Tafuta

Papa Leo XIV: Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wajenge utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha katika vipaumbele na uhalisia wa maisha yao. Papa Leo XIV: Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wajenge utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha katika vipaumbele na uhalisia wa maisha yao.  (ANSA)

Tafakari Dominika ya Tatu ya Mwaka A Kanisa: Toba, Wongofu Na Umisionari

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi, Motu Proprio “Aperuit illis” yaanii: “Aliwafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” (Lk 24:45.” iliyochapishwa kunako tarehe 30 Septemba 2019 alianzisha Dominika ya Neno la Mungu na tarehe 25 Januari 2026 ni Dominika ya Saba ya Neno la Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yao! Liwe ni dira!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 3, mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ni adhimisho la 7 la dominika ya Neno la Mungu tangu ilivyotangazwa rasmi na Baba Mtakatifu Fransisko, 30 Septemba 2019 katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 1600 ya kifo cha Mtakatifu Yehonimo Jalimu wa maandiko Matakatifu, kwa barua yenye kichwa cha habari, “Aperuit illis”, “Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu” (Luka 24:45). Lengo kuu likiwa ni kuhuisha hamu ya kulisoma, kulitafakari, kuliishi na kulifanya Neno la Mungu kuwa taa ya maisha yetu. Mwaka huu baada ya maadhimisho ya Jubilei miaka 2025 ya Ukristo, Mahujaji wa Matumaini. Hati ya Kusikiliza kwa Uchaji Ufunuo wa Neno la Mungu “Dei verbum” inagusia kwa undani kuhusu: Ufunuo wenyewe; Urithishaji wa Ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na Ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale, Agano Jipya; pamoja na Maandiko Matakatifu Katika Maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Ufunuo wa Baba wa milele, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na kujikita katika maisha ya sala! Ni katika kulisoma Neno la Mungu tunapata nafasi ya kuongea na Mungu anayejifunua kwetu kwa Njia ya Mwanae Yesu Kristo. Ujumbe mkuu wa masomo ya dominika hii ni toba, wongofu, na umisionari katika kumfuata Kristo Yesu, Nuru ya kweli ili kuishi kitakatifu na kuingia katika ufalme wake mbinguni. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, mwimbieni Bwana, nchi yote. Heshima na adhama ziko mbele zake, nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake” (Zab. 96:1, 6). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya Mwanzo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, uyaongoze matendo yetu yafuate mapenzi yako, ili kwa Jina la Mwanao mpenzi, tustahili kutenda mema mengi."

Neno la Mungu ni dira na taa ya maisha na utume wa Kanisa
Neno la Mungu ni dira na taa ya maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Isa 9:1-4). Ni utabiri wenye ujumbe wa matumaini kwa Waisareli wakiwa utumwani, hali iliyowafanya watembee katika giza la mauti, ishara ya ukandamizwaji na mateso. Hali hii ilitokea kipindi ambapo makabila ya Zabuloni na Naftali yaliyokaa upande wa Kaskazini mwa Galilaya yalipovamiwa na Waashuru (Waassyria), miji yao ikaharibiwa, watu wake wakachukuliwa mateka na kufanywa watumwa. Katika hali hii watu walikosa imani kwa Mungu, wakifikiri amewaacha kabisa, na hawakuwa na matumaini tena ya kutoka utumwani. Nabii Isaya anawapa ujumbe wa matumaini kuwa Nuru inakuja ikiangaza toka mbali, nayo italishinda giza. Nuru hii inaashiria kuisha kwa utumwa kwa kuvunjwa kwa nira, kuondolewa kwa gongo lake na fimbo ya maadui zao, ishara ya namna walivyochukuliwa wakiwa wamefungwa, huku wakipigwa kwa fimbo, mateso haya sasa yanaenda kuisha. Hali hii inawafanya watu wajae furaha ya pekee mioyoni mwao, furaha kama ya watu wanaobeba mavuno kutoka mashambani, na furaha ya watu wanaogawana nyara baada ya kushinda vita. Nuru hiyo ni ishara ya mwisho wa utumwa, ni mwanzo wa ukombozi kwa kuja kwake Bwana mfalme wa amani. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu. Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu. Nimhofu nani? Neno moja nimelitaka kwa Bwana, nalo ndilo nitakalolitafuta, nikae nyumbani mwa Bwana, siku zote za maisha yangu. Niutazame uzuri wa Bwana, na kutafakari hekaluni mwake. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana, katika nchi ya walio hai. Umngoje Bwana, uwe hodari, upige moyo konde, naam, umngoje Bwana” (Zab. 26:2). Kama ilivyokuwa kwa Waisraeli ndivyo inavyokuwa hata kwetu. Shida na mahangaiko katika maisha; umaskini, magonjwa, njaa, chuki na vita, yanaweza kutukatisha tamaa na kuona kama vile tuko kwenye giza nene, hivyo kuwa na mashaka juu ya uwepo wa Mungu. Hali hii inatokea pale tunapotenda dhambi na kujitenga na Mungu. Lakini Mungu daima yuko nasi. Hivyo tuwe na matumaini na kujikabidhi kwake na kutokuwa na hofu, naye atatuokoa.

Waamini wajenge utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno!
Waamini wajenge utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno!   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 1: 10-13, 17). Ni maonyo na mashauri ya mtume Paulo kwa wakorinto waliokuwa wametengana. Kulitokea mgawanyiko na kukawa na makundi katika jumuiya hiyo ambapo wapo waliojiita wao ni wa Paulo, wengine wa Apollo, wengine wa Kefa na wengine wa Kristo. Kila kundi lilikuwa na msimamo na itikadi zake. Kundi la Kefa/Petro lilishikilia mapokeo ya kiyahudi na sheria za Musa kama vile kutahiriwa, kundi la Paulo liliona sio lazima kuzishika sheria hizo, imani itokanayo na neema ya Kristo  inatosha kwa wokovu, na kundi la Apollo, mzaliwa wa Iskanderia, Mwanafalsafa, na mtu hodari katika Maandiko Matakatifu, liliifanya imani kuwa ya kifalsafa zaidi (Mdo 18:24). Na kundi la waliojiita wakristo wao waliona kwamba kule kuwa wa Paulo, au wa Apollo, au wa Kefa, haidhuru, cha maana ni kumfuata Kristo. Makundi haya yalisababisha giza nene la ubaguzi na utengano katika Jumuia ya Korinto. Mtume Paulo anawakumbusha kuwa mambo haya ni ya aibu hayapaswi kuwepo katika jumuiya ya kikristo. Ujumbe huu ni wetu pia, kuwa Imani kwa Kristo ni moja. Kristo aliyekufa kwa ajili yetu msalabani ni mmoja, hajagawanyika na hawezi kugawanyika. Hatupaswi kuchukiana wala kubaguana kwa ajili ya Kristo, bali kuwa wamoja na kunuia mamoja. Chuki ni mwiko. Tusijigawe kwa itikadi tulizonazo, au kushikamana na Padri huyu au Askofu fulani. Tukumbuke kuwa ubaguzi ni moja ya matendo ya giza, ukisindikizwa na wivu, fitina na uongo. Anayepanda mbegu ya mambo haya, Mungu hayumo ndani mwake.

Tarehe 25 Januari Ni Sikukuu ya Kuongoka kwa Mt. Paulo.
Tarehe 25 Januari Ni Sikukuu ya Kuongoka kwa Mt. Paulo.   (@VATICAN MEDIA)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 4:12-23). Ni simulizi la Yesu kuanza rasmi utume wa kutangaza habari njema ya wokovu na kuwaita mitume wake wa mwanzo – Simoni Petro, Andrea, Yakobo na Yohane – wavuvi wa samaki ili wawe wavuvi wa watu. Hii ni mara baada ya kusikia kuwa Yohane Mbatizaji amefungwa gerezani. Kuhubiri kwake kunaanzia katika mkoa wa Galilaya, Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali. Hii inafanya kutimia kwa utabiri wa nabii Isaya ya miji hii kuona Mwanga mkuu (Isa 9:1-2). Na ujumbe wake ni huu; “Tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Kihistoria, Zabuloni na Neftali ni makabila mawili ya waisraeli yaliyoishi Kapernaumu, mji uliopo kandokando ya ziwa la Galilaya, katika mkoa wa Galilaya uliokaliwa na watu mchanganyiko, wayahudi na watu wa mataifa mengine, ndiyo maana inaitwa pia Galilaya ya mataifa. Sababu ya mchanganyiko huo ni wayahudi kuchukuliwa mateka na kupelekwa utumwani na watu wa mataifa mengine kuletwa kukaa humo, na uwepo wa Askari wa kirumi. Lakini pia huu ulikuwa ni mji wa kibiashara wenye wasomi wengi, na upinzani mkubwa kwa ukoloni wa kirumi ulitokea huko.

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo linahitimishwa tarehe 25 Januari 2026
Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo linahitimishwa tarehe 25 Januari 2026   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hii iliifanya Galilaya kudharauliwa na Mafarisayo na waandishi na jina lake kutumika kama tusi. Nikodemo aliambiwa hivi na Mafarisayo; “Tafuta ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokei Nabii?” (Yn. 7:52). Mungu daima anachagua kilicho dhaifu, kinachozarauliwa na mwanadamu, ili kukiinua na kuonyesha ukuu wake. Hali hii iliwafanya watu wake waonekane kama wanaokaa katika giza nene la dhambi kwa misha yao kugubikwa na starehe na anasa, matajiri waliwanyonya maskini, hivyo walionekana kuwa kama vipofu kwa kutokuona kukosekana kwa haki kuwa ni jambo baya. Ndiyo maana ujumbe wa Yesu unasema; “Tubuni; kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia”. Nasi tunaitwa kufanya toba na kupokea sakramenti ya kitubio kila mara ili tuendelee kuujenga ufalme wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku, ufalme unaojikita katika utamaduni wa haki, usawa, ukarimu, upole, unyenyekevu na uadilifu katika kila nyaja ya maisha. Ni katika kuishi hivyo maisha ya hapa duniani, tutastahilishwa kuingia katika maisha ya uzima wa milele mbinguni. Ni katika muktadha huu mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, upende kuzipokea kwa wema dhabihu zetu. Tunakuomba uzitakase kwa ajili yetu, uzifanye zituletee wokovu”. Na katika sala baada ya komunyo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, sisi tuliopokea neema iletayo uzima wako, tunakuomba utujalie tuone daima fahari juu ya fadhili yako”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Neno la Mungu
22 Januari 2026, 16:59