Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 5 ya Mwaka A wa Kanisa: Chumvi ya Dunia na Nuru ya Ulimwengu. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 5 ya Mwaka A wa Kanisa: Chumvi ya Dunia na Nuru ya Ulimwengu.  (@VATICAN MEDIA)

Tafakari Dominika 5 Mwaka A wa Kanisa: Chumvi na Nuru ya Ulimwengu: Ushuhuda

Liturujia ya Neno la Mungu inatukumbusha juu ya wito wetu wa kuwa, “Chumvi ya Dunia na Nuru ya Ulimwengu” Dominika iliyopita alitufundisha Heri, katiba na mwongozo wa maisha yetu ya ufuasi iwapo tunataka kuipata furaha ya kweli katika uzima wa milele. Katika Dominika hii anatualika si tu kuyasikiliza mafundisho yake, haitoshi tu kuzifahamu Heri, haitoshi tu kulijua Neno lake, bali kuyaweka katika matendo, kwa kupenda, kuhurumia maskini, kusamehe na kuthamini!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 5 ya Mwaka A wa Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: “Amani huanza na utu! Wito wa Kimataifa wa Kukomesha Biashara Haramu ya Binadamu” ndiyo kauli mbiu inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo! Kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. “Amani iwe kwenu.” Yn 20:19. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo kwamba: Hii ni salam ya Kristo Yesu Mfufuka kwa wafuasi wake, sehemu ya mchakato wa upyaisho wa ubinadamu unaotambua ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Liturujia ya Neno la Mungu inatukumbusha kwa kina juu ya wito wetu kama wafuasi wa Kristo kuwa, “Chumvi ya Dunia na Nuru ya Ulimwengu” Dominika iliyopita alitufundisha Heri, katiba na mwongozo wa maisha yetu ya ufuasi iwapo tunataka kuipata furaha ya kweli katika uzima wa milele. Katika Dominika hii anatualika si tu kuyasikiliza mafundisho yake, haitoshi tu kuzifahamu Heri, haitoshi tu kulijua Neno lake, bali kuyaweka katika matendo, kwa kupenda, kuhurumia maskini, kusamehe, kuthamini na kujali. Tunapoishi Imani yetu kwa matendo, tunapoziishi Heri kweli katika maisha yetu ya ufuasi, maisha yetu yanaleta ladha kwa wengine, yanaleta nuru na mwanga kwa wengine. Tuombe neema ya kuyaelewa, kuyashika na kuyaishi mafundisho ya Kristo ili Ufalme wake uendelee kukua na kuenea kati yetu.

Tafakari Dominika ya 5 ya Mwaka A wa Kanisa: Ushuhuda wenye mvuto
Tafakari Dominika ya 5 ya Mwaka A wa Kanisa: Ushuhuda wenye mvuto   (ANSA)

Somo la Kwanza ni kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya 58:7-10. Somo la kwanza tulilolisikia, ni kutoka katika Kitabu cha Tatu cha Nabii Isaya (trito Isaiah), kinachoanzia na Sura ya 56-66. Mazingira ya somo hili ni karibu na karne ya 5 BC mara baada ya Taifa la Israeli (Yuda) kurudi kutoka uhamishoni Babeli. Walikua wametoka utumwani na kurejea Yerusalemu lakini hali yao kiroho na kijamii haikua imetengamaa. Kiroho, Mara baada ya kulijenga upya hekalu kipindi cha Ezra na Nehemia, watu waliendelea tena kushiriki ibada muhimu katika hekalu kadiri ya matakwa ya Torati na dini ya kiyahudi yaani, kusali, kufunga na kutoa sadaka. Licha ya ibada hizo, bado hali ya kijamii haikua imeponywa. Kulikua bado na dhuluma, unyonyaji na ukandamizaji wa maskini na ukosefu wa haki ya kijamii. Hii ikapelekea sala na ibada zao kukosa maana mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mungu hapendezwi tu na sadaka, bali uadilifu, haki na unyofu wa moyo. Watu wakaanza kulalamika kwamba, Mungu hasikii sala zao wala hajibu kufunga kwao. Nabii Isaya katika sehemu hii tuliyosikia leo sura hii ya 58:1-10 anawaeleza wazi sababu kwa nini sala zao hazijibiwi na Mungu na wala mfungo wao haumpendezi Mungu. Anawaeleza wazi kwamba ni kwa sababu ibada yao haikua inaendana na Matendo yao. Anawakumbusha saumu na ibada ya kweli inayompendeza Mungu, kwamba ni kugawia wenye njaa chakula chako na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako. Ni kumvisha nguo aliye uchi. Na matokeo yake mtu wa namna hii Isaya anayaweka bayana, kwamba ndipo nuru yake itakapopambazuka kama asubuhi, afya yake itatokea mara, haki yake itamtangulia na utukufu wa Bwana utamfuata nyuma ili umlinde. Ataita, na Bwana ataitika, atalia naye Bwana atasema Mimi hapa. Kumbe ibada ya kweli yapaswa kuonekana katika Matendo ya wazi ya nje, katika uchaji, uadilifu, huruma na haki na hapo matokeo yake ni kuwa nuru na mwanga.

Nuru Yenu Iangaze kwa ushuhuda wa matendo adili na matakatifu
Nuru Yenu Iangaze kwa ushuhuda wa matendo adili na matakatifu   (@Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 5:13-16. Katika somo la Injili Takatifu, Bwana wetu Yesu Kristo bado anatoa hotuba yake Mlimani. Mara baada ya kutoa mafundisho ya kina juu ya Heri, Injili tuliyoisikia Dominika iliyopita, Bwana wetu Yesu Kristo leo anawapa wafuasi wake wajibu muhimu. Anawaambia, “Ninyi ni chumvi ya dunia, ninyi ni nuru ya ulimwengu” Kwa nini sehemu hii inakuja tu mara baada ya Heri nane? Jibu ni kwamba Heri nane zinaeleza utu wa ndani wa mwanafunzi wa Kristo, ndizo zinazotoa definition au utambulisho wa ndani wa yeye anayetaka kuupata ufalme wa Mbinguni. Lakini utambulisho huu wa ndani wapaswa kuonekana katika maisha ya nje. Ni jinsi gani mfuasi wa Kristo anaziishi Heri katika maisha ya nje ya kila siku katika jamii. Kumbe mwanga na chumvi vinaeleza sasa nafasi ya nje ya mwanafunzi wa Kristo katika jamii. Sehemu ya Injili ya leo yasimama kama Daraja kati ya utambulisho wa mwanafunzi wa Kristo (Heri nane) na wajibu wa kila siku wa mwanafunzi wa Kristo (ushuhuda wa maisha). Kwa nini Yesu anatumia picha ya Chumvi na Nuru/ Mwanga? Mwinjili Mathayo aliandika Injili hii kwa jumuiya ya Wakristo Wayahudi. Hawakuwa bado wengi, kwa kuwa Ukristo ulikua haujasambaa sana bado. Lakini Kundi hili dogo lilikua katikati ya Kundi kubwa ambalo halikuiishi bado Injili na hapa kukawa na hatari sasa au ya kujitenga na dunia kwa wanafunzi hawa, au ya kuyeyuka kwa maana ya kwamba kupoteza utambulisho wao, kupoteza ladha yao kama wafuasi wa Kristo. Ndio maana Kristo Yesu anawafundisha kwamba, matendo yao mema yapaswa kuwa chumvi, kukoleza Injili katika maisha ya wengine. Kama ilivyo chumvi, maisha ya mfuasi wa Kristo yapaswa kuleta uponyaji, yapaswa kuhifadhi dunia dhidi ya uharibifu wa Imani na maadili. Hali kadhalika miji mingi ilijengwa juu ya vilima ili kuonekana kwa wazi kwa wote. Hali kadhalika maisha ya Mwanafunzi wa Kristo yapaswa kuwa wazi, yaonekane na watu kwa njia ya maneno na matendo yao mema. Imani na utakatifu wa ndani wapaswa kuoneakana kwa matendo ya nje ili kuwaangaza waliopo bado gizani ili nao wamtukuze Mungu Baba yetu aliye Mbinguni.

Maisha Yenu yawe ni ushuhuda angavu wa utakatifu wa maisha
Maisha Yenu yawe ni ushuhuda angavu wa utakatifu wa maisha

Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka wa kwanza1 Kor 2:1-5. Sehemu hii ya somo la leo inafuata mara baada ya fundisho muhimu ambalo ndilo kiini cha wakara huu mzima. Dominika iliyopita Mtume paulo alitufundisha namna Mungu anavyofanya kazi kinyume na mitazamo na vipimo vya kidunia. Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviabishe vyenye nguvu, tena Mungu alichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa ili avibatilishe vilivyoko. Ni kwa njia ya msalaba, Mwenyezi Mungu ameamua kudhihisha kwetu nguvu yake na hekima yake. Mtume Paulo anatumia mfano wake binafsi kama ushahidi wa kile anachofundisha. Kumbe nia ya Mungu ni kuonesha kwamba nguvu ya Injili si katika ufasaha wa maneno au hekima ya mhubiri bali katika nguvu ya Mungu anayefungua mioyo ya watu, kama alivyofungua moyo wa Paulo, ili wasadiki. kumbe ukristo na ufuasi wetu sio swala tu la kujionesha, kujikweza na kujisifu, bali kuishi kweli thamani hii kubwa ya ukombozi wetu, iliyopatikana katika unyenyekevu na udhaifu kwa mtazamo wa kidunia, lakini ndicho kipimo kweli cha hekima kwa mtazamo wa Kimungu.

Maisha yenu yawe ni chumvi na nuru kwa wengine
Maisha yenu yawe ni chumvi na nuru kwa wengine   (@Vatican Media)

Ndugu zangu katika masomo yote katika Dominika hii ya tano tuna mafundisho yafuatayo ya kujifunza. Fundisho la Kwanza: Kristo anatualika kuwa chumvi ya dunia. Ni kwa jinsi gani tunakuwa chumvi ya dunia, na nini kinafanya chumvi hiyo kupoteza ladha yake? Liturjia ya Neno la Mungu katika dominika ya leo kama nilivyotangulia kusema katika utangulizi inatukumbusha wajibu wetu wa msingi sana sisi kama wafuasi wa Kristo wa kuwa chumvi ya ulimwengu. Katika ulimwengu wa kale, chumvi ilikua na kazi kuu tatu za msingi. Tukifahamu matumizi haya ya chumvi na umuhimu wake katika ulimwengu wa kale, basi tutaweza kuelewa barabara ni kwa namna gani sisi tunaweza kuwa chumvi katika maisha yetu ya kawaida kabisa ya kila siku. Katika ulimwengu wa kale, chumvi ilikua na kazi kuu tatu zifuatazo. Kwanza, ilitumika kuzuia nyama kuoza na ilihifadhi pia vyakula kwa muda mrefu bila kuharibika, wakati ambapo teknolojia ya uhifadhi wa vyakula haikua kubwa kama wakati wa sasa. Pili, chumvi ilitumika kuleta ladha katika chakula, na bila chumvi chakula hakikuvutia, hata sasa, chakula bila chumvi hakina ladha wala hamu. Tatu chumvi ilileta thamani, ilikua ni bidhaa adimu na yenye thamani kubwa. Aliyemiliki shehena ya chumvi huyo alikua ni tajiri mkubwa. Kumbe ni katika uelewa huo, Kristo anawatuma wafuasi wake kuwa chumvi ya dunia. Kwetu sisi fundisho hili lina maana gani? Na ni kwa jinsi gani tunaweza kupoteza thamani au ladha ya chumvi hiyo?

Maisha Yenu yapate chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu
Maisha Yenu yapate chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Kwanza: Chumvi inahifadhi na hivyo, Maisha yetu yapaswa kuhifadhi: Uhai; jamii, familia, kanisa dhidi ya uharibifu. Maisha ya mfuasi wa Kristo ni maisha ya Heri. Mfuasi wa Kristo ana wajibu msingi wa kuihifadhi jamii, familia na kanisa dhidi ya uharibifu.  Kuwa chumvi ya dunia katika maisha yetu ya kila siku ni kusimama imara dhidi ya uozo wa namna mbalimbali katika familia, katika jamii na katika kanisa. Mambo yote yanayofifisha imani na maadili tunapaswa kuyapatia tiba kwa njia ya maisha yetu ya ufuasi, kwa kuiishi kweli Injili na kusimamia imara mafundisho ya imani, maadili, mila na desturi zetu. Tunaishi katika ulimwengu wenye mambo mengi yanayohatarisha uhai wa familia, jamii na kanisa kwa vizazi vijavyo. Kama chumvi ya dunia, tunapaswa kusimama imara dhidi ya mmomonyoko wa maadili na kiimani kuanzia katika ngazi za familia zetu. Ulevi, matumizi ya dawa za kulevya, matumizi ya vidhibiti mimba, utoaji wa mimba, uregevu dini, mila na desturi zisizofaa, rushwa, ufisadi, unyanyasaji na udhalilishaji wa wengine. Tunapaswa kukemea, kuonya na kufundisha bila kuona aibu, kwa njia hiyo tutahifadhi vizazi vijavyo, tutahifadhi kanisa la kesho, tutahifadhi taifa imara la kesho dhidi ya uharibifu na uozo wowote. Maneno yetu yalete uponyaji, yalete furaha, yalete amani. Maisha yetu yawe tiba, katika ndoa, katika maeneo yetu ya kazi, katika jumuiya zetu za kitawa, katika biashara zetu. 

Chumvi ya Dunia na Nuru ya Mataifa: Ushuhuda wenye mvuto
Chumvi ya Dunia na Nuru ya Mataifa: Ushuhuda wenye mvuto   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pili: Chumvi inaleta ladha, Maisha yetu yapaswa yawe na maana kwa wengine. Chumvi huleta Ladha katika maisha, hali kadhalika maisha yetu ya Mfuasi wa Kristo yapaswa kuwa maisha ya tofauti. Katika somo la kwanza, Nabii Isaya anatuleza nini maana ya kuwa chumvi katika maisha ya wengine, kwa kuiishi vyema kweli Imani yetu katika Matendo. Imani sio swala la kuzungumza tu bali ni Imani nayoonekana kila mara katika Matendo kama anavyotufundisha pia Mtume Yakobo 2:14-26. Tunawezaje basi kuleta Ladha katika maisha ya watu wengine? Tunawezaje kuleta utofauti katika maisha ya wengine? Nabii Isaya anatukumbusha wajibu wetu wa kuwahurumia maskini kwa kuwapa chakula chetu, na kuwapa hifadhi wale wote waliotupwa nje. Ni kuwapa nguo wale wasio na nguo, kuwavika walio uchi. Je ninashiriki namna gani kuleta Ladha katika maisha ya watu wengine? Nipo tayari kutoa sehemu kidogo ya kile Mungu amenijalia ili nilete tabasamu kwa watu wengine? Pengine familia zetu zimepoteza kabisa ladha, huenda unaishi katika ndoa ambapo hakuna kabisa ladha, unaishi katika jumuiya ambapo hakuna ladha tena ya kuishi. Huenda tumeumizwa kwa maneno mabaya, kwa matukio na nyakati za huzuni, kwa kusingiziwa, kwa kusengenywa hata kufikia hatua ya kuona nyumba zetu, familia zetu, ndoa zetu si mahali tena tunaweza kupata furaha na amani ya moyo. Hakuna maana tena kurudi nyumbani kwa wakati, hakuna maana tena kukaa pamoja na kula pamoja katika jumuiya zetu, hakuna maana tena kusali pamoja, hakuna maana tena kusherehekea pamoja. Maisha hayana ladha tena. Kila mara tunapofikiri tunakutana na picha ya maumivu na matukio ya kukatisha tamaa au tuliyowatendea wengine au tuliyotendewa sisi. Kumbe mfuasi wa Kristo apaswa kuwa wa tofauti, apaswa kuleta ladha mpya katika maisha. Alipo Mkristo kuwe pa tofauti, familia na jumuiya zetu ziwe za tofauti, maisha yetu yawe ya tofauti, utendaji wetu uwe wa tofauti. Mkristo apaswa kutenda haki, Mkristo apaswa kusema ukweli, Mkristo apaswa kutia moyo, Mkristo apaswa kusamehe, Mkristo apaswa kuguswa na shida za wengine. Je, nipo wapi? 

Waamini wanaalikwa kuwa ni nuru ya walimwengu
Waamini wanaalikwa kuwa ni nuru ya walimwengu

Tatu: Chumvi huleta thamani, Mkristo apaswa kuitambua thamani yake na kuishi kama mtu mwenye thamani kubwa ndani mwake. Chumvi katika ulimwengu wa kale ilikua na thamani kubwa sana na ilikua ni bidhaa adimu kupatikanika. Kumbe Kristo anatualika kila Mkristo kutambua thamani ya tunu kubwa iliyo ndani mwetu. Kinyume chake tunapoteza thamani ya ufuasi wetu. Mtume Paulo anatukumbusha kuwa Mungu aliamua kuidhihirisha hekima yake katika mambo madhaifu, ambayo kwa mantiki na mtazamo wa kidunia yalionekana yasiyo na maana. Na kwa njia ya Msalaba sisi sote tumepokea hazina hiyo kubwa, zawadi ya ukombozi. Licha ya kuwa tulikua dhaifu, Kristo alituinua, Kristo ametupa thamani kubwa, ametusahilisha tena kuitwa watoto wa Mungu. Je tunatambua thamani hii ya kuwa wakristo? Tunathamini tunu kubwa ya imani, na zawadi ya ukombozi tulioyopewa bure kabisa ba Kristo? Mfuasi wa Kristo apaswa kutambua ya kuwa yeye ni wa thamani kubwa. Tumekombolewa sio kwa fedha wala dhahabu vyenye kuharibika bali kwa damu ya thamani kubwa ya Mwana Kondoo, Bwana wetu Yesu Kristo. Tunaishi katika jamii inayokumbana na changamoto kubwa sana ya kiimani. Tumezaliwa katika imani, tumebatizwa na kupokea Sakramenti nyingine mbalimbali lakini mara kadhaa tunayumbishwa kirahisi kabisa kiimani na kusahau thamani kubwa ya ukombozi tuliyoipata kutoka kwa Kristo Yesu. Leo tupo kanisa hili, kesho tumehamia lile, kesho kutwa tupo kwa mchungaji huyu, mwezi ujao tupo kwa yule. Je, ninatambua thamani ya imani yangu? Ninatambua nguvu ya sakramenti za kanisa, nguvu ya ibada ya misa takatifu, nguvu ya sala na takafakari binafsi katika maisha yangu? Mfuasi wa Kristo apaswa kutambua thamani ya ukombozi wake, inayotoa maana ya thamani yake mwenyewe. Mfuasi wa Kristo anapaswa kutambua thamani ya wengine pia na kuwalinda wale walio dhaifu kama alivyotuambia Nabii Isaya.

Kristo Yesu ni Nuru ya Walimwengu
Kristo Yesu ni Nuru ya Walimwengu

Fundisho la Pili: Kristo anatualika kuwa nuru na mwanga kwa wengine. Kristo ndiye nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu akija ulimwenguni (Yoh 1:10). Yeye ndiye nuru ya ulimwengu na yeye amfuataye hatakwenda gizani kamwe bali atakuwa na nuru ya uzima (Yoh 8:12). Kumbe, Mkristo haangazi kwa sababu ya ubora wake kama anavyotufundisha pia mtume Paulo katika somo la pili, bali anaangaza kwa sababu ya Kristo anaishi ndani yake. Ndugu mpendwa, kazi ya nuru na mwanga ni kufukuza giza, ni kuleta ufunuo. Mfuasi wa Kristo apaswa daima kuishi katika nuru hii ya Kristo kwa kuepuka dhambi na kutamani kila mara maisha ya neema. Ni kuishi kwa uadilifu hata katikati ya dhuluma na kusimama katiak kweli hiyo. Tunaishi katika ulimwengu ambao uongo unapiganiwa kwa gharama kubwa, na anayesema ukweli anapingwa kwa gharama yoyote. Kristo alisema ukweli na kwa sababu hiyo alihukumiwa na kuuwawa. Mitume na manabii hali kadhalika hawakuona haya kuwasha taa ya imani katikati ya giza, hata na hii iliwagharimu maisha yao. Mfuasi wa Kristo apaswa kuonesha njia pale palipo na mkanganyiko. Tunaalikwa kuwasadia watu katika kufanya maamuzi sahihi katika maisha wapo watu wanaopitia nyakati ngumu za kimaamuzi katika maisha, wanaohitaji msaada wa ushauri, nasaha na sala. Tuwasaidie wengine kuwa karibu zaidi na Mungu aliye asili ya mwanga na chemchemi ya uzima wetu. Taa huwekwa juu ya kinara, haifichwi, hivyo imani yetu yapaswa kuonekana, yapaswa kuonesha matokeo halisi ya nje na ya wazi. Ukristo wa siri na kujificha ficha kwa ajili ya kulinda maslahi na faida yetu wenyewe, huo sio ushuhuda wa mfuasi halisi wa Kristo.

Iweni chumvi ya dunia na nuru ya walimwengu: Ushuhuda
Iweni chumvi ya dunia na nuru ya walimwengu: Ushuhuda   (ANSA)

Fundisho la Tatu: Matokeo ya kuiishi imani yetu kiaminifu kama wafuasi kweli wa Kristo. Nabii Isaya anatupa matokeo ya mtu yule anayeishi kweli imani katika matendo. Taifa la Israeli walimlalamika Mungu kwamba, “Mbona tumefunga lakini huoni? Tumejitaabisha nafsi zetu lakini huangalii?  Heunda nasi tumekua mara kadhaa tukilaumu kwa nini Mungu hatujibu sala zetu, kwa nini Mungu haoni mfungo wangu? Tunasahau kutazama na kujichunguza kama kweli tunaomba vile ipasavyo na kuishi maisha yaendanayo kweli na imani yetu. Nabii anawakumbusha kuwa haitoshi tu kufunga, bali mfungo, ibada na sala za kweli zapaswa kugusa uhalisia wa maisha yetu ya nje. Na matokeo yake huonekana wazi. Ni yepi basi matokeo ya kuiishi imani yetu kiaminifu?   Ndugu mpendwa tokeo la kwanza la kuiishi imani yetu katika matendo yaani kuwa nuru ya ulimwengu na kuwa chumvi ya dunia Nabii anasema: “Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, ishara ya mabadiliko ya kweli na ya uhakika yaletwayo na Mungu, Mungu mwenywe atatugusa utu wetu wa ndani na kutubadilisha. Pili, afya yako itatokea mara ishara ya uponyaji wa kweli wa uhakika na wa haraka, wa kiroho, kimwili na kijamii Kutoka kwa Mungu. Tatu, utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde, ishara ya ulinzi imara na thabiti kutoka kwa Mungu, Mungu hawezi kukuacha popote, Mungu hatasahu sala na sadaka yako, hakuachi sehemu yoyote ya maisha yako bila uangalizi wake. Nne, utaita, Bwana ataitika, utalia naye atasema, mimi hapa, Bwana hatanyamaza, Bwana hatakaa kimya. Kumbe matokeo ya sala yetu inayoambatana na matendo ya haki, ibada mfungo na sadaka za kweli, huambatana nasi. Tusalipo na tuombapo, Bwana atatujibu, tumliliapo atasikia mara na kutujibu. Mwenyezi Mungu atusaidie ili kweli maisha yetu yawe chumvi yenye ladha katika ufuasi wetu, maisha yetu yawe nuru itakayowaangazia watu, wapate kuyaona matendo yetu mema na wamtukuze Baba yetu aliye Mbinguni. Hitimisho: Tuombe neema ya kuyaelewa, kuyashika na kuyaishi mafundisho ya Kristo ili Ufalme wake uendelee kukua na kuenea kati yetu.

Tafakari Dominika 5
07 Februari 2026, 09:57