati ya Kaskazini na Kusini ili kulinda makazi yetu ya pamoja."

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

 

17 Machi 2026, 12:52