Tafakari Dominika ya Pili Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Kuombea Umoja wa Wakristo 2026
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu, kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya Pili ya Mwaka A wa Kanisa. Mama Kanisa anaanza Maadhimisho ya Juma la 60 la Kuombea Umoja wa Wakristo yaani kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2026 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujitambulisha kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Tupo tena mbele ya Mungu, tunataka kumwona Yesu na kukesha naye kidogo, tumuambie yetu na tuyasikilize yake, ili baadaye tusiseme yake na kutenda yetu bali tuseme yake na kutenda yake kwa kuuishi ushuhuda kamili. Tunapoendelea na safari ya mwanzo wa mwaka 2026, Kanisa linatupatia masomo yanayotuweka uso kwa uso na utambulisho wa Yesu na utume wetu kama wafuasi Wake. Tumetoka katika nuru ya Epifania—mwanga wa mataifa—na leo masomo yamemiminika moja kwa moja katika swali moja muhimu: swali muhimu kwa kila mmoja wetu “Yesu ni nani kwetu? Na sisi tunapaswa kuwa nani kwa dunia? Injili ya leo inatoa jibu la kwanza: “Huyu ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya dunia.” Somo la kwanza linatoa jibu la pili: “Nimekufanya kuwa Mwanga wa Mataifa.” Na somo la pili linatupatia nguvu ya jibu la tatu: “Amani na neema ya Mungu iwe kwenu.” Hapa ndipo tunaanza mwaka—katika mwanga wa Yesu, walioitwa kuwa watakatifu na waletaji wa amani.
Mungu anazungumza na Mtumishi Wake: “Nimekuitia kuwa mwanga wa mataifa, upate kufikisha wokovu wangu hata mwisho wa dunia.” Huu ni mwito wa kimaana sana: Yesu ndiye mwanga wa wote Si wa Wayahudi tu, si wa Afrika tu, si wa Wakristo tu—bali mwanga wa kila mtu mwenye kiu ya ukweli, haki na amani. (2) Lakini sisi pia tunashiriki mwito huo. Mungu hakusema: “Nitakufanya kuwa taa ya familia yako tu bali: “Mwanga wa Mataifa.” Hii ina maana: tunaitwa kuangazia giza la dhuluma, kuangazia familia zetu zinapogawanyika, kuangazia upendo pale palipo na chuki, kuangazia matumaini kwa vijana waliokata tamaa, kuangazia imani kwa dunia inayopoteza mwelekeo. Mwanga haupiganwi na giza—huingia tu na giza hutoweka. Mtakataifu Paulo katika Somo la Pili (1Kor 1:1-3) anakiri aliitwa kuwa Mtume kwa mapenzi ya Mungu, nasi tupo hapa duniani kwa mapenzi ya Mungu. Kusudi tufaulu kutimiza malengo ya Mungu katika kutuumba sharti tusikilize mafundisho yake kupitia Mwana wake Yesu Kristo na kumakinika katika ushuhuda kamili. Paulo anawaandika Wakoritho, jiji lililokuwa na: ghasia za kijamii, migawanyiko ya kidini, tabia za kupotea kimaadili, watu waliokata tamaa na kufuata falsafa za dunia. Lakini anaanza hivi: “Neema na AMANI iwe kwenu. “Mmeitwa kuwa watakatifu.” Amani na utakatifu ndiyo msingi wa ujumbe wa leo. Utakatifu haumaanishi kutembea na taji ya malaika. Unamaanisha: kuwa mtu wa kusamehe, kuepuka rushwa na udanganyifu, kuishi ukweli katika biashara na familia, kuwa mtu wa heshima na utu, kuwa chombo cha Mungu mahali ulipo. Amani haianza kwa mikataba ya kimataifa—inaanza ndani ya moyo wako na kwa watu wanaokuzunguka. Leo Mungu anatupa barua hii mpya ya mwaka: “Neema na Amani iwe kwenu.”
Somo la Injili (Yn 1:29-34) linamuelezea Yohane Mbatizaji akimshuhudia Kristo kama “Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya Ulimwengu.” Kwa nini Yohane Mbatizaji anamuona Yesu kama mwanakondoo? Yohana Mbatizaji anamwona Yesu na kutangaza: “Tazama Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya dunia!” Kuna ujumbe mkubwa hapa: Yesu ndiye anayebeba mzigo wetu wote Katika ulimwengu unaobeba: maumivu ya vita, mzigo wa dhambi, uzito wa uchungu wa maisha, giza la hofu, Yesu haji kutuhukumu, bali kuvibeba na kutuvua minyororo. PiliYesu ndiye MPATANISHI wetu, Kama Mwana-Kondoo wa Pasaka, Yeye hutoa maisha yake ili dunia ipone, familia zipone, mataifa yapate amani, watu warudiane. Tatu Yohane anatupa kielelezo cha ushuhuda, Anasema: “Mimi nimeona, nami nimetoa ushuhuda.” Sisi pia tunaitwa “kutoa ushuhuda” wa imani yetu: si kwa maneno makubwa—bali kwa tabia, heshima, utulivu, msamaha, na unyoofu.- Yohane alikuwa mtoto wa kuhani Zakaria hivi alijua sadaka ya asubuhi na ya jioni, sadaka hizo za wanyama zilimpendeza Mungu na kuwastahilisha Israeli msamaha lakini hazikutosha kuwa fidia halisi ndio maana zilirudiwarudiwa, ndipo basi huyu Yesu kama Mwanakondoo halisi anazichukua dhambi zetu katika mwili wake kwa kifo chake msalabani kama fidia ya wengi mara moja tu na kwa milele.
“Tazama mwanakondoo…’ ni muhtasari wa yote ambayo Yesu atafanya duniani. Usiku ule mtukufu Israeli alipotoka utumwani walichinja kondoo na kupaka damu yake milangoni wakasalimika kifo. Yesu kama Mwanakondoo anatuokoa na kifo kwa damu yake inayopakwa si milangoni tena ila katika midomo, roho na mioyo ya waamini. Kulikuwa na siku ya toba na upatanisho kitaifa… Yom Kippur.. ambapo mwanakondoo mmoja alichinjwa sadaka na damu yake kunyunyiziwa madhabahu na watu na mwanakondoo mwingine alibebeshwa dhambi za taifa kwa sala na toba kisha kufukuziwa porini alikoaminika kuliwa na mungu aitwaye Azazel. Yesu anazichukua dhambi zetu, anaubeba udhaifu wetu, ni Mwanakondoo wa sadaka. Dunia ya leo inalia kwa sauti za giza: mataifa yanayoendelea kupigana, wakimbizi wanaokimbia kwa hofu, ongezeko la chuki mitandaoni, vijana wanaopotoka kwa kukosa dira, kupanda kwa gharama za maisha, wanawake na watoto wanaoonewa, watu wanaokata tamaa kimoyo. Katika giza hili la dunia, Neno la leo linakuja kama umeme wa matumaini: “Tazama Mwana-Kondoo wa Mungu.” “Nimekufanya kuwa mwanga wa mataifa.” Hapa ndipo ujumbe wa leo una nguvu: Tumeitwa kuleta amani ambapo hakuna amani, kuleta haki ambapo hakuna haki, na kuleta matumaini pale palipo na machozi.
Kwa ubatizo tunaitwa kutoa ushuhuda na kumkiri Kristo kama Yohane mwana wa Elizabeti, tukimpeleka kwa watu ili nao wapate kufaidi matunda ya Ukristo. Lakini bila bahati hatujafaulu bado, kadiri tunavyoagizwa na neno la Mungu hii leo, badala ya kuwa nuru ya mataifa tumekaa kwenye ‘main switch’ tukizima mwanga na kukumbatia giza, watazamaji tu wa mambo yanavyokwenda… tutoke nje na kumshuhudia Kristo kwa watu wote, hasa waliokata tamaa, wasiothaminika, wasioheshimika, wasiotazamika labda kwa sababu ya uchafu wao, harufu yao mbaya, kukosa kwao ajira, uyatima wao, uathirika wao, umasikini wao, kukosa kwao elimu. Ni kwa watu hawa tunatumwa kuwa MASHUHUDA, kuwapelekea mwanga wa Injili na kuwaonyesha “Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu…” Hii si kazi ya Paroko pekee na watawa, Halmashauri ya Walei au Serikali, mashirika na watu tajiri, ni jukumu letu sote. Tupo tunaoona Kanisa lina sehemu 2, wapo wenye Kanisa ndio maaskofu, mapadre, mashemasi, waseminari, watawa, makatekista na wasaidizi wao... halafu wapo waamini “wasio na wito wowote”, wanadaiwa kidogo sana, inawatosha kwenda Kanisani Dominika, kusikiliza neno la Mungu, kupokea sakramenti, maagizo na halafu kutii na kutekeleza. Huu ni uelewa duni wa Kanisa. Nabii Isaya amesema leo kila mmoja anao wito wa kuwa mtumishi wa Mungu na mwanga wa mataifa yote… wito halisi ni mmoja tu wa ‘kuwa watakatifu’ kwa njia ya Daraja takatifu, Nadhiri za kitawa au Ndoa takatifu hivi kila mmoja anahusika 100%... Je, mimi na wewe tu nuru ya mataifa? tujihadhari tusiwe sababu ya kurudi nyuma Injili.
USHUHUDA wetu uonekane pia katika maisha ya jumuiya, tupo tunaoona JNNK hazina uzito, tunamwona Padre wetu ndio kila kitu na kudharau Jumuiya, Kanisa linaanza kwenye familia na kuenea kwenye JNNK hivi Mkatoliki usiyeshiriki vizuri JNNK haufanyi sawa. Tunaingia mwaka 2026 na changamoto zake, lakini masomo yanatupa viungo vitatu vya kuishi mwaka mpya: Utambulisho: Sisi ni watumishi wa Mungu, tulioitwa kung’aa., Mwongozo, Tunamwangalia Yesu, Mwana-Kondoo wa Mungu. Nguvu Tunaishi katika neema na amani yake. Kila mmoja wetu ana nafasi yake: mzazi kuwa mwanga kwa familia, kijana kuwa mwanga shuleni au kazini, mfanyabiashara kuwa mwanga kwa uaminifu, viongozi kuwa mwanga kwa haki, wanajamii kuwa mwanga kwa udugu. Tunaposisitiziwa leo kuwa MASHUHUDA wa Kristo kama Yohane Mbatizaji na nuru ya mataifa tunapewa angalizo la uwepo pia wa mashuhuda wa uongo, kazi yetu iwe pia kuchambua/pembua kwa makini ujumbe tunaoletewa ili kuzitambua roho, nyingine si za Mungu... Sisi pia tusitoe ushuhuda ongo juu ya wenzetu kwa sababu yoyote ile... katika yote upendo utawale, huo unatosha na kuzidi! Masomo ya leo yanatukabidhi ujumbe wa mwaka mzima: Tazama Mwana-Kondoo wa Mungu. Mruhusu akuondolee mzigo. Kisha nenda ukawa mwanga kwa mataifa— mwanga wa amani, mwanga wa haki, mwanga wa upendo, mwanga wa matumaini. Kristo ni mwanga wetu—na sisi tunaitwa kuuangaza mwanga huo duniani. Amina.