Askofu Hiiboro azindua Kituo kipya cha Uchungaji: “Kuwepo, hasa pale mateso yanapozidi”
Na Christine Masivo CPS- Vatican.
Jimbo Katoliki ya Tombura-Yambio huko Sudan Kusini limeashiria hatua muhimu katika kuimarisha utume wake wa kichungaji kwa kuzindua Kituo kipya cha Uchungaji kwa ajili ya Dekania ya Magharibi, kinachoongozwa na Askofu Eduardo Hiiboro Kussala. Hafla hiyo ilihudhuriwa na mapadre, watawa, makatekista na waamini wa jumuiya ya Kikristo ya eneo hilo, ambao walikaribisha Kituo hicho kama ishara ya matumaini na kujitolea upya kwa maisha ya Kanisa. Akizungumza katika uzinduzi huo, Askofu Hiiboro alitoa ujumbe wa dhati uliojikita katika huruma, ustahimilivu, na wito wa amani.
Kwa zaidi ya miaka mitano ni migogoro na mateso
Akitafakari miaka mingi ya migogoro na mateso yaliyovumiliwa na watu wa eneo hilo, alikiri maumivu yao huku akitoa heshima kwa nguvu, uvumilivu na ustahimilivu wao wa kiroho.“Kwa zaidi ya miaka mitano, mmeishi chini ya mzigo mzito wa vurugu, uhamisho, taasisi zilizoharibiwa, na kiwewe kikubwa. Na bado, hamjapoteza ubinadamu wenu,” Askofu alisema. "Nimeguswa sana na upendo, ukarimu, na furaha yenu hata katikati ya maumivu, ustahimilivu wenu umeniacha hoi." Alihimiza jamii kutambua na kulinda nguvu hii ya ndani, akiielezea kama zawadi kutoka kwa Mungu ambayo sasa lazima iwe msingi wa amani. "Amani haitakua kupitia hatia au kisasi," alisema. "Itakua kupitia lugha mpya ya msamaha, uvumilivu, upendo, umoja, upatanisho, na uponyaji."
Umuhimu wa kichungaji katika kituo kipya
Askofu alisisitiza umuhimu wa kichungaji wa Kituo kipya, akieleza " hii ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za kichungaji ndani ya kanisa." Viongozi wote wa kanisa walialikwa kufanya kazi kwa pamoja ili kituo hicho kiwe chombo cha lueneza injili, malezi, na uratibu wa vitendo vya kichungaji. Safari yake ya kuzindua mpango huo ni ziara yenye mahitaji lakini yenye maana kubwa katika Kanisa la Magharibi la Mama Yetu Malkia wa Sudan Kusini. "Baada ya karibu siku kumi za kujitolea kwa bidii kwa kichungaji, maombi, mikutano, dhabihu, na neema, tulirudi Yambio tukifuata njia hiyo hiyo," alisimulia. "Haikuwa safari ndefu tu, bali ni hija ya moyo, kupitia majeraha, imani, uvumilivu, na tumaini la watu wa Mungu."
Katika kila Parokia na Jumuiya Bwana alijifunua
Njiani, alisema, utume wa Kanisa ulithibitishwa kwa nguvu. "Katika kila Parokia na katika kila Jumuiya, Bwana alijifunua kupitia imani thabiti na kilio cha kimya kimya cha amani. Hizi zilikuwa nyakati zilizothibitisha utume wa Kanisa: kuwepo, haswa pale ambapo mateso ni makubwa zaidi." Licha ya barabara ngumu na changamoto nyingi zIlizowakumba, Askofu alisisitiza kwamba shida kama hizo ziliimarisha azimio la uchungaji bora. "Hakuna hata moja kati ya hizi lililotuvunja moyo; kinyume chake, liliimarisha imani yetu kwamba upendo wa kichungaji lazima udumu zaidi ya vikwazo na magumu," alisema.
Kituo kipya kinatarajiwa kuongeza shughuli za uotaji wa huduma kwa waamini wengi huko Tombura
Kituo cha Kichungaji kilichozinduliwa hivi karibuni kinatarajiwa kuongeza utawala wa kichungaji, na kuboresha utoaji wa huduma kwa waamini huko Tombura na parokia zinazozunguka. Askofu Hiiboro aliwahimiza mapadri, makatekista, na viongozi wa walei kutumia Kituo kikamilifu na kwa ufanisi, akibainisha jukumu lake muhimu katika kuboresha uratibu, mipango ya kichungaji, na programu za malezi katika kanisa lote. Kwa jumuiya ya wakristo wa eneo hilo, Kituo kinasimama kama ishara inayoonekana ya ukaribu na kujitolea kwa Kanisa mahali ambapo imani, upatanisho, na matumaini vinaweza kuendelea kukua katika nchi ambayo bado inatamani amani.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here