Tafuta

TALITHA KUM TALITHA KUM 

Bukuru dhidi ya biashara haramu ya binadamu:Kutoka mwathirika hadi shuhuda!

Bukuru Claude,kutoka Burundi,alielezea Vatican News uzoefu wake wa kusafirishwa nje ya nchi na jinsi leo hii anavyoshirikiana na Talitha Kum kuongeza uelewa zaidi na kuzuia majanga mengine yanayohusiana na jambo baya la Biashara haramu ya Binadamu.

Na Moriba Camara, S.J.

Yote haya yalianza baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu nchini Burundi. Kama vijana wengi waliohitimu nchini mwake, Bukuru Claude alijikuta hana kazi, ingawa alitaka sana kuisaidia familia yake. "Nilikuwa nikikabiliwa na kuchanganyikiwa, shinikizo la kijamii, na hamu halali ya kusaidia familia yangu," aliambia Vatican News. Ilikuwa katika muktadha huu wa udhaifu ambapo alikaribiwa na waajiri wasio waaminifu. "Waliniahidi fursa za kazi nje ya nchi, katika nchi kama Kuwait, Lebanon, au Dubai, zenye mishahara ya kuvutia na maisha bora," alielezea.

Talitha Kum Youth Ambassador, Lone Botshelo, during an international gathering in Rome

Bukuru Claude

Bila kujua mifumo ya biashara haramu ya binadamu, aliwaamini: "Nililipa pesa nyingi na miaka mingi ya maisha yangu, nikifikiri nilikuwa nikiwekeza katika mustakabali wangu." Safari ambayo iligeuka kuwa mtego, kwani  Bukuru alitumwa Kenya na akaambiwa kwamba ilikuwa kituo rahisi kabla ya kufika nchi za Ghuba. "Tulipaswa kuelekea nchi za Ghuba. Lakini mara tu tulipofika huko, ukweli ulibadilika kikatili," alisema. "Kuanzia siku ya kwanza kabisa, mtu aliyetusafirisha alikusanya pasipoti na hati zetu. Alituacha katika nyumba, katika chumba ambacho tulikuwa ishirini na mmoja." Hali ya maisha ilikuwa hatarini. Kupata chakula cha kula ilikuwa ngumu sana. “Tulikula kutokana na msaada kutoka kwa familia zetu huko Burundi, mara moja kila baada ya siku tatu," Bukuru alikumbuka. Lakini wakati huo, Bukuru alikuwa bado hajatambua hali hiyo kama biashara haramu ya binadamu: "Wakati huo, sikujua kwamba nilikuwa mwathirika wa biashara haramu ya binadamu. Nilijua tu kwamba kuna kitu kibaya, lakini nilifikiri siku moja angetupeleka pale alipoahidi."

Talitha Kum Kenya

Kutoka  kwa Bukuru kwenye mtego wa wafanyabiashara haramu kulitokana na kukutana kwa njia ya Mungu." Mmoja wa wanafunzi wenzake wa zamani, ambaye alikuwa bruda nchini Kenya, alimsaidia kuelezea kwa maneno kile alichokuwa akipitia. "Aliniambia, ukubali au ukane, umesafirishwa kiharamu," Bukuru alisema. Kupitia mtandao huu wa urafiki na mshikamano, kesi hiyo iliripotiwa kwa Talitha Kum-Kenya. “Ni Talitha Kum-Kenya iliyotuokoa, kufuatia kuingilia kati kwa Mtawa mmoja aliyekuwa Algeria,” Bukuru aliendelea. Hatua hii iliashiria hatua muhimu ya mabadiliko: “Nilipokutana na Mtandao wa Talitha Kum, hatimaye nilielezea kile nilichokuwa nimepitia, biashara haramu ya binadamu.” Mtandao huo ukibadilisha mateso kuwa kujitolea  leo hii, Bukuru Claude anakuwa mhamaishashi  dhidi ya biashara haramu ya binadamu. “Kubadilisha mateso yangu kuwa kujitolea ni muhimu kwa sababu tatu,” alielezea.

Kwanza, “kutoa maana kwa kile nilichopitia, kwa kuongeza ufahamu na kusema ukweli.” Pili, kutokana na mshikamano na vijana ambao, kama alivyokuwa hapo awali, wanakabiliwa na ukosefu wa ajira na umaskini. “Vijana wengi leo wanaishi katika udhaifu uleule niliokuwa nao wakati huo,” alisisitiza. Mwishowe, alisisitiza hisia yake ya uwajibikaji wa kimaadili. “Baada ya kuona mifumo ya biashara haramu ya binadamu kwa karibu, sikuweza kukaa kimya, kwa sababu moyo wangu ulijawa na aina ya ushiriki wa hiari,” alisisitiza.Pamoja na vijana wengine, anafanya vitendo vya kuongeza ufahamu. "Tunazungumzia aina za sasa za biashara haramu ya binadamu na mikakati ya uajiri wa ulaghai. Tunahimiza uangalifu na kuripoti visa vya biashara haramu ya binadamu." Mipango ya uhamasishaji wa mipakani katika Afrika Mashariki pia unazingatiwa. "Hivi ndivyo nilivyojitolea kikamilifu kuwa kama balozi wa vijana kuongeza uelewa, kuzuia, na kutoa tahadhari," alisema.

Kwa kutambua ishara za onyo

Kwa kutumia uzoefu wake, alitambua ishara kadhaa za onyo ambazo zinapaswa kutoa tahadhari kuhusu biashara haramu ya binadamu: "Ya kwanza ni ahadi ambazo ni nzuri sana kuwa kweli: kazi yenye malipo mazuri, bila mkataba ulio wazi, bila sifa zinazohitajika, na kwa kuondoka haraka sana." Pia alibainisha "ukosefu wa uwazi kwa upande wa mwajiri, kutokuwepo kwa hati rasmi, na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu mwajiri, mahali halisi pa kazi, au hali halisi." Au pia "maombi ya malipo ya juu, ili kupata kazi au kusafiri." Ishara zingine za onyo zinaweza kuwa "unapoombwa kuweka mpango huo kuwa siri, hata kwa familia yako," au "kunyang'anywa hati za utambulisho na vikwazo vya harakati."

Ujumbe wa Matumaini

"Hamko peke yenu"kwa wale ambao bado wamenaswa, Bukuru alitoa ujumbe wa matumaini: "Ndugu na dada wapendwa, hamko peke yenu. Maisha yenu yana thamani kubwa, hata kama hali inaonekana kutokuwa na matumaini. Kuna watu na mashirika yaliyo tayari kuwasaidia. Kuthubutu kuzungumza kunaweza kuwa hatua ya kwanza kuelekea uhuru." Na kwa mamlaka, jamii, na vijana vile vile, hili ni jukumu la pamoja. Kwa pamoja, tunaweza kubadilisha mateso kuwa ulinzi na hofu kuwa matumaini," alihitimisha.”

Bukuru Claude

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here.

 

09 Februari 2026, 11:30