Tafuta

Watawa wa Mama Teresa wa Kalkuta. Watawa wa Mama Teresa wa Kalkuta.  (AFP or licensors)

Yemen,Aden:Kukumbuka Mashahidi wa Kristo miaka kumi baadaye!

Miaka kumi baada ya shambulio la kutisha huko Yemen,Kanisa linakumbuka sadaka ya Masista wanne Wamisionari wa Upendo(wa Mama Teresa wa Kalkutta) waliouawa.Misa hiyo iliongozwa na Msimamizi wa Kitume wa Kusini mwa Arabia katika kumbukumbu yao kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu huko Abu Dhabi.

Na Sr. Christine Masivo CPS,- Vatican.

Mnamo tarehe 4 Machi 2026, Kanisa na dunia nzima iliwakumbuka Masista Wamisionari wa nne wa Shirika la Upendo waliouawa huko Aden, nchini Yemen. Imani yao inaendelea kuhamasisha imani, ujasiri na matumaini. Hawa walikuwa ni Sr. Reginette na Sr. Margarita kutoka Rwanda, Sr. Anselma kutoka India, na Sr. Judith kutoka Kenya waliuawa na kundi la kijihadi lililovamia nyumba ya wazee inayoendeshwa na Masista Wamisionari wa Upendo wajulikanao kama wa Mama Teresa wa Kalkuta.

Washambuliaji waliuwaua wafanyakazi 12 wa mataifa na dini tofauti, wakilenga mahali palipokusudiwa kuwatunza maskini na wazee, ambao walikuwa wakiwatunza. Katika shambulio hilo hilo, Padre Tom Uzhunnalil, wa Shirika la Don Bosco, aliyehudumu katika jamii, pia alitekwa nyara na kushikiliwa mateka kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kuachiliwa huru mnamo Septemba 2017. Hata hivyo, licha ya hofu hiyo, urithi wa Masista hao wa huruma unaendelea kung'aa kupitia utume unaoendelea kwa Kanisa huko Yemen.

Ujumbe wa Matumaini

Kulingana na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, Askofu Paolo Martinelli, Msimamizi wa Kitume ya Kusini mwa Arabia, wakati wa Misa Takatifu, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yoseph huko Abu Dhabi, katika kukumbukumbu hiyo alisisitiza kwamba “Hii ni ishara ya matumaini wakati ambapo Ghuba nzima inakabiliwa na mgogoro mkubwa. Masista Wamisionari wa Upendo walitoa maisha yao, na baadhi yao bado wapo Yemen leo hii, wakiwatunza maskini bila ubaguzi, hivyo kutoa ushuhuda wa upendo wa Kristo unaoshinda vikwazo." Tukiwaangalia, tunajisikia kutiwa moyo kuwa wapatanishi katika nchi hii.

Huduma isiyo na mipaka

Masista walijitolea maisha yao kuwatunza wazee na wagonjwa, ambao wengi wao ni Waislamu. Kazi yao haikuchochewa na hamu ya kuwabadilisha wengine, bali ni kujitolea kwao kuwahudumia wale walio na uhitaji zaidi. Huruma na unyenyekevu wao ulipata sifa kutoka kwa jamii ya wenyeji, na waliheshimu kazi yao ya kuwahudumia watu bila kujali dini na malezi. Karama ya Masista Wamisionari wa Upendo inaoneshwa katika kazi yao, kama vile walivyoanzishwa na Mtakatifu Mama Teresa ili kuwahudumia maskini zaidi. Nyumba ya wazee ilifunguliwa mwaka 1992 nchini Yemen kwa ombi la serikali, ikiendeleza uwepo ulioanza mwaka wa 1973. Baada ya shambulio hilo, picha za masista zilisambaa, zikiwaonesha wakiwa wamevaa aproni za jikoni juu ya sare zao za kitawa wakati wa kifo chao, zikiashiria unyenyekevu wao na huduma ya vitendo ambayo ilifafanua huduma yao ya utume kila siku, kusafisha majeraha, kuwalisha wazee, na kuwafariji wale waliokuwa wapweke na wanaoteseka.

Kanisa linalohudumu

"Ushuhuda wa Masista Wamisionari wa Upendo waliouawa huko Aden unaendelea kumwilisha maisha ya Kanisa letu na kututia moyo kuishi imani yetu kwa furaha na kujitolea kila siku," alisema Askofu Martinelli. Alikumbusha pia wito uliotolewa na Askofu Paul Hinder baada ya shambulio la 2016, akisema, "Tunawaomba mashahidi wanne kuombea Yemen na Mashariki ya Kati nzima ili amani iendelee na vurugu ziweze kuisha." Baadhi ya viongozi wa Kanisa wamekuwa wakitafakari maana yenye nguvu ya nguo ya kiuboni(aproni), inayowakilisha Kanisa linalohudumia badala ya kutafuta kutambuliwa, Kanisa linalofuata mfano wa Kristo akiwaosha miguu wanafunzi wake. Masista hao walikufa walipokuwa wakifanya matendo yao rahisi ya upendo.

Ushuhuda wao wa imani unaendelea kulisha maisha ya Kanisa

Askofu Martienelli alisema, ushuhuda wao wa kifo cha imani unaendelea kulisha maisha ya Kanisa na kuwapa changamoto waumini kuishi imani yao kwa furaha na kujitolea. Leo utume wao haujaisha, kwani jamii hizo mbili nchini Yemen zinawahudumia maskini katika miji ya Hodeidah na Sana'a, kwa unyenyekevu kama ishara yenye nguvu ya matumaini. Kumbukumbu ya masista hao wanne ni ukumbusho kwamba hata katika maeneo yaliyojaa vurugu na mgawanyiko, upendo unaoishi kupitia huduma unaweza kuwa ushuhuda wenye nguvu zaidi kuliko chuki.

Asante kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

06 Machi 2026, 14:14