Tafuta

Waamini wanaalikwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa matendo yao adili na matakatifu Waamini wanaalikwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa matendo yao adili na matakatifu  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 5 ya Mwaka A wa Kanisa: Nuru na Chumvi ya Dunia

Ujumbe mkuu katika Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 5 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni huu; tunaalikwa kuwa Nuru na chumvi ya ulimwengu kwa kutenda matendo ya huruma ya kiroho na kimwili, ili kwayo watu wengine waweze kumtambua Mungu wa kweli, muumba wa vitu vyote vinavyoonekana na visivyooneka. Mungu anayetuita tuishi kitakatifu kama yeye alivyo Mtakatifu ili mwisho wa maisha yetu ya hapa duniani ukifika atustahilishe kuishi naye!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya mwaka A wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. “Amani huanza na utu! Wito wa Kimataifa wa Kukomesha Biashara Haramu ya Binadamu” ndiyo kauli mbiu inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo! Kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Ujumbe mkuu katika Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 5 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni huu; tunaalikwa kuwa Nuru na chumvi ya ulimwengu kwa kutenda matendo ya huruma ya kiroho na kimwili, ili kwayo watu wengine waweze kumtambua Mungu wa kweli, muumba wa vitu vyote vinavyoonekana na visivyooneka. Mungu anayetuita tuishi kitakatifu kama yeye alivyo Mtakatifu ili mwisho wa maisha yetu ya hapa duniani ukifika atustahilishe kuishi naye milele yote mbinguni. Mungu anayestahili kuabudiwa na kutukuzwa milele kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba; kwa maana ndiye Mungu wetu” (Zab. 95:6-7). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utulinde sisi watoto wako kwa pendo lisilo na mwisho. Na kwa kuwa twategemea tu neema yako ya mbinguni, utuhifadhi daima kwa ulinzi wako.”

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni nuru ya Mataifa: Ushuhuda
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni nuru ya Mataifa: Ushuhuda   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 58:7-10). Ni mafundisho kwa Wayahudi waliorudi toka utumwani Babeli kuwa maisha ya sala, sadaka na kufunga yanayompendeza Mungu ni yale yanayoenda pamoja na matendo ya huruma kwa wengine, kama vile kuwapa chakula wenye njaa, mahali pa kuishi wasio na makao, kuwavika wasio na nguo. Kwa kufanya hivyo mwanga utawaangaza kama pambazuko, mwanga utaangaza gizani na kivuli chao kitakuwa kama mchana. Ni kwa kufanya hivyo watampendeza Mungu na watakuwa nuru kwa wengine. Ushauri huu unatuhusu sisi sote tuliobatizwa. Mungu atakuwa nuru yetu na nuru hii itakuwa ndani mwetu, tutampendeza na tutakuwa nuru kwa wengine kama sala, sadaka, mfungo wetu utaambatana na matendo ya huruma. Ni katika muktadha huu, Zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; Nuru huwazukia wenye adili gizani; wenye fadhili, huruma na haki. Heri atendaye fadhili na kuponyesha; Atengenezaye mambo yake kwa haki. Kwa maana hataondoshwa kamwe; Mwenye haki atakumbukwa milele. Hataogopa habari mbaya; moyo wake u imara ukimtumainia Bwana. Moyo wake umethibitika hataogopa, hata awaone watesi wake wameshindwa. Amekirimu, na kuwapa maskini, haki yake yakaa milele, pembe yake itatukuzwa kwa utukufu (Zab. 111:4-9.)

Kristo Yesu ni Mwanga kwa Mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli
Kristo Yesu ni Mwanga kwa Mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 2:1-5). Ujumbe ni huu: Mungu anachagua viumbe dhaifu kuwa vyombo vya kulitangaza Neno lake na kuusimika ufalme wake. Utume huu hautegemei hekima ya kibinadamu, ufasaha wa lugha wala maneno ya mhubiri ili kushawishi akili za watu kulipokea na kuliishi Neno la Mungu. Ni nguvu ya Roho wa Mungu na ushuhuda wa kiimani ndivyo vinavyofanya kazi ya kuwavuta watu kwa Mungu. Sisi tumekombolewa kwa msalaba wa Kristo, ulio Nuru na Mwanga wa maisha yetu. Hivyo kila mkristo anapaswa kuunyanyua msalaba wa Kristo juu kwa nuru ya matendo yake ili awamulike wengine wauone na kuukubali kuwa ni njia ya wokovu wetu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo (Mt 5:13-16). Ujumbe wake umejikita katika ishara ya chumvi na nuru, msisitizo ukiwa katika umuhimu wake katika maisha ya kila siku, sio tu kwa mwanadamu bali kwa kila kiumbe hai. Mwaliko ni kuwa kile ambacho chumvi inafanya katika chakula na vitu, na kile ambacho mwanga unafanya katika maisha ya viumbe hai na visivyo hai, ndicho ambacho kila mkristo anapaswa kuwa kwa maneno na matendo yake. Kazi za chumvi ni pamoja na kukipa ladha chakula, kuhifadhi na kutunza vitu visiharibike, ishara na alama ya hekima na busara, kwa kuishi mda mrefu. Ndiyo maana waswahili husema; Mtu amekula chumvi nyingi, kumaanisha kuwa ameishi miaka mingi na ana hekima. Hivi ndivyo inavyompasa kila mkristo kuwa hapa duniani, matendo yake mema ya kama chumvi, yakoleze na kuleta ladha ya maisha, yatunze na kulinda utakatifu wa maisha.

Kristo Yesu ni Jua la Haki
Kristo Yesu ni Jua la Haki

Nuru huondoa giza na hivyo kutuwezesha kuona uzuri, uhalisia na thamani ya vitu jinsi vilivyoumbwa na Mungu na kuvitumia kadiri ya mpango wake. Mwanga unawezesha mimea kukua. Wana sayansi wanatuambia kwamba kama mwanga wa jua ungetoweka duniani, maisha yangetoweka; viumbe hai vingekufa. Kile ambacho mwanga unafanya ndicho anachopaswa kufanya kila mkristo katika maisha ya kila siku, kuwasaidia wengine kukua, kukomaa na kuimarika katika maisha ya kitakatifu. Neno la Mungu ni kama Nuru. Ndiyo maana mzaburi anasema; “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga katika njia yangu” (Zab. 119:105). Mtu anapoliishi Neno la Mungu anakuwa na nuru, anaweza kufuata njia nzuri ya kuishi. Na yeyote anayewajulisha wengine neno la Mungu na Amri zake, anakuwa chanzo cha mwanga kwao, anawatoa katika gizani, ili wamuone Mungu na waione njia ya kuweza kumfikia. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatuelekeza kuwa kwa kutenda dhambi, “mtu amegawanyika ndani yake mwenyewe. Hivyo maisha yake ni mapambano kati ya wema na uovu, kati ya nuru na giza” (KKK 1707). Ili aweze kuushinda uovu, lazima ajivike Mwanga halisi. Lakini yeye peke yake hawezi kujivika mwanga huo. Kanisa ndilo lenye uwezo wa kumvika mtu Mwanga halisi. Lakini “Kanisa halina mwanga mwingine zaidi ya ule wa Kristo Yesu” (KKK 748).

Nuru yenu iwaangazie watu, ili wamshukuru Mungu kwa matendo yenu!
Nuru yenu iwaangazie watu, ili wamshukuru Mungu kwa matendo yenu!   (AFP or licensors)

"Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Mungu ni Nuru halisi” (KKK 214). Ndivyo Kanuni ya Imani ya Nikea inavyoungama kuwa; Kristo Yesu ni “Mwana wa Pekee wa Mungu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli” (KKK 257). Ili Kanisa liweze kutuongoza kwa Kristo, Nuru halisi, lazima tuwe kwanza watoto wake. Ni kwa njia ya ubatizo tunapompokea Roho Mtakatifu, tunafanywa kuwa wana wa Kanisa, watoto wa nuru (rej. KKK 736). “Roho Mtakatifu hutufanya wapya katika nia ya roho zetu. Naye anatuangaza na kututia nguvu ili tuishi kama watoto wa nuru kwa wema wote, haki na ukweli katika mambo yote” (KKK1695). Hivyo, “kwa ubatizo, mbatizwa, anampokea Neno wa Mungu, yaani Kristo Yesu, Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu. Na baada ya kutiwa nuru, anakuwa mwana wa nuru, na nuru yeye mwenyewe” (KKK 1216). “Vazi jeupe analolipokea huashiri kwamba mbatizwa amemvaa Kristo, amefufuka pamoja na Kristo. Mshumaa anaupokea unaowashwa kutoka mshumaa wa Pasaka huashiria kwamba Kristo amemwangaza Mkristo mpya. Hivyo katika Kristo, mbatizwa anakuwa ni nuru ya ulimwengu” (KKK 1243).

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni nuru na chumvi ya Ulimwengu
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni nuru na chumvi ya Ulimwengu   (@Vatican Media)

Lakini pia, “Amri kumi za Mungu ni mwanga uliotolewa kwa dhamiri ya kila mtu ili kumjulisha wito na njia za Mungu na kumkinga dhidi ya uovu” (KKK 1962). “Katika malezi ya dhamiri, Neno la Mungu ni nuru juu ya njia yetu. Tunapaswa kulitumia katika imani na sala na kulitia katika utendaji” (KKK 1785). Ni katika sisi kuishi maisha ya mfano, watu wanapoyaona matendo yetu wanamtukuza Mungu, na wanafahamu wanavyopaswa kuishi kitakatifu. Ni katika mukatdha huu “Kristo, mwanga wa wokovu wa watu wote, anadhihirishwa kwa njia ya maisha ya kiliturujia – huduma – ya Kanisa moja kwa taifa na kwa utamaduni ambako, Kanisa – kila mbatizwa – limetumwa na ambamo limesimikwa” (KKK 1202). Basi, tumwombe Mungu atujalie neema na baraka zake, ili tuwe na ujasiri na moyo wa kujisadaka, tuweze kuwa kweli nuru na chumvi kwa mataifa tukiwa tumeungana na Kristo Nuru na Mwanga wa kweli, na wokovu wetu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana Mungu wetu, umeumba vitu hivi ili vitusaidie hasa katika unyonge wetu. Tunakuomba utujalie viwe pia sakramenti ya kutuletea uzima wa milele”. Na katika sala baada ya Komunyo anasali hivi; “Ee Mungu, umependa tushiriki mkate mmoja na kikombe kimoja. Tunakuomba utujalie kuishi tumeungana na Kristo, tupate kuzaa matunda kwa furaha kwa manufaa ya wokovu wa ulimwengu”. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 5 Mwaka A
05 Februari 2026, 14:54