Tafakari Dominika ya Pili ya Mwaka A wa Kanisa: Mwanakondoo wa Mungu na Nuru ya Mataifa
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya Pili ya Mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Mama Kanisa anaanza Maadhimisho ya Juma la 60 la Kuombea Umoja wa Wakristo yaani kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2026 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujitambulisha kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Ujumbe mkuu katika maadhimisho ya Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni huu; Yesu Kristo, ni Mwana wa Mungu, Mtumishi wake mwaminifu, Mwanakondoo aondoaye dhambi ya ulimwengu, na kuujaza ulimwengu kwa Nuru ya utukufu wake, ili uweza kuwa na Amani tele. Ndiyo maana Zaburi ya wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii inasema; “Ee Mungu, nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia Jina lako, wewe Mtukufu” (Zab. 66:4). Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ndiwe unayeongoza mambo yote mbinguni na duniani. Usikilize kwa wema dua zetu sisi taifa lako, utujalie amani yako maishani mwetu.” Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 49:3, 5-6). Ni sehemu ya utenzi wa pili wa Mtumishi wa Mungu, nao unatueleza kuwa Mtumishi huyu: Atamtukuza Mungu kwa Maisha na kazi zake. Kazi yake ni kutangaza ukombozi kwa dunia nzima, kwa wayahudi na na watu wasio wayahudi. Yeye atawapatanisha watu na Mungu. Kupitia Yeye, Waisraeli pamoja na ulimwengu wote wataonja huruma na upendo wa Mungu. Naye Mungu atamuenzi kuliko viumbe vyote kwa utukufu usiolezeka. Lakini Nabii Isaya anamzungumzia nani anapomtaja Mtumishi wa Mungu?
Mapokeo na mafundisho ya Mababa wa Kanisa yameona na kutambua kuwa Mtumishi huyu si mwingine bali ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye Katekisimu yetu ya Kanisa Katoliki inamuelezea kuwa ndiye Mtumishi wa wote (KKK 786), Nuru ya ulimwengu, Mwanga halisi, na Wokovu wa Mataifa yote, anayewakomboa wote kwa mateso makali (KKK 440, 601), naye alikuwa mtiifu kwa Mungu Baba (KKK 539, 615), katika kuyatimiza mapenzi yake.Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Ndipo niliposema; Tazama nimekuja, kuyafanya mapenzi yako (K). Nalimngoja Bwana kwa saburi, akaniinamia, akakisikia kilio changu, akatia wimbo mpya kinywani mwangu, ndizo sifa zake Mungu wetu. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, masikio yangu umeyazibua. Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka. Ndipo niliposema, tazama nimekuja. Katika gombo la chuo nimeandikiwa, kuyafanya mapenzi yako. Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. Nimehubiri habari za haki, katika kusanyiko kubwa, sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua (Zab. 1, 3, 6-9, (k) 7,8). Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Kwanza Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 1:1-3). Katika somo hili, Mtume Paulo anatoa ushuhuda wa yeye kuitwa kuwa mtume wa Mungu na anawaita wakorintho watakatifu kwa sababu Mungu aliwaweka wakfu kwa njia ya Ubatizo. Kisha kuwatakia neema na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo zikae nao daima, anawaonya wasiuchafue utakatifu huo kwa kujichanganya na malimwengu, bali waepukane na dhambi, ili wawe na uhuru wa kweli. Haya ni mausia kwa wakristo wa nyakati zote katika kuishi kitakatifu maisha ya hapa duniani, ili kuufikia utimilifu wake mbinguni.
Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 1:29-34). Licha ya kuwa katika mzunguko wa mwaka A wa kiliturujia kipindi cha kawaida, tunatafakari Injili ya Mathayo, dominika hii ya pili tunasoma sehemu hii ya Injili ya Yohane inayosimulia Yohane Mbatizaji akishuhudia kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, alikuwapo tangu milele yote; ni Nuru halisi aliyetumwa na Mungu Baba kuja kututoa katika giza la dhambi na mauti; ni Mwana Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu, kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Yohane Mbatizaji ameyafahamu haya si kwa uwezo wake, bali kwa ufunuo wa Roho Mtakatifu (rej. KKK 719). Nasi tukimruhusu Roho Mtakatifu atuongoze, hakika tutayatambua makuu ya Mungu katika maisha yetu. Yohane Mbatizaji alipomwona Yesu, alisema; “Tazama Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu”. Maneno haya yanaashiria kuwa sadaka za kuteketezwa kwa wanakondoo katika kipindi chote cha Agano la kale tangu enzi za Abel, utimilifu wake ni katika Kristo Yesu, kama anavyosali Mama Kanisa katika sala ya Ekaristi ya kwanza; “Ewe Mwenyezi, kati ya zawadi ulizotujalia, tunakutolea sadaka safi na takatifu, yaani mkate mtakatifu wa uzima wa milele na kikombe cha wokovu wa milele. Uwe radhi kuitazama sadaka hii kwa uso wa rehema, uipokee kama ulivyokubali kupokea sadaka ya Abel mtumishi wako mwaminifu, na sadaka ya babu yetu Ibrahimu, na ile sadaka takatifu isiyo na doa aliyokutolea Melkisedek, kuhani wako mkuu.”
Ibrahamu alipewa mwanakondoo amtoe sadaka badala ya mwanaye Isaka (KKK 2572), na tangu enzi za Musa, kila asubuhi na mchana mwanakondoo alitolewa sadaka mbele ya sanduku la Agano na baadae katika Hekalu la Yerusalemu kwa ajili ya dhambi za wana wa Israeli (rej. Kut 29:38-42). Tena, katika kila sherehe ya Pasaka, mwanakondoo alichinjwa katika kila familia ya Myahudi, na nyama yake kuliwa wakati wa mlo wa Pasaka, ili kuwakumbusha kwamba waliwekwa huru kutoka utumwa wa Wamisri kwa njia ya damu ya wanakondoo hao (rej. Kut 12: 1-14). Lakini damu ya wanakondoo hao haikuwa na uwezo wa kuondoa dhambi, bali ishara yao ya toba, ambapo kwayo Mungu alitoa msamaha kwao. Hata hiyo damu za wanakondoo hao ilikuwa ni ishara ya utabiri wa kile ambacho Kristo Yesu angekuja kukifanya. Ndiyo maana alitolea maisha yake kuwa Sadaka siku ya Pasaka ya Kiyahudi, muda na saa ile ambapo Makuhani walikuwa wanatolea wanakondoo kama dhabihu hekaluni. Kristo Yesu ndiye Altare, Kuhani na Mwanakondoo aliyejitoa Sadaka kamili na takatifu Msalabani. Katekisimu yetu ya Kanisa Katoliki inafundisha kuwa nyakati zetu Kanisa linapoadhimisha Ekaristi Takatifu sio tu hufanya ukumbusho wa Pasaka ya Kristo Yesu, bali katika adhimisho hilo huwapo juu ya altare sadaka halisi ya Kristo aliyotolea mara moja tu Msalabani na kazi ya ukombozi hufanyika (KKK 1364), kwa sisi kupata msamaha wa dhambi kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu iliyomwagika msalabani. Katika hili Mtume Petro anasema; sisi tumekombolewa “si kwa vitu vinavyoharibika kama vile dhahabu na fedha, bali kwa damu ya thamani kubwa ya Mwanakondoo asiye na hila wala waa, yaani Yesu Kristo” (1Pet 1:18-19). Hivyo, Kristo Yesu ni Mwanakondoo halisi aondoaye dhambi za ulimwengu (rej. KKK 523, 536, 602, 608, 613).
Hii ndiyo kweli ya imani yetu, nasi tunao wajibu wa kuifundisha, kuisimamia na kuiishi kitakatifu ili tuweze kuwa nasi mwanga wa Mataifa. Yesu anasema; “watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango ili iwaangazie wote waliomo ndani” (Mt 5:15). Kwa ubatizo tumewekwa juu ya kiango, tubaki juu, tusishuke chini, hata watu wakituambia tushuke tusishuke, kwani tukishuka tutakuwa tumeikataa Nuru na kupenda giza na hivyo kuwa waovu kwa maana; “Kila atendaye maovu huogopa mwanga, ili matendo yake maovu yasije yakaonekana wazi” (Yn 3:19). Basi tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atuangaze, atuongoze katika imani sahihi, matumaini thabiti, mapendo kamili, busara na ufahamu, ili tuishi kitakatifu kwa wokovu wa milele. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika Sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana, tunakuomba utujalie kuadhimisha vema mafumbo haya, kwa maana kila tunapoadhimisha ukumbusho wa sadaka hii, kazi ya ukombozi wetu inatendeka”. Na katika sala baada ya Komunyo anapohitimisha maadhimisho haya anasali; “Ee Bwana, sisi uliotushibisha mkate mmoja wa mbinguni, utujaze Roho wa upendo wako, utufanye tuungane katika ibada moj.a” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!