Tafuta

Kanisa Barani Afrika likibidiishwa na imani inayomwilishwa katika Injili ya upendo, Kanisa lazima liwe ni chombo na shuhuda wa upatanisho, haki na amani. Kanisa Barani Afrika likibidiishwa na imani inayomwilishwa katika Injili ya upendo, Kanisa lazima liwe ni chombo na shuhuda wa upatanisho, haki na amani.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 6 ya Mwaka A wa Kanisa: Upatanisho

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anaitaka Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujielekeza zaidi katika amana na utajiri wa Neno la Mungu ili iweze kushiriki kikamilifu katika huduma ya upatanisho, haki na amani kwa kuwa watumishi aminifu wa Neno la Mungu na kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani duniani! Waamini wawe ni mashuhuda wa upendo katika ukweli, kwani hii ndiyo chemchemi ya amani ya kudumu kati ya watu wa Mataifa.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 6 ya mwaka A wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume, “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” analitaka Kanisa Barani Afrika kuwa chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu likibidiishwa na imani inayomwilishwa katika Injili ya upendo, Kanisa lazima liwe ni chombo na shuhuda wa upatanisho, haki na amani. Huu ni utume maalum ambao unapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Kanisa Katoliki Barani Afrika. Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujielekeza zaidi katika amana na utajiri wa Neno la Mungu ili iweze kushiriki kikamilifu katika huduma ya upatanisho, haki na amani kwa kuwa watumishi aminifu wa Neno la Mungu na kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani duniani! Waamini wawe ni mashuhuda wa upendo katika ukweli, kwani hii ndiyo chemchemi ya amani ya kudumu. Waamini wajitahidi kumwilisha ukweli wa Sakramenti ya Upatanisho, wajenge na kudumisha umoja na mshikamano; kwa kukazia utamadunisho wa Injili na uinjilishaji wa utamadunisho. Kiini cha ujumbe umejikita katika uhuru wa mwanadamu kuchagua kati ya mema au mabaya, uzima na kifo. Kwa kuwa “Mungu alimwumba mwandamu mwenye akili kwa kumjalia hadhi ya nafsi kuanzisha na kutawala matendo yake. Naye alitaka mtu aachwe aifuate nia yake ili aweze mwenyewe kumtafuta muumba wake, na akiambatana naye kwa hiari, aweze kufikia utimilifu wa furaha” (KKK 1730).

Kanisa Barani Afrika liwe mjumbe na chombo cha upatanisho
Kanisa Barani Afrika liwe mjumbe na chombo cha upatanisho   (Vatican Media)

Hivyo “Mwanadamu ni mwenye akili, na kwa hiyo anafanana na Mungu, ameumbwa na utashi na uhuru na ni bwana wa matendo yake” (KKK 1730). Lakini kwa kuwa ni kiumbe, anapaswa kuzifuata Amri za Mungu ili aweza kuchagua mema na kuacha mabaya. Ni kwa kufanya hivyo anakuwa chini ya maongozi ya Mungu na baada ya maisha ya hapa duniani atastahilishwa kuingia katika furaha  ya milele yote mbinguni. Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema: “Uwe kwangu mwamba wa nguvu, nyumba yenye maboma ya kuniokoa. Ndiwe genge langu na ngome yangu; kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge” (Zab. 31:2-4). Na Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu, wewe wasema kuwa umo miongoni mwao walio wema na wanyofu. Utujalie kwa neema yako tuishi kitakatifu kusudi upende kukaa ndani yetu”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Yoshua bin Sira (YbS 15:15-20). Ujumbe wake umejikita katika uwezo wa mtu kutumia uhuru na utashi wake kuishi kadiri ya mpango wa Mungu alivyomuumba. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inaeleza vizuri sana ukweli huu ikisema; “Uhuru ukiwa na mizizi katika akili na utashi, ni uwezo wa kutenda au kutokutenda, kufanya hiki au kile, kutenda matendo yake mwenyewe na makusudi. Kwa njia ya utashi huru kila mmoja anajiunda mwenyewe. Uhuru ni nguvu ya ndani ya kukua na kukomaa katika ukweli na wema. Na uhuru hupata ukamilifu wake unapoelekezwa kwa Mungu, heri” ya mwanadamu. Kwa kuwa uhuru haukufungi na Mungu, hivyo “huainisha matendo yaliyo ya kibinadamu…msingi wa sifa au lawama, mastahili au shutuma” (KKK 1731-1732).

Mwanadamu ana utashi kamili wa kuamua mema na mabaya
Mwanadamu ana utashi kamili wa kuamua mema na mabaya   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Heri walio kamili njia zao, waendao katika sheria ya Bwana. Heri wazitiio shuhuda zake, wamtafutao kwa moyo wote. Wewe umetuamuru mausia yako, ili sisi tuyatii sana. Ningependa njia zangu ziwe thabiti, nizitii amri zako. Umemtendea mtumishi wako ukarimu, nipate kuishi, nami nitalitii neno lako. Unifumbue macho yangu, niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako. Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako, nami nitaishika hata mwisho. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, naam, nitaitii kwa moyo wangu wote” (Zab. 118:1-2, 4-5, 17-18, 33-34). Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 2:6-10).  Ujumbe ni huu: Ilikuwa mpango wa Mungu kwa Hekima yake, kutukomboa sisi kwa msalaba wa Yesu Kristo. Hekima hii imefunuliwa kwa wanyofu wa moyo kwa njia ya Roho, maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Hekima hii, wenye kuitawala dunia hawaijui; maana kama wangeliijua, wasingelimsulibisha Bwana wa utukufu. Fundisho kwetu, tuwe wanyoofu wa moyo, tujivike unyenyekevu, ili Roho Mtakatifu aweze kutuongoza katika kuijua hekima ya Mungu, ilipate kutuwezesha kuishi vyema maisha ya hapa duniani kwa kuzifuata amri za Mungu, ili baada ya maisha ya hapa duniani tukastahilishwe kuingia katika furaha ya ufalme wa milele mbinguni.

Waamini wajipatanishe na Mungu pamoja na nafsi zao
Waamini wajipatanishe na Mungu pamoja na nafsi zao   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 5:17-37). Ujumbe msingi ni huu; Torati na Manabii ni jumla ya maongozi ya Mungu kwa mwanadamu aliyoyafunua katika Agano la Kale. Yesu hakuja kutangua chochote, bali kutimiliza yote akikazia kuwa kila wazo, neno na tendo liwe na lengo moja tu: kutimiza mapenzi ya Mungu. Amri zote zinapaswa kufundishwa na kufuatwa kwa ukamilifu wake. Hakuna amri ambayo ni ndogo ya kupuuzwa na kutokufuatwa, zote lazima zifuatwe – kuua, kuwaka hasira, kufyolea, kuapiza, kuzini au kutamani kisicho chako, zote ni dhambi. Ili kuonesha ubaya wake Yesu anatumia lugha ngumu na ya kuogofya kama vile kung’oa jicho au kuukata mkono, na kuvitupilia mbali hivi viungo pale vinapotukosesha. Lakini pia anasisitiza umuhimu wa kusameheana na kusuluhishana maana hicho ndicho kipimo cha sisi kusamehewa na sadaka zetu kukubaliwa mbele za Mungu. Ili tuweze kufanikiwa kuyaishi mausia haya ya Yesu, tunapaswa kutumia vyema akili, utashi na uhuru wetu. Lakini “uhuru wa mwanadamu una mipaka na waweza kukosea. Kwa kweli mtu alikosa. Kwa hiari alitenda dhambi. Kwa kukataa mpango wa Mungu na mapendo, alijidanganya mwenyewe; akawa mtumwa wa dhambi” (KKK 1739). Hivyo Mungu ametuwekea Amri zake zitusaidie kujua na kutofautisha mema na mabaya, ili tuweze kuchagua na kutenda kwa uhuru. Lakini kwa sababu ya mazoea mabaya, vishawishi, na “mzizi wa dhambi unaokuwa ndani ya moyo wa mtu, katika utashi wake huru” (KKK 1853), amri za Mungu zinaonekana kuwa ni kikwazo cha kuwa huru, chanzo cha mateso na mahangaiko. Ili tuweze kuondoka na hali hii yatupasa kuwa na mazoea ya kutenda mema tujijengee fadhila, ili iwe rahisi kwetu kuchagua kutenda mena na kuwa huru zaidi. Ndiyo maana Kristo Yesu anavyotuasa akisema; mmezoea kufanya hivi, mimi nawaambia fanyeni hivi.

Kanisa Barani Afrika liwe ni shuhuda na chombo cha upatanisho
Kanisa Barani Afrika liwe ni shuhuda na chombo cha upatanisho   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika hili Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa; “Kadiri mmoja anavyofanya mema ndivyo anavyokuwa huru zaidi. Hakuna uhuru wa kweli isipokuwa kuhudumia yaliyo mema na ya haki. Kuchagua kukaidi na kutenda uovu ni kutumia vibaya uhuru na hupelekea kwenye utumwa wa dhambi. Uhuru humfanya mtu awe na madaraka juu ya matendo yake pale yanapokuwa ya hiari. Maendeleo katika fadhila, ujuzi wa wema, na kujinyima hukuza nguvu ya utashi juu ya matendo yake” (KKK 1733-1734). Hivyo ili tuweze kufanya mema kwa urahisi lazima tujijengee fadhila kwa kutenda mema kwa kurudiarudia mpaka kuyafanya yawe mazoea. Kwa maana; “Fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu, bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi” (KKK 1803). “Ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo yetu, na zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala, na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Mtu wa fadhila anatenda mema bila kuzuiwa” (KKK 1804). “Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu” (KKK 1803).

Heri waendao katika sheria ya Bwana
Heri waendao katika sheria ya Bwana   (Vatican Media)

Licha ya kuwa “fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu. Ni matunda na mbegu ya matendo mema kimaadili. Zawezesha nguvu za kibinadamu kuungana na upendo wa kimungu” (KKK 1804). Kwa nguvu zetu wenyewe tu, hatuwezi kuimarika. Basi tumwombe Yeye aliyetuumba atujalie neema na baraka zake tuweze kuutumia vyema akili, uhuru na utashi, vipawa alivyotujalia katika kutimiza mapenzi yake ili mwisho wa yote tuweze kupokea taji ya utukufu mbinguni aliko yeye tukafurahi na watakatifu milele yote. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali: “Ee Bwana, tunakuomba kafara hii itutakase na kutufanya wapya; tena ituletee tuzo la milele sisi tunaotimiza mapenzi yako”. Nayo antifona ya Komunyo inasisitza kusema: “Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (Yn. 3:16). Hili ndilo tumaini ambalo mama Kanisa anaweka katika sala baada ya komunyo akisali; “Ee Bwana, tumeshiba chakula cha mbinguni. Tunaomba utujalie tutamani sikuzote chakula hicho kinachotupa uzima wa kweli”. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 6 Mwaka A
11 Februari 2026, 15:50