Tafuta

Timu ya Mpango wa kugawa chakula katika vituo vya kuhamishika. Timu ya Mpango wa kugawa chakula katika vituo vya kuhamishika.  (Archivio SMCB ) #SistersProject

Wakristo wa Siberia wa madhehebu tofauti wanaungana kuwahudumia wasio na makazi

Tangu mwaka 2020,Wakristo kutoka jumuiya za Wakatoliki,Waorthodox na Waprotestanti katika jiji la Krasnoyarsk la Siberia wameungana kuandaa milo ya kila siku kwa ajili ya wasio na makazi.Kwa wanachama wote wa timu hii ya kiekumeni,wakiwemo Masista wa Huruma wa Mtakatifu Karoli Borromeo,kauli mbiu yao imekuwa: "huruma,si kuhusu huruma,bali kuhusu msaada.”

Na Sr Wiera (Elena) Isachenko, SMCB

Kulingana na kampuni huru ya utafiti ya Validata, kuna takriban watu milioni 2.13 wasio na makazi nchini Urusi, zaidi ya 36,000 kati yao wako katika Mkoa wa Krasnoyarsk. Krasnoyarsk ina kituo kimoja tu cha makazi, ambayo hutoa vitanda 33 pekee yake. Kwa miaka mingi, Wakristo wa madhehebu tofauti waliwasaidia wasio na makazi, kila moja kwa njia yake. Tangu 2020, wameungana katika mpango huo uitwao "Mobile Feeding Stations", yaani Vituo vya kulisha vinavyohamishika. Lengo lao ni kutoa milo ya moto ya kila siku kwa wasio na makazi.

Leo hii, kuna maeneo tisa ya kudumu, mawili kati yake ya kituo cha chakula cha mchana cha kila siku. Kila siku ya juma, moja ya jumuiya za Kikristo inawajibika kuandaa na kuhudumia milo:Jumatatu, Wakatoliki, Waorthodox  Jumanne  na  Alhamisi, wakati  jumuiya za Kiprotestanti ni kwa siku zilizobaki. Chakula ni hatua ya kwanza tu katika njia ya kumsaidia mtu mwenye uhitaji, lakini hufungua mlango wa mazungumzo na usaidizi kwa wale wanaokabiliwa na hali zinazoonekana kutokuwa na matumaini.

Wakristo husaidia kurejesha hati zilizopotea, kupata nafasi salama katika vituo vya makazi au ukarabati, na kutoa dawa, nguo, na viatu. Inapohitajika, mazishi ya watu wasio na makazi hulipwa kupitia michango ya pamoja ya jumuiya za Kikristo. Kila mtu alikuja kwenye huduma hii kwa njia yake mwenyewe. Mara nyingi, ilianza na kukutana na mtu mwenye uhitaji.

Lyudmila Samoylova, mjumbe wa jumuiya ya "Maisha ya Kikristo" ya Kiprotestanti, alimkumbuka mwanamume asiye na makazi aliyekutana naye kwenye kituo cha Basi. "Kulikuwa na baridi sana, na hakuwa na pesa zozote za nauli," alisema. "Nilimwona akifukuzwa kutoka kwenye mabasi. Moyo wangu uliuma. Tulipanda Bus lililofuata pamoja. Watu walishangaa kwa harufu mbaya. Nilimlipia. Hakuwa na umbali wa kwenda, vituo viwili tu. Alishuka, nami nikaendelea kutazama nje ya dirisha kwa muda mrefu, nikimfikiria."

Kuwalisha watu wasio na makazi kunaendelea hata katika baridi kali ya Siberia.

Kwa miaka 5 sasa , Masisita wa Shirika la Huruma la Mtakatifu Karoli Borromeo(Sisters of Mercy of St. Charles Borromeo) wamekuwa wakiwahudumia wasio na makazi pamoja na waamini wa Parokia Katoliki ya Kugeuka Sura kwa Bwana. Kila mtu huchangia kwa njia yoyote awezayo. Kwa mfano, familia moja imejitolea kuoka mikate 40 kila Juma kwa ajili ya wale wanaohitaji. "Mungu hutenda kupitia sisi," alisema Sr. Letycja Gorniewicz, SMCB, "kupitia wale wanaoandaa chakula na wale wanaokuja kutafuta msaada. Hapa ni mahali ambapo mtu mmoja hukutana na mwingine."

Karibu watu 100 hufika kwenye vituo vya kulisha chakula kila siku.

Uzoefu wa Sergey, Ivan na Andrey

Kwa miaka mingi, kumekuwa na historia nyingi za kusikitisha na za kutia moyo. Mojawapo ni historia ya Sergey.

"Tulimtoa kwenye takataka," alikumbuka Kristina Kisidi kutoka jumuiya ya Wapentekoste. "Alikuwa amefunikwa na michubuko na hakuona njia ya kutokea. Sasa ana mke mzuri na watoto watatu. Ilikuwa muhimu sana kumsaidia katika wakati huo mgumu." Miongoni mwa historia nyingi za Jumuiya, zile za Ivan na Andrey ndizo ambazo kila mtu anazikumbuka kwa upendo. Ivan alifika Krasnoyarsk kutoka Norilsk, jiji lililo kaskazini mwa Mkoa wa Krasnoyarsk. Aliibiwa kwenye kituo cha reli. Akiwa ameshtuka, alikwenda kwenye daraja akikusudia kujiua. Mwanamume asiye na makazi alimwona hapo. "Njoo nami, nitakupeleka mahali ambapo wanaweza kukusaidia," alisema.

Hivi ndivyo Ivan alivyoishia katika kituo cha usaidizi cha jumuiya ya Maisha ya Kikristo. Alilishwa, akapelekwa polisi, na akasaidiwa kuwasilisha ripoti kuhusu hati na pesa zake zilizopotea. Alipewa nafasi katika makazi na nguo. Siku chache baadaye, hati zake zilipatikana. Mwanamume huyo alithubutu kuwapigia simu familia yake kuomba pesa za tiketi ya kurudi. Pia kulikuwa na Andrey, ambaye alisema kwamba hakuja kwa ajili ya chakula, bali kwa ajili ya mazungumzo ya kirafiki. Siku zote alichukua sehemu yake ya mwisho, na ikiwa mtu angefika akiwa amechelewa na akakosa chakula, angempatia chake. Wakati mmoja, mmoja wa watu wasio na makazi alisema kwamba Andrey alikuwa amefariki. Mwezi mmoja baadaye, alionekana kwenye kituo cha kulishia chakula. Ilikuwa Jumatatu ya Pasaka. Siku hiyo, Wakatoliki walimsalimia kwa furaha: "Kristo si yeye pekee aliyefufuka!"

Kila mtu anastahili sikukuu, Sr. Samuela Walczuk SMCB huoka keki 40 kwa ajili ya wasio na makazi kwa ajili ya Noeli.

Mara kadhaa kwa mwaka, Wakristo wanaohusika katika huduma ya "Vituo vya Kulisha Vinavyohamishika" hukutana ili kusali pamoja na kushiriki mipango na mahitaji yao. Mikutano hii husaidia kuimarisha umoja kila wakati. "Wakristo wanapokuwa wameungana, si 'sisi' na 'wao' ni 'sisi'," alisema Marina Balchugova kutoka Kanisa la Orthodox.

"Uzoefu wetu wa huduma ya kiekumeni, kwangu mimi, ni mfano kwamba Bwana anatamani umoja, na kwamba inawezekana," anasema Sr. Letycja Gorniewicz, SMCB. "Hatuhitaji kusubiri mamlaka ya Kanisa ituunganishe. Tunaweza kuungana karibu na Kristo sisi wenyewe. Kuleta Rehema ya Mungu kwa watu pamoja ni ishara yenye nguvu kwa wote wanaomtafuta Mungu."

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here.

 

16 Februari 2026, 14:26