Tafakari Dominika ya Pili ya Kipindi Cha Kwaresima Mwaka A: Wito
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka Vatican News, leo ikiwa ni Dominika ya pili ya kipindi cha Kwaresima. Kung’ara Bwana ni mwendelezo wa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Ukuu wa Fumbo la Msalaba na Mwanga unaong’ara katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwanga utakaojionesha kwa namna ya pekee, Siku ile Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Msikieni yeye.” Mt 17: 5 Kusikiliza ni sanaa inayohitaji majiundo makini, endelevu na fungamani, mwaliko kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu, ili awasaidie kuwa wasikivu wema na wazuri, tayari kumwilisha kile wanachokisikia kutoka katika dhamiri zao nyofu! Kristo Yesu kama ilivyokuwa kwa Mitume wake wa karibu aliowateuwa kuwa mashuhuda kwa matukio muhimu ya maisha yake yaani: Petro, Yakobo na Yohane, Wakristo pia wanahamasishwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu imefunuliwa kwa njia ya Maandiko Matakatifu katika Sheria na Unabii na kupata utimilifu wake katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu, na kuzaliwa kwake Bikira Maria katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi! Wakristo wanaitwa na wanatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, daima Mwenyezi Mungu anaandama nao katika hija ya maisha yao.
Dominika ya Pili ya Kwaresima hutualika kupanda Mlima pamoja na Yesu. Baada ya Dominika ya Kwanza ambapo tulimwona Yesu akijaribiwa jangwani, leo tunamwona Yesu akibadilika sura mlimani. Mama Kanisa kwa hekima yake linatupa tukio hili katikati ya Kwaresma ili kutukumbusha kwamba kabla ya msalaba kuna mwanga, na baada ya mateso kuna utukufu. Katika safari ya Kwaresima, wengi wetu tunabeba mizigo: matatizo ya kifamilia, kiuchumi, kiafya, migogoro ya kijamii, na hata kukata tamaa kiroho. Dunia mamboleo imejaa vita, chuki, ubinafsi, umaskini, uharibifu wa mazingira na kukosa mwelekeo wa kiroho. Ndani ya hali hii, masomo ya leo yanatupa tumaini la kina. Katika somo la kwanza tunakutana na Abrahamu, mtu anayeitwa na Mungu aache kila kitu:“Ondoka katika nchi yako, jamaa zako na nyumba ya baba yako, uende nchi nitakayokuonyesha.” Huu ni wito mgumu. Mungu hamwambii Abrahamu ataenda wapi, atakuta nini, au atapitia mateso gani. Anachotakiwa ni kuamini na kuondoka. Neema ilioje kuisikia sauti yake Mungu, kuitii na kuinuka ili kuifanya… kwa utii wake kamili kwa Mungu, Abraham amekuwa mfano na baba wa imani katika Agano la Kale alivyo Mama Maria katika Agano Jipya… kutoka kwake ahadi za Mwenyezi Mungu za ardhi nzuri, uzao na baraka zimetufikia katika Kristo Bwana wetu… kwa Babu yetu huyu mwema Agano la Mungu na watu wake limethibitishwa, taifa teule limeratibiwa na Mkombozi Mkuu ametujia… asante sana Baba Abrahamu.
Vile Mzee Abraham alivyoenda asikokujua kama alivyoamriwa na Bwana nasi tunapomaliza Juma la kwanza la Kwaresima tunaitwa kutoka katika nchi yetu ndiyo mazoea, maelekeo na tabia zisizo njema na kwenda katika nchi atakayotuonyesha Bwana, nchi inayofurika maziwa na asali ndio jamii mpya ya kikanisa katika nyakati mpya za kimasiha tukielekezwa kuishi upya wa maisha katika haki, amani, adili na usalama kwa mapendo kamili. Na tuwe na hakika kwamba tukienda na Babu Abraham yote yatakuwa yetu… tunakwenda wapi? Somo la Injili (Mt 17:1-9) linatuunganisha na Mitume Petro, Yohane na Yakobo kuupanda Mlima wa Bwana ili kuuingia utukufu wa Kristo Masiha katika upya wa maisha yetu. Namba tatu, licha ya ufanano wake na Nafsi za Utatu Mtakatifu, ni ishara ya ukamilifu hivi Petro, Yakobo na Yohane wanawakilisha ukamilifu wote wa Kanisa kizazi baada ya kizazi hata Kristo atakapokuja tena… wanayoyashuhudia mlimani ni sote tunayashuhudia na lengo la Kristo kugeuka sura na utukufu wake na yatokanayo yanatugusa moja kwa moja kwa njia ya ubatizo wetu.. sisi letu linabakia kuwa moja tu, ndio kwenda pamoja na Abraham kama Mungu alivyoamuru.
UFAFANUZI: Katika dunia ya leo, watu wengi wanaishi kama Abrahamu bila hiari yao: wakimbizi wa vita, wahamiaji, waliopoteza ajira, waliovunjika moyo. Lakini Abrahamu anatufundisha kwamba Mungu yupo hata pale ambapo njia haionekani. Katika mwaka huu ambapo Kanisa linamuenzi Mt. Fransisko wa Assisi, miaka 800 baada ya kifo chake, tunakumbushwa mfano wa mtu aliyemruhusu Kristo abadilike sura ndani ya maisha yake. Tahere 10 Januari Baba Mtakatifu Leo XIV alizindua rasmi na kutangaza kuenzi maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi utakao hitimishwa tarehe 10 Januari 2027. Mtakatifu Francisko wa Assisi aliishi somo hili kikamilifu. Aliacha mali ya baba yake, akaacha heshima ya kijamii, na akachagua umaskini ili kumfuata Kristo. Kama Abrahamu, aliondoka bila uhakika wa kesho, lakini akawa baraka kwa wengi. Katika somo la pili, Mtume Paulo anatuhimiza: “Shiriki mateso kwa ajili ya Injili kwa nguvu ya Mungu.” Haya si maneno mepesi. Paulo anaandika haya akiwa katika kifungo. Anatambua kuwa kufuata Kristo hakumaanishi maisha rahisi, bali maisha yenye maana. Leo hii, Wakristo wanateswa kwa imani yao katika nchi mbalimbali, Ukweli wa Injili unapingwa,Maadili ya Kikristo yanachukuliwa kuwa ya kizamani. Bwana Yesu anapong’aa juu ya Mlima anatimiliza maono ya Nabii Danieli aliyemuona Mmoja aliye mfano wa wanadamu akija pamoja na mawingu (7:13)… ni tendo lenye kuwajenga na kuwaimarisha wafuasi wa Kristo kukikabili kitendawili cha Msalaba wa Bwana, kwamba Msalaba wake Yesu si kikwazo, si laana, si aibu, si kushindwa bali ni ushindi, utukufu na enzi… ni tendo linalowashusha Musa na Eliya wanaoonekana kumpisha Kristo anayekamilisha Torati yote na Manabii kwa Agano Jipya na la milele katika damu yake mwenyewe.
Ni tukio la kung’ara kwake Kristo linalowezesha nafsi zetu kuvuka na kushinda maumivu ya maisha ya duniani na kumuona Mungu katika utukufu mkuu katika kila jambo tunalokutana nalo na kila hatua tunayopiga… ni tukio linalofunua yasiyojulikana kwa macho ya kawaida, kumbe kuna uhalisia wa vingi tusivyoviona bado, tena vizuri na vya thamani mno… ni tukio ambapo Baba katika Roho Mtakatifu anamuheshimisha Mwana kama Mpendwa wake akimuinua juu ya vyote mbinguni na duniani, juu kabisa ya mamlaka na nguvu nyinginezo zote akibaki pekee kuwa Mfalme na Mtawala. Naye anapong’aa sura yake huyo Mwana mpendwa sana wa Baba anaileta mbingu duniani, walichokishuhudia Petro, Yohane na Yakobo ni kionjo halisi cha mbingu ilivyo, tutamani basi uzuri huo, neema hiyo, baraka hizo, bahati hiyo, heri hiyo kwa kuinuka pamoja na Abrahamu na kwenda tukiitikia wito wetu kama Bwana alivyoamuru… Bwana anapong’aa sura kila kitu kinabadilika… muonekano wake, hali ya hewa, anaozungumza nao, uwepo wa Baba katika sauti yenye kumtambulisha na kuamuru tumsikilize na nguvu ya Roho wa Bwana katika wingu lile jeupe… nasi tunaomfuata sharti tung’ae pamoja naye… si tu sura na muonekano wetu wa nje zaidi sana uangavu wa roho na usafi wa moyo, udumifu wa imani, kuzingatia ya umilele katikati ya yanayopita tu … pale juu mlimani kwa Bwana. Basi Abramu akaenda, kama Bwana alivyomwamuru”.. Ili kukifikia kilele cha Tabor ya kiroho ni lazima kujipatia wepesi na uhuru kwa kutokuwa na mizigo mingi… ukitaka kupanda Mlima Kilimanjaro huanza kwa furaha na kelele, lakini muda unavyoenda ukimya na unyamavu hutamalaki, unapoendelea zaidi kila kitu huwa ni kizito hata mavazi uliyoyavaa, miguu hutetemeka, moyo hunung’unika kifuani na hewa huonekana haitoshi.
Uking’ang’ania vitu vingi kwa hakika hutafikia kilele kile kizuri, cheupe na kirefu zaidi Afrika, kilele cha Uhuru (Chenye urefu 5895m)… ndivyo ilivyo safari ya kiroho, ili kumfikia Bwana anayeng’aa mlimani ni lazima kufanya mazoezi mengi ya utimamu kwa kuacha vingi, kujinyima kwa ajili ya wahitaji, kufunga, kusali na kujisadaka, yaani Kwaresima. Tukiisha kufika na Abrahamu anakotutaka Mungu tufike, mlimani kwa Bwana na kuuona utukufu wake, na kuisikia sauti yake ni lazima tushuke chini ya mlima waliko wenzetu wengi zaidi… wapo katika mahangaiko makubwa ya kibinadamu, wanahitaji tuwapelekee nuru ya Mlima Tabor, na tunapolifanya hili tulifanye kwa nia njema, tulifanye kwa upendo na ukarimu unaowapasa watu wapya walioshuhudia makuu ya Bwana mlimani pa utukufu. Mtakatifu Francisko wa Assisi aliishi Injili kwa unyenyekevu: Alimwona Kristo katika maskini, Aliheshimu viumbe vyote kama ndugu na dada, Alipinga ubinafsi wa dunia kwa maisha ya kujitoa. Katika dunia ya leo iliyojawa na ulafi, vita na uharibifu wa mazingira, mfano wa Mt. Fransisko ni mwito wa wongofu wa kweli. Kama yeye, nasi tunaalikwa kuwa: Vyombo vya amani; Nuru katika giza; Mashuhuda wa matumaini.