Tafuta

Mlimani ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake! Mlimani ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake!  (ANSA)

Tafakari Dominika 4 Mwaka A wa Kanisa: Sifa za Heri za Mlimani!

Sifa za heri zinawafundisha waamini lengo la mwisho: Ufalme, kumwona Mungu jinsi alivyo, kushiriki hali hali ya umungu, maisha na uzima wa milele; kufanya waana; pumziko katika Mungu. Heri ya uzima wa milele ni paji la Mungu tu; ni paji la kimungu kama ilivyo neema inayowaelekeza huko. Sifa za heri zinawaweka mbele ya uchaguzi mkataa kuhusu mambo ya duniani: Zatakasa nyoyo za waamini na hivyo kuwawezesha kumpenda Mwenyezi Mungu kupita vitu vyote.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 4 ya Mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu inatualika, “Kuukumbatia Umaskini wa Roho” Kila mwanadamu katika maisha yake ya kila siku hapa duniani anatafuta kuwa na furaha na heri katika maisha. Heri za Mlimani ni: Katiba, Mwongozo, dira ya maisha na muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu na ni lengo la kila mwamini. Heri hizi ni kiini cha mahubiri ya Kristo Yesu, muhtasari wa ahadi za Mungu kwa Taifa Teule kuanzia Ibrahimu, nazo zatimiliza ahadi hizo si kwa kuzipanga tena kwa ajili ya kupata nchi, bali kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Heri hizi zachora uso wa Yesu Kristo na kufafanua mapendo yake, zaonesha wito wa mwamini anayeshiriki: Utukufu wa Mateso na Ufufuko wake, zinaangaza matendo na hali zilizo za maisha ya kikristo, zinatoa ahadi za matumaini katika taabu, zikitangaza baraka na tuzo ya wokovu, yaani, maisha ya uzima wa milele mbinguni (Rej. KKK 1716-1717). Kimsingi sifa za Heri huzijumlisha na kuzikamilisha ahadi za Mwenyezi Mungu tangu Ibrahimu kwa kuzielekeza kwenye ufalme wa Mungu tangu Mzee Ibrahimu, Baba yetu wa imani kwa kuzielekeza kwenye Ufalme wa mbinguni. Nazo zajibu hamu ya furaha ambayo Mungu ametia katika moyo wa mwanadamu. Sifa za heri zinawafundisha waamini lengo la mwisho ambalo Mwenyezi anawaitia waja wake: Ufalme, kumwona Mungu jinsi alivyo, kushiriki hali hali ya umungu, maisha na uzima wa milele; kufanya waana; pumziko katika Mungu. Heri ya uzima wa milele ni paji la Mungu tu; ni paji la kimungu kama ilivyo neema inayowaelekeza huko. Sifa za heri zinawaweka mbele ya uchaguzi mkataa kuhusu mambo ya duniani: Zatakasa nyoyo za waamini na hivyo kuwawezesha kumpenda Mwenyezi Mungu kupita vitu vyote. Heri za mbinguni huweka vigezo vya utambuzi katika kutumia mambo ya dunia kulingana sheria ya Mwenyezi Mungu. Rej KKK 1725-1739.

Heri za Mlimani ni Muhtasari wa Injili, Dira na Mwongozo wa maisha
Heri za Mlimani ni Muhtasari wa Injili, Dira na Mwongozo wa maisha   (ANSA)

Ndiyo sababu tunapambana kila siku, kufanya kazi kwa bidii na kwa nidhamu kubwa, ili kuweza kufanikisha ndoto ya kupata furaha katika maisha yetu. Dominika ya leo inatupa mtazamo tofauti kabisa wa maisha yetu sisi kama wafuasi wa Kristo. Kristo Yesu anatualika kuukumbatia umaskini wa roho iwapo tunataka kuitafuta na kuipata furaha ya kweli. Kuwa maskini wa roho ni kutambua ya kuwa, hakuna furaha ipatikanayo nje ya Mungu. Ni kutambua kuwa kila tulicho nacho katika maisha yetu kinatoka kwa Mungu na kwamba pasipo yeye hatuwezi jambo lolote. Ni kukiri udogo, unyonge na udhaifu wetu mbele za Mungu na kutegemea daima huruma na msaada wake. Ni kuishi maisha ya utauwa, kuwa wanyenyekevu, kuwajali na kuwasaidia wanyonge, maskini na wanaoonewa, kuvumilia katika mateso, na kuwa wajumbe wa haki na amani hapa duniani. Hizi ndizo heri, hii ndio katiba na mwongozo wa maisha yetu hapa duniani, itakayotupelekea kuipata furaha ya kweli kwa kuungana na na kumwona Mungu uso kwa uso katika uzima wa milele.

Sira za Heri za Mlimani ni dira na mwongoz wa maisha
Sira za Heri za Mlimani ni dira na mwongoz wa maisha

Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Sefania 2:3; 3:12-13. Ili kuelewa ujumbe wa somo hili unavyohusiana na Dominika hii ya nne ya mwaka tunapaswa kuelewa mambo kadhaa. Nabii Sefania alifanya kazi yake ya unabii wakati gani? Je ni mazingira gani yalikuwepo katika jamii wakati huu wa Nabii Sefania? Nabii Sefania alitumwa na Mungu kufanya kazi ya unabii katika taifa la Yuda kati ya miaka 640-622 BC kabla ya taifa hilo kupelekwa utumwani Babiloni. Ilikuwa ni katika utawala wa Mfalme Yosia, aliyetawala baada ya utawala mrefu wa Babu yake Manase na utawala mfupi wa Baba yake Amoni. Katika kipindi hiki, taifa la Yuda lilishuhudia kiwango kikubwa sana cha mmomonyoko wa maadili ya kidini na kijamii (Religious and moral decadency). Kidini, Watu walimwacha Mungu wa kweli na kuabudu miungu ya wapagani (religious syncrentism), Baali, Ashera na miungu mingine ya wakanaani, hata kufikia hatua ya kuweka miungu hiyo katika hekalu la Yerusalemu (2 Kings 21:1-9). Kijamii kulikua na rushwa na unyanyasaji mkubwa wa maskini na wanyonge. Viongozi walitumia vibaya madaraka yao, hawakuwatendea watu kwa haki na usawa, walijiona wanajiweza peke yao wakamsahau Mungu wa kweli, Mungu wa Israeli. Ni katika mazingira hayo Nabii Sefania anakuja kutangaza hukumu ya Mungu. Hukumu hii ya Mungu haiji kwa wale walio maskini na wanyenyekevu bali kwa waliojikweza na kumsahau Mungu. Anatoa ujumbe wa faraja kwa wale waliokuwa maskini na wanyonge wachache, “Mtafuteni Bwana enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mnaozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana” Maskini ni wale wanaotambua kwamba hawana chochote katika ulimwengu huu bali wana Mungu. Maskini ni wale wanaotambua kuwa hata kama wana kila kitu bado bila kuwa na Mungu hawana kitu chochote. Hawa watairithi nchi, hawa wataikwepa hukumu ya Mungu.

Furaha ya kweli inapatikana kwa kumtafuta Mungu katika kweli na haki
Furaha ya kweli inapatikana kwa kumtafuta Mungu katika kweli na haki   (@Vatican Media)

Somo la Injili ni kutoka katika Injili ya Mathayo 5:1-12a. Katika somo la Injili Takatifu, Bwana wetu Yesu Kristo anatoa Hotuba yake Mlimani. Bwana wetu Yesu Kristo alipanda mlimani, na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia, naye akaanza kuwafundisha. Ni watu wa namna gani walimjia Yesu kumsikiliza? Hawa hawakua matajiri, hawakua watawala, wala si mafarisayo na waandishi, hawa walikua ni watu maskini, wavuvi, wakulima na waliojishughulisha na kazi zenye ujira mdogo. Ni watu waliokuwa wanapitia mateso kutoka kwa Watawala wakoloni wa kirumi, lakini pia sheria ngumu za dini ya kiyahudi. Wengi wakakata tamaa, na wakawa na shauku kubwa ya ujio wa Masiha, wakasubiria kwa hamu ukombozi kama taifa la Israeli waliovyosubiri kwa hamu ukombozi wao. Kwa nini Bwana wetu Yesu Kristo alipanda mlimani? Bwana wetu Yesu Kristo katika Agano jipya ndiye Musa mpya. Anakwenda mlimani, vile kama Musa alivyopanda mlimani ambapo ndipo alikwenda kupewa sheria ya Mungu, sheria iliyokuwa mwongozo wa taifa la Mungu ili waweze kuifikia nchi ya Ahadi. Bwana wetu Yesu Kristo, anapanda mlimani na hapo, yeye kama Mwalimu, yeye kama Mungu, anatoa sheria mpya kwa wanafunzi wake, ndizo Heri “Beatitudes, Makarios.“ Ndio katiba na mwongozo wa maisha kwa anayetamani kuingia kwenye ufalme wa Mbinguni. Na sheria ya kwanza anayoitoa ni “Heri walio Maskini wa Roho; Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao” Mwenyezi Mungu anawajali, kuwahurumia na kuwainua wale walio maskini, wanaodharauliwa, wasio na thamani (God’s preferential option for the poor), hao watauona ufalme wa Mbinguni. Wale ambao haki yao hawajaipata hapa duniani, wale waliopitia dhuluma na maumivu hapa duniani, Kristo anawaahidi haki na furaha ya kudumu katika uzima wa milele. Heri ni kwa wale wote wanaotambua ya kuwa maisha yao si kitu bila Mungu, wanaotambua kuwa hawajajitosheleza katika maisha hata kama wana kila kitu, bado wanamhitaji Mungu. Ufalme wa Mungu sio kwa wale wanaojikweza bali wale walio wadogo, na wanyonge mbele za Mungu. Kwa nini Bwana wetu Yesu Kristo anaanza na heri hii kati ya heri zote nane? Ni kwa sababu unyenyekevu, umaskini wa Roho, ndiyo msingi wa fadhila nyingine zote. Fadhila nyingine zote zinajengeka ndani ya mtu anayetambua utupu wa moyo wake mbele za Mungu, na Mungu anatukirimia fadhila nyingine zote.  

Sifa za Heri za Mlimani: Muhtasari wa mafundisho tanzu ya Injili
Sifa za Heri za Mlimani: Muhtasari wa mafundisho tanzu ya Injili   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka 1 Kor 1:26-31: Sehemu hii ya Waraka huu wa Mtume Paulo kwa Wakoritho, 1:26-31 ndio kiini cha Waraka huu mzima wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakoritho. Mtume Paulo anaeleza namna Mungu anavyofanya kazi kinyume na mitazamo na vipimo vya kidunia. Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviabishe vyenye nguvu, tena Mungu alichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa ili avibatilishe vilivyoko. Ni kwa njia ya Msalaba, Mwenyezi Mungu ameamua kudhihisha kwetu nguvu yake na hekima yake. Nasi sote bila ya mastahili yetu, licha ya unyonge wetu bado Mungu ametuhesabu tena kuwa wenye haki mbele zake, kwa njia ya sadaka ya Kristo Bwana wetu. Hivyo sisi hatuna lolote la kujivunia kwa kuwa hii yote ni neema ya bure kutoka kwa Mungu. Ndugu zangu katika masomo yote katika Dominika hii ya 4 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa tuna mafundisho yafuatayo ya kujifunza. Kwanza: Je? ni wapi ilipo furaha yangu ya kweli? Katika maisha yetu ya kila siku kama nilivyosema katika utangulizi kila mwanadamu anapambana kutafuta furaha. Ndio sababu tukiulizana swali moja tu kwa nini tunahangaika kila siku kufanya kazi, nguvu, kwa moyo, kwa juhudi na maarifa na kwa sadaka, moja kati ya majibu ni kwamba, tunataka kufanikiwa, tunataka kupiga hatua katika maisha, tunakata kuukimbia umaskini, tunatafuta furaha.  Mtakatifu Augustino wa Hippo, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anatufundisha tofauti kubwa sana kati ya aina mbili za furaha.

Heri ya Kikristo: Mungu humwita mtu kwenda kwake
Heri ya Kikristo: Mungu humwita mtu kwenda kwake   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Aina ya kwanza anasema ni furaha itokanayo na mambo ya kidunia, yaani “Felicitas Temporalis“ (furaha ya kidunia). Ni furaha itokanayo na vitu vya nje ya nafsi ya mwanadamu, vitu vilivyoumbwa na Mungu ila si furaha itokayo kwa Mungu Muumbaji wetu. Vitu hivi ni mali, heshima, umaarufu, afya, mafanikio ya kijamii na kielimu, anasa na starehe nk. Vitu hivi ni vyema kwa asili yake kwa kuwa vimeumbwa na Mungu lakini si lengo la mwisho la maisha ya mwanadamu.Furaha hii haidumu, ni ya muda kwa kuwa vitu vyote vya dunia hii hubadilika, mwanadamu hubadilika na mazingira pia hubadilika. Hivyo furaha inayotegemea vitu hivyo haiwezi kudumu. Tunaweza kuwa navyo vyote leo ila hatuna uhakika kama kesho vitakuwepo. Furaha inayoweza kupotea hiyo si furaha ya kweli. Mtakatifu Augustino anatufundisha kuwa tatizo kubwa sio vitu vyenyewe bali ni namna vinavyopendwa ambao anaiitwa kwa Lugha ya Kilatini “Ordo amoris“ yaani mpangilio sahihi wa upendo wetu. Furaha ya muda hutokea pale mwanadamu anavyopenda vitu vya muda kama vile ni vya milele. Hapo ndipo nafsi hupotoshwa, ndipo vita hutokea, ndipo unyanyasaji hutokea, ndipo rushwa hutawala, ndipo hofu hujaza mioyo yetu, ndipo wivu na uchoyo huzidi sana. Je, moyo wangu upo wapi? Furaha yangu imejengeka katika nini? Mungu akichukua kila nilicho nacho kama alivyofanya kwa Ayubu Je, bado nitabaki na imani, upendo, matumaini kwa Mungu na kwa watu? Mungu amenijalia mema yake, Je, bado nimebaki kuwa mnyenyekevu? Pale moyo wako ulipo ndipo ilipo na hazina yako.

Heri Wapatanishi wataitwa waana wa Mungu
Heri Wapatanishi wataitwa waana wa Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pili: Furaha ya kweli ipo katika kumtafuta Mungu na kuziishi Heri. Mtakatifu Augustino anatufundisha aina ya pili ya furaha ambayo ndiyo furaha ya kweli, furaha ya kudumu. Furaha ya kweli haitokani na vitu bali inatokana na ushirika wa kudumu na Mungu mwenyewe. Mwenyezi Mungu ndiye wema mkuu (Summum bonum), ndiye lengo la mwisho la maisha yetu (Finis ultimus). Hivyo furaha ya kweli lazima ipatikane pale ambapo upo wema mkuu yaani pale alipo Mungu. Ni furaha ya kweli kwa kuwa, Mungu habadiliki, Mungu hapotei, Mungu hachoki. Na hivyo ushirika naye hauwezi kuvunjwa, na furaha itokanayo na Mungu ni ya milele, ni ya wakati wote. Kumbe, heri ni njia ya kuufika uzima wa milele, ni katiba, ni mwongozo, ni mlango wa kuingia katika uzima wa milele. Mtakatifu Augustino yeye alihangaika kuitafuta furaha katika mambo ya ulimwengu huu, hakufanikiwa. Anasema, “Umetuumba kwa ajili yako Ee Mungu, na mioyo yetu haina raha mpaka ipate raha kwako“ Heri si raha ya muda, bali ni hali nafsi iliyopata pumziko thabiti kwa Mungu, licha ya mateso, maumivu, tabu, dhiki, bado roho i tajiri ndani ya uwepo wa milele wa Mungu. Ni nafsi iliyo katika mpangilio sahihi wa upendo, licha ya utajiri, mali, vyeo bado nafasi ya Mungu ipo pale pale katika nafasi ya kwanza juu ya yote tuliyo nayo katika maisha yetu. Kumbe tunavyohangaika kutafuta maisha yetu ya kila siku, tunavyojishughulisha na mambo mengi ya kupita, tumtafute kwanza Mungu asiyepita kamwe, Mungu asiyesahau, Mungu asiyetuacha nasi tutaipata furaha ya kweli. Mwombe Mungu akupe mpango sahihi wa upendo wako “ordo Amaris“ ili daima uipate furaha ya kweli.

Heri za Mlimani Ni Kiini cha Injili
Heri za Mlimani Ni Kiini cha Injili   (ANSA)

Tatu: Tunaziishije Heri hizi katika maisha yetu ya kila siku? Heri ndiyo katiba, ndiyo mwongozo wa maisha yetu katika kuipata furaha ya kweli. Bwana wetu Yesu Kristo katika hotuba yake ya mlimani kama nilivyotangulia kusema anaanza na „Heri walio maskini wa roho, maana Ufalme wa Mbinguni ni wao“ Kisha zinafuata heri nyingine saba. Heri hizi zina maana gani katika maisha yetu, ikiwa ndio mwongozo wa maisha yetu ya ufuasi? Kwanza: Heri walio maskini wa roho; Kuwa maskini wa Roho ni unyenyekevu wa ndani, kutambua utegemezi kamili kwa Mungu na kukubali kuwa mbele za Mungu hatuna chochote cha kujivunia wala kujisifu., Kristo anatuita sote kuukumbatia umaskini wa roho. Kwa unyenyekevu kutambua daima nafasi yake juu ya yote tuliyo nayo. Kutambua utegemezi wetu mbele zake na kwamba bila yeye sisi hatuwezi jambo lolote. Ni kuacha kiburi na majivuno, kuishi maisha ya imani na sala na kukubali neema ya Mungu ifanye kazi ndani mwetu, sio nguvu na uwezo wetu, si kujitegemea na kuona tunaweza kila kitu bila Mungu. Ni kukiri kwamba yote niliyo nayo ni Mungu ametenda, iwe elimu, iwe familia, iwe mali, iwe mafaniko yoyote yale. Mara ngapi tunatafuta sifa zetu kwanza ndipo badae Mungu? Mara ngapi tunajipongeza kwanza sisi na kujisifu na kumsahau Mungu? Umepata kazi nzuri, umefanikwa katika mipango yako, umefanikiwa katika biashara, shukuru. Umeshindwa pia shukuru, Mungu anaona moyo wako, anatambua mahitaji yako. Thawabu yao wote wanaojishusha na kujinyenyekeza ni kuupata uzima wa milele.

Heri wenye huzuni maana watafarijiwa
Heri wenye huzuni maana watafarijiwa   (@Vatican Media)

Pili: Heri wenye Huzuni, maana watafarijika. Heri hii haimanishi kwamba Mungu anatutia moyo tulie kila siku katika maisha yetu la hasha. Katika maisha yetu ya kila siku wapo watu wanaolia, yawezekana ni mimi na wewe tunaolia kila siku kutokana na unyanyasaji, ukandamizaji, ukosefu wa haki, ukosefu wa amani, ukosefu wa upendo, dhuluma, misiba, chuki nk ndani ya jamii yetu, ndani ya familia zetu, ndani ya nchi yetu, na katika dunia yote. Ndio watu hawa aliokuwa akiwahubiriwa Bwana wetu Yesu Kristo, ndio watu aliowapelea ujumbe wa faraja nabii Sefania. Mungu anawalinda wanyonge, wanaoonewa, wanaolia, wanaodhulumiwa “He has prefential option for the poor“ Kristo amekuja kubadili hali yetu, hakuna kulia tena, hakuna kuhuzunika tena kwa yeye anayetambua kuwa Mungu ndiye hakimu mwenye haki. Kutambua kuwa mbinguni ndipo ilipo haki yetu ya kweli. Wanaowaumiza watu, hawataishi milele, wanaodhulumu na kuwanyanyasa na kuiba haki ya wengine, hawataishi milele. Tunasoma katika Kitabu cha Ufunuo wa Yohane maneno ya kutia moyo haya tuapokuwa Katikati ya kilindi cha huzuni, “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwepo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwepo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita” (Ufu 21:4). Maana ya pili ni kuhuzunika na kuona uchungu kwa sababu ya dhambi na nia ya kufanya toba na kuomba huruma ya Mungu kwa ajili ya dhambi zetu na za dunia nzima.

Heri ya Kikristo ni kuingia katika Furaha ya Bwana
Heri ya Kikristo ni kuingia katika Furaha ya Bwana   (@Vatican Media)

Tatu: Heri wenye upole, maana watairithi nchi. Upole ni kinyume cha hasira. Si dhaifu bali wenye uwezo wa kudhibiti hasira na kuamua kutolipa kisasi bali kusamehe. Ni mara ngapi katika maisha yetu tumekua tayari kuwa wapole, kujishusha daima na kuwa chini ili tu kurejesha tena amani na furaha katika maisha yetu? Katika familia zetu, katika jumuiya zetu, mara nyingi inakua ngumu sana kujishusha, na shauku ya kulipiza kisasi inakua kubwa. Tumwombe Kristo Yesu atusaidie daima tuwe tayari kujishusha. Nne: Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa. Njaa na kiu ya haki ni tamaa kubwa ya kutenda daima mapenzi ya Mungu. Ni shauku na kiu ya kumpa kila mtu kila anachostahili. Ni shauku na kiu ya kupinga dhuluma, uonevu, unyanyasaji. Na kujitahidi kuishi maisha ya uadilifu na kuitafuta haki hata kama itakugharimu. Je, mimi ni mtu wa haki? Je katika kazi yangu, nimekua mtu mwadilifu? Nimepinga rushwa, wizi, ufisadi, unyonyaji, faida kwa njia za wongo, wizi, dhuluma na uporwaji wa haki ya wengine? Kristo anaahidi kuwa wote wenye njaa na kiu ya haki watashibishwa, kwamba tamaa yao na kiu yao ya kutafuta haki haitakosa malipo katika maisha ya sasa na maisha ya umilele. Tusali ili daima tuwe na kiu na njaa ya kutenda tu mapenzi ya Mungu. Tano: Heri wenye rehema maana watapata rehema. Watu wenye rehema ni watu wenye huruma, wenye wema wa ndani unaoonekana nje kwa matendo. Ni kuonesha wema na huruma kwa watu wengine. “Be good, be kind, it costs us nothing to be good“ Haitugharimu kuwatendea wenzetu mema, sema mazuri ya wengine, ona uzuri wa Mungu ndani ya wengine, kuwa na huruma, kuwa na uchungu na maumivu wanayopitia wengine. Je mimi nipoje? Nimeasemea mazuri watu wengine? Nimekua mtu wa msaada kwa wengine hata wa mawazo tu, au faraja tu au nimewazimia watu simu waliponieleza changamoto zao, nikaona kama wananipotezea muda. Kuna nyakati tunawakwepa watu tunaona kama kuwasaidia tutapata hasara, tutapoteza muda. Anayehurumia, naye atahurumiwa na Mungu.

Heri wanyenyekevu na wapole wa moyo!
Heri wanyenyekevu na wapole wa moyo!   (@Vatican Media)

Sita: Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu. Kutoka kwenye Lugha ya Kigiriki “Katharoi tē kardia“ heri hii yamaanisha moyo safi, moyo usiogawanyika. Ni dhahiri kwamba mtu hawezi kumpenda Mungu kwa dhati na kupenda mambo ya dunia. Kristo anatufundisha kuwa hatuwezi kumpenda Mungu vile inavyostahili kama tumejishikila na mambo ya kidunia, hatuwezi kuipata furaha ya kweli. Ni mwaliko wa kuepuka tamaa za kidunia, kutogawanya moyo kwa kupenda mambo ya kidunia kuliko Mungu. Ni kukubali daima kusafishwa na Mungu mwenyewe, kwa kuruhusu mioyo yetu na dhamiri zetu ziongozwe kwa neno lake. Kuruhusu Mungu atakase fikra zetu, atakase mawazo na akili zetu ili daima tuweze kustahili kujongea mbele zake. Saba: Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye mpatanishi mkuu. Alimpatanisha mwanadamu na nafsi yake, mwanadamu aliyemwasi Mungu kwa dhambi. Kristo anatualika sote kuwa wajenzi wa amani. Maana ya wapatanishi hapa katika lugha ya kigiriki makarioi hoi Eirēnopoioi ni waumba amani, waendeshaji wa amani, na watengenezaji wa muungano. Kumbe sisi sote tunaungana na Mungu kuleta upatanisho wa kweli. Zipo familia zenye migogoro, ndoa zenye migogoro, jamii zenye machafuko, tunafanya jitihada kuleta upatanisho wa kweli? Je kuna nia ya dhati ya kuleta upatanisho au ni kuongeza petrol katika moto? Hawa wanaoleta amani, wanaotafuta upatanisho wataitwa wana wa Mungu kwa kuwa wanajenga familia ya Mungu kwa haki, amani na mshikamano.

Sufa za Heri ni Dira, Katiba na Mwongozo wa Maisha
Sufa za Heri ni Dira, Katiba na Mwongozo wa Maisha   (@VATICAN MEDIA)

Nane: Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki maana ufalme wa mbinguni ni wao. Wapo wengi kama nilivyotangulia kusema ambao wanateseka kwa sababu ya kusimamia haki, kwa sababu ya kusema ukweli na hilo likawagharimu. Kristo mwenyewe alituonesha mfano, alisema ukweli, alitetea wanyonge, alikemea maovu, mwisho akasulibiwa msalabani. Kumbe nasi tulio wafuasi wake tutegemee mateso, tutegemee dhuluma, tutegemee kusemewa mabaya, lakini hayo yote si kitu kwa kuwa thawabu yao wanaotetea haki hasa kwa ajili ya maskini na wanyonge ufalme wa Mbinguni ni wao.Hitimisho. Katika Dominika hii tuombe neema ya kupanda daima Mlimani kumsikilia Yesu, katika sala, katika ukimya, kupokea mafundisho yake na kuyaweka katika matendo, kukumbatia fadhila ya unyenyekevu iliyo mama wa heri zote ili tuweze kuipata furaha ya kweli yaani kuurithi uzima wa milele. Yesu nijalie daima nitambue ya kuwa maisha yangu si kitu bila uwepo wako. Nipe nguvu ya kukutumaini wewe siku zote, na kutambua ya kuwa utajiri na furaha ya kweli tutavipata tutakapoungana nawe, tutakapokuona uso kwa uso. Amina.

Tafakari D 4 Mwaka
30 Januari 2026, 09:46