Tafuta

Kardinali  Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Yerusalemu. Kardinali Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Yerusalemu. 

Maandamano ya Dominika ya Matawi Yerusalemu yafutwa kutokana na vita

Upatriaki wa Kilatini wa Yerusalemu wafuta maandamano ya Dominika ya Matawi ya mwaka huu 2026 kutoka Mlima wa Mizeituni hadi Yerusalemu,kutokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.

Na Beatrice Guarrera na Sr. Christine Masivo, CPS

Kardinali Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu, ametangaza kwamba maandamano ya Kiutamaduni ya Dominika, ambayo huanzia Mlima wa Mizeituni hadi Yerusalemu, yamefutwa na yatabadilishwa na wakati wa sala kwa ajili ya jiji katika eneo hilo bado haujabainishwa. Katika taarifa, Kardinali alielezea kwamba Misa ya Alhamisi Kuu Takatifu, ambayo kwa kawaida hufanyika katika Basilika ya Kaburi Takatifu, imeahirishwa hadi tarehe itakayofuata mara tu hali itakaporuhusu na labda ndani ya kipinchi cha Pasaka.

Sherehe za kawaida za umma hazitawezekana

"Vikwazo vilivyowekwa na mgogoro na matukio ya siku za hivi karibuni havioneshi uboreshaji wowote unaokaribia," Kardinali alisisitiza. "Katika mazungumzo ya mara kwa mara na mamlaka husika, pamoja na Makanisa mengine ya Kikristo, tunatathmini jinsi, kwa njia ambazo zitakubaliwa, tunavyoweza kusherehekea Fumbo kuu la wokovu wetu katika mioyo ya Makanisa yetu," alisema. Kardinali Pizzaballa alisisitiza kwamba hali hiyo inabadilika kila mara, na kufanya iwe vigumu kutoa ishara  dhahiri za sherehe za Juma Takatifu. Alisema Utawala wa Upatriaki utalazimika kupanga matukio siku baada ya siku. "Tayari ni wazi kwamba sherehe za kawaida zilizo wazi kwa wote haziwezi kufanyika," Kardinali aliendelea, akielezea uamuzi wa kufuta maandamano ya Dominika ya Matawi na kuahirisha Misa ya Pasaka. Hata hivyo, taarifa hiyo ilibainisha kwamba makanisa ya chini ya  Upariaki yanabaki wazi, na mapadre wa Maparaokia watafanya wawezavyo kuhimiza sala na ushiriki wa waamini katika sherehe za Pasaka.

Jeraha jingine lililosababishwa na mgogoro huo

"Kutokana na vita, mwaka huu hatukuweza kupata uzoefu wa safari ya kiutamaduni ya  Kwaresima huko Yerusalemu, pamoja na sherehe kuu katika Kaburi Takatifu na katika Sehemu Takatifu za Mateso," taarifa hiyo ilieleza. "Ingawa tuliweza kuomba na kujiandaa kibinafsi, tulihisi kupoteza safari ya jumuiya kuelekea Pasaka," alisema Kardinali Pizzaballa. "Ukali wa wakati huu wa vita, unaotuathiri sote," aliendelea, "leo una mzigo wa ziada wa kutoweza kusherehekea Pasaka pamoja na kwa heshima." "Hili ni jeraha linaloongeza mengine mengi yaliyosababishwa na mgogoro. Lakini hatupaswi kujiruhusu kukata tamaa. Ingawa tunaweza tusikusanyike kama tunavyotaka, tusiache maombi."

Maombi ya amani Jumamosi, Machi 28

Kardinali alikumbuka maneno ya Yesu kutoka kutoka Injili ya Luka 18, 1: "Ombeni kila wakati na msife moyo." Aliwaalika watu kufidia vikwazo hivi kwa nyakati za maombi katika familia na jumuiya za kidini. Hasa, aliwaalika kila mtu kuungana katika maombi ya Jumamosi tarehe 28 Machi 2026 kwa kusali Rozari kuomba amani na utulivu, hasa kwa wale wanaoteseka kwa sababu ya mgogoro huo. "Tutafanya hivyo kwa mioyo ya unyenyekevu, tukiwa na uhakika kwamba sala yetu, hata tunapokuwa mbali kimwili, ina uwezo wa kutumia nguvu ya upendo wa Mungu, ambayo hutuunganisha katika roho ya matumaini na uaminifu," Kardinali alisisitiza. Ingawa sala tayari imeenea, alipendekeza siku maalum ambayo watu wanaweza kuhisi wameungana, licha ya wote kuwa katika maeneo yao wenyewe. "Tunatamani amani, kwanza kabisa, kwa mioyo yetu yenye shida. Sala pekee ndiyo inayoweza kuipatia," Kardinali aliandika.

Hakuna giza linaloweza kuwa na neno la mwisho

Siku ya Ijumaa Kuu, waamini Wakatoliki ulimwenguni kote wataalikwa kuunga mkono Nchi Takatifu kupitia Sadaka yao. Jumuiya mahalia, inajiandaa kupata uzoefu wa wakati huu maalum wa kiliturujia kwa maneno ya Kardinali: "Pasaka, ambayo tunasherehekea kwa jina la mateso, kifo, na ufufuko wa Kristo, inatukumbusha kwamba hakuna giza, hata lile la vita, linaloweza kuwa na neno la mwisho. Kaburi tupu ni muhuri wa ushindi wa maisha dhidi ya chuki, wa huruma dhidi ya dhambi. Turuhusu uhakika huu kuangazia hatua zetu na kudumisha tumaini letu."

Sala Inaendelea Katika Maeneo Matakatifu

Katika siku za hivi karibuni, Usimamizi wa Nchi Takatifu ulitoa taarifa ukielezea kwamba watawa wa Wafranciskani waliokuwepo katika Kaburi Takatifu "hawajawahi kuacha, mchana au usiku, kutekeleza sherehe zilizopangwa, ibada, maandamano ya kila siku, na sala za kiliturujia kulingana na masharti ya Hali iliyopo. Hata katika siku hizi,  taarifa hiyo ilisema, ingawa ufikiaji wa Basilika ni wa waamini tu kwa sababu za usalama, sala inaendelea bila kukoma katika Maeneo Matakatifu." Uwepo wa karne nyingi wa Usimamizi wa Nchi Takatifu, na sala inayoinuka hapo kila siku, hutolewa kwa jina la Kanisa lote na kwa manufaa ya wanadamu wote, taarifa hiyo ilieleza. Katika nyakati za kusisimua kama zile tunazopitia sasa, uwepo huu unakusudia kuonesha imani, tumaini, na sala.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

24 Machi 2026, 16:15